Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora

Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora
----------------------WE THANK AND APPRECIATE YOU FOR VISITING CHADEMA DIASPORA BLOG. AGAIN, THANK YOU!-----------------------

Saturday, April 13, 2013

Lissu awachochea wabunge


MBUNGE wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema), amekuja juu na kusema Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, anatakiwa kupigiwa kura ya kutokuwa na imani naye kwa kuwa ameshindwa kumwajibisha Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa. Amesema kitendo cha Waziri Mkuu kushindwa kumwajibisha Dk. Kawambwa kutokana na matokeo mabaya ya kidato cha nne mwaka jana, hakiwezi kuvumiliwa na hivyo wabunge wanatakiwa kumwajibisha Waziri Mkuu. Lissu aliyasema hayo bungeni jana, alipokuwa akichangia bajeti ta Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka wa fedha wa 2013/2014. Pamoja na kutaka hatua hiyo ichukuliwe, Lissu alisema tangu Rais Jakaya Kikwete aingie madarakani mwaka 2005, ufaulu wa wanafunzi wa kidato cha nne umeshuka ikilinganishwa na hali ilivyokuwa enzi za Rais Benjamin Mkapa.

Kwa mujibu wa Lissu, mwaka jana Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, ilitoa ripoti ya takwimu za ubora wa elimu nchini kuanzia mwaka 2007 hadi mwaka juzi ikionyesha kushuka kwa ufaulu nchini. Alisema ripoti hiyo, inaonyesha katika kipindi cha miaka mitano ya mwisho ya utawala wa Serikali ya awamu ya tatu iliyoongozwa na Rais mstaafu Benjamin Mkapa, ufaulu wa wanafunzi ulipanda.

Alisema ufaulu wa wanafunzi ulishuka kuanzia mwaka 2006 (awamu ya nne) ukilinganisha na miaka mitano ya mwisho ya uongozi wa Rais mstaafu Mkapa.


Alisema waliopata daraja la kwanza katika kipindi cha miaka mitano ya mwisho ya awamu ya tatu walikuwa ni asilimia 5.4, waliopa daraja la pili walikuwa ni asilimia saba, daraja la tatu walikuwa ni asilimia 21 wakati wa daraja la nne walikuwa asilimia 52. “Hiyo inamaanisha kuwa, wastani wa ufaulu katika miaka mitano hiyo ulikuwa ni asilimia 84.5 na waliofeli walikuwa asilimia 14.8.

“Lakini, baada ya Rais Kikwete kuingia madarakani, ufaulu ulishuka kutoka asilimia 5.3 hadi 3.3, waliopata daraja la pili walishuka kutoka asilimia 7 hadi 5.8, daraja la tatu walishuka kutoka asilimia 21 hadi asilimia 16.3 wakati daraja nne walishuka kutoka asilimia 52 hadi 51.7 na waliopata daraja sifuri walipanda kutoka asilimia 14.8 hadi asilimia 22.8. “Wastani wa kufaulu katika miaka mitano ya kwanza ya Serikali ya awamu ya nne, ulikuwa ni asilimia 77.2 na hivyo umeshuka kutoka asilimia 84.5.

“Ukiangalia takwimu za kila mwaka, mwaka 2006 wanafunzi ufaulu wa daraja la kwanza ulikuwa ni asilimia 4.9 lakini mwaka juzi ufaulu ulishuka hadi asilimia 2.8 ,”alisema. “Kwa hiyo, ni sahihi kabisa kwamba, kuporomoka kwa elimu ni janga la Serikali ya awamu ya nne na ni sahihi kusema kuwa Serikali CCM ni janga la elimu,” alisema Lissu na kuongeza.

“Wawajibishane, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, amekataa kujiuzulu, anatakiwa kuwajibishwa kwani hili ni janga la elimu. “Waziri Mkuu naye anatakiwa ajiuzulu, kama hataki, apigiwe kura ya kutokuwa na imani naye kwani huu siyo wakati wa kulea uovu na uchafu bali ni wakati wa kuwajibishana,” alisema.

Awali, Mbunge wa Viti Maalum, Pauline Gekul, alipokuwa akichangia bajeti hiyo, alipinga mpango wa Ofisi ya Waziri Mkuu kutenga Sh bilioni 6 kwa ajili ya kukarabati jengo la Bunge. Alisema kwamba fedha hizo ni nyingi na kwamba zinatakiwa kupunguzwa ili kiasi kikubwa cha fedha, kipelekwe kwenye shughuli za maendeleo.

Source: Paul M. (April 2013). Lissu awachochea wabunge. Retrieved from Mtanzania

No comments: