Sakata la suala la ugaidi limeendelea kuitikisa nchi, baada ya jana Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kudai kimegundua njama zinazofanywa na CCM kukififisha chama hicho kwa kukihusisha na ugaidi wakati kinara ni wao. Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Wilbroad Slaa, alitoa madai hayo jana jijini Dar es Salaam wakati wa mkutano wa ndani wa kanda Maalum ya Dar es Salaam na Mkoa wa Pwani uliolenga kutoa mafunzo ya ujenzi wa chama hicho na mpango wa M4C. Dk. Slaa alidai kuwa kama CCM na serikali yake sio magaidi wasingeweza kuwapeleka maofisa wa Chadema chumba namba 223 kuwahonga ili watunge uongo kwenye kesi ya Mkurugenzi wa Usalama Chadema, Wilfred Lwakatare.
Alisema kuwa, Chadema kimejipanga na tayari kimetoa mafunzo kwa viongozi wake 30,000 kwa ajili ya M4C. “Mwitikio wenu leo ni dalili ya ujumbe mzito kwa wenzetu hasa wanaotuita magaidi, wao waendelee kupiga propaganda na porojo lakini sisi tunaenda mbele na mwaka 2015 tutaichukua dola,” alisema na kuongeza: “Tunafurahi wanatuchokoza lakini sisi tutaendelea kuchapa kazi kwa mujibu wa katiba, jana (juzi) bungeni magaidi walijionyesha wenyewe, tunawaambia tupo makini kuliko serikali yao, CCM na usalama wa taifa,” alisema. Aliongeza kuwa, umakini wa Chadema ndio utakaofanikisha mwaka 2015 kuingia Ikulu bila kutegemea vyombo vya dola. Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe, akizungumzia mustakabali wa chama hicho na nchi, alikumbushia kuhusu mambo matano aliyozungumza bungeni kuhusu utamaduni uliotengenezwa na CCM kukichafua chama hicho, elimu, katiba na udini.
Akielezea kuhusu mbinu za CCM kukichafua Chadema, alisema hawaogopi propaganda na kwamba hawawezi kuwagawa Watanzania kwa kuwalimbikizia kesi magerezani kwani asilimia 50 ya watu waliopo magerezani wamebambikiziwa kesi,” alisema. Katika maelezo yake Mbowe alijikuta akikatisha hoja aliyokuwa ametaka kuizungumzia kuhusu Naibu Katibu Mkuu wa CCM Bara, Mwigulu Nchemba na kusema endapo atamzungumzia atampandisha sana. Aidha, alisema ameenda mara tatu gerezani kumtembelea Lwakatare, ambapo huko aliwashangaza maofisa baada ya kumuuliza Lwakatare ameeneza sera za chama kwa kiwango gani huko. “Ndugu zangu msiogope kwenda magereza, huko mkifika endeleeni kueneza sera za chama, CCM mbinu zao zitashindwa mwaka 2015,” alisema.
Alidha alisistiza kuwa “Chadema sio chama cha kikristo wala kiislamu tusimtenge mtu kwa ajili ya kabila, jinsia au dini,”. Kuhusu katiba mwenyekiti huyo alisema katika tume ya katiba, Chadema ina mjumbe mmoja ambaye wameelezwa kila kinachofanyika humo ni siri. “Wenyewe wanaenda Ikulu kupanga mikakati yao, tunawakumbusha kuwa katiba tunayoitaka ni ya taifa sio CCM tunataka ijenge mshikamano na kufuta makovu yaliyokuwapo,” alisema. Akifafanua kuhusu elimu, alisema tume iliyoundwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, ni matumizi mabaya ya fedha za Umma na kuhoji matokeo ya tume ya mwaka 2011 iliyolenga kuangalia kushuka kwa kiwango cha elimu mwaka 2010. Alisema tume hiyo ilitoa mapendekezo 27 na kuihoji serikali haijajua sababu ndio maana imeunda tume nyingine.
Mbowe alilifananisha bunge kama kijiwe cha mipasho na kusema kuwa, mara kwa mara wamekuwa wakimtaka Spika wa Bunge, Anne Makinda kuliendesha kwa mujibu wa kanuni na sio kichama.
“Nasema wabunge wetu wataendelea kushirikiana na wale wanaotaka, kinyume na hapo hatutaogopa vitisho vya spika wala naibu spika, tukizidiwa tutakomaa au tutatoka nje kwa wananchi, wao kama wanafikiria kuwanunua viongozi wetu, sisi tumejiimarisha kuanzia ngazi za chini na matokeo watayaona mwishoni mwa mwaka huu,” alisema. Kuhusu uzinduzi wa kanda unaoendelea nchini, alisema dhana ya Mbowe na Slaa kuonekana ndio wanaofaa kuongoza, imepitwa na wakati hivyo wameamua kujenga mfumo shirikishi utakaowezesha kila mtu kupata nafasi kuanzia chini.
Pia chama hicho kimejigamba kuishangaza CCM mwaka 2015 katika mkoa wa Pwani.

No comments:
Post a Comment