Hassan Nassor Moyo |
Jumuiya ya Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) imesema imechoshwa na vitendo vya muasisi wa chama hicho, Hassan Nassor Moyo, kwa madai ya kukisaliti na kukidhoofisha chama hicho. Akizungumza na waandishi wa habari jana, Naibu Katibu Mkuu wa UVCCM Zanzibar, Shaka Hamdu Shaka, aliwataka viongozi wakuu wa CCM kuchukua hatua za kinidhamu na kumnyang’anya kadi ya uanachama muasisi huyo. Moyo ni Mwenyekiti wa Kamati ya Maridhiano ambayo ilihusika wakati wa kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) na ni mtetezi wa muundo wa serikali tatu.
Shaka alisema kwa muda mrefu Mzee Moyo amekuwa akikihujumu CCM bila ya kuchukuliwa hatua za kinidhamu, na kwamba hali hiyo linakidhoofisha chama hicho na kukivunjia hadhi mbele ya wananchi, hivyo wakati umefika kwa muasisi huyo kufukuzwa CCM. ‘CCM kina mtaji wa wanachama, viongozi na waasisi wengi, si maskini, heri wabaki wachache kuliko kuendelea kubaki na wanachama wasaliti na wakorofi,” lisema Shaka. Shaka alisema Moyo amekuwa akitumia mwavuli wa uanachama wa CCM kukivuruga na kukisaliti chama hicho kupitia Kamati ya Maridhiano ambayo alisema haikuundwa kwa mujibu wa sheria wala Katiba ya Zanzibar na kwamba Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, alishasema hadharani kwamba kamati hiyo haitambui.
“Hii ni kamati ya upekepeke inayomzunguka na kumyumbisha Rais Shein, haikuundwa kisheria, haina hadidu za rejea, haifahamiki kazi zake, kwanini ipande jukwaa la CUF na kuliogopa la CCM?” alihoji Shaka. Mzee Moyo alipoulizwa, alisema hashughulishwi na maneno yao na kuwa ni mwanachama wa CCM, ana haki ya kutoa maoni na anaona Serikali tatu ndizo zinazofaa.
Suleiman R. / IPP Media/Nipashe
No comments:
Post a Comment