Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora

Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora
----------------------WE THANK AND APPRECIATE YOU FOR VISITING CHADEMA DIASPORA BLOG. AGAIN, THANK YOU!-----------------------

Friday, May 24, 2013

Mtwara hakieleweki


WAKATI leo Bunge likitarajia kuendelea na majadiliano ya hotuba ya bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka 2013/2014 hali ya mambo bado si shwari mkoani Mtwara. Wakazi wa mkoa huo siku chache zilizopita waliamua kufanya vurugu kubwa kupinga hatua ya serikali kujenga bomba la gesi kutoka Mtwara kwenda Dar es Salaam. Vurugu hizo zilisababisha vifo vya watu wawili kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara, Linus Sinzumwa ambaye hata hivyo aliwataka wananchi warejee kwenye shughuli zao za kila siku. Tanzania Daima limedokezwa kuwa hofu imetawala katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo hasa baada ya kusikia bajeti ya Nishati na Madini itaendelea leo baada ya Bunge kuiahirisha kwa kile kilichoelezwa kusubiri amani na utulivu vitawale kwenye mkoa huo.

Hofu hiyo inachagizwa zaidi na uwepo wa vikosi vya Jeshi la Wananchi na polisi vikirandaranda ili kudhibiti vurugu zozote zinazoweza kutokea. Baadhi ya wananchi waliozungumza na Tanzania Daima, walisema wamekuwa wakiishi kwa shaka kubwa huku wenzao wakikimbia maeneo yao kukwepa vitendo vya kihalifu wanavyofanyiwa na polisi. Wananchi hao wamewalaumu polisi kwa kutumia nguvu nyingi pamoja na kujihusisha katika uhalifu badala ya kulinda usalama na mali za raia. Shutuma hizo zimetolewa na baadhi ya wananchi waliozungumza na Tanzania Daima, juu ya vitendo vya wizi wa mali madukani, kuchoma nyumba, kuua na kudhalilisha wanawake kijinsia walivyodai vinafanywa na askari waliopelekwa mkoani humo kudhibiti vurugu.

Walibainisha kuwa polisi wamekuwa wakishiriki kwenye vitendo vya kihalifu bila kuchukuliwa hatua, huku viongozi wa juu wakitoa taarifa zisizo sahihi kuhusu vifo vilivyotokea. Mkazi wa Mikindani, Saidi Kajuba alisema alishuhudia ndugu yake Musa Mohamedi akipigwa risasi na polisi waliokuwa kwenye zoezi la kudhibiti vurugu, lakini alishangazwa kusikia ni watu wawili ndio waliopoteza maisha katika vurugu hizo. Mkazi mwingine aliyeogopa kutaja jina lake, alisema kuna watu wawili wameuawa Magomeni-Likombe karibu na eneo la kiwanda cha Olam. Mariamu Abdallah alibainisha kuwa polisi walichoma nyumba yake na hivi sasa yeye na wanawe wanaishi maisha magumu. Aliongeza kuwa baadhi ya wenzao waliamua kukimbilia porini kukwepa shuruba kutoka kwa askari waliopelekwa mkoani humo kutuliza ghasia.


Tanzania Daima liliwasiliana na watu waliojificha porini kukwepa polisi na wanajeshi waliokuwa wakikamata na kupiga raia bila kujali ushiriki wao kwenye vurugu hizo. Baadhi ya watu waliojificha katika pori la Kijiji cha Msakala, Kata ya Ziwani walikuwa ni Amasha Selemani (10), Lukmani Hussein (5), Ashura Ally 18, mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Ziwani, Ziada Hamisi (16), mwanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Ziwani, na mtoto wa miezi miwili Hidaya Saidi aliyekuwa na mama yake. Wengine waliojificha ni Hidaya Abdallah (10), Mohamedi Said (12), Mzee Makokeni (65), Amina Namangwau (55) wote wakazi wa Kata ya Ziwani na Sharifa Dadi (45). Kamanda Sinzumwa alisema hana taarifa za askari kuhusika na uhalifu, lakini atazifanyia kazi na atakayebainika atachukuliwa hatua za kisheria.

Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali James Simbakalia alisema eneo la Mikindani ndilo limeathirika zaidi na vurugu zilizofanywa na watu waliopinga ujenzi wa bomba la gesi kutoka Mtwara kwenda Dar es Salaam. Aliongeza kuwa vitendo vya vurugu ni hujuma zilizofanywa na watu wasioutakia mema mkoa huo ambapo pia walitoa vitisho kwa wananchi. Alisema watu hao wameeneza hofu miongoni mwa wananchi na kusababisha washindwe kufanya shughuli za kawaida zinazowasaidia kujikimu kimaisha. “Napenda kuwatangazia wananchi wote kwamba serikali imekwishakuchukua hatua madhubuti za kuhakikisha ulinzi na usalama wa raia na mali zao… kwani vyombo vya ulinzi na usalama viko timamu na imara kukabiliana hali yoyote itakayojitokeza,” alisema.

Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai  Nahodha jana aliwasili mkoani Mtwara kuwapa pole wananchi, kufanya tathimini na kuona hali halisi iliyojitokeza katika vurugu hizo. Nahodha alisema kwa muijibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano  wa Tanzania wizara yake ina mamlaka ya kulinda maadui wa ndani na nje ya nchi ili amani na usalama wa wananchi uwepo. Aliongeza kwa kusema kuwa jeshi  limepoteza wanajeshi wanne na wengine kujeruhiwa ambapo kati yao wawii hali zao bado ni tete, wanahitaji uangalizi mkubwa ambapo alisema wangesafirishwa kwenda jijini Dar es Salaam katika hospitali ya jeshi kwa matibabu zaidi.

CUF yalia na ahadi za CCM

Chama cha Wananchi (CUF) kimesema kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimepoteza dira kutokana na ahadi wanazozitoa kushindwa kutekeleza na badala yake wanataka kuwagawa Watanzania. Akizungumza na waandishi wa habari jana Mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Ibrahimu Lipumba alisema kuwa kupoteza dira kwa CCM kumejionesha katika vurugu za wananchi Mtwara wanaotaka kupata haki yao ya gesi.Lipumba alisema kuwa wananchi wa Mtwara waliahdiwa kupelekekewa miradi mingi ya maendeleo lakini hakuna hata mmoja uliotekelezeka hivyo kuwafanya wakose imani na serikali yao.

Alisema sh milioni 540  kwa ajili ya kujenga kituo cha umeme wa megawati 300 upo katika mpango wa serikali, lakini kwenye bajeti ya Wizara ya Nishati  ya mwaka wa fedha 2013/2014 haipo jambo linalowafanya wananchi wa Mtwara wanaona kiini macho wanachofanyiwa. Lipumba alisema kuwa CCM ndio ilikuwa kinara katika kuwa na wapiga kura wengi katika mikoa ya Kusini, lakini katika mambo ambayo wanawafanyia wananchi wamekosa sifa tena ndio maana wameamua kutaka haki yao ya gesi. Alisema kuwa Serikali ya CCM ndiyo inataka kuwagawa wananchi wa Mtwara, juu ya kutaka gesi yao iwanufaishe hilo sio la msingi kwani watu wengine watakwenda kutafuta ajira na hakuna mtu ambaye atawazuia.

Lipumba alisema kuwa wanasiasa katika suala gesi hawahusiki ila serikali inatafuta mchawi katika kujinasua katika suala hilo ambalo wamesababisha kufikia hatua ya vurugu na kupoteza watu maisha. Taarifa hii imeandaliwa na Fatuma Mnyeto (Mtwara) na Josephat Isango, na Chalila Chibuda (Dar)

Source: Tanzania Daima (May 2013). Mtwara hakieleweki. Retrieved from Tanzania Daima

No comments: