MKUU WA KAMBI YA UPINZANI MHESHIMIWA JOSEPH O. MBILINYI
(MB) KUHUSU MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA WIZARA YA HABARI, VIJANA,
UTAMADUNI NA MICHEZO KWA MWAKA WA FEDHA 2013/2014
(Inatolewa chini ya Kanuni ya 99(9) ya kanuni za Bunge toleo la
mwaka 2013)
1. UTANGULIZI
Mheshimiwa Spika,
Dira ya Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo ni “kuwa
na taifa lililohabarishwa vizuri, lina vijana wenye uwezo na malezi bora,
linathamini utamaduni wake na linakuwa mahiri katika michezo ifikapo mwaka
2025.” Aidha, ‘dhamira’ ya wizara hii ni ‘kuendeleza utambulisho wa taifa kwa
kuwezesha upatikanaji mzuri wa habari, kuwawezesha vijana kiuchumi na kukuza
utamaduni na michezo kwa umma kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi.’
Mheshimiwa Spika,
Kwa maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Serikali hii ya
CCM imeshindwa kutekeleza dira na dhamira iliyotajwa katika maandiko ya kisera
ya Wizara. Badala yake, chini ya usimamizi wa Wizara hii, Tanzania imegeuka
kuwa taifa lisilotaka watu kuhabarishwa vizuri juu ya matendo ya watawala.
Tanzania imegeuka kuwa taifa linalofungia magazeti yanayofichua ufisadi, uchafu
na matumizi mabaya ya madaraka miongoni mwa viongozi, watendaji na watumishi wa
Serikali hii ya CCM. Tanzania imegeuka, chini ya usimamizi wa Wizara na
Serikali hii ya CCM, kuwa taifa linaloteka nyara wanahabari, kuwatesa kwa
kuwang’oa kucha na meno, kuwatoboa macho, kuwamwagia tindikali na hata kuwaua.
Tanzania sio nchi inayoandaa vijana wake tena. Haiwapi tena elimu bora wala
kuwapatia maarifa, uwezo na malezi bora; ni nchi isiyowawezesha wala
kuwathamini vijana wake; ni nchi inayoruhusu vijana wake kunyonywa na
kutoendelezwa; na ni taifa ambalo limeachia utamaduni utambulisho wake kama
taifa kupotea kabisa. Aidha, katika fani ya michezo ya aina zote, Tanzania imeporomoka
kutoka taifa lililokuwa linaheshimika kimataifa katika miaka ya sabini na kuwa
alichokiita rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi, ‘kichwa cha mwendawazimu’ ambacho
kila kinyozi anajifunzia kunyolea!
2. UHURU WA UHARIRI NA USALAMA WA WANAHABARI
Mheshimiwa Spika,
Kwa masikitiko makubwa, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni
inalitaarifu Bunge lako tukufu kwamba sasa Tanzania imeingia rasmi katika
orodha ya fedheha (The List of Shame) ya mataifa ambayo taaluma ya habari ni
taaluma ya hatari kwa wale wote wanaoitumia kama sehemu ya wajibu wao kwa taifa
na kama ajira yao. Kwa mujibu wa taarifa ya Kamati ya Kulinda Waandishi wa
Habari Ulimwenguni (the Committee to Protect Journalists - CPJ) iliyotolewa
mwaka huu 2013, kwa mara ya kwanza tangu kuanzishwa kwa CPJ mwaka 1992,
Tanzania imeingizwa kwenye orodha ya nchi 20 ambazo ni hatari kwa waandishi wa
habari kufanya kazi zao kutokana na hatari ya kuuwawa kwa mwaka 2012 (20
Deadliest Countries in 2012). Kwa mujibu wa taarifa hiyo, ilishikilia nafasi ya
7 ulimwenguni kati ya nchi 20 zinazoongoza kwa kuhatarisha maisha ya waandishi
wa habari.
Mheshimiwa Spika,
Kwa mujibu wa taarifa ya CPJ, tishio kubwa kwa waandishi wa
habari duniani ni kuuwawa kwa kutekwa na kuteswa na/au kutishiwa maisha. Aidha,
Serikali na vyombo vyake vya ulinzi na usalama ni washiriki wakubwa wa mauaji
ya waandishi wa habari. Kwa mujibu wa takwimu za CPJ, kati ya waandishi
waliouwawa mwaka 2012, karibu ya 20% waliuwawa ama na maafisa wa serikali au na
majeshi yake. Karibu idadi hiyo hiyo ya waandishi wa habari waliuawa kwa sababu
ya kufuatilia taarifa za kiuchunguzi na za hatari. Taarifa hiyo inaonyesha
kwamba hadi kufikia Aprili 2013, waandishi wa habari wapatao 30 tayari
wamekwishauawa ulimwenguni wakati wakitimiza wajibu wao; wakati mwaka 2012 waandishi
wa habari 103 waliuwawa ulimwenguni kote.
Mheshimiwa Spika,
Taarifa ya CPJ inaungwa mkono na ushahidi wa matukio mengi
yanayodhihirisha kwamba maisha ya waandishi wa habari wa Tanzania yako hatarini
kutokana na vitendo na vitisho kutoka kwa Serikali na watendaji wake ambao
hawataki kusikia ukweli dhidi yao ukianikwa hadharani. Kudhihirisha kauli hii
tunaomba kumnukuu mwanahabari mahiri na mmoja wa wahanga wa vita dhidi ya
wanahabari na uhuru wa habari hapa nchini, Mzee Ndimara Tegambwage:
“Mwaka 2006, waliojiita wananchi wakazi wa jiji la Mwanza,
walikusanywa na wenye uwezo kufanya maandamano makubwa kwa walichoita ‘kupinga
mwandishi Richard Mgamba kuandika uongo’ na kudai kwamba alikuwa Mkenya na
‘siyo raia wa Tanzania.’ Desemba 2009, mwandishi Frederick Katulanda wa Mwanza,
alivamiwa nyumbani. Wavamizi walikuwa wakipaza sauti na kudai kuwa ana nyaraka
za akaunti za benki za Halmashauri ya Jiji la Mwanza. Walikuwa na mapanga.
Walikuwa wakichagizana kwa kusema, “Kata kichwa! Kata kichwa!” Waliondoka na
mafaili. Walimwachia kilema mguuni na makovu mikononi.
“Mwezi Septemba, 2010 wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu, katika
eneo la Nyambiti, Jimbo la Sumve wilayani Kwimba, mkoani Mwanza, mwandishi
Frederick Katulanda alivamiwa na kupigwa na watu wapatao 15 waliojiita “Green
Guard” - wa “chama cha kijani.” Katika “kumshughulikia,” Katulanda anasema,
walikuwa wakionyesha kuwa na ujuzi mkubwa wa judo na karate huku wakidai kuwa
anawaandika ‘vibaya’ Chama Cha Mapinduzi (CCM).
“Mwaka 2011 mwandishi Richard Massatu alikutwa amekufa katika
eneo la Igoma, jijini Mwanza. Vyombo vya habari viliripoti kuwa macho yake yalikuwa
yametobolewa na kuwekwa gundi aina ya super glue; mguu wa kushoto na mbavu
vilikuwa vimevunjika. Vyombo vya habari viliripoti kuwa Massatu aliyekuwa
mmiliki na mhariri mkuu wa gazeti la Kasi Mpya (sauti ya umma), alionekana mara
ya mwisho usiku wa kifo chake akiwa na maofisa wa polisi na usalama katika baa
iitwayo Cross Park katika eneo la Igoma.
“Tarehe 3 Januari, maiti ya mwandishi Issa Ngumba iliokotwa
katika pori la mlima Kajuruheta, kijiji cha Mhange, wilayani Kakonko katika
mkoa wa Kigoma.Ngumba alikuwa mwandishi wa habari wa Redio Kwizela. Tangu mwezi
uliopita Machi, mwandishi wa habari Erick Kabendera anayeishi Dar es Salaam,
anaishi kwa wasiwasi. Wazazi wake waishio Bukoba, wamehojiwa na ‘ofisa usalama’
kwa kile kilichoitwa ‘uhalali wa uraia wao.’
“Kuuwawa kwa aliyekuwa mwandishi wa habari wa Kituo cha Luninga
cha ITV, John Lubungo ambaye alikuwa mfuatiliaji mahiri wa habari zinazohusu
wafanyabiashara au biashara haramu ya dawa za kulevya ambayo inadaiwa kufanywa
na watu wakubwa nchini, wakiwemo vigogo serikalini. Kuna orodha ndefu ya
waandishi wa habari waliotishwa na wanaoendelea kutishwa; waliopigwa na polisi
na askari magereza (Ukonga, Dar es Salaama) kwa tuhuma mbalimbali; waliotishiwa
maisha kwa simu na hata kwa kufuatiliwa na watu wasiowafahamu.”
Kwa sababu ya uadilifu na kutopenda kujikweza, Mzee Tegambwage
hakutaja shambulio la tindikali na mapanga dhidi yake na mwandishi mwenzake
Saed Kubenea wa gazeti la Mwanahalisi, ambalo baadae lilifungiwa na Serikali
hii ya CCM.
Mheshimiwa Spika,
Katika Maoni yake wakati wa mjadala wa bajeti ya Wizara ya
Katiba na Sheria ya tarehe 3 Mei mwaka huu, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni
ilielezea kwa kirefu jinsi ambavyo Serikali hii ya CCM imekuwa tishio kwa
maisha ya waandishi wa habari na kwa uhuru wa habari katika nchi yetu. Kambi
Rasmi ya Upinzani Bungeni ilirejeaRipoti ya Timu Maalum ya Uchunguzi
Iliyoteuliwa na Baraza la Habari Tanzania (MCT) na Jukwaa la Wahariri Tanzania
(TEF) Kuchunguza Mazingira Yaliyopelekea Kuuawa kwa Mwandishi wa Habari Daudi
Mwangosi Septemba 2, 2012 Katika Kijiji cha Nyololo, Wilaya ya Mufindi, Mkoani
Iringa, iliyotolewa na Baraza la Habari Tanzania (MCT) na Jukwaa la Wahariri
Tanzania (TEF), taasisi mbili huru zinazojihusisha na masuala ya habari
Tanzania.
Kwa mujibu wa Ripoti ya MCT/TEF, matokeo ya uchunguzi wao “...
yanadhihirisha bila wasi wasi kwamba polisi kwa makusudi waliwavurumisha
waandishi waliotoka Iringa wakati wakikusanya habari za shughuli za CHADEMA
katika kijiji cha Nyololo. Zaidi ya hapo, Daudi Mwangosi mwenyewe aliuawa akiwa
mikononi mwa polisi huku wakisimamiwa moja kwa moja na Kamanda (wa Polisi wa
Mkoa wa Iringa SACP Michael) Kamuhanda.” Ripoti hiyo inaelezea jinsi Marehemu
Mwangosi alivyouawa: “Alipoangalia nyuma, Daudi Mwangosi aliona kikundi cha polisi
wakimpiga mwandishi mkuu wa gazeti la Nipashe wa Iringa, Godfrey Mushi....
Wakati mwandishi Godfrey Mushi akiwa bado anapigwa na polisi, marehemu Mwangosi
aliwakimbilia akiwaomba waache kumdhuru zaidi Mushi kwa kuwa alikuwa mwandishi
tu. Polisi hawakumsikiliza. Badala yake wakamburuta mwandishi huyo ambaye
tayari alikuwa amepoteza fahamu na kumweka kwenye gari lao na wakamgeukia Daudi
Mwangosi mwenyewe, wakampiga kwa nguvu mpaka akapoteza fahamu.”
Hata amri ya Mkuu wa Kituo cha Polisi Mafinga Mwampamba kuwataka
askari polisi waache kumpiga marehemu Mwangosi haikusikilizwa na askari hao.
Ili kujiokoa, marehemu Mwangosi alimkumbatia OCS Mwampamba na “baadaye
kumwangukia miguuni mwake kuepuka kipigo zaidi.” Kwa mujibu wa Ripoti ya
MCT/TEF, “picha za mgando zinaonyesha polisi mmoja akipiga bomu la machozi
tumboni mwa marehemu Mwangosi kwa karibu kabisa.” Bomu hilo liliusambaratisha
mwili wa marehemu Mwangosi aliyekufa papo hapo. Kwa sababu marehemu Mwangosi
alikuwa chini ya miguu ya OCS Mwampamba, “naye pia alijeruhiwa vibaya.”
Mheshimiwa Spika,
Sio MCT/TEF pekee zilizofanya uchunguzi wa mauaji ya Marehemu
Mwangosi. Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora nayo ilitoa Taarifa ya Tume
ya Haki za Binadamu na Utawala Bora ya Uchunguzi wa Tukio Lililopelekea Kifo
cha Daudi Mwangosi Kilichotokea Septemba 2, 2012 Kijijini Nyololo, iliyobaini
kwamba Marehemu Mwangosi “... alizingirwa na askari, aliteswa na hatimaye ...
alipigwa bomu na kufa papo hapo.” Aidha, kwa mujibu wa Taarifa hiyo, “... Tume
imejiridhisha kuwa tukio la lililopelekea kifo cha Daudi Mwangosi limegubikwa
na uvunjwaji wa haki za binadamu na ukiukwaji wa misingi ya utawala bora.”
Taarifa ya Tume inafafanua kuwa, “... Tume imejiridhisha kuwa Jeshi la Polisi
limevunja haki ... ya kuishi, haki ya kutoteswa na kupigwa, haki ya usawa mbele
ya sheria na haki ya kukusanyika na kutoa maoni.”
Mheshimiwa Spika,
Siku moja baada ya mauaji ya Daudi Mwangosi, Jeshi la Polisi
lilianza kampeni kubwa ya kujaribu kuficha ukweli juu ya kuhusika kwake, kwa
kuhamishia lawama kwa watu wengine wasiohusika na mauaji hayo. Kwa mfano,
Kamanda Kamuhanda alinukuliwa na vyombo vya habari akidai kwamba marehemu
Mwangosi alifariki “kutokana na kitu kizito kilichotupwa na waandamanaji.”
Aidha, siku iliyofuata Kamishna wa Operesheni wa Jeshi la Polisi Paul Chagonja
alidai kwamba baada ya ghasia kudhibitiwa, marehemu Mwangosi alikimbilia
walipokuwa polisi na “kitu kama bomu kikarushwa na kundi la watu wanaokimbia
hovyo na kumlipua Mwangosi.”
Njama hizi za kuficha ukweli zimeumbuliwa na Ripoti ya MCT/TEF
inayobainisha kwamba marehemu Mwangosi “aliuawa chini ya usimamizi wa moja kwa
moja wa RPC Michael Kamuhanda.” Ripoti hiyo pia imeelezea kwa kirefu jinsi
Jeshi la Polisi lilivyotoa taarifa zinazokinzana juu ya kuhusika kwake na mauaji
ya Mwangosi. Hivyo, kwa mfano, wakati Waziri wa Mambo ya Ndani Mheshimiwa
Emmanuel Nchimbi alidai tarehe 4 Septemba 2012 kwamba marehemu aliuawa na bomu
la machozi ambalo ‘halikulipuliwa kitaalamu na polisi’, Kamanda Kamuhanda
alitokea kwenye televisheni siku iliyofuata “akitangaza habari za kuwatupia
lawama wafuasi wa CHADEMA kwa kutupa kitu kizito kilicholipuka na kumuua
Mwangosi....”
Mheshimiwa Spika,
Hata Taarifa ya Uchunguzi wa Kifo cha Mwandishi wa Habari wa
Channel Ten Bw. Daudi Mwangosi, iliyoandaliwa na Kamati iliyoundwa na
Mheshimiwa Nchimbi na kuongozwa na Jaji Stephen Ihema imethibitisha kuhusika
kwa Jeshi la Polisi na mauaji ya Marehemu Mwangosi. Baada ya kuzunguka huku na
huko ikijaribu kulisafisha Jeshi la Polisi kutoka kwenye lawama ya kumuua
Marehemu Mwangosi, Taarifa ya Kamati hiyo inasema: “Hapakuwepo na uhalali wa
kutumia Bomu la Kishindo kwani lengo la ulipuaji wake ni ili watu waogope na
kukimbia.” Aidha, Kamati hiyo inakiri kwamba “hapakuwepo umuhimu wa kutumia
Bomu la Kishindo kwa sababu hata ingekuwa ukamataji tayari askari polisi
wapatao sita walikuwepo eneo la tukio.” Kwa misingi hiyo, “… Kamati imeona
kwamba … tukio la kuuawa Bw. Daudi Mwangosi na kuumizwa baadhi ya askari polisi
halikustahili kabisa.”
Mheshimiwa Spika,
Kuna uthibitisho mkubwa kwamba Serikali hii ya CCM na Jeshi la
Polisi wamekuwa wanawalenga kuwaua au kuwaumiza waandishi wa habari wanaoandika
zisizowapendeza viongozi wa Serikali au Jeshi la Polisi. Kwa mfano, Ripoti ya
MCT/TEF inaashiria kuwa sababu ya Marehemu Mwangosi kuuawa ni kwamba yeye “...
ndiye mwandishi pekee aliyemuuliza RPC (Kamuhanda) ‘maswali magumu’ kiasi cha
kumkera kiongozi huyo wa jeshi la polisi.” Ripoti hiyo inafafanua kwamba “baada
ya mkutano huo na waandishi, ... baadhi ya polisi ... waliwaonya wasiende
Nyololo kwa ajili ya kukusanya habari za shughuli za kisiasa za CHADEMA
kutokana na uwezekano wa kutokea kwa hali hatarishi.” Aidha, “baada ya mkutano
wa waandishi wa habari wa asubuhi katika ofisi za RPC (Kamuhanda), ... askari
mmoja mpelelezi alimfuata Mwangosi na kumwambia: ‘Ina maana gani kwenda Nyololo
kuandika habari za Chadema ambazo zinaweza kuishia na kifo chako?’” Vile vile,
Ripoti ya MCT/TEF inabainisha, ni “... wazi kwamba Polisi walikuwa wanawawinda
waandishi wa Iringa ambao walikuwa wakiwajua.”
Mheshimiwa Spika,
Siku tatu baada ya mauaji ya Daudi Mwangosi, Mkurugenzi wa
Upelelezi wa Makosa ya Jinai katika Jeshi la Polisi Robert Manumba alitoa kauli
kwa vyombo vya habari kuhusu matukio ya kuuawa kwa waandishi wa habari ambapo alisema
“….matukio ya aina hii yapo na yataendelea kuwepo.” Katika kuthibitisha kwamba
Serikali hii ya CCM ina sera isiyo rasmi ya kulenga kuwadhuru waandishi wa
habari wanaowaandika watawala vibaya na hata kuwaua, kauli ya DCI Manumba
imerudiwa tena na Mkuu wa Mkoa wa Arusha Magessa Mulongo wakati wa sherehe za
Mei Mosi mwaka huu jijini Arusha. Kwa mujibu wa vyombo vya habari, Mkuu huyo wa
Mkoa aliwatahadharisha waandishi kwa kuwaambia kwamba “unapoingia katika
mkakati wa kumdhalilisha kiongozi wa Serikali unaiweka roho yako rehani….
Kuweni makini.”
Mheshimiwa Spika,
Katika Maoni yake kwenye mjadala wa Wizara ya Katiba na Sheria,
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni iliyaita matamshi ya DCI Manumba na Mkuu wa
Mkoa Mulongo kuwa ni ‘matendo ya kigaidi’ kwa mujibu wa Sheria ya Kuzuia
Ugaidi, 2002, ambayo inafafanua ‘matendo ya kigaidi’ kuwa ni pamoja na vitisho
vinavyohusu mtu kusababishiwa maumivu au majeraha makubwa kimwili, kuhatarisha
maisha ya mtu na vinavyohusu usalama wa umma ambavyo vimelengwa au ambavyo kwa
hulka au muktadha wake vinaonekana vimelengwa kutishia umma au sehemu ya umma.
Kwa mara nyingine tena Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka
Serikali kutoa kauli rasmi mbele ya Bunge hili tukufu kama tafsiri hiyo ya
Sheria ya Kuzuia Ugaidi ni sahihi au la. Na kama ni sahihi, Kambi Rasmi ya
Upinzani inataka kujua ni kwa nini DCI Manumba na Mkuu wa Mkoa Mulongo bado
hawajakamatwa na kufunguliwa mashtaka ya ugaidi hadi sasa? Kama tafsiri hiyo
sio sahihi, basi Serikali hii ya CCM itamke mbele ya Bunge lako tukufu kwamba
ni sera yake rasmi kwamba waandishi wa habari wanaoiandika Serikali au viongozi
wake vibaya ‘wanaweka roho zao rehani’!
Mheshimiwa Spika,
Kauli ambazo zimetolewa na Serikali hii ya CCM ndani ya Bunge
lako tukufu zinathibitisha kuhusika kwa Serikali katika, kama sio kupanga basi
angalau kubariki, mauaji yanayofanywa na vyombo vya usalama vya Serikali kwa
waandishi. Na moja ya kauli za Serikali ambazo zimeifadhaisha na kuisikitisha
sana Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ni ile iliyotolewa na Mnadhimu Mkuu wa
Serikali na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera Uratibu na Bunge, Mh.
William Lukuvi pale alipomsifu Kamanda Kamuhanda wakati wa mjadala wa Wizara ya
Mambo ya Ndani: “Katika kitabu hiki cha Kambi ya Upinzani, wamekutaja sana
(Kamuhanda), hawawezi kukupongeza. Huko Iringa Kamanda unafanya kazi nzuri
sana, usitetereke na makamanda wako wa huko Iringa.”
Ikumbukwe, Mheshimiwa Spika, kwamba mtu anayesifiwa kwa
‘kufanya kazi nzuri sana kule Iringa’ ni yule yule ambaye aliyelaumiwa na Tume
ya Haki za Binadamu – ambayo Makamishna wake wote ni wateule wa Rais kwa mujibu
wa Katiba – kuwa alikiuka sheria za nchi yetu na misingi ya utawala bora
kufuatia tukio la mauaji ya Marehemu Mwangosi! Mtu anayeshauriwa na Waziri
Lukuvi kwamba ‘asitetereke’ ni yule yule ambaye MCT/TEF imemhusisha na
usimamizi wa moja kwa moja wa mauaji ya Mwangosi. Needless to say, mtu
huyu bado yuko huru na hajachukuliwa hatua yoyote licha ya mshangao mkubwa
kitaifa na kimataifa!
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kutoa kauli
rasmi mbele ya Bunge lako tukufu kama kauli ya Mheshimiwa Lukuvi kuhusu
kuhusika kwa Kamanda Kamuhanda na Jeshi la Polisi katika mauaji ya Marehemu
Mwangosi ndio msimamo rasmi wa Serikali hii ya CCM. Aidha, Kambi Rasmi ya
Upinzani Bungeni inaitaka Serikali hii ya CCM kuliambia Bunge lako tukufu ni
nini msimamo wake rasmi juu ya Taarifa ya Tume ya Haki za Binadamu na Ripoti ya
MCT/TEF kuhusu kuhusika kwa Jeshi la Polisi na Kamanda Kamuhanda katika mauaji
ya Marehemu Mwangosi. Kwa maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, kimya cha
Serikali hii ya CCM juu ya maswali haya muhimu ni ushahidi dhahiri kuwa mauaji
haya ni sehemu ya mkakati ulioasisiwa na Serikali hii ya CCM wa kuwanyamazisha
waandishi wa habari kwa nia moja tu: kufifisha uhuru wa kupata na kutoa habari
muhimu zinazohusika kashfa za ufisadi na matumizi mabaya ya madaraka
serikalini.
Mheshimiwa Spika,
Miezi sita baada ya Jeshi la Polisi kumuua Daudi Mwangosi,
mwandishi mwingine mwandamizi na Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF),
Absalom Kibanda, alitekwa nyara na kuteswa vibaya nje ya nyumba yake baada ya
nyendo zake kufuatiliwa na polisi na watu wengine wanaodhaniwa kuwa watumishi
wa Idara ya Usalama wa Taifa na Ujasusi (TISS). Badala ya kuchukua hatua za
dhati kuwachunguza na kuwakamata wale wote waliohusika na tukio hilo la
kigaidi, Jeshi la Polisi likishirikiana na Idara ya Usalama wa Taifa, maafisa
waandamizi katika Ofisi ya Rais Ikulu na viongozi waandamizi wa CCM chini ya
Naibu Katibu Mkuu wake Mheshimiwa Mwigulu Nchemba na baadhi ya waandishi habari
maslahi, walianzisha kampeni kubwa ya kuipakazia CHADEMA na Mkurugenzi wake wa
Ulinzi na Usalama Wilfred Lwakatare kwa madai ya kuhusika na ugaidi kutokana na
ushahidi wa kutunga!
Mheshimiwa Spika,
Kwa vile njama dhidi ya CHADEMA na Bw. Lwakatare zimegonga
mwamba baada ya Mahakama Kuu ya Tanzania kuyatupilia mbali mashtaka ya ugaidi
dhidi yake, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali hii ya CCM kutoa
taarifa rasmi mbele ya Bunge lako tukufu juu ya waliohusika na jaribio la
kumuua Bw. Kibanda. Aidha, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali
hii ya CCM itoe kauli rasmi mbele ya Bunge lako tukufu juu ya kuhusika kwa
Jeshi la Polisi, Idara ya Usalama wa Taifa, Ikulu na CCM katika kutengeneza
ushahidi wa uongo dhidi ya CHADEMA na Bw. Lwakatare ili kuwapumbaza Watanzania
wasihoji shambulio la kigaidi dhidi ya Bw. Kibanda.
Kutoa taarifa ya uongo kwa lengo la kuanzisha mashtaka ya jinai
mahakamani au kutengeneza ushahidi wa uongo kwa lengo la kuipotosha mahakama ni
makosa ya jinai yenye adhabu ya kifungo cha miaka saba kwa mujibu wa Sheria
ya Adhabu ya Tanzania. Ni muhimu kwa ukweli wa jambo hili kujulikana sio tu
kwa ajili ya kuwawajibisha kijinai wahusika, bali pia kwa lengo la kulinda
demokrasia na utawala wa sheria katika nchi yetu. Kama alivyosema Chris
Conybeare, Katibu Mkuu wa Chama cha Mabaraza ya Habari Duniani (WAPC) katika
ujumbe wake kwa Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Mheshimiwa Dk.
Fenella Mukangara juu ya mauaji ya Marehemu Mwangosi: “Waandishi wa habari
wanapouawa demokrasia pia inakufa.”
3. MAELEZO NA UHURU WA HABARI
Mheshimiwa Spika,
Idara ya Habari (MAELEZO) ilikasimiwa majukumu na mali za
lililokuwa Shirika la Habari Tanzania (SHIHATA) na Sheria ya Kufuta Shirika la
Habari la Tanzania, Na. 7 ya mwaka 2000. Wakati SHIHATA ilikuwa na ukiritimba
wa kukusanya habari pamoja na mamlaka ya kusajili waandishi wa habari,
ukiritimba huo na mamlaka ya usajili wa waandishi wa habari yalifutwa kabisa
kama sehemu ya utekelezaji wa mapendekezo ya Tume ya Rais ya Mfumo wa Chama
Kimoja au Vyama Vingi vya Siasa Tanzania, 1991 (‘Tume ya Nyalali’),
iliyobaini kwamba Sheria ya SHIHATA ilikuwa inakiuka misingi ya uhuru wa mawazo
na uhuru wa habari.
Kwa sababu hiyo, majukumu mapya ya Idara ya Habari, kama
yalivyofafanuliwa katika kifungu cha 4(2) cha Sheria ya Kufuta SHIHATA, ni
pamoja na kutoa, kuendeleza na kuhamasisha uanzishwaji na uendeshaji wa za
kukusanyia na kusambaza habari; kukusanya na kusambaza habari na kuishauri
Serikali juu ya masuala yanayohusu usambazaji habari na utendaji wa mashirika
ya habari. Idara ina ofisi katika baadhi ya mikoa ya Tanzania Bara.
Mheshimiwa Spika,
Tofauti na SHIHATA, Idara ya Habari haina na haijawahi kupewa
jukumu la kisheria la kuwa msimamizi wa vyombo vya habari na wanahabari nchini.
Hata hivyo, kama ilivyokuwa kwa SHIHATA, Idara hii imekuwa inawauzia waandishi
wa habari vitambulisho (press cards) ambavyo vimekuwa vinatumika kama
vitambulisho cha kazi kwa waandishi wa habari hapa nchini. Vitambulisho hivyo
vimekuwa vinauzwa kwa shilingi za Tanzania elfu ishirini, lakini Kambi Rasmi ya
Upinzani Bungeni ina taarifa kwamba bei ya vitambulisho hivyo imepanda mwaka
huu hadi kufikia shilingi elfu thelathini. Aidha, vitambulisho hivyo hutolewa
kila mwaka katika Ofisi za MAELEZO Dar es Salaam na hivyo kusababisha gharama
na usumbufu mkubwa kwa waandishi wa habari walioko mikoani.
Mheshimiwa Spika,
Vitendo hivi vya Idara ya Habari ni kinyume cha Sheria ya Kufuta
SHIHATA. Kwa sababu hiyo, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali hii
ya CCM itoe kauli rasmi mbele ya Bunge lako tukufu Idara ya Habari imetoa wapi
mamlaka ya kusajili waandishi wa habari kwa kuwalazimisha kununua vitambulisho
vya uandishi habari. Aidha, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inataka Serikali
itoe kauli rasmi mbele ya Bunge lako tukufu kama kuna masharti yoyote ya
kisheria yanayolazimu waandishi wa habari wasajiliwe na MAELEZO kwa kupatiwa
vitambulisho vya kazi na Idara hiyo.
Mheshimiwa Spika,
Sio tu kwamba Idara ya Habari imejitwalia mamlaka ya kusajili
waandishi wa habari kwa kuwalazimisha kununua vitambulisho vya taaluma yao,
lakini pia imeendelea kuwa kikwazo kikubwa kwa kupanuka kwa demokrasia na uhuru
wa habari katika nchi yetu. Historia yake inaanzia miaka ya mwanzo ya utawala
wa kikoloni wa Kiingereza wakati walipotunga Sheria ya Magazeti ya 1928. Chini
ya Sheria hiyo, wakoloni walidhibiti ukuaji wa vyombo vya habari vya wenyeji wa
Kiafrika kwa kuviwekea masharti ya kusajiliwa baada ya kutoa dhamana ya fedha
taslimu.
Marekebisho ya Sheria hiyo yaliyofanywa mwaka 1952 yaliweka
masharti magumu zaidi ya usajili wa magazeti pamoja na kuongeza kiwango cha
dhamana kutoka pauni za Kiingereza 160 hadi pauni 520. Kwa mujibu wa Martin
Sturmer katika kitabu chake The Media History of Tanzania, wakati
magazeti ya Wamisionari na yale yaliyokuwa yanaunga mkono sera za utawala wa
kikoloni katika Tanganyika hayakudaiwa kulipa dhamana, magazeti yaliyokuwa na
mrengo wa upinzani wa sera za dola ya kikoloni yalilazimika kulipa dhamana
hiyo.
Baadae mwaka 1955 dola ya kikoloni iliongeza udhibiti zaidi wa
vyombo vya habari kwa kuingiza katika Sheria ya Adhabu vifungu vipya
vilivyokataza uchapishaji wa jambo au taarifa yoyote lenye uwezo wa kuleta
chuki dhidi ya serikali ya kikoloni au watendaji wake. Kama anavyosema Sturmer,
kutokea hapo sheria hiyo ya uchochezi ndio imekuwa kizingiti kikubwa kwa uhuru
wa magazeti katika Tanzania. Haiwezi kuwa ajabu kwamba wahanga wa kwanza wa
sheria hiyo ya uchochezi walikuwa mabwana Kheri Rashidi Baghdelleh na Robert
Moses Makange waliokuwa wahariri wa gazeti la Mwafrika; na mhariri wa
gazeti la Sauti ya TANU aliyejulikana kama Julius Kambarage Nyerere!
Mheshimiwa Spika,
Kitu cha ajabu ni kwamba sheria iliyotungwa na wakoloni wa
Kiingereza kwa lengo la kuwadhibiti wenyeji wa Kiafrika wasidai uhuru au
kuanika uchafu na uonevu wa dola ya kikoloni haikufutwa mara baada ya uhuru.
Badala yake, sera za habari za dola ya uhuru sio tu zilipokea na kuzidisha
masharti ya kisheria dhidi ya uhuru wa habari kwa kutunga Sheria ya Magazeti
ya mwaka 1976 iliyoongeza makali ya sheria ya uchochezi, bali pia zilitaifisha
magazeti na vyombo vingine vya habari binafsi vilivyokuwepo wakati wa uhuru.
Hivyo, kwa mfano, Shirika la Utangazaji la Tanganyika (TBC)
lilitaifishwa kwa Sheria ya Bunge ya tarehe 16 Machi 1965 na kubatizwa jina
jipya la Radio Tanzania Dar es Salaam (RTD). Aidha, tarehe 5 Februari, 1970,
gazeti binafsi la The Standard lilitaifishwa na Serikali. Na ilipofika
tarehe 26 Aprili, 1972, The Daily News, gazeti jipya la Serikali
lilianzishwa kwa kuunganisha The Standard na gazeti la The Nationalist
lililokuwa linamilikiwa na TANU. Hivyo basi, kama anavyosema Sturmer katika
historia yake ya vyombo vya habari Tanzania, “kufikia mwaka 1976 Serikali ya
Nyerere ilishafanikisha lengo lake kuu la sera ya habari – kuwa na udhibiti juu
ya vyombo vyote vikuu vya habari....”
Mheshimiwa Spika,
Utaratibu huu wa udhibiti juu ya vyombo vya habari kwa kutumia Sheria
ya Magazeti ulishambuliwa na Tume ya Nyalali kwa kukiuka matakwa ya ibara
ya 18 ya Katiba inayotoa uhuru wa mawazo na uhuru wa habari. Kwa maneno ya Tume
hiyo, Serikali inakiuka uhuru wa mawazo na wa habari “... kwa kujihusisha na
kuchuja habari zinazotolewa kwa wananchi.” Tume ilipendekeza marekebisho
makubwa katika Sheria ya Magazeti “... ili kuruhusu uhuru mkubwa zaidi wa
habari na wa mawazo na kulegeza uchujaji wa habari.” Mapendekezo haya ya Tume
ya Nyalali hayajatekelezwa hadi leo hii, zaidi ya miaka ishirini na mbili tangu
Tume hiyo iwasilishe Taarifa yake kwa Rais Ali Hassan Mwinyi.
Mheshimiwa Spika,
Wakati Tanzania imebakia mateka wa sera za habari za kikoloni na
za utawala wa kiimla wa chama kimoja, jirani zetu wa Kenya na marafiki zetu wa
Zimbabwe wamepiga hatua kubwa katika kupanua uhuru wa habari. Hivyo, kwa mfano,
Katiba Mpya ya Jamhuri ya Zimbabwe iliyopitishwa kwa kura ya maoni ya wananchi
wa nchi hiyo mwezi Februari mwaka huu inatoa uhuru wa mawazo ambao unajumuisha
uhuru wa kutafuta, kupokea na kusambaza mawazo na habari nyingine; uhuru wa
mawazo ya kisanii na wa utafiti wa kisayansi na uhuru wa taaluma.
Aidha, Katiba hiyo inatoa uhuru wa habari ambao ni pamoja na
ulinzi wa vyanzo vya habari vya waandishi wa habari; na uhuru wa uanzishaji wa
vyombo vya utangazaji ambavyo havitakiwi kuwa chini ya udhibiti wa serikali au
maslahi ya kisiasa au kibishara. Vile vile, Katiba Mpya ya Zimbabwe inavilazimu
vyombo vya habari vinavyomilikiwa na Serikali kuwa huru kuamua mambo gani ya
kutangaza; kutokupendelea na kutoa fursa sawa kwa ajili ya kutangaza maoni
tofauti na mawazo yanayokinzana.
Mheshimiwa Spika,
Katiba Mpya ya Zimbabwe inatoa pia uhuru wa taarifa (access to
information). Hivyo, kwa mfano, kila raia au mkazi wa kudumu wa Zimbabwe, ikiwa
ni pamoja na makampuni na vyombo vya habari, ana haki ya kupatiwa taarifa
yoyote inayodhikiliwa na Serikali au na taasisi au shirika lolote la serikali
katika ngazi zote, kama taarifa hiyo inahitajika kwa ajili ya maslahi ya
uwajibikaji kwa umma. Zaidi ya hayo, kila mtu, ikiwa ni pamoja na vyombo vya
habari vya Zimbabwe, ana haki ya kupatiwa taarifa inayoshikiliwa na mtu yeyote,
pamoja na Serikali, kama taarifa hiyo inahitajika kwa ajili ya kufurahia au
kulinda haki yake. Kama ilivyo kwa Zimbabwe, Katiba Mpya ya Kenya nayo pia
imetoa uhuru mpana wa habari kwa wananchi wa Kenya.
Kwa maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, ni fedheha kwamba
nchi yetu iliyokuwa ya kwanza kupata uhuru katika ukanda wa Afrika Mashariki,
Kati na Kusini inaelekea kuwa ya mwisho katika masuala ya uhuru wa habari kwa
watu wake. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali hii ya CCM
kulieleza Bunge lako tukufu ni lini italeta muswada wa sheria kwa lengo la
kufuta urithi huu wa fedheha wa sheria za kikoloni ili Tanzania iendane na
karne mpya ya uhuru wa habari na wa mawasiliano.
Mheshimiwa Spika,
Kwa sasa vyombo vya habari vya Serikali yaani, Radio na
Television za Taifa ndio vinatoa matangazo kwa wananchi kuhusu kile
kinachoendelea Bungeni. Kwa bahati mbaya ni kwamba Radio ya Taifa ambayo
inasikilizwa na watanzania wengi wa hali ya chini na kati katika maeneo mengi
ya mijini na vijijini wanashindwa kusikiliza mijadala inayoendelea Bungeni,
kwani matangazo yanakatishwa pindi kipindi cha maswali na majibu
kinapomalizika. Matangazo ya mjadala wa Bunge yanaendelea kurushwa kwenye
Television ya Taifa hadi Bunge linapoahirisha shughuli zake kwa siku.
Mheshimiwa Spika,
Huku ni kutowatendea haki watanzania wengi kwa kuwapa fursa
kusikiliza nini wawakilishi wao wanachokiongea katika mijadala mbalimbali
Bungeni. Kambi Rasmi ya Upinzani inaona sasa ni muda mwafaka kwa sekta binafsi
nazo kufanyakazi hiyo ambayo inaonyesha imevielemea vyombo hivyo vya serikali
na kuondoa ukiritimba uliopo wa kurusha matangazo ya Bunge.
3.2 Matangazo ya serikali kwenye vyombo vya habari
Mheshimiwa Spika,
Suala la matangazo ya serikali katika vyombo vya habari si
kwamba limekuwa likitumika kuminya uhuru wa habari katika baadhi ya vyombo vya
habari hususan vinavyoonekana kuwa vinafanya utafiti katika habari zake kwa
masuala mbalimbali ya kisiasa, kijamii na kiuchumi na hivyo kuweka hadharani
mapungufu na uchafu wa Viongozi waliopewa dhamana na wananchi.
Mheshimiwa Spika,
Suala hilo la matangazo badala ya kuviimarisha vyombo vya habari
ili viweze kusimama na kufanyakazi bila ya kuingiliwa, sasa linatumika kama
njia ya kufifisha uhuru wa kutafuta na kutoa habari na kuvifanya vyombo vya
habari kuachana na uhandishi wa uchunguzi na hivyo kukiuka haki za walaji za
kupata taarifa kwa mujibu wa Ibara ya katiba ya 18 (d).
Mheshimiwa Spika,
Sasa kumezuka mtindo mwingine wa kuhamishia raslimali za
Serikali kwenye chama kwa ajili ya kuiokoa CCM na wanasiasa wengine. Tutatoa
mfano hai wa hivi karibuni kabisa. Kwa wafuatiliaji wa habari katika vyombo vya
habari, bila shaka watakumbuka kuwa siku ya Mei Mosi, Gazeti la CCM linaloitwa
Uhuru, lilikuwa na kurasa 79, ikiwa ni ongezeko la karibu mara tatu ya gazeti
hilo linavyotoka kwa siku za kawaida kama halina matangazo.
Kinachoweza kuwa kimewasikitisha wafuatiliaji makini wa masuala
ya habari ni kwamba matangazo hayo hayakuwa ya watu au kampuni binafsi yalikuwa
ni matangazo ya serikali na taasisi zake, kwa maana ya kwamba yaligharimu mamilioni
ya shilingi za walipa kodi wa Tanzania, ambayo kimsingi yalipotumika ‘hovyo’
kama tutakavyoonesha kwa hoja hapa;
Mheshimiwa Spika,
Tatizo hapa si tu kwamba gazeti hili ni la CCM, bali pia kuna
masuala ya msingi kadhaa ambayo kwa kweli mtu yeyote makini, anayejua biashara
ya matangazo, hasa kutangaza kupitia vyombo vya habari, anapaswa kuzingatia
mara zote kabla hajaamua kutumbukiza mamilioni kwa ajili ya kujitangaza;
Kwanza, kama chombo hicho ni gazeti, basi linapaswa kuwa na
wasomaji wengi na pia mzunguko mkubwa sokoni kwa maana ya kuwafikia watu wengi
kutokana na kusambaa maeneo mengi ndani (na nje ikibidi) ya nchi. Mfuatiliaji
yeyote makini wa vyombo vya habari anajua wazi kuwa gazeti hilo la CCM, halina
sifa hizo.
Kama serikali na taasisi zilizotumia gazeti hilo la CCM kama
njia ya kujitangaza zingekuwa makini na matumizi halali ya fedha za Watanzania,
lazima zingezingatia kanuni za kawaida kabisa; yaani kuhakikisha wanapata
wasomaji na soko kubwa katika bidhaa na huduma zao wanazotangaza, hivyo
wangepaswa kutangaza katika magazeti yanayosomwa na yenye mzunguko mkubwa.
Mheshimiwa Spika,
Kinachoonekana hapa ni kwamba, baada ya njia nyingine za
kifisadi za kupata fedha kuisaidia CCM kushtukiwa, sasa zimebuniwa mbinu
nyingine za kifisadi za kusaka fedha kwa ajili ya chama hicho, mojawapo ikiwa
ni hii ya utoaji wa matangazo kwa vyombo vya habari vya CCM, visivyokuwa na
sifa stahili. Haya ni matumizi mabaya ya matangazo yenyewe na fedha za umma! Ni namna ile ile ya kutoa zabuni kwa Kampuni ya CCM, ifanye
upanuzi wa eneo la bandari kwenye eneo la CCM, bila makampuni yenye uwezo
kushindanishwa ili kupata moja iliyo makini na yenye vigezo vya kufanya kazi
husika.
3.3 TCRA NA UANGALIZI WA VYOMBO VYA HABARI VYA KIELEKTRONIKI
Mheshimiwa Spika,
TCRA ndiyo yenye mamlaka ya kusimamia vyombo vya elkroniki kama
Radio na Televisdion, lakini imeshindwa kabisa kusimamia vyombo hivyo
walivyovipatia leseni ya kufanyakazi, kwani baadhi ya vituo ukisikiliza
vinafanya uchochezi wa kisiasa, kidini, ukabila wa wazi lakini vimeachwa hadi
matatizo ya udini yaliposhika kasi ndio Serikali ikaanza kukimbia kuchukua
hatua.
Mheshimiwa Spika,
Hivi sasa intaneti haitawaliwi na sheria yoyote nchini, baadhi
ya vipindi vya redio na televisheni havizingatii maadili ya Kitanzania, maeneo
mengi ya vijijini hayana huduma ya televisheni. Kambi Rasmi ya Upinzani inasema
kuwa huu ni udhaifu wa wazi kwa mamlaka hiyo iliyopewa jukumu la kusimamia.
Hivyo basi tunaitaka Serikali itoe kauli kuhusiana na udhibiti wa TCRA katika
suala hilo.
ka 2013)
3.4 SHIRIKA LA UTANGAZAJI TANZANIA (TBC)
3.4.1 TBC na matukio muhimu ya Kitaifa
Mheshimiwa Spika,Ikiwa imepita takribani miaka
mitano tangu Mhe. Raisi alipozindua rasmi Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC)
mwezi mei 2008. Kwa kuwa, pamoja na uchakavu na ukosefu wa vifaa TBC imeweza
kupanua masafa yake ya utangazaji karibu nchi nzima ,na kwa kuwa hili ni
shirika la umma, ni matumaini makubwa kwa watanzania kuwa TBC ingekua mstari wa
mbele katika kuripoti na kutangaza matukio muhimu yanayoendelea katika nchi
yetu.
Mheshimiwa Spika, Kwa masikitiko makubwa TBC
imekua nyuma katika kuripoti matukio muhimu na badala yake imekua ikiweka
vipindi visivyoendana na matukio yanayolikabili taifa. Hii ni dharau kwa
watanzania wengi hasa ukizingatia kuwa hili ni shirika la umma na si la mtu
binafsi hivyo wajibu wake mkubwa ni kumpa taarifa mtanzania kwa wakati hata
pale inaposhindwa kutoa taarifa ama kuwepo eneo la tukio basi lazima programu
zake ziendane na hali halisi.
Mheshimiwa Spika, Kwa masikitiko makubwa
wakati wa ajali ya meli ya MV Skagkit iliyotokea mwaka jana, 2012, wakati kuna
taarifa za awali za ajali, TBC ilikua ikiweka na kupiga muziki wa taarabu bila
ya kuzingatia uzito wa ajali ile, hata siku iliyofuata kwa ajili ya shughuli za
uokoaji TBC iliendelea kuweka programu ambazo hazikuendana na uzito wa tukio
lile licha ya kuwa mamia ya watanzania walipoteza maisha na huku tafrani
ikizuka kwa baadhi ya watanzania ambao ndugu zao walikua katika tukio lile.
Mheshimiwa Spika,Katika kuonesha kuwa TBC
haijifunzi kutokana na makosa, ama labda imekosa uongozi wenye weledi na
umakini tangu kuisha kwa ajira ya mkurugenzi wao makini Tido Muhando, mwezi wa April
2013 ambako kulikua na mlipuko wa bomu Arusha,tukio ambalo lilikuwa kubwa
kwenye historia ya nchi yetu kwani ni mara ya kwanza tukio kama hilo kutokea,
TBC iliendelea na urushaji wa matangazo na vipindi tofauti huku televisheni na
vituo vingine vya binafsi vilikuwa vinajulisha taifa kuhusiana na tukio hilo.
Mheshimiwa Spika, Tukiwa katika mijadala ya
muhimu ya mustakabali wa taifa letu, ambapo tunajadili na kupitisha bajeti kwa
ajili ya watanzania, TBC hukata matangazo ya vipindi vya Bunge wakati
uwasilishaji wa hoja muhimu ukiendelea. Wakati wa hotuba ya Mambo ya ndani,
wakati msemaji mkuu wa kambi ya upinzani anakaribia kuanza kusoma maoni ya Kambi
ya Upinzani , TBC walikata matangazo na kuweka sherehe za Mwenge.
Mheshimiwa Spika,Pamoja na hayo yote, TBC bado
inaendelea na kauli mbiu yake ya 'Ukweli na Uhakika' kauli ambayo
haiendani na uhasilia wa uratibu wa vipindi vyake vya matangazo na uwasilishaji
wa taarifa kwa umma. Mara nyingi kwenye mijadala na hoja nzito ambazo Serikali
inakua ina hali mbaya, matangazo ya bunge hukatwa kwa kisingizio kuwa mitambo
au matatizo ya kiufundi yametokea, mbona matangazo au hitilafu za ufundi
hazitokei katika sherehe za Mwenge?Ama hitilafu kwenye kuonesha ujio wa rais wa
China ? TBC inatumika na imeendelea kutumiwa na Serikali ya CCM katika kuminya
haki ya mtanzania ya kupata habari si kwa sababu ya ufinyu wa bajeti peke yake
bali kuwaridhisha watawala. Lazima TBC ibadilike na kujua kuwa ina dhamana
katika kupeleka habari na taarifa sahihi kwa umma kwa wakati na si kwa
kuendeshwa kama roboti.
4.0 MASUALA YA VIJANA
4.1 UUNDAJI WA BARAZA LA VIJANA LA TAIFA
Mheshimiwa Spika, suala la mchakato wa
uundwaji wa Baraza la Taifa la Vijana, sasa umekuwa si tu wimbo bali zimwi la
muda mrefu linaloiandama serikali ya CCM na imeshindwa kabisa kuepukana
nalo.Sera ya zamani ya maendeleo ya vijana ya mwaka 1996 ilitamka kwamba
kutaanzishwa Baraza la Vijana na suala hilo kurudiwa katika Sera mpya ya mwaka
2007; hata hivyo Serikali imekuwa ikiwepa kuhakikisha kwamba matakwa hayo ya
sera tajwa yanatekelezwa pamoja na kuwa suala hilo linahusu mustakabali wa
maendeleo ya vijana nchini. Kambi Rasmi ya Upinzani inatambua kwamba katika
ilani za uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 vyama mbalimbali viliahidi kuhakikisha
kwamba Baraza la Vijana la Taifa linaundwa.
Mathalani, CHADEMA katika Ilani yake 2010-2015 kipengele 6.4.1
(viii) ilitamka “Kwa kuwa vijana ndio kundi kubwa hapa nchini, na kwa kuwa uhai
wa muda mrefu wa taifa letu upo mikononi mwa vijana, Serikali ya CHADEMA
itawezesha vijana kuunda Baraza la Vijana (BAVITA) ambalo limekwamishwa na
Serikali ya CCM kwa muda mrefu”.
CCM nayo kupitia ilani yake ya katika kipengele 80 (k)
“Kuhamasisha ushiriki wa vijana katika ngazi mbalimbali za maamuzi ikiwa ni
pamoja na kukamilisha uanzishaji wa Baraza la Vijana”.Hivyo, Kambi Rasmi ya
Upinzani inatarajia kwamba wabunge wa pande zote katika suala hili la
kuanzishwa kwa Baraza la Vijana la Taifa kuungana kuwa kitu kimoja kuisimamia
Serikali itekeleze Sera na ahadi badala ya kuitetea kwa udhaifu iliyouonyesha.
Mheshimiwa Spika; Katika Hotuba ya Msemaji wa
Kambi Rasmi ya Upinzani Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo juu ya mapitio
ya utekekelezaji kwa mwaka 2010/2011 na makadirio ya mapato na matumizi kwa
mwaka 2011/2012 tulihoji ni lini hasa Serikali ingewezesha kuanzishwa kwa
Baraza la Vijana la Taifa. Aidha, Kambi Rasmi ya Upinzani ilirudia tena kuhoji
suala hili wakati wa mjadala wa mapitio ya utekelezaji kwa mwaka 2011/2012 na
makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka 2012/2013. Hata hivyo, kwa nyakati
zote hizo Serikali katika majumuisho imekuwa irudia tena ambayo imekuwa
ikitolewa kwa miaka zaidi ya miaka 17 ya kukamilisha mchakato wa kuanzishwa kwa
baraza la Vijana la Taifa; bila utekelezaji kamili na wa haraka.
Mheshimiwa Spika; Kambi Rasmi ya Upinzani
inayo taarifa kwamba kufuatia hali hiyo mwezi Januari 2013 mbunge wa Ubungo,
Mheshimiwa John Mnyika aliwasilisha kwa Katibu wa Bunge muswada binafsi wa
sheria kuwezesha kuundwa kwa Baraza la Taifa la Vijana. Katika Hotuba yake juu
ya mapitio ya utekelezaji kwa mwaka 2012/2013 na makadirio ya mapato na
matumizi ya mwaka 2013/2014 ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Kiongozi wa Kambi ya
Upinzani Mheshimiwa Freeman Mbowe alihoji ni lini Serikali itawasilisha bungeni
miswada binafsi ya wabunge ukiwemo muswada huo.
Mheshimiwa Spika; kwa mujibu wa Kitabu cha
hoja za wabunge na majibu ya Serikali kuhusu Hotuba ya Bajeti ya Ofisi ya
Waziri Mkuu na Taasisi zake kwa mwaka wa fedha 2013/2014 juu ya muswada huo
“Ofisi ya Katibu wa Bunge imemwandikia Mwanasheria Mkuu wa Serikali kupata
ufafanuzi kama Muswada unaohusu uanzishwaji wa Baraza la Vijana la Taifa
hautakuwa na athari zozote za kiwango cha matumizi ya fedha kutoka Mfuko Mkuu
wa Hazina kama ilivyoanishwa katika Kanuni ya 95 ya Kanuni za Kudumu za Bunge
toleo la mwaka 2007”.
Mheshimiwa Spika; Kambi Rasmi ya Upinzani
inayo taarifa kwamba Mwanasheria Mkuu wa Serikali ametoa ushauri kuwa muswada
huo hauwezi kuchapishwa katika gazeti la Serikali kwa kuwa umekiuka masharti ya
ibara ya 99 ya Katiba ya Nchi. Kambi Rasmi ya Upinzani ina taarifa kuwa
Mwanasheria Mkuu wa Serikali ametoa ushauri huo kwa kuwa muswada unalenga
pamoja na mambo mengine kupitia kifungu cha 31 kipengele cha kwanza kuanzisha
Mfuko wa Maendeleo ya Vijana kwa madhumuni ya kugharamia shughuli za baraza la
vijana la taifa, mipango ya baraza na kutekeleza miradi ya vijana kwa ajili ya
maendeleo ya vijana.
Mheshimiwa Spika; Kambi Rasmi ya Upinzani
inaitaka Serikali kueleza iwapo katika kutoa ushauri huo ilizingatia kwamba
kifungu cha 31 kipengele cha pili cha muswada huo kinataja vyanzo mbalimbali
vya fedha za mfuko ikiwemo kutaja kuwa fedha za mfuko zitatokana na fedha
zilizotengwa na Serikali na Bunge kwa ajili ya Baraza kwa mujibu wa Ibara ya
135 kifungu cha pili cha katiba ya Nchi.
Mheshimiwa Spika; Ibara ya 135 (2) ya Katiba
ya Nchi inatamka kuwa “fedha ambazo hazitawekwa kwenye Mfuko Mkuu wa Hazina ya
Serikali ni zile zote ambazo zimetajwa na sheria ya kwamba zitumike kwa
shughuli maalum au ziwekwe kwenye mfuko mwingine kwa ajili ya matumizi maalum”.
Kambi Rasmi ya Upinzani inataka ufafanuzi kutoka kwa Serikali ni
kwanini haikutoa ushauri wa kufanya ibara hiyo ya Katiba ya Nchi kutumika
kuwezesha kuanzishwa kwa Baraza la Vijana na Mfuko wa Maendeleo ya Vijana bila
kufungwa na Ibara ya 99 ya Katiba kifungu cha kwanza ambacho kimeweka masharti
kuwa “Bunge halitashughulikia jambo lolote kati ya mambo yanayohusika na ibara
hii isipokuwa kama Rais amependekeza kwamba jambo hilo lishughulikiwe na Bunge
na pendekezo hilo la Rais liwe limewasilishwa kwenye Bunge na Rais.”
Mheshimiwa Spika; Kambi Rasmi ya Upinzani
inatambua kuwa Kifungu cha pili kinataja mambo yanayohusika na ibara hiyo ya 99
ni pamoja na muswada wa sheria kwa ajili ya “kuagiza kwamba malipo au matumizi
ya fedha yafanywe kutokana na Mfuko Mkuu wa Hazina ya Serikali au mfuko
mwingine wowote au kubadilisha kiwango hicho kwa namna nyingine yoyote
isipokuwa kupunguza”. Hata hivyo, kwa zaidi ya miaka 17 maraisi na mawaziri
wenye dhamana wamekuwa wakiacha kutumia madaraka hayo ya kikatiba kuleta
muswada bungeni wa kuwezesha kuundwa kwa Baraza la Vijana la Taifa; hivyo
kitendo cha Serikali kupitia kwa Mwanasheria Mkuu kuendeleza vikwazo hata kwa
muswada binafsi wa mbunge kuhusu suala hilo kunaashiria ukosefu wa nia njema
kwa upande wa Serikali katika mchakato wa kuundwa kwa Baraza la Vijana la
Taifa.
Mheshimiwa Spika; Kambi Rasmi ya Upinzani
inatoa mwito kwa Serikali na Uongozi wa Bunge kuwezesha muswada wa Baraza la
Taifa la Vijana kuwasilishwa kwenye mkutano huu wa kumi na moja wa Bunge
unaoendelea iwe ni kupitia muswada binafsi, muswada wa kamati au muswada wa Serikali
kwa kuwa tayari maoni yameshakusanywa kwa miaka mingi kinachohitajika sasa ni
utekelezaji wa Sera na ahadi.
Kambi rasmi ya upinzani, Tunataka kujua msimamo wa Serikali
katika bunge hili, ituambie muda mahsusi (time frame) lini hasa mchakato wa
uundwaji wa baraza hilo utakamilika na hatimaye kuanza kufanya kazi kwa Baraza
la Vijana la Taifa kwa ajili ya maslahi ya vijana wa nchi hii. Iwapo Serikali
ya CCM itaendelea kupiga dana dana muswada wa sheria wa kuundwa kwa chombo hiki
muhimu kwa maendeleo ya vijana; Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni inayoongozwa na
CHADEMA itawahamasisha vijana nchi nzima kuelekeza nguvu na uwingi wao katika
kuishinikiza Serikali sikivu ya CCM, kufanya mabadiliko yenye kuwezesha matakwa
ya vijana kutekelezwa kwa wakati.
4.2 Sekta ya maendeleo ya vijana
Mathalani katika utekelezaji wa bajeti ya mwaka jana, kazi pekee
ambazo zimekuwa zikipewa kipaumbele na sekta hii ni kukimbiza mbio za mwenge na
kuratibu maadhimisho ya wiki ya vijana kitaifa. Aidha kwa mwaka jana, sekta
hii, kwa mujibu wa maelezo ya wizara, ilifanya uratibu wa mafunzo ya
kuwawezesha vijana kuwa na mawazo ya kimkakati ya ubunifu na ujasiriamali
katika mikoa ya Mbeya, Mwanza, Mara, Morogoro, Geita, Njombe, Kigoma na Arusha!
Kambi ya Upinzani Bungeni inaitaka wizara kulieleza bunge lako
hili kwa takwimu na maelezo ya kina ni kiasi gani mbio za Mwenge ambazo
zimekuwa zikitumia mabilioni ya fedha ‘kuingiza’ mamilioni ya fedha, zimeweza
kuwasaidia vijana wa Tanzania kupambana na tatizo kubwa linalowakabili la
ukosefu wa ajira na ujira wenye staha. Je, wizara inaweza kutoa takwimu hapa
kuonesha namna ambavyo mabilioni ya fedha waliyotengewa mwaka jana kwa ajili ya
uratibu wa mafunzo ya ubunifu na ujasiriamali, wameweza kufundisha vijana
wangapi na katika maeneo yapi hasa ya utaalamu na taaluma, kwa kiwango gani ili
kuweza kuwajengea uwezo wa kuajiriwa na kujiajiri kwa ajili ya kupata ujira
wenye staha.
4.3 Mikataba, mipango, sera na utekelezaji
Mheshimiwa Spika, Mwaka mzima baada ya
serikali kusimama hapa bungeni na kulipatia bunge lako matumaini na kutoa ahadi
kemkem wakati wa kupitisha Azimio la Mkataba wa Kimataifa wa Vijana wa Afrika,
hadi sasa wizara hii imeendelea kusuasua na kuzidi kutoa ahadi juu ya ahadi
kuhusu kuweka utaratibu wa kisheria wa utekelezaji wa mkataba huo.
Mheshimiwa Spika, Baada ya bunge hili katika
mkutano wake wa mwezi Februari mwaka jana kupitisha azimio hilo, katika hotuba
ya bajeti mwaka jana, wizara hii ilisema kuwa, kwa kushirikiana na Ofisi ya
Mwanasheria Mkuu wa Serikali imeanza kuchukua hatua za kuandaa muswada wa
sheria ya utekelezaji wa mkataba huo.
Mheshimiwa Spika, Lakini katika kuonesha kuwa
serikali hii haikuwa wala haina nia ya dhati kuweka utaratibu wa kisheria ili
kusaidia utekelezaji wa azimio hilo, katika malengo yake ya utekelezaji wa
mpango wa bajeti kwa mwaka wa fedha 2013/14, imeshindwa kabisa kuzungumza
chochote juu ya suala hilo.
Kambi rasmi ya Upinzani, inaona kuwa huu ni
mwendelezo tu wa serikali hii ya CCM kuendelea na utamaduni wake wa
kuwatelekeza,kuwapuuza na kuwadharau vijana wa nchi hii.Aidha , tunataka kujua
ni lini wizara italeta mswada huo hapa Bungeni kwa ajili ya kupitishwa na Bunge
na kuwa sheria.
4.4 Mbio za Mwenge wa Uhuru
Mheshimiwa Spika,mara kadhaa sasa Kambi rasmi
ya Upinzani Bungeni imekuwa ikihoji maswali anuai kuhusu jambo hili lakini
bahati mbaya yamekuwa yakitolea majibu yasiyokidhi haja. Nasi kwa ajili ya
kutimiza wajibu wetu wa kuwasemea Watanzania wasiokuwa na sauti ndani ya
mhimili huu, tutaendelea kukumbushia na kuhoji hadi majibu mujarabu
yakakapotolewa.
Mathalani, katika moja ya malengo ya utekelezaji wa mpango wa
bajeti wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo ni ukimbizaji wa
Mwenge wa Uhuru. Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni, si tu kwamba imekuwa ikihoji
maana nzima ya kuendelea kutumia mabilioni ya walipa kodi maskini kwenye mbio
za mwenge, badala ya kuuweka makumbusho na kuufanya kuwa moja ya vivutio vya kiutamaduni.
Mheshimiwa Spika, mtu yeyote makini hawezi
kuona mantiki ya mbio za mwenge ambazo zimekuwa zikitumia mabilioni ya fedha
kuzunguka nchi nzima kuzindua miradi ya mamilioni ya watu binafsi! Kama vile
bar, nyumba za kulala wageni na mingineyo.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka huu wa fedha
tumeendelea kutenga fedha kwa ajili ya kukimbiza mwenge, randama ya wizara
inaonyesha kuwa ,kijifungu 210319 zinaombwa shilingi 3,000,000 ‘kwa ajili ya
kulipa matibabu na bima kwa wakimbiza Mwenge wa uhuru’,kijifungu 210315
zinaombwa shilingi 64,200,000 ‘kwa ajili ya kulipa posho za kujikimu kwa
wakimbiza mwenge wa uhuru, kijifungu 220302 zinaombwa shilingi 57,750,000 ‘kwa
ajili ya kununulia dizeli ya magari mawili yatakayotumika kwenye sherehe za
uzinduzi na kilele cha mbio za mwenge wa uhuru’,.
Aidha, kijifungu 220604 sare, wizara inaomba kiasi cha shilingi
8,886,000 ‘kwa ajili ya sare za wakimbiza Mwenge kitaifa’, kijifungu 220708
zinaombwa shilingi 25,000,000 ‘kwa ajili ya kukodi ndege kwa shughuli za mbio
za Mwenge wa uhuru’, kijifungu 220709 ,zinaombwa jumla ya shilingi 7,200,000
zinaombwa kwa ‘ajili ya ununuzi wa vifaa vya mkutano wa tathimini ya mbio za
mwenge wa uhuru’,kijifungu 221005 zinaombwa shilingi 78,500,000 ‘kwa ajili ya
posho ya safari za kikazi ndani ya nchi kwa wakimbiza mwenge kitaifa’
,kijifungu 221406 zinaombwa shilingi 15,000,000 kwa ajili ya ‘...kuandaa tuzo
...wakati wa mbio za mwenge’,
Mheshimiwa Spika, Pamoja na kutengwa kwa
fedha zote hizi kiasi cha shilingi 259,536,000 pesa ambazo
zingewekezwa kwenye mfuko wa kuwakopesha vijana zingeweza kuwakwamua kwenye
tatizo la ajira, serikali inaomba fedha hata kwa ajili ya kukodi ndege kwa
ajili ya kukimbiza mwenge , mwaka huu tutashuhudia mwenge ukikimbizwa angani!
bado mwenge umeendelea kupoteza mwelekeo
Mheshimiwa Spika, katika kuthibitisha kuwa
Mwenge umepoteza mwelekeo katika mwaka huu wa fedha katika kijifungu 230600 ‘matengenezo
ya mashine’ katika kijifungu 230605 ‘mikataba ya matengenezo kutoka
nje’ randama uk.86 inasema ‘mwaka 2013/2014 sh.366,000 zinaombwa kwa
ajili ya kupata wataalamu nje ya wizara kwa ajili ya kutoa huduma ya
matengenezo ya chombo cha Mwenge wa uhuru’. Unaweza kuona kuwa chombo
hiki kinatafutiwa mtaalamu kutoka nje ya wizara na malipo ya mtaalamu huyo ni
shilingi laki tatu! Hii ni dalili ya wazi kuwa chombo hiki yafaa kikawekwa
kwenye jumba letu la makumbusho.
Kambi Rasmi ya Upinzani, haikubaliani na serikali kutumia kiasi
cha shilingi 259,536,000 kwa ajili ya posho za kukimbiza mwenge, tunataka fedha
hizi ziingizwe kwenye programu za maendeleo ya vijana ili waweze kujiajiri na
mwenge uwekwe kwenye jumba la makumbusho, kwani umekuwa ni kero kwa wananchi
vijijini kuchangishwa fedha za mwenge bila hata kujua zinaenda kufanya nini.
5.0 USIMAMIZI WA MICHEZO NA MUSTAKABALI WAKE KWA TAIFA
Mheshimiwa Spika, Pamoja na hazina ya
wanamichezo nchini, lakini michezo mingi nchini haipewi kipaumbele na
serikali.Mara kadhaa vyombo vya habari vimekua vikiupa kipaumbele mchezo wa
soka kana kwamba michezo mingine haina tija kwa taifa. Leo hii kuna michezo
ambayo kama ikipewa uzito wa kutosha italeta taifa hili heshima katika medani
za kimataifa.
Mheshimiwa Spika,Labda kwa kuwa tumeshindwa
kuwekeza kwenye michezo mingine kwa vipaumbele ambavyo vinaweza kuiweka
Tanzania katika ramani ya michezo, hii imefanya michezo hiyo kufa na hazina ya
taifa ya vipaji mbalimbali nayo kufa bila kutumika. Mfano katika michezo ya 30
ya Olimpiki iliyofanyika jijini London, Uingereza Julai mwaka 2012, Tanzania
ilipeleka jumla ya wanamichezo 7 ambao hawakuambulia medani yoyote .
Mheshimiwa Spika,Wakati Afrika ya Kusini
ilipeleka wanamichezo 125 kwa jumla ya michezo 17,sisi tulipeleka 7 tu. Kuna
jambo kuu la kujifunza kutokana na jinsi ambavyo Serikali, sikivu , ya CCM
inaendesha nchi yetu. Jambo ambalo linastaajabisha na lenye maswali mengi
yasiyo na majibu, Je Wizara hii ina kazi gani? Ina mikakati gani ya jumla
katika kusimamia vyama vya michezo nchini ili viwe na tija? Je wizara hii ina
uchungu na fedha za kodi za wananchi hii kwa matumizi yasiyo na tija katika
sekta ya michezo? Je taifa hili limekosa kutumia michezo kama njia mojawapo ya
kutangaza jina la Tanzania na kuliweka katika ramani ya dunia kwa kuwa na
wanamichezo bora na si bora wanamichezo?
Kambi rasmi ya Upinzani, inapendekeza kwa msisitizo mkubwa kuwa
katika kipindi hiki ambacho taifa letu lipo katika mpasuko na mgawanyiko wa
masuala mbalimbali kuanzia udini,mchakato wa katiba nk , katika kipindi hiki
ambacho mshikamano na umoja wetu kama taifa upo katika hatari ya kusambaratika,
jambo ambalo linaweza kutuunganisha kama taifa moja lililobakia ni michezo .
Hivyo basi tuhakikishe kwamba timu ya taifa ya mpira wa miguu
inaandaliwa vya kutosha na tuweze kuingia kwenye fainali za kombe la dunia
ifikapo 2014, tuna kazi ndogo ya kuifunga Morocco kwao, tunatakiwa kuifunga
Ivory coast hapa kwetu, tunaamini inawezekana kama mipango madhubuti ikiwekwa
sasa.
5.1 Chama cha Riadha Tanzania.
Mheshimiwa Spika, Mwaka 2012, katika mashindano
ya taifa ya riadha kulikua na changamoto kubwa ya wanariadha kushiriki katika
mashindano ya taifa bila ya maandalizi ya kutosha, huku baadhi ya wanariadha
wakishiriki katika mashindano bila ya kuwa na viatu. Haya ni mashindano ya
taifa, Chama cha Riadha (RT)nchini, kimeyandaa bila ya kuwa na mikakati ya
kitaifa ya kuhakikisha kuwa vigezo na viwango vimefuatwa.
Aidha , chama hiki kimekuwa kikilalamikiwa sana na wadau wake
kutokana na hisia kwamba kunakuwa na upendeleo katika kutuma wanariadha ambao
wamekuwa wakiwakilisha taifa letu katika michezo mbalimbali ya kimataifa.
Kambi rasmi ya upinzani, inataka kujua serikali
imechukua hatua gani dhidi ya viongozi wa chama hiki ambao badala ya kusimamia
riadha wamekuwa hawafanyi hivyo , aidha kuna mikakati na mipango gani ya kuinua
kiwango cha riadha hapa nchini ili kurudhisha heshima ya taifa kwenye mchezo
huu maarufu duniani kote?
5.2 Mapato ya viwanja vya Taifa.
Mheshimiwa Spika, Kwa mujibu wa randama uk
102 katika mapato kuna kifungu 140259 ambacho kinahusu mapato ya viwanja vya
michezo (uhuru na Taifa) makadirio yalikuwa kukusanya shilingi 400,000,000
kwa mwaka 2012/2013 ila mapato halisi yaliyokusanywa kutokana na asilimia 15 ya
mapato yote yanayokusanywa kutokana na kutumika kwa kiwanja hicho mpaka
februari 2013 yalikuwa 329,814,400 tu.
Kambi rasmi ya upinzani, inataka kujua mapato hayo
yalikusanywa kutokana na michezo mingapi na fedha hizo zilitumika katika
kufanya kazi gani za kuendeleza michezo hapa nchini.
5.3 Malipo kwa makocha wa kigeni.
Mheshimiwa spika, katika mwaka huu wa fedha
serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni 1.230 katika kifungu 6004-280518
(Baraza la Michezo la Taifa –Makocha)(chanzo:randama, jedwali namba 8)
kwa ajili ya matumizi mengineyo (OC),Aidha kwenye fungu hilo hilo 6004 kwenye
matumizi ya kawaida (chanzo randama ;jedwali namba 6) zimetengwa
jumla ya shilingi milioni 586,079,000 kwa ajili ya mishahara na matumizi
mengineyo zimetengwa shilingi 1,917,960,000
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa randama ya
wizara uk.93 kijifungu 270800 ‘ruzuku kwa asasi na vituo’ zimetengwa
jumla ya shilingi 1,564,382,000 na katika kijifungu kidogo cha 270813 ‘Baraza
la Michezo la Taifa’ zimetengwa shilingi 1,524,382,000 kwa ajili ya ‘mishahara
ya Makocha wa Kigeni’ na matumizi ya Baraza la michezo la Taifa. Aidha
katika mwaka wa fedha 2012/2013 kwenye kijifungu hiki zilitengwa jumla ya
shilingi 823,546,000 tu kwa ajili ya mishahara kwa makocha wa kigeni.
Wakati kichwa cha habari cha kasma hii na kijifungu hiki kikisema
ni ‘ruzuku kwa asasi na vituo’ , ruzuku inayokwenda kutolewa ni kiasi cha shilingi
milioni 40 tu kama ambavyo inaonekana kwenye kijifungu 270839 kituo cha
michezo Arusha shilingi milioni 20 na kijifungu 270840 kituo cha michezo Songea
shilingi milioni 20.
Kambi rasmi ya upinzani, inaona kuwa fedha hizi ni
nyingi sana kwa ajili ya mishahara na marupurupu ya makocha wa kigeni, hivyo
basi tunataka kujua yafuatayo;
i. Ni makocha wangapi watalipwa na ni wa michezo gani?
ii. Wanapewa marupurupu gani kama stahili zao?
iii. Kwanini serikali na wizara hii isiwapeleke makocha wa
kitanzania mafunzoni nje ya nchi ili waweze kutumikia taifa lao pindi
wakimaliza masomo yao?
6.0 BARAZA LA KISWAHILI TANZANIA
Mheshimiwa Spika,Wizara inao wajibu wa
kuimarisha, kukuza na kuendeleza lugha yetu ya Kiswahili kwa ajili ya
kurahisisha mawasiliano ikiwa ni pamoja na uratibu na kuhakikisha ustawi na
maendeleo ya utumiaji wa Kiswahili kwa kushirikiana na asasi zile ambazo
zinahusika na uendelezaji wa lugha hii hapa nchini. Baraza lina wajibu wa
kuhakikisha kuwa matumizi ya Kiswahili yanapewa kipaumbele katika maisha ya
kila siku ya mtanzania, ikiwemo katika shughuli za kitaifa na kimataifa ambazo
viongozi wa taifa letu wanahudhuria.
Mheshimiwa Spika, Pamoja na nyimbo ambazo
Serikali ya CCM imekua ikiziimba mara kwa mara kuwa inataka kukuza lugha ya
Kiswahili ili kuutangaza utamaduni wa Tanzania katika jumuia ya kimataifa ni
aibu kubwa kwa taifa letu pale ambapo viongozi wake waandamizi wanapokuwa
watumwa wa lugha za nchi za Magharibi!
Mheshimiwa Spika, Kwa kuwa Serikali ya CCM
imeamua kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia na nchi ya China, ni kitendo cha
kusikitisha na aibu kuona kuwa wakati wa ziara yake nchini, Raisi wa China,
alihutubia na kuzungumza kwa ufasaha lugha ya taifa lake wakati Rais wa
Tanzania na Waziri wa Mambo ya nje na ushirikiano wa kimataifa wakitumia lugha
ya Kiingereza. Swali la kujiuliza, kama Raisi wa nchi pamoja na waziri wake
wanaona ugumu kutumia lugha ya taifa wakati mgeni wao ametumia lugha ya taifa
lake wakati walengwa wa ujio ule na wageni wengi waliokuwa katika uzinduzi wa
Ukumbi wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere wengi walikua ni watanzania, je itakuaje
kwa mwananchi wa kawaida leo? Lugha ya Kiswahili haiwezi kukua wala kupewa
umuhimu na mataifa mengine ikiwa viongozi wa Serikali wanaonesha hadharani
utumwa wa utamaduni wa nchi za magharibi, lazima kwa nguvu zote Bunge na taifa
tukatae aina hii ya utumwa kwa maana kuwa hata Serikali inayotakiwa kuhimiza
matumizi ya lugha ya Kiswahili na kukitangaza, wamekua mstari wa mbele kutumia
lugha ya Kiingereza.
Mheshimiwa Spika, kambi rasmi ya upinzani
tunajiuliza hivi, Hata kama Serikali ya CCM imeshindwa kulinda tembo wetu basi
hata Kiswahili mshindwe kukilinda? Tunarudia tena, huu ni utumwa! Haukubaliki!
Tutumie na kukitangaza Kiswahili kwenye dhifa na hafla za kimataifa, kwa kuwa
Kiswahili ndiyo urithi wetu.
7.0 USIMAMIZI WA HAKI ZA WASANII NA USHIRIKI WA SERIKALI KATIKA
UTEKELEZAJI
Mheshimiwa Spika, Sheria ya hakimiliki inayotumika
sasa katika kusimamia hakimiliki na hakishiriki za wasanii , ni sheria
iliyopitishwa na Bunge inayojulikana kama Sheria ya Hakimiliki na Hakishiriki
namba 7 ya 1999. Hii iliiondoa sheria ya awali Sheria ya Hakimiliki namba 61 ya
1966. Sheria hii imeendelea kutumika baada ya kutungwa kanuni mbalimbali mwaka
2000 na kuanza kutumika zikiwemo sheria iliyounda COSOTA. COSOTA ilianza kwa
kuwa na bodi iliyokuwa mchanganyiko wa wajumbe waliochaguliwa na wasanii na
wajumbe walioteuliwa na Waziri wa Viwanda na Biashara. Na hali hii ya kuwa na
wawakilishi wasanii katika COSOTA iliendelea mpaka baada ya uchaguzi mkuu wa
chama hicho 2007, ambapo Waziri hakuweza kuteua Mwenyekiti wa bodi ya chombo
hicho na hivyo kuzuia Bodi kuweko.
Mheshimiwa Spika,hata alipoulizwa na Mh.
Martha Mlata kwenye bunge la bajeti 2008 aliahidi kushughulikia na hakufanya
hivyo hata akaulizwa tena bunge la bajeti 2009. Hivyo hatimaye 2011 ikateuliwa
Bodi ambayo haikuwa na muwakilishi kutoka wasanii japokuwa COSOTA iliendelea
kukusanya mirabaha ‘kwa niaba ya wasanii’.
Kambi rasmi ya upinzani, inataka kujua ni kwanini bodi hii haina
mwakilishi wa wasanii kama sheria inavyotaka? Lini mwakilishi huyo atateuliwa
na wizara?
7.1 Kulinda kazi za wasanii
Mheshimiwa Spika, Mwaka 2001, ilitengenezwa kamati
iliyoitwa National Anti Piracy Committee ikiongozwa na Mwenyekiti John Kitime,
iliyokuwa chini ya COSOTA, kazi yake kubwa ni kuwezesha kutengeneza sheria na
kanuni za kuwezesha kazi za audio na video kuwa na stika za mapato. Kazi hii
ilifanyika na kukamilika na kanuni hizo zilipita kwa usimamizi wa Waziri Mh.
Juma Ngasongwa kabla tu ya uchaguzi wa mwaka 2005, lengo likiwa ni kupata
sapoti ya wasanii.
Mheshimiwa Spika, Baada ya jitihada za hapa na
pale, Serikali kwa kupitia TRA wameleta stika mpya, ambazo Tatizo moja tu hapa
ni kuwa TRA kazi yao ni kukusanya kodi tu na sio kulinda hakimiliki, hivyo
stika ya TRA ni stika ya kukusanya kodi na italeta mkanganyiko katika
utekelezaji wa taratibu za hakimiliki. Je, wizara imepanga mikakati gani
kuhakikisha kuwa kazi za sanaa hazidurufiwi, kuuzwa na kusambazwa bila ya
ridhaa za wasanii nchini? Kambi rasmi ya upinzani bungeni inarudia kuitaka
Serikali kuifumua COSOTA na kuunda chombo kipya kitachokuwa na uwezo wa
kusimamia kazi za sanaa.
7.2 Nyimbo za wasanii na Mapato kwao.
Mheshimiwa Spika, Mwaka 2003 zilipitishwa
kanuni zilizoagiza wenye vyombo vya utangazaji nchini ziwalipe wanamuziki
kutokana na matumizi ya nyimbo zao mbalimbali ambazo wanazitumia kwenye vipindi
mbalimbali. Ni jambo la kushangaza kuona kuwa Serikali ya CCM inayojitapa kuwa
na utawala wa sheria inashindwa kudhibiti vyombo vya habari na utangazaji
ambavyo vimeendelea kutumia kila aina ya ubabe na njia za kiunyonyaji ili
visilipe fedha hizi kwa wasanii. Leo hii wasanii wanalazimishwa kuandika barua
kuwa wametoa nyimbo zao kwa vyombo hivyo zipigwe bila kulipia na kutokana na
mazingira yaliyotengenezwa, wanamuziki wanajikuta ni lazima wahonge! ili nyimbo
zao zipigwe ili waweze kupata soko la kazi zao.
Mheshimiwa Spika,Wizara hii ambayo inasimamia
TBC, televisheni na redio ya Taifa, imeshindwa kuvichukulia hatua za kisheria
vyombo vyake ambavyo vimekua moja wapo ya wakiukaji wa sheria hii. Ni kejeli
kwa taifa, ni kejeli kwa wasanii wanaopata shida kujikwamua kimaisha. TBC leo
inapiga na kucheza nyimbo za wasanii bila kuwalipa, huku wizara inayotakiwa
kusimamia vyombo hivi inashuhudia sheria zilizopitishwa na bunge hili
zinavunjwa.
Mbaya zaidi TBC inauza CD na kanda za nyimbo zilizoko katika
maktaba yake bila kutoa hata senti kwa wanamuziki waliorekodi nyimbo hizo, iko
wapi tofauti yao na maharamia wengine? Leo hii wizara inawezaje kusema kuwa wao
ni wasafi? Ni aibu kwa wizara, ni aibu kwa watendaji wake, ni aibu kwa serikali
, sikivu, ya CCM!
7.2 Harakati za kudai haki za wasanii.
Mheshimiwa Spika, sanaa imeendelea kufanywa
mtaji wa biashara na watu wachache ambao wanatumia nguvu waliyo nayo katika
jamii na uwezo wao wa kifedha katika kukandamiza maslahi ya wasanii hapa
nchini. Katika harakati za kutafuta haki za wasanii hapa nchini, mimi binafsi
pamoja na wasanii wengine wachache, tulianzisha harakati za kudai haki kwa
kupitia programu maarufu iliyojulikana kama 'Anti Virus' chini ya
'Vinega' ikiwa na lengo na juhudi za kudai haki za wasanii dhidi ya
ukandamizaji unaofanywa na wajanja wachache kwenye muziki, ambao wametumia
nafasi kama njia ya kutumia mitaji yao ya fedha kuwaendesha wasanii jinsi
wanavyotaka wao.
Mheshimiwa Spika, Kama ilivyo kawaida, wasanii
wengi walidharau jitihada zetu na kutotuunga mkono. Leo hii katika tasnia ya
muziki, kuna mgogoro mkubwa uliofuka moto kati ya msanii maarufu Lady Jaydee
dhidi ya wamiliki wa radio ya Clouds FM hatua iliyosababisha nyimbo za
wanamuziki wa kizazi kipya maarufu kama 'Bongo Flavour' kutopigwa kwa
siku moja katika kituo hicho. Sasa, ukiangalia kilio cha Lady Jaydee ni kilio
kilekile kilichopelekea VINEGA kuingia vitani.
Mheshimiwa Spika, kama msemaji mkuu wa kambi
ya upinzani bungeni, na mwenye dhamana na uchungu na tasnia ya sanaa nchini,
niweke wazi kwa umma wa watanzania kuwa, tumefikia hapa tulipo si kwa kuwa na
sheria kandamizi tu bali pia kwa kukosekana kwa umoja wa wasanii nchini. Wakati
tukiwa na juhudi za kutetea maslahi ya watanzania kupitia Anti Virus, ni
wasanii wachache ambao walituunga mkono na wengi wao wakibeza jitihada zetu,
wakiwemo hawa ambao leo wanalalamika kuwa wananyonywa haki zao. Wengine
walifikia hatua ya kusema kuwa tumepewa fedha ili kuzima harakati
tulizozianzisha.
Mheshimiwa Spika, Umoja wa wasanii hasa wa
muziki wa kizazi kipya nchini, unasimamiwa na chombo halali kinachojulikana
TUMA-‘Tanzania Urban Music Association’, lakini kutokana na ujanja wa watu
wachache, waliudhoofisha umoja huu kwa kuanzisha kampuni iliyosajiliwa kama TFU-
‘Tanzania Flavour Unit’ iliyowalaghai wasanii kuwa ni muungano wa wanamuziki wa
Bongo Fleva na kuhodhi majukumu ya TUMA ambacho ni chama halali cha kusimamia
wanamuziki wa Bongo Fleva. Mpaka tunapoongea leo hii, hata Studio iliyotolewa
na Mheshimiwa Raisi, bado ipo katika mikono ya TFU pamoja na Serikali kuamuru
irudishwe katika mikono ya Serikali ili ikabidhiwe kwa wasanii wote chini ya
chama halali cha TUMA. Sasa tunataka wasanii wote nchini waache uoga na unafiki
na wajiunge na vyama vyao halali ili viwatete haki zao.
Mheshimiwa Spika,Kumekuwa na upotoshaji
mkubwa wa utetezi wa haki za wasanii kwa kuwa wanaotuhumiwa kunyonya haki za
wasanii wameweza kutajirika na kuneemeka kwa kupitia jasho na mgongo wa
wasanii. Hawa hawa wanaotuhumiwa kuhujumu wasanii ndio wanatumia nafasi yao
kuupotosha ukweli wa tuhuma dhidi yao. Wanatumia fedha na rasilimali walizo
nazo katika kunyanyasa wasanii, kuwakandamiza, kuwapokonya haki zao na
kuwadhalilisha kuwa bila wao, wasanii wasingekua kitu.
Mheshimiwa Spika, Leo hii wasanii wanaishi
kwenye hali ngumu, umasikini mkubwa lakini bado wanatolewa maneno ya kashfa na
dharau na Serikali imeendelea kukaa kimya. Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni,
inaitaka Serikali kuacha siasa kwenye kutatua migogoro ya taifa hili. Siasa
zimetumika sana katika kuzima jitihada za wanyonge kwenye taifa hili, leo hii
wananchi hawana imani na Serikali kwa kuwa imeonesha wazi imeshindwa! Kushindwa
kwa Serikali katika kutatua migogoro ya wasanii kwa kutotekeleza makubaliano
mbalimbali yanayoafikiwa kati yake na wasanii, yameshusha hadhi yake kwa
wasanii. Swali kubwa kwa Serikali sikivu ya CCM, Je mnasubiri migogoro mingapi
ili mjue kuwa wasanii hawatendewi haki? Je mnasubiri vikao vingapi vya
upatanishi na usuluhihishi ili mjue kuna tatizo? Ama mnataka wasanii wagombane,
wapigane, wauane ili mjue kuwa kuna tatizo?
Mheshimiwa Spika,Leo hii, Serikali bila ya
kukaa na wadau wa muziki wa dansi, taarabu, bongo fleva, hip hop, mnanda na
mahadhi mengine na kuwasikiliza kwa makini wamejikuta wanajihusisha na mambo ambayo
hawajui. Watendaji wa Serikali wameendelea kuwaingiza mkenge viongozi wa
Serikali katika masuala ya sanaa nchini. Hivi karibuni,hapa Dodoma, bila ya
kuwa na taarifa muhimu juu ya unyonyaji wa haki za wasanii, waziri Mkuu Mh.
Mizengo Pinda, alishiriki katika tamasha la kudai haki za wasanii ambalo
liliandaliwa na baadhi ya watu ambao kwa muda mrefu wamekua wakituhumiwa kuwa
ni wanyonyaji wa kazi za wasanii. Kiongozi mkuu wa Serikali, unashiriki katika
kupiga mihuri na kuhalalisha mikakati ya kimafia ya kuua umoja wa wasanii bila
ya kuwa na taarifa sahihi. Je, waziri mkuu ana taarifa kuwa walioandaa tamasha
la kudai haki za wasanii ndio walalamikiwa namba moja nchini dhidi ya haki za
wasanii hasa wa muziki? Tuinataka Serikali na wanasiasa wote kuacha kutumia
wasanii kwa faida zao binafsi bali wasaidie kutatua matatizo halisi ya wasanii
ili waondokane na umasikini.
8.0 UTAMADUNI NA MALIKALE NCHINI
Mheshimiwa Spika, zipo njia mbalimbali ambazo
zinatambulisha utamaduni wa mtanzania kwa mataifa mengine. Utamaduni wetu
unatambuliwa kwa kupitia lugha, mavazi, vyakula, sanaa, maadili na malikale za
taifa letu. Leo hii ukiangalia makumbusho ya taifa, haina vitu vya msingi vya
kufanya makumbusho kuwa chanzo cha kuliingizia taifa fedha za kigeni kwa njia
ya utalii. Sehemu nyingi nchini ambazo zinaelezea utamaduni wetu na asili ya
taifa letu, kama Bagamoyo, Kilwa Masoko, Kilwa Kivinje, Isimila, Zanzibar
haziwekwi katika mazingira ya kuyatunza kwa ajili ya kuelezea asili ya taifa
letu.
Leo hii , Serikali ya CCM ikijitetea kuhusu kuboresha ama
kutunza malikale za taifa letu ikiwemo majengo ya kale, itajigamba kuwa
imeyapaka rangi. Lakini ni maajabu kuona majengo yale, yamepakwa rangi nyeupe,
chokaa hali inayoyafanya majengo haya kuwa na rangi za kijani zenye ukungu
inapokuja suala la ukarabati wake. Ukiangalia marekebisho ya majengo hayo,
yamefanyika na kuondoa uasilia wa majengo hayo kama yalivyokua zamani,.
Kambi rasmi ya Upinzani, inaiuliza Serikali
je,imeshindwa kutafuta wataalamu wa majengo wenye kuweza kurekebisha na
kuyatunza majengo katika hali ilokuwa bila ya kuyaharibu zaidi? Ni mikakati ipi
ambayo Serikali imejiwekea kwa mwaka huu wa fedha wa 2013/2014 katika kuyatunza
na kuyatengeneza majengo ya kale ili kutunza utamaduni wa taifa letu?
10.0 UCHONGAJI WA VINYAGO NA THAMANI YAKE KWA TAIFA
Mheshimiwa Spika,Kama kawaida Serikali ya CCM
imeendelea kutawala huku kukiwa hakuna utaratibu mzuri wa kusimamia maslahi ya
wachongaji wa vinyago hapa nchini. Wachongaji wa vinyago ambao wamesaidia kwa
kiasi kikubwa kutangaza utamaduni wa taifa letu kwa kutumia kazi zao za sanaa
hapa nchini hasa katika kutangaza utalii.
Kwa taarifa tulizonazo kutoka kwa wachongaji vinyago ni
malalamiko ya kazi zao za sanaa kununuliwa na kisha kusafirishwa kuelekea nchi
za nje ambapo huko hupigwa mihuri kuwa imetoka katika nchi za jirani. Hii imeua
soko la vinyago hapo nchini na kukandamiza maslahi ya wachongaji hawa ambao ni
hazina kwa taifa letu. Wachongaji vinyago wana umuhimu mkubwa katika kulinda
utamaduni wa nchi yetu kwa kuwa ni urithi tuliopewa na ni lazima Serikali iweke
mikakati ya kuhakikisha kuwa soko la vinyago ndani na nje ya nchi linamufaisha
mchongaji kimapato.
Kambi rasmi ya upinzani bungeni,
inaitaka Serikali kutoa kauli hapa bungeni ina mkakati gani uliowekwa kwa mwaka
huu wa fedha katika kuhakikisha kuwa wachongaji vinyago wananufaika kwa kazi
zao hasa ukizingatia kuwa, soko la ndani la vinyago halina faida ya kutosha na
usimamizi wa kina. Vinyago ambavyo vinachongwa Tanzania vimeendelea kuuzwa nje
ya nchi na kuzipatia nchi hizo mapato makubwa na baadhi ya kazi hizo
hazitambuliwi kuwa zinatoka nchini.
11.0 USIMAMIZI WA HAKI ZA WASANII KATIKA UUZAJI WA MIITO YA SIMU
Mheshimiwa Spika,Biashara ya miito ya simu,
inayofanywa na makampuni ya simu nchini ni biashara ya siri ya kimafia
inayohitaji kuwekwa wazi kwani kuna ukwepaji mkubwa wa kodi na haki za wasanii,
ambapo pamoja na waliojiunga kihalali kutopata haki yao wako wale wanaokuta
nyimbo zao zinatumika bila kujua zimepelekwa huko na nani na kwa mikataba ipi.
Leo vyombo vyote vya Serikali vinavyotakiwa kusimamia sheria na kanuni za
hakimiliki zinakaa kimya huku wasanii wakipokwa haki zao, taifa likipoteza
mapato na kuubariki wizi huu wazi wazi.
Mheshimiwa Spika,Hivi karibuni tumeshuhudia
Serikali ya CCM kupitia wizara yake yenye dhamana ya kufuatilia biashara ya
miito ya simu, wizara ya mawasiliano, sayansi na teknolojia imeshindwa kutoa
majibu ya ufuatiliaji wa tozo na mapato ya miito ya simu, Mmeshindwa kutimiza
wajibu wenu kwa wananchi lakini pia mmeshindwa kutimiza wajibu wenu katika
kutekeleza matakwa ya katiba ya nchi hii, kuulinda uhuru na haki za wananchi
wake kama ambavyo muasisi wa taifa hili alijitahidi kufanya.
12.0 TASNIA YA FILAMU NA MCHANGO WAKE KATIKA KUKUZA UCHUMI
NCHINI
Mheshimiwa Spika,Tasnia ya filamu nchini
imeendelea kukua kila siku huku kukiwa na usimamizi mdogo wa Serikali katika
kuhakikisha kuwa sekta hii inatumika vizuri kama chanzo cha kukuza ajira nchini
lakini pia kama moja ya njia ya kuwaongezea wananchi kipato na Serikali kukuza
uchumi kwa kupitia kodi mbalimbali. Leo hii, soko la filamu nchini Nigeria
limeweza kuingiza takribani kiasi cha dola 250 milioni kwa mwaka kama mapato ya
filamu zinazotengenezwa kwa soko lao la Nollywood, je Serikali kupitia wizara
hii imefanya tathmini gani kwa kupitia mamlaka za mapato na kujua soko la
filamu kwa mwaka linaingiza kiasi gani hapa nchini? Kambi rasmi ya Upinzani,
inaitaka Serikali ya CCM kuacha kufanya kazi kwa mazoea sasa na badala yake
ivisimamie vyombo husika kuhakikisha kuwa sekta ya filamu inapewa kipaumbele
pia na thamani ili kuweza kukusanya kodi na kupunguza umasikini nchini. Tasnia
ya filamu si tu inaweza kuliingizia soko hili fedha bali pia ikipewa thamani
inauwezo mkubwa kwa kutatua tatizo la ajira hapa nchini. Kwa kuwa mpaka sasa,
Tanzania imeshatoa filamu nyingi na soko lake kupanuka katika nchi za Afrika
Mashariki na kati, je tasnia hii mpaka sasa imeweza kuzalisha ajira ngapi?
Kambi rasmi ya upinzani, inaitaka wizara kuja na takwimu rasmi za ajira
zilizotokana na tasnia hii kufikia mwezi Machi mwaka huu.
Mheshimiwa Spika,Tanzania ambayo imebarikiwa
kwa kuwa na vivutio mbalimbali vya utalii, ikiwemo Mlima Kilimanjaro, mbuga za
wanyama za Serengeti, Ngorongoro, Manyara, Mikumi pamoja na hifadhi za wanyama
kama Selous, Tarangire, maziwa makubwa ya Victoria, Tanganyika na Nyasa, sehemu
zenye asili ya utumwa kama Bagamoyo, Zanzibar, Kilwa Masoko, misitu mikubwa,
mito na vivutio mbalimbali; ina nafasi kubwa ya kutumika kama moja ya 'film
destinations' duniani kama ambavyo nchi nyengine imewekeza.
Mheshimiwa Spika,Nchi mbalimbali zimeweza
kujiingizia fedha za kigeni kila mwaka kutokana na kutumia vivutio walivyo
navyo na mandhari ya nchi zao kupitia tasnia ya filamu. Nchini Afrika Kusini,
tasnia ya filamu ina thamani ya kiasi cha takribani randi 12 bilioni sawa na
shilingi trilioni 2.17 za kitanzania huku ikichangia kiasi cha shilingi 1.4
bilioni kwenye uchumi wa taifa na ongezeko la kiasi cha shilingi milioni 400
kwa mwaka katika kipindi cha miaka minne toka mwaka 2008 walipoamua kufanya
mabadiliko ya tasnia ya filamu. Zaidi , tasnia ya filamu imeweza kuongeza soko
la ajira kwa kutoa karibu ajira 30,000.[1]Afrika kusini imeweza
kutumia sekta hii kwa kwa kutumia mandhari waliyo nayo ambayo inafanana na
mandhari za takribani nchi 57 ulimwenguni na kutumika kutengeneza filamu zenye
mafanikio Hollywood. Ipo haja ya wizara hii kwa kushirikiana na wizara ya
maliasili na utalii kufanya tathmini ya kina na kutengeneza mazingira ya
kutumia vivutio tulivyo navyo ili kuifanya Tanzania sehemu bora zaidi Afrika
kwa ajili ya kutengeneza filamu kwa kupitia mandhari zake. Lazima Serikali
itengeneze mkakati endelevu wa kuendeleza sekta ya filamu nchini kwa kuitangaza
Tanzania katika anga za kimataifa kama 'film destination' bora zaidi Afrika.
13.0 MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI 2013/2014
Mheshimiwa Spika, katika makadirio ya mapato
na matumizi ya wizara hii kwa mwaka wa fedha 2013/14, jumla ya shilingi 21,
328,045,000, zimeombwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida na miradi ya maendeleo. Aidha, kama ilivyo ada ya miaka yote kwa bajeti za serikali hii
ya CCM, katika wizara zote, fedha za matumizi ya kawaida ni nyingi kuliko fedha
ambazo zinatarajiwa kutumika katika miradi ya maendeleo.
Mheshimiwa Spika, Suala linaloweza kumuumiza
mdau yeyote ambaye angependa kuona wizara hii ikisonga mbele ni pale ambapo
miradi ya maendeleo imetengewa sh. 600,000,000 pekee, wakati kuna kiasi cha
takriban bilioni 10 zimetengwa kwa ajili ya kitu kinachoitwa ‘matumizi
mengineyo’.
Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni,
inahoji hayo matumizi mengineyo yasiyojulikana au kuelezwa hapa mbele ya bunge
lako lakini yanatengewa karibu nusu yote ya bajeti ya matumizi ya kawaida, ni
nini na yapi?
Mheshimiwa Spika, Baada ya kusema hayo kwa
niaba ya Kambi Rasmi ya Upinzani, naomba kuwasilisha.
.............................. .........
Joseph Osmund Mbilinyi (Mb)
Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani-Wizara ya Habari,Vijana,
Utamaduni na Michezo.
20.05.2013
No comments:
Post a Comment