CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimesema kuwa kimepokea kwa masikitiko na majonzi makubwa taarifa za msiba wa Mjumbe wa Kamati Kuu ya Taifa, Bi. Shida Salum ambaye ameaga dunia leo jijini Dar es Salaam. Akizungumza kwa niaba ya chama, Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, Freeman Mbowe amesema kuwa Bi. Shida ambaye pia hadi anafariki alikuwa Mjumbe wa Bunge Maalum la Katiba, ameacha pengo kubwa kutokana na utumishi wake wa muda mrefu ndani ya chama.
“Kwa niaba yangu,viongozi wa wenzangu ndani ya chama, wanachama, wapenzi, mashabiki na wafuasi wetu nchi nzima, kwa masikitiko makubwa natoa salamu za rambirambi kwa familia ya Mama Shida Salum.
“Tunaungana na familia hiyo, ndugu, jamaa na marafiki na watu wote walioguswa na msiba huu katika wakati huu mgumu. Tunaomba sana Mwenyezi Mungu awatie nguvu na kuwapatia moyo wa subira kuukabili wakati huu wa msiba wa kuondokewa na mpendwa Mama Shida Salum,” amesema Mwenyekiti Mbowe. Ameongeza kusema kuwa CHADEMA taarifa hizo za kushtua za kuondokewa na Mjumbe wa Kamati Kuu, zimewakuta viongozi mbalimbali wa chama hicho wakiwa wametawanyika katika maeneo mbalimbali nchini kwa majukumu ya kichama.
Mwenyekiti Mbowe ameongeza kusema kuwa kutokana na hali ya uharaka wa chama kushiriki kikamilifu katika mazishi ya Bi. Shida Salum yanayotarajiwa kufanyia kesho Jumatatu mkoani Kigoma, amemteua Mjumbe wa Kamati Kuu ya CHADEMA, Ezekiel Wenje (MB) ambaye pia ni Waziri Kivuli katika Kambi ya Upinzani Bungeni, kukiwakilisha chama, huku viongozi wengine nao wakijaribu kutafuta njia ya kuweza kuwahi mazishi hayo. “Tayari tumepata ndege ya kukodi ambayo Wenje ataitumia kwenda Kigoma kuwahi mazishi ya Bi. Shida Salum. Wenje alikuwa mmoja wa viongozi waliokuwepo Dar es Salaam. Hadi Mama Shida anaaga dunia leo, Wenje alikuwepo hospitalini akituwakilisha kumjulia hali mama,” amesema Mwenyekiti Mbowe.
Mwenyekiti Mbowe amesema kuwa Mama Shida daima atakumbukwa kwa namna alivyokipigania chama chake, familia yake na alivyokuwa mtetezi wa makundi maalum katika jamii, kwa muda mrefu wa maisha yake hapa duniani.
Imetolewa leo Juni 1, 2014 na
Kurugenzi ya Mawasiliano na Uhusiano
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA)
No comments:
Post a Comment