Kazi ya Usalama wa Taifa ni nini (TISS)?
Waziri wa mahusiano Ikulu, Steven Wassira amefanya kazi
nzuri bila kujua. Ni wakati alipouliza, mjini Dodoma, “Kibanda ni nani” hadi
afanyiwe unyama kama aliofanyiwa.
1. Kauli ya Wassira imeonyesha kuwa KWELI Idara ya
Usalama wa Taifa "hushughulikia" watu fulani; jambo ambalo wamekuwa
na kigugumizi kusema. Sasa amelitoa. Ambalo hakusema ni kushughulikia namna
gani; lakini inaonyesha ni kama alivyofanyiwa Absalom Kibanda, mhariri mkuu wa
New Habari Corporation na mwenyekiti wa Jukwaa la Wahari – kupigwa, kung’olewa
meno, kucha, kutobolewa jicho…
2. Wassira amesema Idara ya Usalama wa Taifa inaweza
kushughulikia watu kama Dk. Slaa na Freeman Mbowe – viongozi wa Chama cha Demokrasia
na Maendeleo (Chadema). Hakueleza kwanini; lakini tunajua ni kwa kuwa wanataka
kushika madaraka – kuyatoa mikononi mwa CCM. Hili linazaa jambo lingine; kwamba
3. Sasa yeyote kati ya hao wawili atakayejikwaa, sharti
tumtafute Wassira. Yawezekana hili lilimtoka kwa bahati mbaya au alikuwa na
ghadhabu; lakini tayari tunalo. Kwamba hawa ndio lengo la idara ya usalama wa
taifa na si mwingine, angalau kwa sasa.
4. Lakini uwindaji haumo katika Chadema peke yao. Upo pia
ndani ya CCM. Tuweke masikio tayari kusikia ni akina nani ndani ya CCM ambao
wataelekezewa usalama wa taifa kwa kuwa hawako pamoja na mrengo mkuu. Chanzo
chetu, bila shaka, kitakuwa Wassira.
5. Sasa Kibanda ni nani? Anauliza. Tusimpe jibu. Tuseme tu
kwa sasa, kwamba, kama usalama wa taifa wana uwezo wa kushughulikia wakubwa,
sembuse wadogo kama Kibanda. Tumwachie Wassira kazi ya kumweka Kibanda pale
anapoweza kumweka au aulize usalama wa taifa ambao wanaweza kumwambia mara
moja.
6. Tusilokuwa na uhakika nalo ni kama Wassira alitumwa
kuweka hadharani kwamba Slaa na Mbowe wanaandaliwa "kitu" na usalama
wa taifa. Yawezekana amepayuka, jambo ambalo linaweza kumweka pabaya; au
kaagizwa na hivyo atapewa nishani kwa “ujasiri” wa kutoboa siri.
7. Tusubiri. Tutaona.
Source: Tegambwage N. (April 2013). Wasira katumwa au kapayuka?. retrieved from Ndimara blog

No comments:
Post a Comment