NAIBU Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Bara, Mwigulu Nchemba, juzi alilazimika kuwapigia magodi wanawake wa jamii ya Kimaasai akiwasihi wasimrudishie kadi ya chama hicho, walizokuwa wamezikusanya wakipinga hatua ya serikali kutaka kuwanyang’anya ardhi yao. Katika kutapatapa huko, Nchemba pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro, Elias Wawa Lali walibaini kuwepo kwa waandishi wa habari katika kikao hicho baada ya kumwona mwakilishi wa Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) Kanda ya Afrika Mashariki na Kati, Jason Paktin na hivyo kuwaamrisha polisi wamkamate.
Eneo la Loliondo limekuwa na mgogoro mkubwa wa ardhi ambapo wananchi wa jamii ya Kimaasai wanapinga mpango wa serikali kutwaa hekta 1,500 za mraba kutoka ardhi ya vijiji. Hatua hiyo inafuatia uamuzi wa serikali kupitia kwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Hamis Kagasheki kutangaza kutwaa hekta 1,500 kutoka hekta 4,000 za vijiji saba vilivyopo ndani ya eneo la pori tengefu la Loliondo. Uamuzi huo ulifanyika wakati vijiji hivyo vimesajiliwa na kupewa hati miliki inayozuia mtu au mamlaka yoyote kuingilia mipango na matumizi ya ardhi hiyo bila kwanza kushauriana na kukubaliana na vijiji husika. Mgogoro huo ulifikia hatua mbaya baada ya viongozi wote wa kuchaguliwa wa CCM kuanzia ngazi za vijiji, madiwani na mbunge wao Lekule Laizer kuachia ngazi endapo serikali itaendelea kushikilia msimamo wake.
Kufuatia hali hiyo, Katibu Mkuu wa CCM, Abdulraham Kinana aliunda tume ya kutafuta ufumbuzi ambayo inaongozwa na Nchemba ambaye alifuatana na viongozi wengine wa chama hicho Mkoa wa Arusha na Manyara. Akiwa katika eneo la Olorien Magaiduri juzi kwenye mkutano wa kuwaangukia kinamama hao wa Kimaasai ili wasirudishe kadi, Nchemba na viongozi wengine wakiwemo Laizer, Christopher ole Sendeka na Marry Chatanda walishtuka kuwaona wanahabari. “Baada ya Nchemba kubembeleza kwa takribani saa moja huku akiwaomba wampe siku saba awe amelifikisha kwa viongozi wa juu na kulipatia ufumbuzi, ghafla walimwona Paktin wa BBC na kumtilia shaka,” kilisema chanzo chetu.
Nchemba na Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro walianza kumhoji wakitaka kujua nani amemleta mkutanano hapo na kisha waliamriwa polisi wamkamate na kumpeleka kituoni Loliondo.
Wakati askari hao wakielekea Loliondo na Paktin ambaye amefanya utafiti wa mgogoro huo muda mrefu, aliwasiliana na rafiki yake kwa simu ili amtafutie wakili wake. Ndipo akaunganishwa na Lissu ambaye alimkataza asikubali kuhojiwa bila yeye kufika. Paktin aliwajulisha askari wale kuwa hatahojiwa hadi wakili wake afike kama baada ya dakika 15 zijazo. Lakini walitaka kumfahamu wakili wake ni nani.
“Baada ya kutajiwa jina la Lissu walihamaki na kuhoji tena… umesema nani? Akawajibu Lissu… ndipo ghafla wakamwachia mwandishi huyo wa kizungu bila masharti yoyote kabla ya kumfikisha kituoni kama walivyoamriwa,” aliongeza mtoa taarifa.
Hata hivyo baada ya mzungu huyo kufukuzwa mkutanoni, Nchemba na Wawa Lali waliendela kuwa na wasiwasi kuhusu uwepo wa waandishi wengine na katika kuangalia zaidi waliwabaini wengine kama sita wa vyombo tofauti ambao hata hivyo walikimbia na kutokomea porini kabla ya kukamatwa.
Lissu, Msigwa wanena
Lissu ambaye pia ni Mkurugenzi wa Sheria na Haki za Binadamu wa CHADEMA na Waziri Kivuli wa Maliasili na Utalii, Mchungaji Peter Msigwa waliwasili Loliondo tangu juzi kukutana na kuzungumza na waathirika wa mgogoro huo.
Lissu alihutubia mkutano mkubwa wa hadhara katika Kijiji cha Soitsambu juzi ambapo zaidi ya wana CCM 680 walihama na kujiunga CHADEMA. Katika hotuba yake, alisema kuwanyang’anya ardhi Wamaasai ni muendelezo wa dhuluma inayofanywa na serikali dhidi ya jamii hiyo tangu enzi ya ukoloni ambapo walifukuzwa kutoka eneo la hifadhi ya sasa ya Serengeti mwaka 1958/59.
Alisema baada ya uhuru, serikali iliendelea kutwaa ardhi za Wamaasai kwa kuanzisha hifadhi za taifa za Manyara, Tarangire na Arusha huku maeneo mengine katika wilaya za Simanjiro, Monduli, Kiteto na Longido yakigeuzwa mapori ya akiba. Lissu alisema kuwa hayo yamefanyika wakati uchumi wa jamii hiyo inayotegemea mifugo ukididimia kwa mifugo yao kufa kwa kukosa malisho na maji.
“Matukio haya yamewafanya Wamaasai ambao kihistoria ni wahifadhi wa mazingira na wanyamapori kuwa maskini zaidi kulinganisha na miaka 50 iliyopita,” alisema. Aliongeza kuwa baadhi yao wameanza hata kula wanyamapori tofauti na mila na desturi yao kutokana na mifugo yao kwisha. Lissu alisema kuwa badala ya kufikiria kuwahamisha wafugaji hao, ilipaswa kuwapongeza kwa kumudu kuhifadhi mazingira na wanyamapori katika maeneo yao tofauti na makabila mengine nchini yaliyoharibu mazingira na kuua wanyamapori kwenye maeneo yao.
“Haiwezekani fadhila ya ulinzi na utunzaji wa mazingira na wanyamapori unaofanywa na Wamaasai iwe ni kuwafukuza kutoka kwenye maeneo yao kupisha wawekezaji. Hapana. Wamaasai sasa wakatae unyanyasaji huu,” alisema. Naye Mch. Msigwa aliwataka Wamaasai kuonyesha hasira yao kwa kukinyima kura Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika chaguzi zijazo kuanzia serikali za mitaa mwakani na uchaguzi mkuu ujao 2015.
Viongozi wengine wa CHADEMA waliohudhuria mkutano huo na kuzungumza na wananchi kwa nyakati tofauti ni Katibu wa Kanda ya Kaskazini, Amani Golugwa, Mwenyekiti wa BAVICHA Mkoa wa Arusha, Ephata Nanyaro na Katibu wa BAVICHA Wilaya ya Arusha, Glory Kaaya.
Source: Tanzania Daima. (March 2013). Mwigulu alikoroga Loliondo. Retrieved from Tanzania Daima

No comments:
Post a Comment