Kwao Nyerere siyo "Baba wa Taifa" tena;
kwao ni "Mzee Nyerere"; kwa watawala wetu hawa walioshindwa wanasema
wamefanya mambo mengi sana ya maendeleo kkuliko "Wakati wa Nyerere".
Wanajitamba kuwa wao wamekuza sana demokrasia na kuwa hata "Nyerere"
hakuweza kufanya waliofanya wao. Katika upotofu wao wanaamini kabisa kuwa wao
wanapendwa zaidi; na wanapendwa kwa sababu wamefanya mengi mno na
hawaelewi kwanini watu hawaoneshi shukrani!
Ndio maana kila kukicha hawaachi
kubembeleza kwa wananchi kuwa "hamuoni tunayofanya" na kuwa watu
wanalaumu tu lakini hawatoi pongezi kwa "mazuri mengi". Imefika
mahali Kikwete mwenyewe amedai mahali fulani anataka kukumbukwa kuwa ni
"bwana maendeleo"; anasema hivi kwa sababu anapokaa ofisini anaamini
kabisa kuwa ameweza kuwapatia Watanzania 'vitu" vingi sana vya maendeleo
kuliko wakati wowote wa historia - vitu ambavyo hata Nyerere hakuweza
kuwapatia. Kikwete anataka awe juu ya Nyerere kwa kila kipimo kwani kipimo
kilichowekwa ni Nyerere. Na bila ya shaka kuna sababu - Nyerere hakuamini kuwa
walikuwa tayari kuwaongoza Watanzania - hawa kina Kikwete na Lowassa.
Sasa
katika kumdunisha Nyerere ili wao wakue wameacha propaganda chafu dhidi ya
Nyerere na uongozi wake. Leo hii tunashuhudia mambo ambayo - pamoja na 'ubaya'
wote wa Nyerere hayakuwahi kutokea chini ya "dhaalim Nyerere"!
Matukio yanayotokea leo hii ukiwaambia watu walioshi wakati wa Nyerere, chini
ya chama kimoja na uongozi thabiti hawawezi kuelewa yanawezekana vipi kutokea.
Watu wa enzi za Mwalimu wanakumbuka vizuri kuwa kiongozi aliyefanya madudu
hakuvumuliwa; na bahati mbaya wakati ule hatukuwa na wasomi wengi na watu wengi
wenye udhoefu lakini Nyerere hakuwaonea huruma. Wapo ambao hadi leo wana
kinyongo na Nyerere kwa sababu hakuwapa nafasi nyingine.
Lakini katika kumdharaulisha
Nyerere na kujaribu kupuuza mafanikio yake makubwa zaidi wamejikuta hawana pa
kukimbilia! Tuliokuwa wakati wa Nyerere hatukumbuki jinsi JWTZ likitumiwa
kisiasa kama linavyotumika hivi sasa! Fikiria ndege ya jeshi itumwe kumchukua
raia kumpeleka Mahakamani!? Kwamba, ati vurugu za uchaguzi zilazimishe JWTZ
kuingilia kati! Kwamba vikosi vya kutuliza ghasia vya polisi vizidiwe nguvu na
mara moja kuliingiza jeshi kufanya kazi za jeshi la polisi! Unthinkable! Lakini
wao wanaamini wako sawa!
Lakini siyo kwamba wamedharaulisha na kumtupa nje
Nyerere ni zaidi ya hivyo; wameitupa misingi ya taifa letu. Wanataka kujenga
kwa misingi ya mabua! Waliachiwa misingi ya zege lakini wao wakiamini ni
'magenius" wameamua kutengeneza 'taifa jipya' nje ya misingi iliyounda
Tanzania. Leo hii Watanzania kwa mamilioni wananung'unika moyoni kwani
hawatambui kama hili ndilo Taifa waliloachiwa kama urithi. Sasa hivi inaonekana
Tanzania inazidi kufanana zaidi na mataifa mengine ya Afrika kiasi kwamba
linaweza lisitofautike tena mbele ya umma.
Wameitupa misingi sasa hawana cha
kujengea; wamebakia kutumainia vitisho, dharau na matumizi ya nguvu.
Wameshindwa kabisa kujenga hoja - kwa mfano kwenye hili suala la gesi. Hawana
ushawishi wa hoja na badala yake hata kauli zao wanazotoa zimejaa dharau
(contempt) na matokeo yake watu nao wanawadharau! Wanafikiri vitisho na kejeli
zinajibu hoja!
Kushindwa kwa sera zao mbalimbali ni matokeo ya kuachana na
misingi ya taifa; wanafikiri wanaweza kutengeneza sera nzuri nje ya misingi ya
taifa! Matokeo yake:
Sera ya Nishati na Madini imeshindwa
Sera yao ya Gesi
imeshindwa - hata kabla haijaanza!
Sera yao ya Elimu imeshindwa
Sera yao ya
siasa imeshindwa
Sera yao ya Sayansi na Teknolojia imeshindwa
Sera yao
Mazingira imeshindwa
N.k
Wameshindwa lakini hawaamini wameshindwa na badala
yake wanawalaumu wanaowaambia wameshindwa kwa kushindwa kwao! Kana kwamba,
wanaowalaumu wakinyamaza basi wao wataweza! Wenyewe wanaambizana kuwa wakipewa
nafasi nyingine 2015 basi wataaanza kuweza; na wapo watu wanaamini kuwa hilo
linawezekana; kwamba pundamilia anaweza kugeuka na kuwa farasi! Kama wenyewe
wameshindwa kuvuana magembe licha ya mbwembwe zote za "kuvuana
magamba" kweli kuna uwezekanow wataweza? Na ukweli ni kuwa walipofika sasa
hawawezi kurudi kwenye misingi ya Nyerere na Taifa letu; kwa sababu kurudia
misingi hiyo ni kujishtaki katika historia.
Kuna namna moja ttu ya
kuwasaidia... kuendelea kuwakataa.
Maskini CCM!
Maskini Kikwete
Maskini
Tanzania chini yao!
Mimi Mwanakijiji

No comments:
Post a Comment