NIANZE makala hii kwa kutoa salamu zangu za pole kwa
Watanzania waliokumbwa na janga la kuangukiwa na jengo la ghorofa zaidi ya 10
jijini Dar es Salaam, Ijumaa iliyopita. Inasikitisha kuona uhai wa wenzetu umepotea katika
mazingira ambayo kimsingi yangeweza kuzuilika. Baada ya salamu hizo, tuelekee katika mada ya wiki hii
ambayo inajadili kauli ya hivi karibuni ya Rais Jakaya Kikwete kuhusu kushuka
kwa uzalendo miongoni mwa Watanzania.
Akizungumza hivi karibuni na vijana ya Taasisi ya
Maendeleo ya Vijana (UVIKITA) jijini, Rais alielezea kushangazwa na tabia ya
baadhi ya Watanzania kuona ufahari 'kuiponda' nchi yao, na kuwasifia wale
wanaoisema vibaya, na kudai hali hiyo imetokana na wao kutojali uzalendo kwa
taifa lao. Kadhalika Rais Kikwete alidai kuwa zamani haikuwa rahisi
kuwapata watu wenye tabia hiyo kutokana na utaratibu uliokuwapo. Vile vile
alieleza wakati huo mtu akisema vibaya nchi yake aliwekwa katika wakati mgumu,
na kwamba mabadiliko yalianza kujitokeza katika kipindi cha utawala wa Rais Ali
Hassan Mwinyi, ambapo kiongozi huyo alikuja na “moto wake wa ruksa.”
“Mabadiliko haya yalianza na Mzee Mwinyi, enzi zetu
pamoja na kipindi kuwa kigumu , hakuna aliyeisema vibaya akaachwa, sijui
tumeteleza wapi? Mimi nadhani kuna mahala tumepotoka,” alisema Rais, na
kuongeza, “Cha kushangaza hata wakimsikia mtu anaisifia Tanzania, wao
wanapinga, na hii inatokana na wengi wao kutokuwa na moyo wa kujitolea kwa nchi
yao tofauti na ilivyokuwa zamani.”
Kwanza, ninaafikiana na Rais Kikwete kuwa nchi yetu kwa
sasa inakabiliwa na uhaba mkubwa wa uzalendo. Lakini pengine kabla hata ya
kuanza kulijadili suala hili pengine ni vema kujiuliza swali hili: kama Rais
hajui kwa nini tumefika hapa, tutarajie nini kutoka kwa mwananchi wa kawaida?
Pili, wakati ni kweli anachosema Rais kuwa kabla ya
utawala wa Mwinyi haikuwa rahisi kwa mtu kuisema vibaya nchi yetu, ni muhimu
kutambua kuwa zama hizo licha ya kuwa ni za siasa ya chama kimoja ambapo
mtizamo tofauti na chama tawala ulikuwa sawa na uhaini, lakini pia siasa za
wakati huo zilikuwa na chembe za udikteta kwa maana ya kuminya uhuru wa kutoa
mawazo (freedom of expression).
Ni kweli pia kama alivyosema Rais kuwa mtu yeyote
aliyejaribu kuisema vibaya nchi yetu aliwekwa kwenye wakati mgumu, lakini pia
mawazo hayo hayo ambayo zama hizo yangeweza kumweka mtu katika wakati mgumu
ndiyo yanayokumbatiwa hivi leo. Ni nani asiyejua kuwa baadhi ya watu tunaowaita
wawekezaji leo hii ndiyo tuliowaita mabepari au makabaila zama hizo?
Wakati Rais Kikwete ana kila sababu ya kukerwa na hali
hiyo ya uhaba wa uzalendo, cha muhimu zaidi si kukerwa tu bali kuchukua hatua
stahili kurekebisha au kuondoa kabisa tatizo hilo. Katika uelewa wangu mdogo wa
dini ya Kiislamu ninafahamu kuna mafundisho haya muhimu dhidi ya jambo baya:
“ukiona jambo baya basi aidha lichukie, au likemee kwa nguvu zako zote, au
ikiwezekana liondoe, hata kwa nguvu ikibidi” (nukuu hii sio rasmi).
Sasa katika kipindi hiki ambacho Rais Kikwete amebakiwa
na chini ya miaka miwili kabla ya kustaafu kwake anafanya jitihada gani za
kurejesha uzalendo miongoni mwa Watanzania (tukiweka kando ukweli aliokiri
mwenyewe kuwa hajui kwa nini tumefika katika hali hiyo)?
Tatu, siamini kabisa kuwa kila Mtanzania anayeisema
vibaya nchi yake ana makosa. Hivi ni kosa kulaumu viogozi na nchi kwa ujumla
kwa kutofanya jitihada za kurejesha mabilioni yetu yaliyofichwa Uswisi na wezi
ambao licha ya kufahamika lakini baadhi yao bado wapo madarakani (na pengine
wakiendelea kutuibia)?
Je, ni kosa ‘kuisema vibaya’ nchi yetu pale majambazi wa
EPA wanapoonewa huruma na ‘haki zao za kibinadamu’ kupewa kipaumbele, na hivyo
kuambiwa walipe taratibu fedha walizotuibia, huku yule jambazi mkuu wa kampuni
ya Kagoda aliyeiba zaidi ya shilingi bilioni 40 za EPA akisitiriwa na watawala
ambao wamegoma katakata kumtaja hadharani (japo wengine tunamfahamu bayana)?
Na je, ni dhambi ‘kuisema vibaya’ nchi yetu wakati huu
tunaomboleza vifo vya wenzetu (walioangukiwa na jengo jijini Dar Ijumaa
iliyopita) ambapo mwaka 2008 kulitokea ajali kama hiyo, na aliyekuwa Waziri
Mkuu wakati huo, Edward Lowassa aliunda tume na kutoa mapendekezo lakini yakipuuzwa,
na sasa tumejikuta kwenye majonzi ambayo yangeweza kabisa kuepukika?
Ni hivi, Rais, tatizo si Mtanzania kuisema vibaya nchi
yake. Tatizo ni kuisema vibaya pale inapostahili kusifiwa. Ndiyo maana hakuna
Mtanzania yeyote mwenye akili timamu aliyediriki ‘kuiponda’ nchi yetu pale
Taifa Stars ilipotoa ‘kipigo cha nguvu’ kwa Morocco hivi karibuni.
Kadhalika, baadhi ya tuonakerwa na ‘sifa za kutuvika
kilemba cha ukoka’- kama hizo za baadhi ya taasisi za fedha za kimataifa
zinazodai kuwa uchumi wetu unakua kwa kasi ilhali nchi ipo gizani kila baada ya
saa na umasikini ukizidi kuongezeka- si kama hatuipendi nchi yetu bali
tunakerwa na unafiki wa aina hiyo.
Moja ya sababu kubwa kabisa ya kupotea kwa uzalendo ni
kuruhusu ufisadi uwe sehemu muhimu ya maisha ya Mtanzania. Hata katika ngazi ya
familia tu, ni mtoto gani atakayempenda mzazi anayekwapua fedha za matumizi
muhimu ya nyumbani na kwenda kuzitumia kwa anasa zake?
Nihitimishe kwa kusema kwamba japo ni jukumu la kila
Mtanzania kuipenda nchi yetu (na nina hakika Watanzania wengi wanaipenda kweli
nchi yao maana vinginevyo wasingevumilia jitihada za mafisadi kukomba karibu
kila rasilimali tuliyonayo kila kukicha) lakini watawala wetu wana dhamana
kubwa ya kuwa mfano sahihi wa uzalendo.
Kadhalika, kama kweli Rais Kikwete anakerwa kwa dhati na
kushuka kwa uzalendo (na sina sababu ya kuamini vinginevyo) basi na aende mbali
zaidi ya kukerwa tu au kujiuliza kwa nini hali imekuwa hivi, aanze jitihada za
makusudi za kurejesha uzalendo.

No comments:
Post a Comment