MAONI NA MAPENDEKEZO YA CHAMA CHA
DEMOKRASIA NA MAENDELEO (CHADEMA) JUU YA RASIMU MUONGOZO ULIOTOLEWA NA TUME YA
MABADILIKO YA KATIBA KUHUSU MABARAZA YA KATIBA YA ASASI, TAASISI NA MAKUNDI
YENYE MALENGO YANAYOFANANA.
1.0. UTANGULIZI
Sheria ya Mabadiliko ya Katiba Sura
ya 83 (kifungu cha 18 (3)) imetoa wajibu kwa tume wa kuunda Mabaraza ya Katiba
kwa ajili ya kupitia na kutoa maoni juu ya Rasimu ya Katiba iliyoandaliwa na
Tume. Kifungu cha 17 (8) kinaeleza kuwa,
isipokuwa kama mazingira yatahitaji vinginevyo, Tume itabuni utaratibu
unaofanana ambao utatumika kila upande wa Muungano.
Kifungu cha 18 (6) kinaeleza aina
nyingine ya Mabaraza ya Katiba kwa kueleza kuwa Tume inaweza kuruhusu Asasi,
Taasisi au Makundi ya Watu kuwasilisha maoni yao kuhusu Rasimu ya Katiba. Ikumbukwe kwamba Kamati Maalum ya
CHADEMA ilikutana na Tume ya Mabadiliko ya Katiba tarehe 7 Januari 2013
kuwasilisha maoni ya CHADEMA kuhusu katiba mpya kama ilivyoalikwa lakini pia
kutumia fursa hiyo kuwasilisha mapendekezo ya CHADEMA kuhusu marekebisho na
maboresho yanayohitajika kuhusu mchakato wa mabadiliko ya katiba ili kupata
katiba bora.
Tarehe 31 Januari 2013 Tume ya
Mabadiliko ya Katiba ilitoa taarifa kwamba imeamua kuwa Mabaraza ya Katiba
yatakuwa katika makundi mawili yafuatayo: Mabaraza ambayo Tume itayasimamia na
kukusanya Maoni (Mabaraza ya Katiba ya Wilaya – Ngazi ya Mamlaka ya Serikali za
Mitaa) na Mabaraza ambayo Tume haitayasimamia. Mabaraza hayo yatajisimamia
yenyewe na kukusanya maoni yatakayowasilishwa kwenye Tume kwa mujibu wa
maelekezo. (Mabaraza ya Katiba ya Asasi, Taasisi na Makundi ya Watu).
CHADEMA baada ya kupitia muongozo huo
na kwa kuzingatia kuwa tayari tume ilishafanya uamuzi kuwa mabaraza ya katiba
yatakuwa ya wilaya, tarehe 14 Februari 2013 kiliwasilisha maoni na mapendekezo
yake kuhusu uteuzi wa wajumbe ambayo kwa sehemu kubwa hayakuzingatiwa na Tume
ya Mabadiliko ya Katiba na hivyo kusababisha matatizo makubwa katika mchakato
mzima wa uteuzi wa mabaraza ya katiba ya wilaya.
Kufuatia hali hiyo katika Maoni ya
Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kuhusu hoja ya Ofisi ya Waziri
Mkuu, tulitangaza kwamba CHADEMA itajitoa ushiriki wake katika mchakato wa
Katiba Mpya endapo mambo yafuatayo hayatapatiwa ufumbuzi hadi kufikia tarehe 30
Aprili, 2013:
“Mosi; Kufutwa kwa uchaguzi wa
wajumbe wa mabaraza ya wilaya ya Katiba uliofanywa na Kamati za Maendeleo za
Kata, na badala yake wajumbe wa mabaraza ya katiba ya wilaya wachaguliwe moja
kwa moja na wananchi wa Kata husika bila kuchujwa na WDC;
Pili: Serikali ilete mbele ya Bunge
hili tukufu Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba
yatayofanyia maeneo yafuatayo marekebisho.”
2.0 MAONI NA MAPENDEKEZO KUHUSU
MWONGOZO WA MABARAZA YA ASASI, TAASISI NA MAKUNDI YENYE MALENGO YANAYOFANANA:
Bila kujali upungufu uliokuwepo
katika uteuzi wa mabaraza ya katiba ya wilaya, Tume ya Mabadiliko ya Katiba
imetoa rasimu ya Mwongozo kuhusu Mabaraza ya Katiba ya Asasi, Taasisi na
Makundi yenye malengo yanayofanana; hivyo, CHADEMA kinatoa maoni kuhusu rasimu
hiyo kama ifuatavyo:
1. Uendeshaji (2.2) ; makundi
yaliyotajwa ni yale yanayoanzia chini mpaka taifa na taifa: wakati ambapo kuna
makundi ya ngazi ya chini pekee mathalani taasisi za jumuiya (CBOs), au taasisi
iliyosajiliwa kwenye ngazi ya wilaya au hata mitandao ambayo haijasajiliwa,
hivyo wigo upanuliwe kuruhusu makundi yote.
2. Utaratibu wa kutambua makundi
(3.0); kipengele cha kutaka kuwasilishwe ‘taarifa ya kusudio’ kiondolewe,
kinaongeza urasimu hasa kwa kuzingatia kwamba taarifa hizo zinawasilishwa tume
makao makuu. Tume ikishatoa muongozo maana yake ni kwamba tayari imefungua
mlango kwa makundi kujadili rasimu, hivyo ngazi pekee itayobaki iwe ni 4.0 ya
kuwasilisha maoni. Hatua hii itachelewesha makundi ya kijamii kutumia haki na
uhuru wako wa kikatiba wa kujumuika na kuwasilisha maoni.
3. Utaratibu wa kuwasilisha (4.0),
maneno “Tarehe zitazoelekezwa na tume ya mabadiliko ya katiba” katika sentensi
ya kwanza, kwa sababu inaweza kuleta tafsiri ya kwamba tume itayapangia tarehe
za kukutana mabaraza hayo ya makundi ya kijamii ambayo kimsingi ni kuyaingilia.
Tume ipange tu tarehe ya mwanzo wa kupokea maoni na mwisho wa kupokea maoni kwa
awamu ya mabaraza. Tarehe ya kuanza uendeshaji imeshatajwa kwenye 2.2 “wakati
wowote kuanzia tarehe itayotangazwa na tume”, tarehe ya mwisho wa kuwasilisha
maoni imewekewa utaratibu kwenye 4.0 “ maoni yatawasilishwa kwa tarehe
zitazoelekezwa na Tume”; hivyo sentensi hiyo ya kwanza haina haja ya kuwepo.
4. Uzito wa maoni (6.0), maelezo ya
kwamba ‘maoni yatakuwa na uzito ulio sawa’, yanapaswa kufafanuliwa; kwa mantiki
ya sentensi hii ni kwamba makundi yenye malengo yanayofanana hata yawe mengi
kiasi gani yatakuwa na uzito sawa na mabaraza yatayosimamiwa na tume ambayo
tayari yameshalalamikiwa kwamba yana hodhi ya chama kimoja na hayana uwakilishi
wa moja kwa moja wa wananchi. Hivyo, tafsiri itolewe ambayo itahakikisha kwamba
maoni ya wengi na matakwa ya umma yatatamalaki.
5. Tume kualikwa kusikiliza; Pamoja
na kwa mujibu wa kipengele 2.2 mabaraza ya makundi yenye malengo yanayofanana
‘yatajisimamia na kujiendesha yenyewe’, pawepo na kipengele kwamba iwapo asasi,
taasisi au kundi husika linaweza kuomba tume itume maafisa wake
kuangalia/kusikiliza moja kwa moja ziada/zaidi ya utaratibu uliotajwa kwenye
4.0
3.0 MAONI NA MAPENDEKEZO JUU YA
MASUALA MENGINE KUHUSU UENDESHAJI WA MABARAZA NA UTOAJI MAONI JUU YA RASIMU:
Aidha, pamoja na maoni kuhusu
muongozo; CHADEMA kinatoa maoni ya ziada kwa Tume kuzingatia yafuatayo:
• Muongozo wa kwanza uliotolewa na
Tume ya Mabadiliko ya Katiba ulihusu “Muundo, utaratibu wa kuwapata wajumbe wa
mabaraza ya katiba ya wilaya (Mamlaka za Serikali za Mitaa) na uendeshaji
wake”. Hata hivyo, muongozo uliotolewa ulijikita katika muundo wa mabaraza na
mchakato wa uteuzi wa wajumbe wa mabaraza hayo, lakini haujatoa maelezo na
maelekezo ya kutosha kuhusu namna mikutano ya mabaraza ya katiba ya wilaya
itavyoendeshwa na utaratibu mzima utakaotumika kujadili rasimu ya katiba mpya
katika mabaraza hayo. Aidha, CHADEMA kinapendekeza kwa mara nyingine kwamba
tume itoe muongozo mwingine mahususi kuhusu uendeshaji wa mabaraza ya katiba
ikiwemo utaratibu utakaotumika wakati wa kujadili rasimu katika mabaraza; aidha
kabla ya muongozo huo kuanza kutumika wananchi wapewe nafasi ya kutoa maoni na
mapendekezo kama ilivyokuwa kwa muongozo huu kuhusu uteuzi wa wajumbe.
• Kwa kuwa mpaka awamu ya nne ya
ukusanyaji maoni ya wananchi binafsi ilipokamilika wananchi waliotoa maoni kwa
njia ya simu walikuwa 16,261 tu kati ya idadi ya wateja wa makampuni ya simu za
mkononi ambao watajwa kuwa zaidi ya milioni 20 (mobile phone subscribers); Tume
ya Mabadiliko ya Katiba iweke mfumo wa wananchi binafsi kuweza kutoa maoni
kuhusu rasimu ya katiba kupitia simu za mkononi. CHADEMA kinarudia kutoa mwito
kwa tume kushirikiana na makampuni ya simu kuwezesha ujumbe wa simu ya mkononi
kutumwa kwenye kila mtanzania mwenye simu kumpa dondoo juu ya rasimu ya katiba
na kumpa namba anazoweza kutuma maoni kwa njia ya simu na pia maelekezo ya
namna ya kutuma ujumbe wa bure wa maoni yake. Hii itafanya wananchi wengi
kuweza kushiriki kutoa maoni. Aidha, pawepo na uwazi katika mfumo mzima wa
maoni yanayokusanywa kwa njia ya simu na mitandao mingine ili kusiwe na
uwezekano wa ‘kuchakachua’.
4.0 HITIMISHO:
Pamoja na kuwasilisha maoni na
mapendekezo haya izingatiwe kuwa madai ya Kambi ya Upinzani inayoongozwa na
CHADEMA kuhusu kufutwa kwa chaguzi za mabaraza na kuwasilishwa bungeni kwa
muswada wa sheria ya marekebisho ya sheria ya mabadiliko ya katiba katika
mkutano wa kumi na moja wa Bunge unaoendelea hayajatimizwa. Waziri Mkuu aliahidi (wakati wa
kuhitimisha hoja ya Ofisi ya Waziri ) kwamba Serikali italeta Muswada wa
Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba kabla ya mwisho wa Mkutano huu wa
Bajeti.
CHADEMA kinasubiri ahadi hiyo
kutekelezwa katika kipindi hiki ambacho kitaenda sambamba na Tume kutoa Rasimu
ya Kwanza ya Katiba Mpya kwa ajili ya kuanza kujadiliwa na Watanzania. Endapo hadi kufikia mwisho wa kipindi
hicho Serikali itakuwa haijaleta Muswada wa marekebisho yanayotakiwa; au endapo
Muswada utakaoletwa hautakidhi matakwa ya kuboresha mchakato wa upatikanaji wa
Katiba Mpya; basi CHADEMA itawaalika wanachama, wafuasi na mashabiki wake
Tanzania nzima, pamoja na taasisi za kiraia na za kidini, vyama vya siasa na
Watanzania wote wenye nia njema na taifa hili kuhamasisha umma kuikataa Rasimu
ya Katiba Mpya kwenye kura ya maoni itakayofanyika kwa ajili ya kuihalalisha
Katiba hiyo mbovu.
Naomba kuwasilisha,
John Mnyika (Mb)
Kny. Katibu Mkuu
19/05/2013
No comments:
Post a Comment