Gari la maji ya kuwasha lachomwa, nyumba
Madaraja muhimu yavunjwa, shule zafungwa
VURUGU kubwa zimeibuka tena mkoani
Mtwara jana na kulazimisha Jeshi la Polisi kutumia risasi za moto, mabomu ya
machozi na kila aina ya mbinu, kupambana na wananchi wanaopinga kitendo cha
Serikali kutaka kusafirisha gesi kwenda Dar es Salaam. Taarifa kutoka Mtwara, zinasema hadi
jana jioni kulikuwa na uharibifu mkubwa wa miundombinu na uchomaji wa nyumba za
watumishi wa Serikali na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Mbali ya matukio hayo, inadaiwa
kulikuwa na mauaji ya askari polisi kadhaa, huku wananchi wengi wakitiwa
mbaroni kutokana na vurugu hizo. Chanzo cha vurugu hizo, kinadaiwa
kilitokana na hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini kusomwa Bungeni
na Waziri Sospeter Muhongo, ambapo alisisitiza mradi wa gesi wa Mtwara
utatekelezwa bila kutaja faida za moja kwa moja kwa wananchi hao. Wananchi hao, walianzisha vurugu
jana, huku wakiwa na kauli mbiu yao isemayo "Gesi haitoki hata kwa bomba
la peni". Inaelezwa kuwa kuna kituo cha mafuta cha Total kimechomwa moto
wakati wa vurugu hizo.
Taarifa zinasema katika eneo la
Mikindani ofisi zote za serikali, zilivamiwa na kuchomwa, likiwamo daraja la
Mikindani. Katika eneo hilo ambako kuna daraja
maarufu la Mikindani, lilivunjwa, baada ya kulipuliwa na kitu kinachosadikiwa
kuwa bomu. Kutokana na hali hiyo, askari
wanafanya msako wa nyumba hadi nyumba maeneo ya Magomeni na Mangowela. “Hali ni mbaya mno, polisi
wamelazimika kutumia helkopita kupita maeneo yote ya mjini, hakuna biashara
wala huduma za kijamii.
“Uharibifu ni mkubwa, sijui
nisemeje, na inawezekana kuna polisi karibu watano wameuawa, kwani wananchi nao
wana bunduki za magobore wanajibu mapigo. “Jambo la kushangaza ni kwamba,
wananchi wengi wanaonekana kuwa na mabomu ya kuulia samaki, sijui wameyatoa
wapi. “Wametumia mabomu kubomoa daraja la
Mpakula na Mikindani, eneo hili ndilo linaunganisha mikoa ya Mtwara na Lindi,
hadi tunavyozungumza hapa hakuna mawasiliano yoyote,” kilisema chanzo chetu. Alisema hali ilianza kuwa mbaya
zaidi ilipofika saa 4 asubuhi, ambapo wananchi walianza kujikusanya na kupitapita
mitaani, huku wakipishana na polisi.
Chanzo hicho, kinasema katika vurugu
hizo, gari la polisi lenye namba za usajili PT 2028 ambalo lilikuwa limebeba
maji ya kuwasha, lililipuliwa vibaya na kitu kinachosadikiwa kuwa bomu, baada
ya kurushwa na wananchi. “Huwezi amani, lile gari lenye maji
ya kuwasha, limelipuliwa vibaya mno, hatujui wananchi wale walitumia kitu
gani,” kilisema chanzo chetu.
UCHOMAJI NYUMBA
Habari zinasema kadiri muda
ulivyozidi kwenda, makundi ya wananchi walivamia nyumba ya Diwani wa Kata ya
Chikongola, aliyetajwa kwa jina moja la Chihako, ofisi za CCM Wilaya ya Mtwara
ambazo ziko eneo la Magomeni na nyumba ya mtangazaji wa Shirika la Utangazaji
Tanzania (TBC), Kassim Mikongolo. Pia wananchi hao, walichoma nyumba
moja ya kulala wageni ya Shengena Lodge, ambayo inadaiwa kuhifadhi askari
polisi, waliokuwa wametolewa mkoani Dar es Salaam. Taarifa hizo, zinasema hali ilikuwa
mbaya zaidi katika Mtaa wa Mdenga, ambako wananchi kadhaa wanadaiwa walikuwa
wakitumia bunduki aina ya magobore kujibu mapigo dhidi ya polisi.
MATAIRI
Kila kona ya mji wa Mikindani,
ilitawaliwa na uchomaji mwingi wa matairi. Kutokana na hali hiyo, polisi na
askari wa Kikosi cha Zimamoto, walikuwa na kazi ngumu ya kuzima na kufukuza
wananchi.
Source:
Mtanzania (May 2013). Vita mtwara. Retrieved from Mtanzania

No comments:
Post a Comment