Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora

Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora
----------------------WE THANK AND APPRECIATE YOU FOR VISITING CHADEMA DIASPORA BLOG. AGAIN, THANK YOU!-----------------------

Wednesday, January 30, 2013

TANGA WATAKA MGAWANYO WA RASILIMALI ZA NCHI KIKATIBA


WAKAZI wa Jiji la Tanga wameitaka Tume ya Mabadiliko ya Katiba kuweka wazi uwiano wa mgawanyo wa rasilimali za nchi kati ya Serikali na wananchi wake ili kuepusha mivutano kati ya wananchi na dola.
Wamesema kama suala hilo lingewekwa wazi katika Katiba ya sasa mgogoro uliopo kati ya wananchi wa Mtwara na Serikali usingelikuwepo na hivyo kuikumbusha Tume ya Mabadiliko ya Katiba Mpya kuweka kifungu kitakachoweka wazi suala la rasilimali za nchi.

Wakazi wa Mtwara wanaona kuwa gesi iendapo Dar es Salaam inaweza kuwakosesha fursa mbalimbali zikiwemo ajira kwa vijana pamoja na kushuka kwa pato la mkoa wao na hivyo kupinga gesi hiyo kusafirishwa jambo ambalo limeingia katika mgogoro wa kisheria.
Wamesema Katiba Mpya inatakiwa kueleza wazi mahala ambapo kutapatikana rasilimali kama gesi au petroli na kuwepo utaratibu wa mapato kutokana na Katiba isemavyo ili kuondosha mivutano baina ya pande hizo mbili.



“Kama wakazi wa Mtwara wangejua hilo wasingekuwa na sababu ya kuzuia gesi kwenda Dar es Salaam kwani wangejua kuwa faida ambayo itapatikana ingerudi kwao, lakini Katiba iliyopo haisemi hivyo,” alisema Paskal Mgama.
Mgama alisema wakazi wa Mtwara hivi sasa wana hofu kwamba gesi yao ikisafirishwa wao hawatapata kitu na mkoa wao utazidi kuwa nyuma kimaendeleo jambo ambalo kama Katiba ya sasa ingeweka bayana namna ya rasilimali za nchi zinavyokuwa kusingekuwepo na mvutano uliopo.
Alisema ni wakati mwafaka wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Mpya kujikumbusha kwa tukio la Mtwara ili Katiba ijayo ikaweka wazi mambo yanayoigusa jamii na pale wataalamu wanapogundua rasilimali ambazo upande mmoja huenda ikawa ni ukombozi wa maisha yao ikaeleweka wazi.
Naye mkazi wa Kwanjeka, Mashango Ali alisema ni vyema Tume ya Mabadiliko ya Katiba Mpya ikaunda kikosi maalumu cha kufuatilia mambo ya kisheria kati ya wananchi na Serikali ili Katiba Mpya ijayo ikaondosha migogoro kati ya pande mbili hizo.
Mashango aliwataka wananchi kukitumia kipindi hiki ambacho kimebaki cha kutoa maoni mbele ya Tume ya Kukusanya Maoni kwa kuyasema yote ambayo wanahisi kwao yanaweza kuwa na masilahi kwao na Taifa kwa jumla.
Aliwataka kutumiwa vyema kipindi hiki na kuacha kujikita katika mambo mengine ambayo yanaweza kuwapotezea muda na kuja kujutia wakati Katiba Mpya inayotarajiwa itakuwa mwongozo kwa Watanzania kwa miaka mingi.

Source: Mohamed S. ( January 30, 2013). Mwananchi

No comments: