![]() |
Mmoja wa wahitimu wa mafunzo ya jinsia ngazi ya cheti akitunukiwa cheti cha mafunzo ya GTI na mgeni rasmi, John Mnyika.
|
MBUNGE wa Jimbo la Ubungo kupitia tiketi ya
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), John Mnyika ameahidi kumsomesha
mwanafunzi bora wa Chuo cha Jinsia (GTI) kupitia sehemu ya
mshahara wake wa
ubunge. Mbunge huyo alitoa ahadi hiyo jana jijini Dar es Salaam katika
sherehe za Mahafali ya Kwanza ya Chuo cha Jinsia, GTI alipokuwa mgeni rasmi.
Alisema anatambua mchango wa chuo hicho katika kuiandaa jamii kupigania usawa
wa rasilimali za taifa, hivyo kupitia mshahara wake wa ubunge atatoa mchango wa
kumlipia ada mwanafunzi bora wa chuo hicho mwakani. Mbunge huyo aliupongeza uongozi wa GTI kwa mafanikio waliofikia
ya kuanzisha chuo kinachotoa mafunzo ya jinsia kwa jamii na kushauri uongozi
kujipanga na kuwasilisha ombi la kuomba fungu la fedha kutoka Mfuko wa Mbunge
wa Maendeleo wa Jimbo ili kukiwezesha chuo hicho kufanya shughuli zake
kiufanisi.
Awali akizungumza katika mahafali hayo, Mkuu wa Chuo cha GTI,
Dk. Diana-Bupe Mwiru alisema mahafali hayo ni ya kihistoria kutokana na kwamba
yanafanyika kipindi ambacho Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) ambao ni wamiliki
wa chuo hicho wakisherehekea miaka 20 tangu kuanzishwa kwa taasisi hiyo. “TGNP inasherehekea miaka 20 ya harakati za ukombozi wa mwanamke
kimapinduzi dai kuu likiwa rasilimali za nchi kunufaisha watu wote na hasa wale
walioko pembezoni. Mwanamke wa kitanzania amekuwa miongoni mwa makundi yaliyoko
pembezoni kutokana na mila na sheria kandamizi ambazo zilishindwa kutambua
mchango wa mwanamke katika jamii na majukumu makubwa ambayo ameyabeba ili
kuhakikisha kuwa jamii inaendelea kuwepo,” alisema Dk. Mwiru.
Aliongeza kuwa GTI tangu kuanzishwa kwake imekuwa ikitoa mafunzo
kwa umahiri mkubwa katika soko la ndani na nchi za jirani, huku kikiwa
kimefundisha washiriki zaidi ya 6000 kutoka nchi za Msumbiji, Nigeria, Malawi,
zambia, Kenya, rwanda, Uganda, Ethiopia, Norway pamoja na Tanzania yenyewe. “Kutokana na umahiri wake katika kutoa mafunzo GTI imeweza
kutambuliwa kimataifa kama chuo kilichotukuka katika kutoa maarifa na stadi
katika nyanja ya jinsia na maendeleo kwa Afrika Mashariki na Kati. Kwa GTI hii
ni hatua ya mafanikio ambayo tuna kila sababu ya kujivunia,” alisema Mkuu wa
Chuo hicho.
Aidha Dk. Mwiru alitoa shukrani kwa mashirika mfadhili wa GTI
ambayo ni ‘Foundation for Civil Society, UN Women, UNFPA, Deloitte, Action Aid
na SIDA kupitia TGNP na RATN ambayo yamekuwa sehemu ya mafanikio ya chuo hicho.
Ikiwa ni pamoja na kuiomba Serikali pamoja na taasisi zake nayo kuanza
kukitumia chuo hicho. Akizungumza kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi, Mwenyekiti wa
Bodi ya GTI, Profesa Saida Othman aliiomba Serikali kushughulikia changamoto ya
ubora wa elimu kiujumla kwani matokeo yanavyokuwa mabaya hata vyuo
vinavyotegemea wanafunzi hukosa wanafunzi wenye sifa kujiunga na vyuo hivyo. Jumla ya wahitimu wa 11 walifanikiwa kutunukiwa vyeti vya
mafunzo ya jinsia katika mahafali hayo ya kwanza.
Source: Mushi J. (March 2013). Mbunge Mnyika Ahaidi Kumsomesha Mwanafunzi Bora Chuo cha Jinsia.The habari

No comments:
Post a Comment