Waliokufa wafikia 31, JK atembelea majeruhi
WAKATI miili ya watu waliokufa kwa kuporomokewa na jengo la ghorofa jijini Dar es Salaam ikiongezeka na kufikia 31, Waziri wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta amesema matukio mengi mabaya kama hayo nchini yamekuwa yakisababishwa na mafisadi wasiojali maisha ya wengine. Sitta ambaye pia ni Spika mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano alitoa kauli hiyo Dar es Salaam jana, alipotembelea eneo la ajali kuwapa pole wafiwa waliopoteza ndugu zao, akisema kama sheria na kanuni za ujenzi zingezingatiwa tukio hilo lisingetokea. Alisema kinachosikitisha katika nchi hii ni kushuka kwa maadili, tukio alilodai kuwa limesababishwa na mafisadi wanaotamani faida kubwa kila kukicha bila ya kujali maisha ya watu wengine.
Sitta alifafanua kuwa ili kudhibiti matukio hayo ni lazima serikali ihakikishe inasimamia sheria na kanuni za ujenzi ili kuepuka nchi kuwa na majengo mabovu ambayo matokeo yake yanasababisha majanga. “Ni dhahiri kanuni katika ujenzi wa jengo hili hazikusimamiwa ipasvyo, hivyo ni wakati kwa serikali kufanya uchunguzi wake ili kuwabaini mafisadi wote waliosababisha tukio hili la kusikitisha,” alisema. Kwa mujibu wa Sitta, sekta zote nchini zinakabiliwa na mporomoko wa maadili kwa baadhi ya watendaji kujijengea ujasiri usiofuata sheria kwa kufanya kazi watakavyo. Alisema ili kumaliza vitendo hivyo viovu vinavyofanywa na baadhi ya watu wachache, Watanzania wanahitaji mjadala mpana ili kurudisha maadili yaliyotoweka katika jamii. “Siku hizi vitendo vya wizi vimekuwa vya kawaida kwa mfamo hivi sasa Tanzania ndiyo nchi inayoongoza Afrika Mashariki kwa wizi kwenye ATM, pia wengine wanaibiwa kwenye daladala mchana kweupe na hakuna anayejali.
“Tunahitaji mabadiliko ya fikra mpya ili tuweze kumaliza vitendo hivi vya kushuka maadili katika jamii yetu ya Kitanzania,” alisema Sitta. Naye Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadik alilitaka Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kusimamia shughuli zote za mazishi ya watu waliofariki katika tukio hilo kwa sababu vimesababishwa na mbia wao Raza Damji. Pia alilitaka shirika hilo kusimamisha mikataba ya nyumba tatu ambazo wapangaji wake wametakiwa kuhama ili kupisha uchunguzi wa kuzibaini kama ziko hatarini kutokana na mtikisiko uliotokana na kuporomoka jengo jirani. Alizitaja nyumba hizo kuwa ni zile zilizoko kwenye vitalu Na. 2083/73, 1210/73 na 1960/73. Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova alisema hadi sasa watu wanane wanashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa ajili ya uchunguzi wa kuporomoka kwa jengo hilo.
Watu hao ni Raza Damji, Ogare Salu, Goodluck Mbaga, Ally Damji, Ibrahim Kisoki na wengine. Aidha, amesema kuwa majeruhi waliobaki Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ni wanne baada ya wengine sita kuruhusiwa. Katika hatua nyingine, Rais Jakaya Kikwete aliwatembelea majeruhi wa ajali hiyo waliolazwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili ili kuwafariji.
Mbatia: Dar si salama
Mbunge wa kuteuliwa ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha NCCR-Mageuzi, James Mbatia, alibainisha kuwa jengo hilo lililoporomoka ni miongoni mwa majengo ambayo yanasubiri kuliangamiza Jiji la Dar es Salaam hasa Kariakoo. Mbatia ambaye pia ni mtaalamu wa kupambana na majanga, alisema majengo mengi yaliyopo katikati ya jiji hasa Kariakoo ni janga kubwa ambalo litapoteza watu wengi kama hatua za haraka hazitachukuliwa. “Katika Jiji la Dar es Salaam karibuni majengo yote makubwa yapo kwenye hatari ya kuleta majanga endapo ikitokea tetemeko kidogo tu, na itasababisha vilio,” alisema. Aliitaka serikali kuchukua hatua za kuwaondoa wananchi kwa muda na kuwahifadhi sehemu maalumu ili uchunguzi wa kina ufanyike kwa majengo yote kubaini yasiyokidhi viwango.
Mbatia pia alilishukia Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kuwa nalo libanwe kwa kushindwa kuchukua hatua za haraka ikiwemo kutokagua vifaa vinavyotumika kwenye majengo mengi. Alisema kitaaluma TBS inatakiwa kuchunguza bidhaa muhimu ikiwemo nondo na saruji ambazo nyingi zimekuwa zikitumika bila kukaguliwa na hata kusababisha majanga ya kujitakia kama hilo.
Soource: Tanzania Daima. (March 2013). Sitta: Ufisadi umeporomosha majengo. Retrieved from Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment