AMTAKA AELEZE TRILIONI 1.7/- ZILIVYOTUMIKA, LEMA AWASHA MOTO
WAKATI
serikali ikishindwa kutoa maelezo ya namna fedha zilizotolewa na serikali na
kuidhinishwa na Bunge kwa ajili ya kuhuisha uchumi (Stimulus Package) sh
trilioni 1.7 zilivyotumika, Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa amefufua
kadhia hiyo, sasa akimtaka Rais Jakaya Kikwete kuwaeleza Watanzania fedha hizo
ziko wapi. Akizungumza
katika mkutano wa hadhara jana katika Kiwanja cha Kwaraa, Babati mjini katika
siku ya kwanza ya ziara yake kutembelea maeneo mbalimbali ya wilaya zote za
Mkoa wa Manyara, Dk. Slaa alisema serikali haijawahi kutoa majibu sahihi juu ya
namna fedha hizo za wananchi zilivyotumika. Alisema
taarifa kutoka ndani ya serikali zinadai kuwa fedha hizo ziliwanufaisha watu wa
karibu na Rais Kikwete. Slaa
alisema katika ukaguzi wa fedha za serikali, taarifa muhimu zilizotakiwa
zilifichwa, huku Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Serikali (CAG) akishindwa kupata
hesabu za matumizi ya sh bilioni 48 zilivyotumika.
Aliongeza
kuwa fedha hizo zingetumika kwa ajili ya manufaa ya Watanzania hasa kwa
kuwekeza katika kilimo, nchi ingeweza kuepukana na aibu ya kuwa ombaomba hadi
wa chakula kutoka nchi ndogo kama Thailand, Taiwan na Japan. “Wananchi
wa Babati nimezungumzia masuala ya kilimo hapa kwa sababu najua ninyi ni
wakulima na hata matatizo yenu mengi huku ni juu ya ardhi yenu ambayo imekuwa
ikiporwa au kuhodhiwa kinyemela, huku serikali ikiangalia tu. Wameendelea
kutudanganya kama ilivyo kawaida yao kwa muda mrefu sasa, wanadanganya wananchi
waliowapatia dhamana ya kuongoza. “Tunamtaka
Kikwete awaambie Watanzania fedha zetu trilioni 1.7 tulizopitisha pale bungeni
serikali yake ikisema kuwa ni kwa ajili ya kuwainua wakulima waliopata hasara
kutokana na anguko la uchumi, hivyo fedha hizo zilikusudiwa kufufua uchumi,
atuambie ziko wapi, zilitumikaje, akina nani walinufaika? Tunasema hivyo kwa
sababu taarifa za ndani tulizonazo ni kwamba walipewa maswahiba wa Kikwete.
“Mwaka
juzi, Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali au CAG kama anavyoitwa na
wengi, alibaini kuwepo kwa ubadhirifu mkubwa katika fedha hizo, kiasi kwamba
serikali ilikataa kumpatia taarifa kamili ya matumizi ya fedha hizo ili
azifanyie ukaguzi. Sasa tunamtaka Rais Kikwete maana yeye ndiye alipeleka
bajeti ile bungeni kupitia kwa Waziri wa Fedha, atuambie fedha zetu ziko wapi,”
alisema Dk. Slaa. Aliongeza
kusema kuwa fedha hizo zingewekezwa kwenye kilimo kupitia mipango mbalimbali
yenye nia ya kuwakomboa Watanzania asilimia 74 wanaotegemea sekta hiyo, huku
nchi pia ikitegemea kilimo kwa ajili ya uchumi wake, zingeweza kuwa mkombozi na
nchi ingepiga hatua kubwa. Dk. Slaa
ambaye leo anatarajiwa kufanya mikutano ya hadhara katika maeneo ya Balangida
na Gendabi, alisema ni aibu kwa nchi yenye utajiri kama Tanzania kuwa ombaomba
hadi wa chakula kutoka nchi za nje.
“Ndugu
zangu uhuru wetu kama nchi uko shakani mno, tunavyozungumza hapa tumefika
mahali tumekuwa ombaomba wa chakula kutoka nje ya nchi, tena kutoka katika nchi
ndogo ambazo hazina rasilimali kama hapa, nchi kama Japan, Thailand...“Naambiwa
wakubwa serikalini na washirika wao ndio wanaomiliki maduka makubwa yanayouza
chakula kama mchele, ndiyo maana hawataki kuwajali wakulima wetu hapa nchini,
badala yake wanatuletea vyakula kutoka Thailand ili wakulima wetu wafe, wao
wanufaike,” alisema. Dk. Slaa
alidai kuwa kutokana na wakubwa serikalini na watu aliowaita kuwa ni washirika
wao, kumiliki biashara kubwa za uagizaji wa chakula kama mchele na sukari
kutoka nje, yametengenezwa mazingira yanayowaathiri wakulima wa Tanzania na
wananchi kulazimika kulishwa vyakula visivyokuwa na ubora kutoka nje ya nchi
vinavyouzwa madukani. “Hata sasa
kuna chakula kibovu kimeingizwa huko Zanzibar, nasikia wanataka kukivusha bara
ili eti kiteketezwe, si ajabu wanatafuta njia ya kukiingiza sokoni kama ilivyo
kawaida yao, imefikia mahali watu hawa hawajali chochote kabisa kufanya ufisadi
hata unaohatarisha afya za wananchi,” aliongeza.
Utendaji
wa Bunge
Wakati
mjadala wa namna Bunge la Tanzania linavyotekeleza utendaji kazi wake mbele ya
macho ya Watanzania, hasa namna ambavyo linadaiwa kuwa mhuri wa kupitisha
kiulaini hoja za serikali ukizidi kupamba moto katika mijadala mbalimbali
nchini, Dk. Slaa amewapongeza wabunge wake, akisema sasa Bunge limefika patamu. Akiwapongeza
wabunge wake, kwamba wamekuwa wakisimama kidete ndani ya Bunge kuiwajibisha
serikali kwa niaba ya wananchi tofauti na wanavyofanya wabunge wa CCM walio
wengi bungeni, Dk. Slaa alisema kuwa ni unafiki kuzungumzia nidhamu bungeni,
wakati serikali inashindwa kusimamia nchi kwa niaba ya Watanzania na kuzuia
ufisadi. Dk. Slaa
aliwataka wabunge wake kuongeza kasi kwani waliyonayo sasa bado ni ndogo,
kulinganisha na matarajio ya Watanzania wengi aliosema wanataabika kwa kukosa
uongozi.
“Wakati
nikiwa bungeni, aliyekuwa Spika wa Bunge la Kenya wakati ule, nafikiri anaitwa
Kapalo... Francis Ole Kapalo kama sijakosea, alikuja bungeni wakati wa semina
moja hivi, akatuambia Tanzania bado haijawa na Bunge, alituambia kuwa ule
ulikuwa ni mkusanyiko tu wa mashehe na wachungaji wanaopiga mihuri hoja za
serikali. “Akasema
hadi siku atakaposikia ngumi zimerushwa bungeni, pale atakapoona wabunge wanachachamaa
dhidi ya serikali kwa niaba ya wananchi waliowatuma, bila kujali chochote
isipokuwa kuwa wawakilishi wa sauti za wasiokuwa na sauti, ndiyo ataamini
tumeanza kuwa na Bunge, nami nilikubaliana naye,” alisema Dk. Slaa.
CHADEMA
wazindua kampeni Arusha
Katika
hatua nyingine, CHADEMA imezindua kampeni zake jijini Arusha kwa ajili ya
uchaguzi wa madiwani wa kata nne; Elerai, Kaloleni, Themi na Kimandolu ambazo
madiwani wake walifukuzwa uanachama na chama hicho huku kikitamba kuwa hakina
uchaguzi Arusha ila CCM ndio wenye uchaguzi. “Arusha
CHADEMA hatuna uchaguzi, sisi tuna ushindi ila CCM ndio wana uchaguzi,” alisema
Godbless Lema, Mbunge wa Arusha Mjini aliyekuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa
kampeni hizo. Lema
alitumia muda mwingi kunadi sera za CHADEMA na kuongeza kuwa madiwani
waliofukuzwa ndani ya chama hicho, walipokea rushwa na katika kampeni zao
kwenye kila kata, watatoa ushahidi jinsi walivyopokea rushwa. Huku
akishangiliwa na wananchi wa Arusha, Lema alimuonya Mkuu wa Mkoa wa Arusha na
Mkuu wa Wilaya hiyo kujiepusha na kampeni na kutoa tahadhari kuwa wakibainika
wanafanya kampeni itakuwa ni makosa makubwa kwao.
Katika
kampeni hizo, Lema alirudia kauli yake kuwa mwasisi wa siasa za udini nchini ni
Rais Jakaya Kikwete na akaonya siasa zozote za ubaguzi wa kidini wala ukabila
huku akiwaasa watu wa Arusha kuonesha ukomavu na kuchana na ukabila. Lema pia
alisema anaendelea na msimamo wake wa kutomtambua Meya wa Jiji hilo, Gaudence
Lyimo hivyo anawaomba wana Arusha kumuunga mkono. Kwa mujibu
wa Lema, hayuko tayari kupeleka ushahidi bungeni kuonesha rais ni mdini na
ndiyo maana wanaogopa kumdai ushahidi huo. “Ushahidi
huo ninao tayari, upo mwingi ndiyo maana hawawezi kunilazimisha kuwasilisha,
mimi nataka kuwasilisha kwa uwazi, sipeleki ushahidi uchochoroni,” alisema Lema
huku akishangiliwa. CHADEMA
katika uchaguzi huo imewasimamisha Injinia Jeremiah Mpinga katika Kata ya
Elerai, Emanuel Kessy (Kaloleni), Melansi Kinabo (Themi) na Rayson Ngowi katika
Kata ya Kimandolu.
Uchaguzi
huo unafanyika baada ya kufukuzwa kwa aliyekuwa Naibu Meya na Diwani wa
Kimandolu, Estomih Mallah; Diwani wa Elerai, John Bayo ambaye kwa sasa
amesimama kugombea kwa tiketi ya CUF; aliyekuwa Diwani wa Themi, Reuben Ngowi;
aliyekuwa Diwani wa Kaloleni, Charles Mpanda na Diwani wa Viti Maalumu, Rehema
Mohamed.
Source; Isango J. (May 2013). Dk. Slaa ambana JK. retrieved from Tanzania Daima

No comments:
Post a Comment