Wiki moja baada ya Waziri wa Maliasili na Utalii, Khamis Kagasheki kusema Serikali isingebadili msimamo wake kuhusu kutenga ekari 1,500 za mraba za eneo la pori tengefu la Loliondo kwa manufaa ya umma, timu ya viongozi wa CCM iliyoteuliwa na chama hicho kuchunguza mgogoro huo imeibuka na kudai uamuzi huo wa Serikali umekiuka sheria na una athari kwa wananchi wa Loliondo. Bila kutaja sheria iliyokiukwa na bila kujali kwamba Serikali iliyopo madarakani inatokana na chama hicho, hivyo kutambua kwamba kuishambulia na kuidhalilisha hadharani kunaweza kuharibu taswira ya serikali yake mbele ya wananchi, kiongozi wa timu hiyo ya CCM, Mwigulu Nchemba juzi aliwahutubia wananchi wa Loliondo na kutoa maneno makali dhidi ya Waziri Kagasheki na kumlinganisha na muuza duka ambaye akiwaudhi wateja na wakaanza kuondoka, mwenye duka (CCM) hulazimika kumdhibiti muuza duka ili duka hilo lisifungwe.
Timu hiyo ya CCM ilikwenda Loliondo baada ya chama hicho kupata habari za viongozi wote wa kisiasa katika eneo hilo, akiwamo mbunge kuazimia kujiuzulu nyadhifa zao ili kuunga mkono hatua ya wananchi wa Loliondo kupinga uamuzi wa Serikali wa kuwaachia wananchi hao ardhi ipatayo kilomita za mraba 2,500 na Serikali kubakia na kilomita za mraba 1,500 la pori tengefu la eneo hilo. Maneno makali ya kiongozi huyo wa CCM dhidi ya Waziri Kagasheki yalionekana kusababishwa na hali hiyo tete ya kisiasa aliyoikuta Loliondo, kwani kabla hajahutubia mkutano huo, wananchi wa Kijiji cha Olorien Magaiduru walikuwa tayari wamemkabidhi mfuko wenye zaidi ya kadi 2,000 za CCM, bendera na sare za chama hicho.
Hofu ilitanda kwamba wananchi hao wangejiunga na Chadema, hivyo akalazimika kuwahakikishia wananchi hao kwamba timu yake imeridhika kwamba hoja zao kupinga hatua ya Serikali ni sahihi. Ni bahati mbaya kwamba CCM imeligeuza suala hilo la Loliondo kuwa la kisiasa. Wakati Waziri Kagasheki alipotangaza uamuzi wa Serikali kwa waandishi wa habari wiki iliyopita, tulidhani alitoa maelezo ya kuridhisha, hasa alipoelezea umuhimu wa kuacha eneo hilo la kilomita za mraba 1,500 katika himaya ya Serikali kwa ajili ya kunusuru ikolojia ya Hifadhi za Serengeti, Ngorongoro na pori tengefu la Loliondo.
Alisema kufanya hivyo kungelipa hadhi pori tengefu na kuliwezesha kulinda mazalia ya wanyamapori, mapito ya wanyama na vyanzo vya maji kwa ajili ya ustawi wa hifadhi za taifa. Ni jambo la kushangaza kuwa, pamoja na mgogoro huo wa ardhi kuwapo kwa miongo miwili sasa, CCM ndiyo kwanza inaona umuhimu wa kuutatua. Wanaopinga hatua ya Serikali hawajui kwamba wananchi wanaoishi katika eneo hilo sasa ni wavamizi, kwani eneo hilo la kilomita za mraba 4,000 lilitangazwa katika gazeti la Serikali kupitia Notisi Namba 269 mwaka 1974 kuwa hifadhi kabla ya kuvamiwa na wananchi waliomo hivi sasa.
Serikali itumie busara badala ya mitulinga kutatua mgogoro huo. Ni jambo la kheri kwamba tayari imewatengea wananchi hao kilomita za mraba 2,500 na bado inao uwezo wa kuwapa motisha nyingine kwa lengo la kupata mwafaka. Tunaitaka Serikali iendeleze mazungumzo na tusikubali wanasiasa wageuze suala hili kuwa la kisiasa.
Sourece: Mwananchi (March 2013). CCM imejidhalilisha mgogoro wa Loliondo. Retieved from Mwananchi

No comments:
Post a Comment