Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora

Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora
----------------------WE THANK AND APPRECIATE YOU FOR VISITING CHADEMA DIASPORA BLOG. AGAIN, THANK YOU!-----------------------

Saturday, June 29, 2013

Bunge lajikoroga kwa kombati za CHADEMA



     LICHA ya kanuni za Bunge kuruhusu vazi la safari suti yenye mshono kama kombati zinazovaliwa na baadhi ya wabunge wa CHADEMA, wiki hii uongozi wa Bunge umezinduka usingizini na kudai kuwa vazi hilo haliruhusiwi kuvaliwa bungeni kwa vile ni sare ya chama. 
Kufuatia uamuzi huo, kiongozi wa kambi rasmi ya upinzani bungeni, Freeman Mbowe na wabunge wanzake watatu, Tundu Lissu (Singida Mashariki), Godbless Lema (Arusha Mjini) na Ezekiel Wenje (Nyamagana) walizuiliwa na askari wakielezwa kuwa wamevalia sare za chama. Lissu aliwaeleza waandishi kuwa walishangazwa na uamuzi huo wakati mavazi hayo wamekuwa wakiyavaa miaka yote na kuingia nayo bungeni hasa Mwenyekiti wao, Mbowe.

       “Sisi hali hiyo tulianza kuishtukia tangu asubuhi tulipoingia kwenye eneo la Bunge, kama mligundua kulikuwa na askari wengi sana kila kona kuliko kawaida. Kinyume cha utaratibu wa kanuni askari wa kawaida walingia hadi bungeni. “Tulipofika wakati wa kuingia ukumbini mimi, Mbowe, Lema na Wenje tuliambiwa haturuhusiwi kwa kuwa tumevaa sare za chama. Tulipouliza nani kaagiza, wakasema uongozi wa juu, yaani Spika. Kanuni za Bunge ziko kimya kuhusu uvaaji wa sare ya chama bungeni, isipokuwa zimeainisha aina za mavazi ya kuvaliwa na wabunge wanawake na wanaume. Kwa mujibu wa kanuni ya 149 (3)(b) Kwa wanaume wanaruhusiwa kuvaa 

(i) Suti ya Kiafrika au safari ya mikono mirefu au mifupi yenye ukosi au shingo ya mviringo na yenye fulana au bila fulana ndani, ya rangi moja, isiyokuwa na nakshi, pamoja au bila baragashia.

(ii) Vazi la kimwambao yaani kanzu rasmi na nadhifu, koti, baraghashia na makubadhi au viatu; 

(iii) Suti kamili ya Kimagharibi ya rangi kadiri isiyomeremeta; 

(iv) Koti aina ya blazer na tai, pamoja na suruali yoyote ya heshima; au (v) Tarbushi na kilemba cha Singasinga, au kilemba chochote kinachovaliwa kwa mujibu wa masharti ya imani au mila.

Utetezi wa Bunge


Mkurugenzi wa shughuli za Bunge, John Joel, alisema suti hizo zinazovaliwa na wabunge wa CHADEMA zinakiuka kanuni ya 149 (3) (b) (i). Joel alifafanua kuwa yawezekana huko nyuma wamekuwa wakifanya makosa kwa kuwaruhusu wabunge hao kuingia na suti hizo lakini kuanzia sasa wameamua kuanza kuchukua hatua ya kuwazuia. “Zile wanasema si sare ya chama lakini wote tunawaona kwenye mikutano na shughuli za chama ndizo zinavaliwa na isitoshe tuliwahi kuwatahadharisha kuwa ziko kinyume cha kanuni wasizivae bungeni ila wamekuwa wakiendelea kuzivaa,” alisema.

    Alipoulizwa ni kwanini waliendelea kuruhusiwa kuingia bungeni ikiwa kombati zao zinakiuka kanuni, Joel alisema kuwa: “Ni kweli pengine tulizembea kuchukua hatua lakini ndiyo maana tumeanza sasa, hatutaruhusu tena.” Licha ya kanuni hiyo kuwa kimya kuhusu kuvaa sare za vyama bungeni, Joel alisema kuwa uamuzi huo ulikuwa ni busara ya Spika wa wakati huo, Samuel Sitta, lakini haijaingizwa kwenye kanuni kimaandishi. Tanzania Daima lilitaka kufahamu ni kwanini uamuzi huo ukaanza ghafla juzi baada ya wabunge wa CHADEMA kurejea kutoka jijini Arusha, ambapo Joel bila kufafanua alisema: “Kawaulize walipanga nini wakiwa Arusha? Ndiyo maana tukaamua kuchukua hatua.

      “Bora tukaonekana tumeonea kuliko kuendelea kufumbia macho kanuni. Tuwe wawazi, kombati zao zina nakshi kupitiliza kwa mujibu wa kanuni,” alisema. Lakini Mkurugenzi wa Mawasiliano na Habari wa CHADEMA, John Mnyika, alisema Joel hajui kanuni za Bunge ndiyo maana amekuwa anampotosha spika na viongozi wa Bunge kufanya maamuzi ya ajabu. “Wametuzuia juzi kwa sababu ya maelezo ya kina Pinda na serikali ya CCM, si kwa sababu ya ukiukwaji wa kanuni za Bunge. Kumekuwa na utamaduni wa hovyo wa kutafsiri vibaya kanuni za Bunge kwa lengo moja tu kuwadhibiti CHADEMA,” alisema.

Wasusia bajeti

     Mnadhimu wa kambi hiyo, Lissu alisema baada ya kukutana na kujadiliana kwa kirefu waliafikiana kuwa hawakuwa na sababu ya kuingia. “Tukio la bomu kwa wafuasi wetu jijini Arusha halikuwa la bahati mbaya lakini tumejiuliza ni kwanini Bunge halikuahirishwa walau kwa siku moja kama ilivyo utamaduni ili kushiriki kuomboleza msiba huo,” alisema. Alisema kuwa pamoja na kwamba kiongozi wao wa kambi, Mbowe na Lema ndio walikuwa wamelengwa kulipuliwa lakini wakanusurika, Spika wa Bunge, waziri mkuu hakuna hata mmoja aliyetuma salamu za pole kwa viongozi hao. “Waliolengwa kulipuliwa ni Mbowe, Lema na James ole Millya lakini hata risasi zilizowaua wale wafuasi wetu wanne zilikuwa zikielekezwa kwa viongozi wetu.

   “Sasa tunajiuliza Bunge limeona waliokufa Arusha ni Watanzania lakini kwa vile walikuwa kwenye mkutano wa CHADEMA haiwahusu, hivyo kama wanajifanya kama hakuna kilichotokea sisi tunaingia ndani kufanya nini?” alihoji. Lissu aliongeza kuwa kila unapotokea msiba mkubwa kwa wananchi wakati Bunge likiendelea, wamekuwa wakitumwa wawakilishi lakini kwa tukio la Soweto, Arusha Bunge halikutuma mwakilishi. Alifafanua kuwa sababu kubwa iliyowafanya wakifie uamuzi huo ni kutokana na hatua ya Spika wa Bunge kupindisha ratiba ya Bunge ili kuwanyima nafasi wasijadili bajeti hiyo.

Serikali yaufyata kwenye mafuta

     Hatimaye serikali imeridhia uamuzi wa wabunge na kukubali kufuta pendekezo la kuongeza ushuru wa bidhaa kwenye mafuta ya dizeli na petroli. Katika marekebisho hayo, Waziri wa Fedha na Uchumi, William Mgimwa, alikuwa amependekeza kuongeza ushuru wa mafuta hayo kwa sh 2 kwenye dizeli na sh 61 kwenye petroli kwa lita. Kwa mantiki hiyo, alisema kuwa wataendelea kutoza ushuru wa bidhaa wa sh 333 kwa lita katika mafuta ya petroli na sh 215 kwa lita kwenye dizeli. Wakijadili muswada wa sheria ya fedha wa mwaka 2013, wabunge walipinga mapendekezo hayo na kuishauri serikali itafute mapato kutoka kwenye vyanzo vipya vilivyoanishwa na Kamati ya Bunge ya Bajeti badala ya kuongeza gharama za maisha kwa wananchi.

     Waziri Mgimwa alisema walikubali ushauri huo ili kuleta unafuu kwa wananchi na kuzuia mfumuko wa bei unaoweza kujitokeza. Alisema serikali itaendelea kutoza ushuru wa sasa bila kuongeza hata senti lakini wameongeza ushuru wa mafuta ya taa kufikia sh 425 kwa lita badala ya sh 400.30 zinazotozwa sasa hivi.
Alisema kuwa hatua hizo ni pamoja na kudhibiti uchakachuaji wa dizeli uliokuwa ukifanywa kwa kutumia mafuta ya taa, hivyo kuingiza nchi katika hatari zaidi. Pia Waziri Mgimwa alisema kuwa serikali imeongeza ushuru wa mafuta ya petroli (fuel levy) kutoka sh 200 hadi 263 kwa lita ikiwa ni lengo la kuongeza mapato ya mfuko wa barabara nchini ili kugharamia barabara zinazopaswa kujengwa.

     “Tumeongeza ushuru wa mafuta ya dizeli (fuel levy) kutoka sh 200 hadi 263 kwa lita lengo hili mbali na kuongeza mapato pia nazo zitasaidia kugharamia ukarabati wa barabara,” alisema. Waziri pia alifafanua kuwa ushuru wa bidhaa kwenye simu hautatozwa kwenye huduma za kutuma na kupokea fedha bali kwenye huduma nyingine kama kupiga, kutuma ujumbe mfupi au picha. “Baada ya kuchunguza kwa undani na kupokea maoni ya kamati ya bajeti, tumeona kweli kuna uwezekano wa mtu kutozwa kodi mara mbili pale anapokuwa ameunganishwa kutoka mtandao mmoja wa simu na mwingine. Hilo tutakaa na wenzetu wa TCRA kuliangalia,” alisema.

   Aliongeza kuwa serikali imeafikiana na kamati ya bajeti kwamba mapendekezo ya msamaha wa kodi ya zuio kwa ndege za kukodi yasogezwe mbele hadi mwaka ujao wa fedha ili kutoa muda kwa serikali na wafanyabiashara wa sekta ya anga kuendelea kujadiliana. “Serikali pia imeridhia mapendekezo ya kamati ya bajeti ya kukusanya mapato kutoka uvuvi wa bahari kuu na sasa linafanyiwa kazi ili kiwe moja ya vyanza vipya vya mapato vitakavyotupa mapato makubwa pamoja na uwekezaji kwenye migodi mikubwa,” alisema.

Spika awatwisha zigo waandishi

    Katika hali isiyotarajiwa, Spika wa Bunge, Anne Kaminda, amejivua lawama za upendeleo kwa chama chake zinazotolewa kwa kiti chake na wapinzani akidai waandishi wa habari ndio wenye tabia ya kupotosha watu kuhusu jambo hilo. Spika Makinda alitoa tuhuma hizo nzito kwa waandishi wa habari muda mfupi kabla ya kuliahirisha Bunge akisema kuwa kila siku wanaandika kuwa anapendelea, jambo ambalo halipo. “Waandishi kila siku wataandika tu Spika kapendelea…jamani kwa jina la Mungu kazi hiyo haipo. Kama ninavyofanya hivi napendelea, siku nikipendelea itakuwaje? Si itakuwa hatari kweli.

    “Mimi napenda muamini kabisa kuwa tunafuata kanuni za Bunge na pale tunapopotoka tunasahihishwa, tafadhali waandishi wa habari acheni tabia ya kudanganya watu kuwa tunaendesha Bunge kwa kupendelea,” alisema. Makinda aliongeza kuwa wangekuwa wanapendelea kuna watu wengine wasingepata nafasi hata ya kuzungumza, kwamba Bunge ni wote, kila mtu anapewa haki ya kusema kwa mujibu wa kanuni zao. “Nafahamu kuna waandishi wa habari wana matatizo yao. Ondoeni matatizo yenu mjue pia Mungu anawaangalieni. Taifa lolote lisilomuogopa Mungu ni taifa lililokwisha,” alisema.

   Aliwasihi wabunge kubishana kwa hoja na kutowekeana chuki baada ya kutoka bungeni, kwamba mambo yote yaliyotokea na wakati mwingine wabunge hao kutofautiana yanabakia ndani humo humo. “Wananchi wafahamu kuwa tunavyo vyama vingi, tunao wajibu wa kuviheshimu vyama vyetu lakini isiwe sababu ya kutenga wala kugawa watu,” alisema. Tangu kuanza kwa Bunge la kumi chini ya Spika Makinda, Bunge limekuwa likilalamikiwa na wananchi kuwa linaendeshwa kwa ubabe na ukiukwaji wa kanuni kutokana na yeye, naibu wake na wenyeviti kulalamikiwa kuwabana wapinzani. Wadadisi hao wa masuala ya kibunge wanalitazama Bunge hili kama limekosa msisiko likilinganishwa na lile la mtangulizi wake, Samuel Sitta, lililokuwa maarufu kama la ‘kasi na viwango’.

Mdee, Lissu wajibu mapigo

      Wabunge wa CHADEMA, Halima Mdee (Kawe) na Tundu Lissu (Singida Mashariki), wamejibu mapigo kwa serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuwa inapotosha taarifa za mlipuko uliotokea Arusha kwenye mkutano wa kampeni za chama chao. Mdee alisema bungeni kuwa serikali ilitumia nafasi ya kutokuwapo kwa wabunge wa CHADEMA kutoa kauli zenye utata na zenye upotofu mkubwa kuhusu tukio la mlipuko huo wa bomu. Licha ya kutomtaja kwa jina lakini Mdee ni kama alimlenga Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, ambaye ndiye alitoa kauli hiyo bungeni kwa niaba ya serikali akisema wafuasi wa CHADEMA waliwazuia polisi kumkamata mlipuaji.

     Lukuvi katika taarifa hiyo alisema kuwa polisi walimwona mlipuaji wa bomu hilo liliosababisha vifo vya watu wanne na wengine 70 kujeruhiwa lakini kutokana na uchochezi wa wanasiasa, wakati wakimfukuza kumkamata wafuasi wa CHADEMA walianza kuwashambulia kwa mawe. Mbali na Lukuvi, pia Naibu Katibu Mkuu wa CCM, Mwigulu Nchemba na mawaziri, Hawa Ghasia na Mary Nagu nao walikitwisha lawama CHADEMA wakidai kuwa kilihusika na mlipuko huo. Mdee wakati akichangia Muswada wa Sheria ya Fedha mwaka 2013, alitumia dakika chache za mwanzo kugusia tukio hilo la Arusha akisema: “Kwa kuwa ni mara yangu ya kwanza kuzungumza humu bungeni baada ya tukio la mlipuko wa bomu, naomba nichukue nafasi hii kuwapa pole Wana-Arusha.

      “Lakini vile vile nichukue nafasi hii kulaani vikali kauli zenye utata na zenye upotofu mkubwa zilizotolewa na serikali hapa bungeni. Serikali inajua nini kilichotokea Arusha, ilitumia kutokuwapo kwetu kupotosha lakini nashukuru kwamba ukweli utadhihiri,” alisema. Mdee alisema kuwa watakuwa ni wendawazimu kama chama kujilipua mabomu wenyewe ili wapate umaarufu. “Hiki chama mnajua kasi yake na mnajua muziki wetu 2015 utakuwaje,” alisema. Naye Lissu alisema kuwa manyanyaso na mateso wanayoyapata Watanzania kutoka kwa serikali ni mapito kwenye bonde la mauti ya kifo kuelekea kilele cha uhuru.
Lissu alinukuu kauli ya rais wa zamani wa Afrika Kusini, mzee Nelson Mandela, aliyoitoa Septemba 21, mwaka 1953.

    “Mtoto wa Afrika wa pili ninayemzungumzia yuko kitandani anaweza kufa wakati wowote. Mwaka huo alisema maneno hayo baada ya kuwa amepigwa marufuku yeye na viongozi wenzake wa ANC kukutana. “Alisema maneno hayo kwa kuandika, hakwenda kwenye mkutano kwamba: ‘Barabara ya kwenda kwenye uhuru si rahisi mahali popote na wengi wetu watapita mara kwa mara katika bonde la mauti ya kifo kabla ya kufika kwenye kilele cha matazamio yetu’,” alisema. Lissu aliongeza kuwa leo nchi yetu tumefika mahali serikali inapiga watu mabomu kwenye mikutano ya hadhara, inapiga wabunge, inakamata watu na kuwatesa huko Mtwara, kwamba wanakamatwa usiku, wanapigwa viboko na kumwagiwa maji ya chumvi.

     “Watanzania wanateswa, tunapita kwenye bonde la mauti ya kifo…mtasema sana. Watu wamekufa, watu wameuawa, Bunge linaendelea na vikao kama kawaida,” alisema. “Kwa hiyo, maneno ya mzee Mandela ya hakuna njia rahisi kuelekea kwenye kilele cha uhuru, na wengi wetu lazima tutapita kwenye bonde la mauti kabla ya kufika kwenye uhuru…ni maneno mhimu na tutayakumbuka siku kama ya leo ambapo mzee Mandela yupo kitandani,” alisisitiza. Hata hivyo, baada ya kutoa kauli hiyo Spika wa Bunge, Anne Makinda, alisimama akasema: “Mheshimiwa Tundu Lissu yote uliyoyasema ni sawa, lakini hilo la kwamba Bunge hatukuacha kwa sababu uliyoisema si sahihi.”

Source: Kamkara E. (June 2013). Bunge lajikoroga kwa kombati za CHADEMA. Retrieved from Tanzania Daima

No comments: