Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora

Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora
----------------------WE THANK AND APPRECIATE YOU FOR VISITING CHADEMA DIASPORA BLOG. AGAIN, THANK YOU!-----------------------

Friday, June 14, 2013

Bajeti: Maumivu


Petroli, dizeli nazo juu
Magari madogo kodi juu
Simu za mikononi kodi mpya


Serikali imetangaza bajeti yake ya mwaka wa fedha wa 2013/14 ambayo imepandisha kodi za …… ili kufanikisha lengo la kukusanya jumla ya Sh. trilioni 18.249 kutoka kwenye vyanzo vya ndani na nje.

Akitangaza kodi hizo mpya bungeni Dodoma jana ambazo zitaendelea kuumiza wanywaji bia, mvinyo na wavutaji sigara na hata wamiliki wa magari, Waziri wa Fedha na Uchumi, Dk. 
William Mgimwa alisema mapato ya kodi na mapato yasiyo ya kodi yanatarajiwa kufikia Sh. trilioni 11.154 sawa na asilimia 20.2 ya Pato la Taifa. 

Aliainisha vipaimbele vya bajeti kuwa ni Mpango wa Maendeleo wa mwaka 2013/14 na mfumo mpya wa utekelezaji wa vipaumbele vyenye matokeo makubwa na ya haraka (Big Results Now – BRN).

Kingine ni kuendelea na utekelezaji wa awamu ya Pili ya Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umasikini (MKUKUTA II); Malengo ya Maendeleo ya Milenia 2015; Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010; na programu za maboresho katika sekta ya umma. Lengo likiwa ni kufikia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025.

Dk. Mgimwa alitaja matarajio ya serikali kuwa ni pato halisi la Taifa linatarajiwa kukua kwa asilimia 7.0 mwaka 2013, na asilimia 7.2 mwaka 2014; kuendelea kudhibiti kasi ya upandaji bei ili ibaki kwenye viwango vya tarakimu moja, huku akisisitiza kuwa mfumuko wa bei unatarajiwa kushuka zaidi kufikia asilimia 6.0 Juni 2014.

Alisema mapato ya ndani yataongezeka kufikia uwiano wa Pato la Taifa kwa asilimia 20.2 mwaka 2013/14 ikilinganishwa na matarajio ya asilimia 17.7 kwa mwaka 2012/13;

Aligusia pia nakisi ya bajeti (ikijumuisha misaada) kuwa itafika asilimia 5.0 ya Pato la Taifa mwaka 2013/14; kudhibiti ongezeko la ujazi wa fedha kwa tafsiri pana zaidi (M3) katika wigo wa asilimia 15.0 Juni 2014  utakaowiana na malengo ya ukuaji wa uchumi na kasi ya upandaji bei.

Katika mwaka wa fedha utakaoanza Julai mosi mwaka huu, malengo ni kuhakikosha kuwa akiba ya fedha za kigeni inakuwako ya kuwezesha kukidhi mahitaji ya uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nje kwa kipindi kisichopungua miezi minne mwaka 2013/14.

MISINGI YA BAJETI 

Alisema bajeti hiyo imejiegemeza kwenye misingi mikubwa saba; mosi kuendelea kuimarisha na kudumisha amani, usalama, utulivu na utengamano; mbili, kuendelea kuboresha viashiria vya uchumi jumla na maendeleo ya jamii vikiwamo Pato la Taifa, biashara ya nje, fedha, mapato na matumizi na viashiria vya huduma za jamii; tatu kuongeza mapato ya ndani kwa kuimarisha vyanzo vilivyopo na kubuni vyanzo vipya vya mapato; nne, kuboresha usimamizi wa fedha za umma; tano kuimarisha mfumo wa IFMS na kuhakikisha unatumika kuweka mihadi ya huduma na bidhaa kabla ya malipo.

Msingi wa sita ni kuzingatia vipaumbele vilivyopo katika Mpango wa Kwanza wa Maendeleo wa Miaka Mitano hasa vipaumbele vyenye matokeo makubwa na ya haraka pamoja na MKUKUTA II; na saba kuboresha mfumo wa utekelezaji wa vipaumbele na uwajibikaji.

SERA ZA MAPATO

Katika kutekeleza hayo, aliainisha sera za mapato kuwa kupanua wigo wa kodi kwa kubainisha vyanzo vipya na kuimarisha usimamizi wa ukusanyaji wa mapato kutoka vyanzo vilivyopo.
 
“Aidha, hatua zaidi zitachukuliwa kudhibiti na kupunguza misamaha ya kodi. Kwa ujumla, sera na hatua zitakazotekelezwa katika mwaka wa fedha 2013/14 zinalenga kuimarisha uwezo wa Serikali kukusanya mapato ya ndani ili kupunguza utegemezi kutoka nje, na kupunguza kutegemea kodi zinazotokana na biashara za kimataifa,” alisema.

Mapato hayo pia yataongozwa na sera ya kubuni vyanzo vya mapato kama kuanza kuuza vitalu vya misitu na uwindaji kwa njia ya mnada na kufanya tathmini ya mali na ardhi ili kuimarisha makusanyo ya tozo ya mali na kodi ya ardhi. 

Dk. Mgimwa alianisha hatua nyingine kuwa ni kuangalia upya misamaha ya kodi kwa lengo la kupunguza misamaha ya kodi kwa kufuta msamaha wa kodi ya ongezeko la thamani kwenye huduma za utalii na Sheria ya Uwekezaji itafanyiwa marekebisho ili kupunguza misamaha ya kodi na kubakiza misamaha yenye tija na yenye kuchochea uwekezaji mkubwa katika sekta za uchumi za kimkakati.

Nyingine ni kuendelea kuunga mkono jitihada za kuanzisha kituo kimoja cha kutoa huduma bandarini (one stop centre) katika bandari. 

Kuendelea kuwajengea uwezo watumishi wa Serikali wakiwamo wa Mamlaka ya Mapato ili kupata ujuzi wa kudhibiti mbinu za kukwepa kodi zinazotumiwa na kampuni kubwa hasa katika sekta za mawasiliano, madini na gesi ukiwamo ujuzi wa kukagua uhamishaji wa gharama yaani  “transfer pricing” hivyo kudhibiti mianya ya kupotea kwa mapato.

Alitaja hatua nyingine kuwa ni TRA kuendelea kuimarisha matumizi ya mashine za kieletroniki za kutoa risiti (Electronic Fiscal Devices-EFDs) ambazo zimeunganishwa moja kwa moja na Mamlaka hiyo kwa mtandao wa kompyuta ili kuhakikisha kuwa Serikali inapata mapato yake stahiki.  

Alisema TRA itaanzisha mfumo mpya ujulikanao kama Revenue Gateway ambao utaanza kutumika rasmi kuanzia tarehe 1 Julai 2013 ili kuboresha mifumo iliyopo ya ulipaji kodi na upatikanaji wa taarifa za malipo ya kodi kwa njia ya mtandao. 

Aidha, mfumo huo utarahisisha uhamishaji wa fedha kutoka kwenye benki za biashara hadi Mfuko Mkuu wa Serikali.  Vilevile, mlipakodi atalazimika kujisajili kwa ajili ya kufanya malipo kupitia tovuti ya Mamlaka ya Mapato Tanzania kabla ya kulipa kupitia mfumo wa Tanzania Interbank Settlement System (TISS). 

KUKUSANYA MAPATO

Dk. Mgimwa alisema mafanikio ya mikakati hiyo yataifanya serikali ikusanye mapato ya kodi na yasiyo ya kodi ya Sh. trilioni 11.154 sawa na asilimia 20.2 ya Pato la Taifa. 
Alisema kati ya kiasi hicho, mapato ya kodi ni Sh. Trilioni 10.413, na mapato yasiyo ya kodi ni Sh. bilioni 741.1 Mapato yanayotokana na vyanzo vya Halmashauri ni Sh. bilioni 383.5 sawa na asilimia 0.7 ya Pato la Taifa. 

MIKOPO YA NDANI

Alisema Serikali itakopa Sh.trilioni 1.700 katika mwaka 2013/14 kutoka soko la ndani. Kati ya kiasi hicho, Sh. bilioni 552.3 sawa na asilimia moja ya Pato la Taifa ni kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo na kiasi cha Shilingi Trilioni 1.147 ni kwa ajili ya kulipia hatifungani na dhamana za Serikali za muda mfupi zinazoiva.

MISAADA NA MIKOPO YA MASHARTI NAFUU

Katika mwaka 2013/14, alisema Serikali inatarajia kupata misaada na mikopo yenye masharti nafuu kiasi cha Sh. Trilioni 3.855 kutoka kwa Washirika wa Maendeleo. Kati ya fedha hizo, misaada na mikopo ya kibajeti ni Sh. trilioni 1,163.1; misaada na mikopo kwa ajili ya miradi ya maendeleo ni Sh. bilioni 2,191.6; na mifuko ya kisekta ni Sh. bilioni 500.

MIKOPO YA NJE YENYE MASHARTI YA KIBIASHARA

Waziri Mgimwa alisema Serikali itakopa kutoka nje mikopo yenye masharti nafuu ya kibiashara Sh. Trilioni 1.156, sawa na Dola za Marekani milioni 700. Mikopo hiyo itatumika kugharimia miradi ya maendeleo kama ilivyoainishwa kwenye Mpango wa Maendeleo wa mwaka 2013/14. 
 Hata hivyo, alisisitiza kuwa uamuzi wa kuendelea kukopa kwa masharti nafuu ya kibiashara unazingatia uhimilivu wa Deni la Taifa uliopo. 

SERA ZA MATUMIZI

Waziri huyo alisema ili kutekelezwa ipasavyo kwa bajeti hiyo serikali itaongozwa na sera za matumizi zifuatazo; kuwiainisha matumizi na mapato yanayotarajiwa; nakisi ya bajeti (ikijumuisha misaada) haitazidi asilimia 5.0 ya Pato la Taifa; Mafungu yatazingatia viwango vya matumizi vitakavyoidhinishwa na Bunge; Kutenga fedha za kutosha katika kutekeleza miradi ya vipaumbele vilivyoainishwa katika Mpango wa Maendeleo; na Kuzingatia Sheria ya Fedha za Umma na Sheria ya Ununuzi wa Umma.

MGAWO WA FEDHA

Aliainisha mgawo wa fedha kuwa utazingatia kugharamia nyongeza ya mishahara pamoja na kulipa mishahara kwa wakati; kuboresha huduma za kiuchumi na maendeleo ya jamii; kukamilisha mchakato wa upatikanaji wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; kuendelea na utoaji wa vitambulisho vya Taifa na kukamilisha uchambuzi wa takwimu za sensa ya watu na makazi.

Maeneo mengine ni maandalizi ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015; na kuendelea kulipa madeni ya ndani na nje yaliyoiva pamoja na madai mbalimbali ya watumishi na wazabuni yaliyohakikiwa.

KUBANA MATUMIZI

Alisisitiza kuwa serikali itaendelea kubana matumizi kwa kupunguza matumizi yasiyo ya lazima katika maeneo mbalimbali kama vile semina, usafiri wa ndani na nje, ununuzi wa samani, maonesho mbalimbali na katika magari. 

HATUA MPYA

Alitaja hatua mpya za kubana matumizi kuwa ni kuanza kwa mfumo wa malipo ya simu kabla ya huduma; kutumia utaratibu wa ununuzi wa magari wa pamoja ambao utapunguza gharama za ununuzi na kupunguza matumizi ya magari ya Serikali kwa kuanzisha utaratibu wa kuwakopesha magari watumishi wa Serikali wanaostahili.

Nyingine ni Kuainisha kanuni za ununuzi wa umma za Serikali Kuu na Serikali za Mitaa kwa lengo la kuimarisha ununuzi katika Mamlaka za Serikali za Mitaa na kuhimiza matumizi ya samani zinazotengenezwa nchini.

MATUMIZI YA MAENDELEO

Alisema mgawo wa bajeti utakwenda kwa vipaumbele vya miundombinu ya nishati; usafirishaji (barabara, reli, viwanja vya ndege, usafiri wa majini); TEHAMA; maji safi na maji taka na umwagiliaji.

Nyingine ni kilimo ikijumuisha mazao ya chakula na biashara, malighafi ya viwandani, ufugaji, uvuvi na misitu; 

Viwanda vinavyotumia malighafi hususan za ndani, na kuongeza thamani, viwanda vikubwa vya mbolea na saruji, viwanda vya kanda maalum za kiuchumi, kielektroniki na TEHAMA.

Maendeleo ya rasilimali watu na Ujuzi kwa kutilia mkazo sayansi, teknolojia na ubunifu; uendelezaji wa huduma za utalii, biashara na fedha; na  huduma za jamii: kuimarisha upatikanaji na ubora wa huduma za jamii.

MGAWO KISEKTA

Waziri alisema katika mwaka 2013/14, Serikali imeweka kipaumbele katika kutatua kero ya maji kwa wananchi ambapo Sh. bilioni 747.6 zimetengwa kwa ajili ya kuimarisha miundombinu ya maji mijini na vijijini. 

Alisema ili kuimarisha miundombinu ya uchukuzi ambayo inajumuisha barabara, reli, madaraja, bandari na viwanja vya ndege, Serikali imetenga Sh. trilioni 2.1690 katika mwaka 2013/14 ikilinganishwa na Sh. trilioni 1.940 mwaka 2012/13. 

Katika fungu hilo Sh. bilioni 196.8 ni kwa ajili ya kuimarisha miundombinu ya reli ikilinganishwa na Sh. bilioni 134.2 zilizotengwa mwaka 2012/13, sawa na ongezeko la asilimia 46.6. 

Alisema jumla ya Sh. trilioni 1.116 zimetengwa kwa ajili hiyo ya umeme na miundombinu yake ikilinganishwa na Sh. bilioni 731.8 mwaka 2012/13, sawa na ongezeko la asilimia 52.5. 

FEDHA

Serikali inatarajia kutunga sheria ya Mfumo wa Malipo nchini kwa ajili ya kuwa na utaratibu wa usimamizi wa mifumo ya malipo nchini ili kuboresha matumizi ya kielektroniki katika kufanya malipo.

Walengwa wakuu wa sheria hii ni pamoja na kutumia simu za mikononi, huduma za benki kwa njia ya mtandao, vituo vya mauzo na mashine za kutolea fedha (ATM); Pia serikali inaandaa Sera ya Bima ya Taifa; na kufanya mapitio ya Sera ya Taifa ya Taasisi ndogo za Fedha, 2002.

HIFADHI YA JAMII

Mwaka wa fedha unaokuja pia serikali inaandaa kanuni na miongozo ambayo itajikita katika kuboresha sekta ya hifadhi ya jamii na kuifanya kuwa endelevu na yenye mchango katika maendeleo ya wanachama wa mifuko na nchi kwa ujumla.

Kusajili mifuko, mameneja uwekezaji (Fund Managers) na watunza mali (Custodians) kwa ajili ya kutenganisha majukumu kwenye uendeshaji wa Mifuko ili kuleta ufanisi zaidi na kutoa elimu kwa umma kuhusu sekta ya hifadhi ya jamii.

DENI LA TAIFA

Katika kuimarisha usimamizi wa Deni la Taifa, alisema Serikali inakamilisha taratibu za kuanzisha Idara ya Usimamizi wa Deni la Taifa ndani ya Wizara ya Fedha ambayo itaanza kazi mwaka 2013/14.

MAPATO

Serikali imepanga kukusanya jumla ya Sh. bilioni 18,249 kutoka kwenye vyanzo vya ndani na nje. Mapato ya kodi na mapato yasiyo ya kodi yanatarajiwa kufikia Sh. bilioni 11,154.1 sawa na asilimia 20.2 ya Pato la Taifa. 

Halmashauri zitakusanya Sh. bilioni 383.5 sawa na asilimia 0.7 ya Pato la Taifa. 
Washirika wa Maendeleo watatoa misaada na mikopo ya jumla ya Sh. trilioni 3.855, kati ya fedha hizo, Sh. trilioni 1.163 ni misaada na mikopo ya kibajeti na Sh. Trilioni 2.692 ni mikopo na misaada kwa ajili ya miradi ya maendeleo, na Mifuko ya Pamoja ya Kisekta Sh. bilioni 500.4. 

MATUMIZI YA KAWAIDA

Katika matumizi ya jumla ya Sh. trilioni 18.249, matumizi ya kawaida ni Sh. trilioni 12.574 ambayo yanajumuisha Sh. trilioni 4.763 kwa ajili ya mishahara ya watumishi wa Serikali, Taasisi na Wakala wa Serikali; Mfuko Mkuu wa Serikali Sh. trilioni 3.319 na matumizi mengineyo Sh. bilioni 4,492.

MATUMIZI YA MAENDELEO 

Sh. trilioni 5.674 zimetengwa kwa ajili ya matumizi ya maendeleo, kati yake Sh. trilioni 2.982 kitagharimiwa kwa fedha za ndani. Kati ya kiasi hicho, Sh. bilioni 552.3 zinatokana na mkopo kutoka vyanzo vya ndani, Sh. trilioni 1.156 ni mikopo ya masharti ya kibiashara, Sh. bilioni 386.2 ni mikopo ya kibajeti, na Sh. bilioni 887.1 zitatokana na asilimia 8 ya mapato ya kawaida. Kiasi cha Sh. trilioni 2.692 kitagharamiwa kwa fedha za nje, misaada na mikopo ya miradi ya maendeleo ikijumuisha Mifuko ya Pamoja ya Kisekta.



Source: Mgeta M. (June 2013). Bajeti: Maumivu. Dodoma. Retrieved from Ippmedia/Nipashe

No comments: