MBUNGE wa
Meatu, Meshack Opulukwa (Chadema), amemtuhumu Waziri wa Maji, Profesa Jumanne
Maghembe, kwa kujitengea Sh bilioni 30 kwa ajili ya mradi wa maji katika wilaya
yake. Akiuliza swali bungeni jana, Opulukwa alisema fedha hizo zimetengwa mwaka
wa fedha 2013/14 na kutaka zigawanywe katika halmashauri zote. “Serikali
ina mkakati gani wa kuhakikisha inamega fedha hizo, hivyo badala ya kupelekwa
katika wilaya hiyo moja zigawanywe katika wilaya nyingine?” alihoji Mbunge
huyo.
Akijibu
swali hilo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais asiyekuwa na Wizara Maalum, Profesa
Mark Mwandosya, alisema hafahamu kama Wilaya ya Mwanga, imetengewa kiasi hicho
cha fedha, bali anaufahamu mradi wa maji Mwanga kwa kuwa aliuanzisha yeye
wakati akiwa Waziri wa Maji. “Wote tunafahamu matatizo ya maji katika miji
ya Mwanga, Same, Korogwa na Olkasment, tulipata fedha kutoka BADEA na Sekta ya
Mandeleo ya Maji, bahati nzuri Profesa Maghembe kawa Waziri wa Maji na kaukuta
mradi ulioanzishwa na mimi katika wilaya yake,” alisema Profesa Mwandosya.
Awali
akijibu swali la msingi la mbunge huyo, Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu,
Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Agrey Mwanry, alisema Serikali
inatambua tatizo la maji katika kata za Wilaya ya Meatu. Alisema katika
mwaka 2011/12, utekelezaji wa mradi wa maji umefanyika katika kijiji cha
Mwang’umbi kilichopo katika kata ya Ilamaseko.
Alisema
mwaka 2012/13, shughuli ya usanifu wa mradi mkubwa wa maji katika Kata ya
Bukundi Kijiji cha Bukundi, umeshafanyika na kukamilika na ujenzi wa
miundombinu utaanza katika mwaka wa fedha 2013/14. “Kupitia fedha za Mfuko
wa Kuchochea Maendeleo ya Jimbo la Meatu, Kijiji cha Mwanyahina kitapelekewa
maji kwa kuongeza vituo vya maji viwili.
“Serikali
itaendelea kuweka kipaumbele cha utekelezaji wa miradi ya maji katika maeneo
mengine yaliyobaki kadri fedha zitakavyopatikana,” alisema Mwanri. Katika
swali lake la msingi, Opulukwa alitaka kujua mpango wa Serikali wa kuwapatia
maji safi na salama wakazi wa Kata za Mwabuzo, Bukundi, Mwanjolo, Mwamishali,
Mwanyahima, Nkoma na Ilamalaseko.
Source: Sanja D. (April 2013). Waziri atuhumiwa kukwapua Sh bilioni 30.
Dododma. Retrieved from Mtanzania

No comments:
Post a Comment