MAONI YA WAJUMBE WALIO WA WACHACHE KATIKA KAMATI NAMBA NNE
KUHUSU SURA YA KWANZA NA SURA YA SITA YA RASIMU YA KATIBA YA JAMHURI YA
MUUNGANO WA TANZANIA
[Kanuni ya 32(4) ya Kanuni za Bunge Maalum, 2014]
UTANGULIZI
Mheshimiwa Mwenyekiti,
Sura ya Kwanza na Sura ya Sita ya Rasimu ya
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (‘Rasimu’) ndizo msingi ambao Rasimu
yote imejengwa juu yao. Wakati Sura ya Kwanza inagusa suala la muundo wa
Muungano katika ibara moja tu kati ya ibara tisa, Sura yote ya Sita inahusu
‘Muundo wa Jamhuri ya Muungano.’ Suala la Muungano na hasa Muundo wake
limetawala mjadala wa kisiasa na kikatiba wa Tanzania kwa zaidi ya miaka
thelathini. Ndio maana katika waraka wake wa siri kwa Halmashauri Kuu ya Chama
cha Mapinduzi (‘CCM’), Idara ya Siasa na Uhusiano wa Kimataifa ya chama hicho
imetamka kwamba “muundo wa Muungano ndiyo moyo wa Rasimu na ndiyo unaoamua
ibara nyingine zikae vipi.”
Suala hili pia limetawala mchakato wa Katiba
Mpya tangu ulipoanza miaka mitatu iliyopita. Kama alivyosema Mwenyekiti wa Tume
ya Mabadiliko ya Katiba Joseph Sinde Warioba wakati wa kuwasilisha Ripoti ya
Tume yake kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano na Rais wa Zanzibar tarehe 30
Disemba, 2013: “Moja ya mambo ambayo yamejadiliwa sana na kwa hisia kali tangu
Rasimu ya awali ilipotolewa ... ni Muungano wa Tanzania. Jambo kubwa limekuwa
juu ya muundo wa Muungano.”
Umuhimu wa suala hili unathibitishwa pia na
uamuzi wa Kamati ya Uongozi ya Bunge Maalum kuelekeza kwamba Kamati zake Namba
Moja hadi Kumi na Mbili zianze kujadili Sura ya Kwanza na ya Sita ya Rasimu.
Haya ni maoni ya wajumbe walio wachache wa Kamati Namba Nne juu ya Sura hizi
mbili.
Mheshimiwa Mwenyekiti,
Mjadala wa Kamati Namba Nne kuhusu Sura za
Kwanza na Sita za Rasimu unathibitisha pia umuhimu wa suala la muundo wa
Muungano katika mjadala mzima wa Rasimu. Kama Taarifa ya Kamati yetu
inavyoonyesha, Kamati Namba Nne imeshindwa kufanya uamuzi kuhusu suala hili
katika ibara za 1 na 60 za Rasimu. Katika ibara ya 1 ya Sura ya Kwanza, wajumbe
walio wengi walipata kura 22, ambayo ndiyo theluthi mbili ya kura za wajumbe
wote 33 wa Tanzania Bara wa Kamati Namba Nne. Kwa upande wa Zanzibar, wajumbe
walio wengi walipata kura 9 ambayo ni pungufu ya kura 13 zinazohitajika ili
kufikisha idadi ya theluthi mbili ya wajumbe wote 19 wa Zanzibar.
Kwa upande wa ibara ya 60, wajumbe walio wengi
walipata kura 22 za wajumbe kutoka Tanzania Bara, ambazo ni theluthi mbili ya
idadi ya wajumbe wote 33 kutoka Tanzania Bara. Aidha, kwa Zanzibar, wajumbe
walio wengi walipata kura 8, ambazo pia ni pungufu ya kura 13 zinazotakiwa
kufikisha idadi ya theluthi mbili ya wajumbe wote 19 kutoka Zanzibar. Kwa
sababu hiyo, ibara za 1 na 60 za Rasimu hazikupitishwa au kuamuliwa na Kamati
Namba Nne kama inavyotakiwa na kifungu cha 26(2) cha Sheria na kanuni ya 64(1)
ya Kanuni.
Mheshimiwa Mwenyekiti,
Sasa tunaomba kwa ridhaa yako, tuwasilishe hoja
na sababu za maoni ya wajumbe walio wachache katika Kamati Namba Nne kuhusu
Sura hizi mbili ambazo ndio ‘moyo wa Rasimu.’
SURA YA KWANZA
Sura ya Kwanza ya Rasimu inahusu ‘Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania.’ Sehemu ya Kwanza ya Sura hiyo inazungumzia ‘jina,
mipaka, alama, lugha na tunu za Taifa.’ Ibara ya 1 inaitambulisha Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania; ibara ya 2 inatangaza ‘eneo la Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania’; na ibara ya 3 inaweka utaratibu wa ‘alama na sikukuu za Taifa.’ Vile
vile ibara ya 4 inaweka utaratibu wa lugha ya Taifa na lugha za alama, wakati
ibara ya 5 inahusu ‘tunu za Taifa.’
Kwa upande wake, Sehemu ya Pili ya Sura ya
Kwanza inaweka masharti ya ‘mamlaka ya wananchi, utii na hifadhi ya Katiba.
Ibara ya 6 ya Sehemu hiyo inatoa ufafanuzi wa ‘mamlaka ya wananchi’; ibara ya 7
inafafanua uhusiano kati ya ‘watu na Serikali’; ibara ya 8 inashurutisha ‘ukuu
na utii wa Katiba’; na ibara ya 9 na ya mwisho inaweka ‘hifadhi ya utawala wa
Katiba."
IBARA YA 1
Mheshimiwa Mwenyekiti,
Kama maelezo yake ya pembeni (marginal note)
yanavyoonyesha, ibara ya 1 inaitambulisha ‘Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.’
Ibara ya 1(1) inatamka kwamba “Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni Shirikisho
lenye mamlaka kamili ambayo imetokana na Muungano wa nchi mbili za Jamhuri ya
Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar ambazo kabla ya Hati za Makubaliano
ya Muungano ya mwaka 1964 zilikuwa nchi huru.”
Wajumbe walio wachache wa Kamati Namba Nne
wanapendekeza mabadiliko ya jina la nchi yetu kutoka jina la sasa la ‘Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania’ kuwa jina jipya la ‘Shirikisho la Jamhuri za
Tanganyika na Zanzibar.’ Aidha, wajumbe hao wanapendekeza kuacha kutajwa kwa
Hati ya Makubaliano ya Muungano ya mwaka 1964 katika ibara ya 1(1) na (3) ya
Rasimu. Badala yake, inapendekezwa kwamba Katiba hii ndiyo iwe msingi wa
Shirikisho la Jamhuri za Tanganyika na Zanzibar.
Kwa mapendekezo haya, ibara ya 1(1) itasomeka
kama ifuatavyo: “Shirikisho la Jamhuri za Tanganyika na Zanzibar ni
Shirikisho ambalo limetokana na Muungano wa nchi mbili za Jamhuri ya Tanganyika
na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar.” Kwa mantiki hiyo, ibara ya 1(2) itasomeka:
“Shirikisho la Jamhuri za Tanganyika na Zanzibar ni Shirikisho la
kidemokrasia linalofuata mfumo wa vyama vingi vya siasa, usawa wa binadamu,
kujitegemea, utawala wa sheria, kuheshimu haki za binadamu na lisilofungamana
na dini.” Aidha, ibara ya 1(3) itasomeka: “Katiba hii ndio msingi mkuu
wa Shirikisho la Jamhuri za Tanganyika na Zanzibar.” Zifuatazo ni hoja na
sababu za mapendekezo haya
SHIRIKISHO AU MUUNGANO?
Katika nusu karne ya uhai wake, nchi yetu
imeitwa ‘Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.’ Hata hivyo, katika kipindi chote
hicho, Katiba na Sheria za nchi yetu hazijawahi kufafanua kwa uwazi aina au
haiba ya ‘Muungano’ huu. Matokeo ya kukosekana kwa ufafanuzi huu ni kwamba
katika nusu karne hiyo, kumekuwa na mjadala mkubwa wa kikatiba, kisiasa na
kitaaluma kuhusu suala la kama Jamhuri ya Muungano ni dola ya muungano (a
unitary state), au ni dola ya shirikisho (a federal state). Majibu
ya swali hili yamekuwa na athari za moja kwa utambulisho, haki, maslahi na
wajibu wa Washirika wa Muungano huo, yaani Tanganyika na Zanzibar, na hasa kwa
wananchi wa nchi hizi mbili.
Mheshimiwa Mwenyekiti,
Kukosekana kwa ufafanuzi wa aina ya muungano
wetu haujawa suala la mijadala ya kisiasa na kikatiba peke yake, bali kumekuwa
ni chanzo cha migogoro mikubwa ya kisiasa baina ya Serikali ya Jamhuri ya
Muungano na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar. Migogoro hii ilianza tangu mwanzo
kabisa wa Muungano wakati wa sakata la kuwa na ubalozi wa iliyokuwa Ujerumani
Magharibi kwa upande wa Tanganyika na ubalozi wa iliyokuwa Ujerumani Mashariki
kwa upande wa Zanzibar.
Aidha, kati ya mwaka 1964-1967 ulizuka mgogoro
mkubwa kuhusiana na uwakilishi wa Zanzibar katika iliyokuwa Bodi ya Sarafu ya
Afrika Mashariki na uanzishwaji wa Benki Kuu ya Tanzania; kuunganishwa kwa
vyama vya ASP na TANU na kuundwa kwa CCM mwaka 1977, na katika mjadala wa
marekebisho ya Katiba wa mwaka na baadae ‘kuchafuka kwa hali ya hewa ya kisiasa
Zanzibar’ mwaka 1983/1984.
Baadae mwaka 1988 ulitokea mgogoro mkubwa
uliopelekea kung’olewa madarakani kwa Waziri Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi
Zanzibar Maalim Seif Shariff Hamad na baadae kufukuzwa katika CCM; wakati wa
harakati za kudai kura ya maoni kuhusiana na Muungano mwaka 1989/1990; wakati
wa mjadala wa kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa mwaka 1991; wakati
wa sakata la Zanzibar kujiunga na Umoja wa Nchi za Kiislamu (Organization of
Islamic Countries - OIC) mwaka 1993; wakati wa mjadala wa G-55 na madai ya
kuanzishwa kwa Serikali ya Tanganyika ndani ya Muungano mwaka 1994, na Uchaguzi
Mkuu wa 1995 huko Zanzibar.
Milenia Mpya ilipoanza ilianza na mgogoro
kuhusu matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2000 uliopelekea mauaji ya Januari
2001 huko Zanzibar. Mgogoro huo ulifuatiwa na mgogoro juu ya suala la ugunduzi
wa mafuta visiwani Zanzibar; harakati za kuanzishwa kwa Shirikisho la Afrika
Mashariki na hivi karibuni kupitishwa kwa Marekebisho ya Kumi ya Katiba ya Zanzibar
ya 1984 mwaka 2010.
Zaidi ya migogoro hii, Serikali ya Jamhuri ya
Muungano na ile ya Mapinduzi zanzibar zimeunda tume na kamati nyingi ili kupata
dawa ya ‘Kero za Muungano.’ Serikali ya Mapinduzi Zanzibar peke yake imeunda
tume na kamati 13 katika kipindi kifupi cha miaka 12 kuanzia mwaka 1992 hadi
2004; wakati Serikali ya Jamhuri ya Muungano imeunda tume na kamati nane
kushughulikia matatizo hayo. Licha ya jitihada zote hizo, ‘Kero za Muungano’
hazijapatiwa ufumbuzi wa kudumu.
Tangu miaka ya mwanzo ya Jamhuri ya Muungano
kulikuwa na mitazamo miwili tofauti miongoni mwa waasisi na viongozi wakuu wa
Jamhuri ya Muungano. Mitazamo hii tofauti inathibitishwa na kauli ya Mwalimu
Julius K. Nyerere, mwasisi na Rais wa Kwanza wa Jamhuri ya Muungano katika
Mkutano Maalum wa Halmashauri Kuu ya CCM uliofanyika Dodoma kati ya tarehe
24-30 Januari, 1984: “... Muungano wa Tanzania ukiangalia kwa jicho la
Zanzibar ni wa shirikisho lakini ukiangalia kutoka upande wa Tanzania Bara ni
Serikali moja.”[2]
Mwalimu alikuwa akimjibu Makamu Mwenyekiti wa
CCM, Makamu wa Rais na Rais wa Zanzibar wakati huo, Alhaj Aboud Jumbe Mwinyi
aliyesema kwamba Muungano wa Tanzania umeunda Shirikisho (Federation) na
sio Serikali moja (Unitary State). Mjadala huo ulipelekea ‘kuchafuka kwa
hali ya hewa ya kisiasa Zanzibar’ na kung’olewa madarakani kwa Jumbe, Waziri
Kiongozi wake Ramadhani Haji Faki na Mwanasheria Mkuu Bashir Kwaw Swanzy.
Aidha, Wolfgang Dourado, aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar wakati Hati ya
Muungano inasainiwa, na mkosoaji mkubwa wa Muungano huo, aliwekwa kizuizini kwa
kuunga mkono hoja za Rais Aboud Jumbe.
Miaka kumi baada ya ‘kuchafuka kwa hali ya hewa
ya kisiasa Zanzibar’ Jamhuri ya Muungano ilikabiliwa na mgogoro mwingine tena
wa kikatiba na kisiasa, mara hii ukitokana na Zanzibar kujiunga na OIC. Kitendo
hicho kilizua tafrani kubwa ya kisiasa pale Bunge la Jamhuri ya Muungano
lilipopitisha Azimio la kutaka kuanzishwa kwa Serikali ya Tanganyika ndani ya
Muungano mwezi Agosti, 1993. Azimio hilo liliungwa mkono na Serikali ya Jamhuri
ya Muungano, kitendo kilichomfanya Mwalimu Nyerere kuingilia kati na kuzima
jaribio hilo.
Baadae Mwalimu aliandika kitabu alichokiita Uongozi
Wetu na Hatima ya Tanzania kilichochapishwa mwaka 1994. Katika kitabu
chake, Mwalimu anarejea mkanganyiko ambao umekuwepo kuhusu aina ya Muungano huu
kwa maneno yafuatayo:
“Nchi zinapoungana na kuwa
nchi moja mifumo ya kawaida ya miundo ya Katiba ni miwili: Kwa mfumo wa kwanza
kila nchi itafuta serikali yake, na nchi mpya inayozaliwa itakuwa ni nchi moja
yenye serikali moja. Katika mfumo wa pili kila nchi itajivua madaraka fulani
ambayo yatashikwa na serikali ya shirikisho, na itakuwa na serikali ambayo
itakuwa na mamlaka juu ya mambo yaliyobaki. Mambo yatakayoshikwa na serikali ya
shirikisho ni yale ambayo yakibaki katika mamlaka ya nchi zilizoungana, basi
kwa kweli nchi hizo zitakuwa hazikuungana kuwa nchi moja, bali zinaendelea kuwa
nchi mbili zenye ushirikiano mkubwa katika mambo fulani fulani.... Shirikisho
halisi la nchi mbili litakuwa ni nchi moja yenye serikali tatu, Serikali ya
shirikisho na serikali mbili za zile nchi mbili za awali zilizoungana kuzaa
nchi mpya moja.”[3]
Mwaka ambao Mwalimu Nyerere alichapisha Uongozi
Wetu na Hatima ya Tanzania, Makamu Mwenyekiti wake wa CCM na Makamu Rais
wake hadi Januari 1984, Alhaj Aboud Jumbe, aliyekuwa pia Waziri wa Afya wa
Zanzibar wakati Muungano unazaliwa na baadae Rais wa Pili wa Zanzibar, naye
alichapisha The Partnership: Muungano wa Tanganyika na Zanzibar: Miaka 30 ya
Dhoruba.[4] Katika
kitabu hicho, Alhaj Jumbe anathibitisha kwamba “Ibara za Mkataba wa Muungano
ziliweka bayana mfumo ambao serikali kuu na serikali shiriki katika Muungano
kuwa na nguvu zinazoendeana, yaani, mfumo wa shirikisho ambao kuna mgawiko wa
mahakama, baraza la kutunga sheria na urais baina ya serikali kuu na serikali
mbili au zaidi, na kila serikali ikiwa na nguvu kamili ndani ya mamlaka yake.”[5]
Aina ya dola iliyotokana na Hati ya Makubaliano
ya Muungano haikuwahangaisha waasisi wa Muungano ama viongozi wake wakuu peke
yao. Hata ndani ya makorido ya mamlaka, mjadala juu ya suala hili umekuwa
mkubwa na umeundiwa Tume na Kamati mbali mbali za kulichunguza. Kwa mfano, hata
kabla ya kuchapishwa kwa Uongozi Wetu na Hatima ya Tanzania na The
Partner-ship, tarehe 6 Aprili, 1992, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza
la Mapinduzi Zanzibar, Dk. Salmin Amour aliunda Kamati ya Baraza la
Mapinduzi ya Kujenga Hoja Juu ya Masuala ya Muungano wa Tanzania, maarufu
kama Kamati ya Amina Salum Ali kutokana na jina la Mwenyekiti wake. Mheshimiwa
Ali Juma Shamuhuna, ambaye ni mjumbe wa Bunge hili Maalum, alikuwa Katibu wa
Kamati hiyo.
Pamoja na mambo mengine, Kamati ya Amina Salum
Ali ililichunguza suala la aina ya Muungano uliozaliwa na Hati ya Makubaliano
ya Muungano. Jibu la Kamati hiyo lilikubaliana na nusu ya hoja ya Mwalimu
Nyerere na nusu ya hoja ya Alhaj Aboud Jumbe: “... Muungano wa Tanzania,
haidhuru unaitwa ‘Union’, lakini uko kati na kati baina ya ‘Union’ na
Shirikisho. Kuwepo kwa Serikali ya Muungano yenye madaraka makubwa ni kielelezo
cha sura ya ‘Union’. Sura hii inazidi kutiliwa nguvu na kile kitendo cha
Tanganyika kuvua madaraka yake yote na kuyaingiza katika Serikali ya Muungano.
Kwa upande mwengine kuwepo kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar yenye madaraka
kamili Zanzibar juu ya mambo yote yasiyokuwa ya Muungano, ni kielelezo dhahiri
cha sura ya Shirikisho. Kwa hivyo, Muungano huu ni wa aina yake.”[6]
MTAZAMO WA KITAALUMA
Mheshimiwa Mwenyekiti,
Hati ya Makubaliano ya Muungano wa Jamhuri ya
Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar imejadiliwa sana na kwa miaka mingi
katika ulingo wa kitaaluma. Mjadala huu umehusu, kwa kiasi kikubwa, aina na
muundo wa Muungano huu. Katika kitabu chake Tanzania: The Legal Foundations
of the Union, kilichochapishwa kwa mara ya kwanza mwezi Januari, 1990,
Profesa Issa Shivji alisema, baada ya uchambuzi wa kina wa Hati ya Muungano,
kwamba Makubaliano ya Muungano yalitengeneza katiba ya shirikisho. Kwa mujibu
wa Profesa Shivji, katiba za shirikisho zina sifa kuu zifuatazo ambazo alisema
zipo katika Hati ya Muungano:[7]
a. Kuna mgawanyo wa wazi wa
madaraka kati ya serikali kuu na serikali za sehemu za muungano ambayo yapo
katika ngazi moja;
b. Mamlaka ya serikali kuu
yaliyowekewa mipaka ya wazi wakati mamlaka yaliyobaki yako mikononi mwa
serikali za sehemu za muungano;
c. Serikali zote, yaani
serikali kuu na serikali za sehemu za muungano zinagusa maisha ya wananchi wao
moja kwa moja tofauti na serikali ya mkataba (confederation) ambako
serikali za sehemu ndizo zinazogusa maisha ya wananchi moja kwa moja.[8]
Kwa maneno ya Profesa Shivji, kwa kuyaangalia
Makubaliano ya Muungano kutoka upande wa Zanzibar na Tanganyika na kwa ujumla
wao, “... msingi wa shirikisho ndio wenye nguvu na Makubaliano ya Muungano
yanaweza kutafsiriwa kwa usahihi kama katiba ya shirikisho.”[9] Kwingineko katika kitabu
hicho, Profesa Shivji alidai kwamba: “Kwa vyovyote vile, ni wazi kwamba
Makubaliano ya Muungano sio katiba ya muungano (unitary constitution).”[10]
Mheshimiwa Mwenyekiti,
Msimamo wa Profesa Shivji kuhusu Makubaliano ya
Muungano kuwa ni katiba ya shirikisho umeshikiliwa kwa miaka mingi na wasomi
wengine wa Muungano huu. Hivyo, kwa mfano, katika kitabu chao cha Tanzania
Treaty Practice kilichochapishwa mwaka 1973, Earl E. Seaton na S.T. Maliti
walikubali kwamba Makubaliano ya Muungano yaliunda katiba ya shirikisho na sio
katiba ya muungano.
Miaka kumi baadae, Wolfgang Dourado, aliyekuwa
Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar wakati Hati ya Muungano inasainiwa, naye alidai
kwamba Makubaliano ya Muungano hayakutengeneza dola la muungano bali
yalitengeneza ‘shirikisho la kweli.’[11] Wasomi wengine ambao wameitaja Katiba ya Tanzania kama katiba
ya shirikisho na wala sio ya muungano ni Profesa B.P. Srivastava katika makala
yake ya mwaka 1984 ‘The Constitution of the United Republic of Tanzania
1977: Some Salient Features, Some Riddles’[12], na Profesa Palamagamba J.A.M. Kabudi, katika International
Law Examination of the Union of Tanganyika and Zanzibar: A Federal or Unitary
State?, ambayo ni matokeo ya utafiti aliouwasilisha mwaka 1986 kwa ajili ya
Shahada yake ya Uzamili ya Kitivo cha Sheria cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Mwaka 2009 The Legal Foundations of the
Union kilichapishwa kwa mara ya pili, mara hii kikiwa na Utangulizi wa
Profesa Yash Ghai, Mkuu wa Kitivo cha Sheria cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
wa kwanza kutoka Afrika Mashariki na Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba
ya Kenya iliyozaa Katiba Mpya ya Kenya ya mwaka 2010.
Kwenye Utangulizi wake Profesa Ghai anasema
kwamba licha ya Tanzania kutokuwepo katika orodha za mashirikisho
zilizoandaliwa na wasomi au na Jukwaa la Kimataifa la Mashirikisho (International
Forum of Federations); na licha ya Katiba ya Tanzania kutokutumia neno
‘shirikisho’, bado Tanzania ni shirikisho.
“Tanzania inakidhi vigezo
vingi vya rasmi vya shirikisho: mahusiano kati ya sehemu zake tofauti yamewekwa
katika katiba, ambayo ni sheria kuu, na hayawezi kubadilishwa katika
ushirikisho wao bila kuungwa mkono na idadi mahsusi ya wabunge wa kutoka
Zanzibar na Bara ... wakipiga kura tofauti tofauti. Katiba inaweza kufanyiwa
marejeo na mahakama. Kuna aina mbili za serikali (serikali kuu na serikali za
sehemu za shirikisho), kila moja ikiwa na mamlaka yaliyoainishwa wazi. Kuna
mabunge ya shirikisho na ya sehemu yake ... na sheria za shirikisho na za
sehemu yake zikitumika katika nchi.”[13]
Tume ya Mabadiliko ya Katiba (‘Tume’) imetoa
maelezo marefu kuhusu madhumuni, lengo na sababu za mapendekezo ya ibara ya 1
ya Rasimu. Pamoja na mengine, kwa mujibu wa Tume, “... lengo la ibara hii ni
kuainisha aina na hadhi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa ni Muungano wa
Shirikisho lenye Mamlaka Kamili (Sovereign Federal State). Hatua hii ina lengo
la kuimarisha Muungano kwa kuipa Mamlaka ya Kidola Jamhuri ya Muungano na
kubainisha utambulisho, uwezo na mamlaka ya Nchi Washirika katika Muungano.”[14]
Malengo mengine ambayo Tume imeyataja malengo
mengine kuwa ni “... kuainisha mfumo wa utawala wa Jamhuri ya Muungano na
kupanua misingi muhimu ya nchi ...”; na kuonyesha kuwa “Hati ya Muungano
ya 1964 ndio chimbuko la Muungano wa Tanzania ... na ... kuipa hadhi ya
kikatiba Hati hiyo ... kwa ... (kuiingiza) ndani ya Katiba kama ibara
inayosimama yenyewe.”[15]
Tume imetaja sababu za mapendekezo haya kuwa ni
kutekeleza matakwa ya kifungu cha 9(2)(a) cha Sheria ya Mabadiliko ya
Katiba, Sura ya 83, yaliyoitaka Tume “... kuongozwa na misingi mikuu ya
kitaifa na maadili ya jamii ya kuhifadhi na kudumisha kuwepo kwa Jamhuri ya
Muungano.”[16] Aidha, kwa mujibu wa Tume, mapendekezo haya yatahifadhi asili,
taswira na hadhi ya Jamhuri ya Muungano katika jumuiya ya kimataifa kama
inavyotakiwa na Mkataba wa Montevideo Kuhusu Haki na Wajibu wa Nchi wa
mwaka 1933, ambao unatambua nchi yenye muundo wa shirikisho kuwa ni dola katika
sheria za kimataifa.[17]
Tume imetambua ukweli wa kihistoria kwamba
kumekuwepo mjadala wa miaka mingi miongoni mwa Watanzania “kuhusu aina ya
Muungano uliopo Tanzania iwapo ni shirikisho au la.”[18] Kwa sababu hiyo,
pendekezo hili litaondoa “utata wa aina na muundo wa Muungano ambao
umesababisha kuvunjwa kwa Katiba ya Jamhuri ya Muungano na Serikali zote mbili
mara kadhaa.”[19]
Tume iliridhika kwamba Jamhuri ya Muungano ni
Shirikisho. Kwa maneno yake: “Shirikisho hili linatokana na muungano wa
hiari wa Tanganyika na Zanzibar ambazo zilikuwa Jamhuri zenye mamlaka kamili
kabla ya kuungana tarehe 26 Aprili 1964.”[20] Tume inafafanua kwamba,
kwa kawaida nchi ambazo zimeingia katika muungano zinaweza kuchukua moja kati
ya sura tatu:
i. Muungano wa Serikali Moja (Unitary State);
ii. Muungano wa Shirikisho (Federation); na
iii. Muungano wa Mkataba (Confederation).
Kwa mujibu wa Tume, “... mfumo wa shirikisho
unakuwepo pale ambapo nchi mbili au zaidi zimeungana na hazikuunda serikali
moja. Kwa maana hiyo shirikisho ... linamaanisha mfumo wa utawala wa nchi wenye
sifa zifuatazo:
1. Kunakuwa na ngazi mbili za serikali zonazotawala eneo moja la
nchi na raia wale wale; moja ikisimamia mambo ya muungano (shirikisho) na
nyingine mambo yasiyo ya muungano (yasiyo ya shirikisho);
2. Kila ngazi ya serikali, yaani ile ya shirikisho na ile ya nchi
washirika inakuwa na mamlaka kamili na maeneo ya utendaji na uhakikisho wa
kikatiba wa uhuru wa kutoingiliana baina ya serikali hizo katika maeneo waliyo
na madaraka nayo bila ya kushauriana....;
3. Katika muundo huu, serikali ya muungano ndiyo yenye mamlaka juu
ya masuala yote yaliyokubaliwa kuwa ya muungano (shirikisho). Serikali za nchi
washirika zinakuwa na mamlaka ya kikatiba ya kushughulikia mambo yasiyo ya
muungano katika maeneo yao ya utawala; na
4. Katika muungano wa
shirikisho mamlaka kuu ya kidola (sovereign powers and
functions) yapo chini ya serikali ya shirikisho
(muungano).”[21]
Pamoja na kushindwa kufikisha idadi ya kura
inayotakiwa na kifungu cha 26(2) cha Sheria na kanuni ya 64(1), Wajumbe walio
wengi – karibu wote wanachama wa CCM – wamependekeza kufutwa kwa ibara ya 1(1)
na (2) ya Rasimu. Badala yake, wajumbe hao wanapendekeza ibara mpya ya 1(1)
isomeke kama ifuatavyo: “Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni nchi yenye
mamlaka kamili ambayo imetokana na Muungano wa nchi mbili za Jamhuri ya
Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar, ambazo kabla ya Hati ya Makubaliano
ya mwaka 1964 zilikuwa nchi huru.”[22]
Tofauti pekee ya mapendekezo haya na
mapendekezo ya ibara ya 1(1) ya Rasimu ni neno ‘Shirikisho.’ Hii ina maana
kwamba, licha ya ushahidi mkubwa wa kitaalamu tuliouonyesha hapa, wajumbe walio
wengi wa Kamati Namba Nne wanaamini kwamba Jamhuri ya Muungano sio Shirikisho.
Kwa mapendekezo haya, wajumbe na wanachama hawa wa CCM wanapendekeza kuendeleza
status quo, yaani sintofahamu ya kama Muungano huu ulitengeneza dola ya
ki-Shirikisho au dola ya ki-Muungano, ambayo imeugubika Muungano kwa nusu karne
ya uhai wake. Mapendekezo haya yataendeleza pia migogoro ya kikatiba na ya
kisiasa ambayo imekuwa ni sehemu ya uhai wa Muungano huu katika kipindi hicho
hadi kubatizwa jina la ‘Kero za Muungano.’
Mheshimiwa Mwenyekiti,
Kwa kuzingatia uchambuzi huu, ni wazi kwamba
kuendelea kutumia jina la ‘Jamhuri ya Muungano wa Tanzania’ kunaendeleza hisia
potofu kwamba Makubaliano ya Muungano yalianzisha dola ya muungano (unitary
state) na sio dola ya shirikisho (federal state). Aidha, kufanya
hivyo ni kuendeleza migogoro ya kisiasa na ya kikatiba ambayo, kama
tulivyoonesha, imetokana na kukosekana kwa ufafanuzi juu ya aina ya muungano
uliotokana na Hati ya Makubaliano ya Muungano. Hii, kwa maoni yetu, haiwezi
kuwa dawa ya matatizo ya Muungano huu.
Kwa sababu hiyo, ili kuweka wazi aina ya
muungano uliozaliwa na Hati ya Makubaliano ya Muungano; ili kuondoa hisia
potofu kwamba Makubaliano hayo yalizaa dola ya muungano, ili kupata ufumbuzi wa
kudumu wa ‘Kero za Muungano’, tunapendekeza kwamba maneno ‘Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania’ yaliyoko katika ibara ya 1 na ya 2 na katika ibara nyingine zote
za Rasimu yafutwe, na badala yake maneno ‘Shirikisho la Jamhuri za Tanganyika
na Zanzibar’ yaingizwe katika ibara husika.
Mapendekezo yetu yana manufaa makubwa
yafuatayo. Kwanza, yanaweka wazi kwamba muungano huu ni wa dola ya
ki-Shirikisho na wala sio dola ya ki-Muungano. Pili, mapendekezo haya yanaweka
bayana ukweli kwamba ni nchi mbili huru, yaani Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri
ya Watu wa Zanzibar ndizo zilizoungana. Uzoefu wa nchi nyingine zilizoungana
unaonyesha kwamba jina la muungano huweka bayana kwamba zilizoungana ni nchi
zaidi ya moja. Mifano ya wazi ya jambo hili ni majina ya Marekani (United
States of America); Uingereza (United Kingdom of Great Britain and Northern
Ireland), na Umoja wa Falme za Kiarabu (United Arab Emirates). Aidha, Urusi ya
zamani ilijulikana kama (Union of Soviet Socialist Republics) na Yugoslavia ya
zamani ilikuwa inaitwa Federal Socialist Republics of Yugoslavia.
Mheshimiwa Mwenyekiti,
Kuna sababu nyingine ya kuacha kutumia jina la
‘Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.’ Sababu hiyo ni utata wa kisheria na kikatiba
ambao umegubika jina la ‘Tanzania’ tangu lilipoanza kutumiwa nusu karne
iliyopita. Ili kufahamu vyema jambo hili ni vizuri kuanzia ‘Hati ya Kuzaliwa ya
Muungano’, yaani Hati ya Makubaliano ya Muungano. Kwa maudhui yake, Hati hiyo
inaonyesha wazi kwamba jina la Jamhuri mpya itakayoundwa kwa mujibu wake ni
‘Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.’
Jina hili linathibitishwa na Sheria ya
Kuthibitisha Mapatano ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar,[23] iliyotungwa na Bunge la
Jamhuri ya Tanganyika, siku tatu tu baada ya Hati ya Muungano kusainiwa: “Jamhuri
ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar zitakuwa, kuanzia Siku ya Muungano
na milele baada ya hapo, zimeungana kuwa Jamhuri moja yenye mamlaka kamili
itakayoitwa Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.”[24]
Sheria hiyo ilitungwa na Bunge Maalum, sio na
Bunge la kawaida, na kwa sababu hiyo ina haiba ya katiba. Ndio maana tangu
mwaka 1965 kwenye Katiba ya Muda, na hadi sasa kwenye Katiba ya Jamhuri ya
Muungano, Sheria hiyo ni Nyongeza kwenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano na
haiwezi kubadilishwa bila kuungwa mkono na theluthi mbili ya wabunge wote wa
Bunge la Jamhuri ya Muungano wakikaa kama wajumbe wa Bunge Maalum.[25]
Hata hivyo, mnamo tarehe 3 Disemba, 1964, Bunge
la Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar – likiwa limekaa kama Bunge la
kawaida - lilitunga Sheria ya Kutangaza Jina la Jamhuri ya Muungano, ya
mwaka 1964, yaani, The United Republic (Declaration of Name) Act, 1964.[26] Sheria hiyo ilibadilisha masharti ya kifungu
cha 4 cha Sheria ya Kuthibitisha Mapatano ya Muungano ambacho
kilitangaza jina la Jamhuri ya Muungano kuwa ni ‘Jamhuri ya Muungano wa
Tanganyika na Zanzibar.’
Kifungu cha 2(1) cha Sheria hiyo mpya kilitamka
kwamba: “Bila kujali masharti ya kifungu cha 4 cha Sheria za Muungano wa
Tanganyika na Zanzibar, inatangazwa kwamba kuanzia sasa Jamhuri ya Muungano wa
Tanganyika na Zanzibar itajulikana kama Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na
sheria zilizopo za Tanganyika na Zanzibar zitatafsiriwa hivyo hivyo.”
Mabadiliko haya ya jina la Jamhuri ya Muungano ni mfano mwingine wa utamaduni
wa ukiukaji sheria (culture of illegality) ambao umegubika Muungano huu
tangu siku ya kwanza ya kuzaliwa kwake:
(a) Kwa mujibu wa aya ya (iv) ya Hati ya Makubaliano ya Muungano,
Bunge la Jamhuri ya Muungano halikuwa na mamlaka ya kubadilisha jina la Jamhuri
ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar;
(b) Kwa kuwa Sheria ya Kuthibitisha Mapatano ya Muungano ilitungwa
na Bunge Maalum, na kwa hiyo ina haiba ya Katiba, Sheria ya Kutangaza Jina la
Jamhuri ya Muungano – ambayo ni sheria ya kawaida – ni batili kwa vile na kwa
kiasi inavyokinzana na Sheria ya Kuthibitisha Mapatano ya Muungano;
(c) Jina la ‘Jamhuri ya Muungano wa Tanzania’ lilianza kutumiwa hata
kabla ya Sheria ya Kutangaza Jina la Jamhuri ya Muungano kutungwa:
(i) Kifungu cha 2(2) cha Sheria hiyo kinasema kwamba “kutajwa kwa
Jamhuri ya Muungano kama Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kipindi
chochote kati ya tarehe ishirini na nane ya Oktoba, 1964 na kuanza kutumika kwa
Sheria hii kutachukuliwa kuwa ni kutajwa kihalali na muafaka na uhalali wa
tendo lolote hautahojiwa kwa sababu tu ya matumizi ya (jina hilo) badala ya
lile la Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.” Hii inadhihirisha
kwamba jina la ‘Jamhuri ya Muungano wa Tanzania’ lilianza kutumika tarehe 28
Oktoba, 1964, bila ya uhalali wowote wa kisheria[27];
(ii) Tarehe 2 Novemba, 1964, yaani mwezi mmoja kabla ya Sheria ya
Kutangaza Jina la Jamhuri ya Muungano kutungwa, Ubalozi wa Kudumu wa
Jamhuri ya Tanganyika katika Umoja wa Mataifa mjini New York, Marekani,
ulimtumia Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa waraka wa kidiplomasia (note
verbale) ukimjulisha kwamba “Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na
Zanzibar, kuanzia sasa, itajulikana kama Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.”
Waraka huo haukuwa na jina, cheo wala sahihi ya
Ofisa wa Ubalozi wa Kudumu aliyeutuma lakini uligongwa muhuri wenye nembo ya
taifa iliyoandikwa ‘Jamhuri ya Tanganyika.’ Kifungu cha 12 cha Sheria ya
Nembo za Taifa, yaani National Emblems Act, Sura ya 10 ya Sheria za
Tanzania, kinaelekeza kwamba “popote nembo ya taifa inapotumiwa katika
waraka au kitu chochote, matumizi hayo yatahalalishwa au kuthibitishwa na
sahihi ya mtunzaji wa nembo hiyo.”
Kwa vile note verbale iliyomjulisha Katibu
Mkuu wa Umoja wa Mataifa juu ya mabadiliko ya jina la Jamhuri ya Muungano wa
Tanganyika na Zanzibar na kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliwekewa nembo
ya taifa ya Tanganyika bila kusainiwa na mtunzaji wa nembo hiyo, ni wazi kwamba
note verbale hiyo haikuwa na uhalali wowote.
Kwa sababu ya mazingira ya kisiasa ya utawala
wa kiimla wa chama kimoja, kwa miaka mingi ilikuwa vigumu kuhoji uhalali wa
matumizi ya jina la ‘Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.’ Hata hivyo, wapo watu
wachache ambao wamehoji uhalali wa jina hili. Hivyo, kwa mfano, marehemu George
Liundi, aliyekuwa Msajili wa Vyama vya Siasa wa kwanza mara baada ya kurudishwa
kwa mfumo wa vyama vya siasa nchini aliwahi kusema yafuatayo katika Kongamano
la Vyama vya Siasa lililofanyika katika Hotel ya Golden Tulip, Dar es Salaam,
kati ya tarehe 12-14 Disemba, 2002:
“Prior to the enactment of
the Interim Constitution of 1965, another constitutional problem appears to
have been created by the change of name of the United Republic of Tanganyika
and Zanzibar to the United Republic of Tanzania, with effect from 11th
December 1964.... This change of name calls for scrutiny, because on the face
of it the measure appears to have put into question the constitutional status
(in terms of national sovereignty) of both the territories formerly
constituting the Republic of Tanganyika and Zanzibar respectively.”
Kwa maneno mengine:
“Kabla ya kutungwa kwa
Katiba ya Mpito ya 1965, tatizo lingine la kikatiba linaelekea lilitengenezwa
na mabadiliko ya jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kwenda
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kuanzia tarehe 11 Disemba, 1964.... Mabadiliko
haya ya jina yanahitaji kuchunguzwa kwa sababu, kwa juu juu tu hatua hii
inaonekana ilihoji hadhi ya kikatiba (kwa maana ya uhuru wa kitaifa) wa maeneo
ambayo yalijumuisha Jamhuri za Tanganyika na Zanzibar.”[28]
Ni wazi, kwa misingi hii ya kisheria, jina la
‘Jamhuri ya Muungano wa Tanzania’ ni batili kisheria, licha ya ukweli kwamba
limetumika kwa nusu karne. Kwa maoni yetu, kama kweli tunaamini – kama
inavyopendekeza Tume - kwamba ‘msingi mkuu’ wa Jamhuri ya Muungano ni Hati ya
Makubaliano ya Muungano, wakati umefika wa kuyaheshimu Makubaliano ya Muungano
kwa kurudisha matumizi ya jina lililotumiwa katika Makubaliano hayo, yaani
Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Tarehe 22 Aprili, 1964 Rais wa Jamhuri ya
Tanganyika, Mwalimu Julius K. Nyerere, na Rais wa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar,
Sheikh Abedi Amani Karume walitia saini Hati ya Makubaliano ya Muungano kati
ya Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar. Hati hiyo ndiyo
inayotajwa katika ibara ya 1(1) na (3) ya Rasimu. Wakati wa mjadala wa Sura ya
Kwanza na ya Sita, wajumbe wa Kamati Namba Nne – kama ilivyokuwa kwa wajumbe wa
Kamati nyingine za Bunge lako tukufu – waliletewa nakala ya Sheria ya
Kuthibitisha Mapatano ya Muungano, Sheria Na. 22 ya 1964, yaani The Union
of Tanganyika and Zanzibar Act, Sura ya 557 ya Sheria za Tanzania. Nakala
ya Sheria hiyo ilitolewa baada ya baadhi ya wajumbe wa Bunge Maalum kuomba
kupatiwa nakala halisi ya Hati ya Makubaliano ya Muungano iliyosainiwa na
Mwalimu Nyerere na Sheikh Karume.
Ijapokuwa nakala ya Sheria ya Kuthibitisha
Mapatano ya Muungano waliyogawiwa wajumbe imeambatanisha Hati ya Makubaliano
ya Muungano kati ya Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar
kama Nyongeza ya Sheria hiyo, hicho sicho walichoomba wajumbe wa Bunge Maalum.
Nakala ya Sheria ya Kuthibitisha Mapatano ya Muungano sio, na haiwezi kuwa,
mbadala wa nakala halisi ya Hati ya Makubaliano ya Muungano. Hii ni kwa sababu,
Nyongeza ya Sheria waliyogawiwa wajumbe – ambayo inadaiwa kuwa ndio Hati ya Makubaliano
ya Muungano - haina saini za Mwalimu Nyerere na Sheikh Karume. Ni vigumu, kwa
hiyo, kuthibitisha kama kweli kile kinachodaiwa kuwa ni Hati ya Makubaliano ya
Muungano ndicho hicho walichokubaliana waasisi hao wa Muungano kwa kutia saini
zao.
Suala la kushindwa kupatikana kwa nakala halisi
ya Hati ya Makubaliano ya Muungano sio jambo dogo. Suala hili ndio ufunguo wa
kuelewa mgogoro mkubwa wa kikatiba na kisiasa ambao umeugubika Muungano katika
nusu karne ya maisha yake. Hii ni kwa sababu, katika kipindi chote hicho,
kumekuwa na mgogoro mkubwa kuhusu kitu gani hasa Mwalimu Nyerere na Sheikh
Karume walikubaliana kwa niaba ya nchi zao. Bila kupatikana kwa nakala halisi
ya Hati, uhalali mzima wa Muungano wenyewe, na wa mambo yote yaliyofanyika kwa
jina la Muungano kwa takriban nusu karne, unakuwa kwenye mashaka makubwa.
Siku moja baada ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanganyika na Zanzibar kuzaliwa, yaani tarehe 27 Aprili 1964, Mwanasheria Mkuu
na Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Bw. C.A. Stavropoulos alimwandikia
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Bw. U Thant, waraka wa kiofisi uliohusu
‘Uanachama Katika Umoja wa Mataifa wa Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na
Zanzibar.’ Kwa mujibu wa Bw. Stavropoulos, waraka wake ulitokana na taarifa za
vyombo vya habari zilizoonyesha kwamba Tanganyika na Zanzibar, ‘ambazo kabla
zilikuwa wanachama tofauti wa Umoja wa Mataifa’, zilikuwa zimeungana na
kuunda dola moja yenye uwakilishi wa pamoja nchi za nje. Kwa vile Serikali za
Jamhuri ya Tanganyika na Serikali ya Jamhuri ya Watu wa Zanzibar zilikuwa
hazijapeleka taarifa rasmi Umoja wa Mataifa juu ya Muungano wa nchi zao, Bw.
Stavropoulos alipendekeza kwamba “mwakilishi wa Tanganyika ataarifiwe juu ya
haja ya kupata tamko rasmi kutoka kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano ...
kuhusu kuanzishwa kwa Jamhuri hiyo ... na hati mpya za utambulisho wa
mwakilishi mmoja kutoka Jamhuri (ya Muungano). (Itakuwa vizuri vile vile kwa
mwakilishi husika kutupatia nakala ya makubaliano yaliyopelekea Muungano huo.)”
Ijapokuwa tarehe 6 Mei, 1964, Wizara ya Mambo
ya Nje ya Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ilipeleka taarifa ya
maandishi iliyodai kuambatanisha nakala ya Hati ya Makubaliano ya Muungano,
kuna mashaka ya msingi kama kweli Hati hiyo ilipelekwa Umoja wa Mataifa. Hii ni
kwa sababu, tarehe 14 Mei, 1964, yaani wiki moja baadae na takriban wiki tatu
baada ya Muungano, Bw. Stavropoulos alimwandikia Deputy Chief de Cabinet wa
Umoja wa Mataifa Bw. Jose Rolz-Bennett kumwelekeza apeleke ujumbe wa simu ya
maandishi kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano, kuhusu masharti ya kusajili Hati
ya Makubaliano ya Muungano katika Sekretarieti ya Umoja wa Mataifa kama
inavyotakiwa na ibara ya 102 ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa. “... Serikali
inayosajili inatakiwa kuwasilisha kwa Sekretarieti nakala moja ya Makubaliano
iliyothibitishwa kwamba ni nakala ya kweli na kamili ... nakala mbili za ziada
na taarifa inayohusu tarehe na namna ya kutiliwa nguvu Makubaliano hayo.”[29]
Mheshimiwa Mwenyekiti,
Sasa kuna uthibitisho kwamba Serikali ya
Jamhuri ya Muungano haijawahi kuwasilisha Hati ya Makubaliano ya Muungano
katika Sekretarieti ya Umoja wa Mataifa. Tarehe 25 Machi 2009, Afisa Habari za
Kisheria kwenye Kitengo cha Mikataba ya Kimataifa katika Ofisi inayoshughulikia
masuala ya kisheria ya Umoja wa Mataifa Bw. Andrei Kolomoets, alimtaarifu
mtafiti mmoja kwa maandishi kwamba: “Hakuna ushahidi wowote kwamba Hati ya
Makubaliano ya Muungano ilisajiliwa kwenye Sekretarieti ya Umoja wa Mataifa. Kama
ingesajiliwa, kungelikuwa na hati ya usajili iliyoambatanishwa. Nimeangalia,
hakuna kitu hicho.
Mheshimiwa Mwenyekiti,
Kwa miaka yote hamsini ya Muungano, nakala ya
Hati ya Makubaliano ya Muungano haijawahi kuonyeshwa hadharani. Aidha, hata
ilipodaiwa mahakamani katika Mahakama Kuu ya Zanzibar, Mwanasheria Mkuu wa
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Iddi Pandu Hassan, alisema katika barua yake ya
tarehe 22 Juni, 2005 kwamba: “Ofisi yangu haikuweka kumbu kumbu ya nakala ya
mkataba wa asili (original) wa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar hapo tarehe
26 Aprili, 1964.”[30]
Kwa ushahidi huu kutoka Makao Makuu ya Umoja wa
Mataifa, na wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, hakuna shaka tena kwamba
Hati ya Makubaliano inayozungumzwa katika ibara 1(1) na (3) ya Rasimu haijawahi
kuwepo. Hii ndio kusema kwamba hakuna ajuaye ni kitu gani hasa Mwalimu Nyerere
na Sheikh Karume walisaini siku hiyo ya tarehe 22 Aprili, 1964. Kwa maoni yetu,
hiki ndio chanzo cha sintofahamu na migogoro yote kuhusu Muungano huu.
UTEKELEZAJI WA ‘MAKUBALIANO YA MUUNGANO’
Hata kama tukikubali, in arguendo,
kwamba kile kilichopo kwenye Sheria ya Kuthibitisha Mapatano ya Muungano ndio
Hati yenyewe ya Makubaliano ya Muungano, bado kuna hoja kubwa na ya msingi
kwamba Hati hiyo haiwezi kuwa msingi wa Shirikisho la Jamhuri za Tanganyika na
Zanzibar tunalolipendekeza. Hii ni kwa sababu, katika miaka hamsini tangu
kusainiwa kwa Hati ya Makubaliano ya Muungano na kuzaliwa kwa Muungano,
Makubaliano hayo yamechakachuliwa na kuvunjwa karibu kila mahali na kwa kipindi
chote cha kuwepo kwa Jamhuri ya Muungano. Kabla hatujaanika uchakachuaji huu,
ni muhimu tuyarejelee masharti yaliyomo kwenye hiyo inayoitwa Hati ya
Makubaliano ya Muungano.
Aya ya (i) ya Hati ya Makubaliano inatamka
kwamba “Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar zitaungana na
kuwa Jamhuri moja huru.” Aya ya (ii) inaweka Kipindi cha Mpito cha kuanzia
tarehe ya kuanza kwa Muungano hadi tarehe ya Bunge Maalum kukutana na kupitisha
Katiba kwa ajili ya Jamhuri ya Muungano. Katika kipindi hicho “... Jamhuri
ya Muungano itaongozwa kwa mujibu wa masharti ya aya za (iii) hadi (vi) za Hati
ya Makubaliano.”
Masharti hayo ni kuwa katika kipindi hicho cha
mpito, Jamhuri ya Muungano itaongozwa na Katiba ya Tanganyika ambayo
itarekebishwa ili kuwezesha kuwepo kwa bunge na serikali ya na kwa ajili ya
Zanzibar ambayo itaundwa kwa mujibu wa sheria za Zanzibar na yenye mamlaka
kamili ndani ya Zanzibar kwa mambo yote isipokuwa kwa mambo ambayo yametengwa
kwa ajili ya Bunge na Serikali ya Jamhuri ya Muungano.[31]
Aidha, kutakuwa na Makamu wawili wa Rais ambapo
mmoja wao (ambaye kwa kawaida ni mkazi wa Zanzibar) atakuwa Mkuu wa Serikali ya
na kwa ajili ya Zanzibar na atakuwa msaidizi mkuu wa Rais wa Jamhuri ya
Muungano katika utekelezaji wa majukumu yake kuhusu Zanzibar.[32] Vile vile, kutakuwa na uwakilishi wa Zanzibar
katika Bunge la Jamhuri ya Muungano[33]; na mambo mengine yatakayohitajika ili kuipa uwezo Jamhuri ya
Muungano na Hati za Muungano.[34]
Masharti mengine ni kuwapo kwa orodha ya Mambo
ya Muungano ambayo Bunge na Serikali ya Jamhuri ya Muungano zilipewa mamlaka
kamili kwa Jamhuri ya Muungano yote nje ya mamlaka yake kamili kwa mambo
yasiyokuwa ya Muungano ya na kwa ajili ya Tanganyika.[35] Mambo ya Muungano ni pamoja na Katiba na
Serikali ya Jamhuri ya Muungano; mambo ya nje; ulinzi; polisi; mamlaka ya hali
ya hatari; uraia; uhamiaji; biashara ya nje na mikopo; utumishi wa umma wa
Jamhuri ya Muungano; kodi ya mapato, kodi ya mashirika na ushuru wa forodha na
wa bidhaa; na bandari, usafiri wa anga, posta na simu.
Masharti mengine ni kwamba sheria zilizokuwepo
Tanganyika na Zanzibar kabla ya Muungano zitaendelea kutumika ‘katika maeneo
yao’ hadi hapo zitakaporekebishwa ili kutilia nguvu Muungano na Hati za
Muungano; au sheria mpya zitakapotungwa na mamlaka husika au kutolewa kwa amri
ya Rais wa Jamhuri ya Muungano kwa ajili ya utekelezaji wa Mambo ya Muungano
kwa upande wa Zanzibar. Masharti ya mwisho ni kutangazwa kwa Mwalimu Julius K.
Nyerere kuwa Rais wa kwanza wa Jamhuri ya Muungano[36], na Sheikh Abeid Karume kuwa Makamu wa Rais
kutoka Zanzibar.[37]
Mheshimiwa Mwenyekiti,
Kwa mujibu wa aya ya (vii) ya Hati ya Muungano,
Rais wa Jamhuri ya Muungano alipaswa, kwa makubaliano na Makamu wa Kwanza wa
Rais, kuteua Tume kwa ajili ya kuandaa Katiba ya Jamhuri ya Muungano[38]; na kuitisha Bunge Maalum lenye wawakilishi
kutoka Tanganyika na kutoka Zanzibar na kwa idadi watakayoamua kwa lengo la
kujadili na kupitisha Katiba ya Jamhuri ya Muungano.[39] Bunge hilo Maalum lilitakiwa kuitishwa ndani
ya kipindi cha mwaka mmoja kuanzia tarehe ya kuzaliwa Muungano, yaani tarehe 26
Aprili, 1964.[40] Hiki ndicho kilikuwa
kipindi cha mpito kinachotajwa katika aya ya (ii) ya Hati ya Makubaliano.
Aya ya (viii) na ya mwisho ya Hati ya
Makubaliano ililazimu Hati ya Makubaliano ya Muungano kuthibitishwa kwa Bunge
la Tanganyika na Baraza la Mapinduzi na Baraza la Mawaziri la Zanzibar kutunga
sheria za kuridhia Hati ya Makubaliano na kuanzishwa kwa Serikali ya Jamhuri ya
Muungano na ya Zanzibar kwa mujibu wa Hati ya Makubaliano.
Sasa tunaomba tuthibitishe hoja yetu kwamba
miaka hamsini ya Hati ya Makubaliano ya Muungano na ya Muungano ni nusu karne
ya uchakachuaji na ya nchi yetu kuishi kwa uongo na ujanja ujanja:
1. Wakati Bunge la Tanganyika
liliitishwa kwa dharura tarehe 25 Aprili, 1964 ili kupitisha sheria ya
kuthibitisha Hati ya Makubaliano ya Muungano, na lilipitisha Sheria ya
Kuthibitisha Mapatano ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, upo ushahidi
wa kutosha kwamba Baraza la Mapinduzi na Baraza la Mawaziri la Zanzibar
halijawahi kutunga sheria yoyote ya kuthibitisha Hati ya Makubaliano ya
Muungano kwa kipindi chote cha maisha ya Muungano huu:
(a). Profesa Issa G. Shivji katika kitabu chake Pan Africanism or
Pragmatism? Lessons of Tanganyika – Zanzibar Union amethibitisha kwamba
kile kinachoitwa Sheria ya Kuthibitisha Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ya
mwaka 1964 “... iliandaliwa na kuandikwa na maafisa wa sheria wa Tanganyika
wakiwa Tanganyika.... Hii ni kwa sababu ya ukweli wa kisiasa uliokuwapo wakati
huo ambapo Baraza la Mapinduzi kwa ujumla wake halikuukubali Muungano. Hakuna
shaka kwamba Muungano ‘ulilazimishwa.’ Hivyo, maafisa wa kisheria wa kigeni wa
Serikali ya Tanganyika (waliokuwa pia marafiki wa Nyerere) walitumia mbinu ya
kisheria ya kuchapisha Sheria ya Kuthibitisha Muungano wa Tanganyika na
Zanzibar, 1964, (inayodaiwa kutungwa na Baraza la Mapinduzi Zanzibar)
waliyoitengeneza wao, katika Gazeti rasmi la Serikali ya Jamhuri ya Muungano
chini ya saini ya (Kaimu Mwanasheria Mkuu wa Tanganyika) P.R. Nines Fifoot.”
(b)Aliyekuwa Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu wa Baraza la
Mwaziri wa Serikali ya Jamhuri ya Watu wa Zanzibar kati ya tarehe 18 Januari na
Juni 1964, Salim Said Rashid ametamka yafuatayo kwa kiapo cha tarehe 22 Aprili
2006:
(i) Kwamba hakuwahi “... kupokea maagizo kutoka kwa Rais wa
Zanzibar kwa ajili ya kuitisha kikao cha kujadili na kupitisha mkataba wa
kuunganisha Jamhuri ya Watu wa Zanzibar na Jamhuri ya Tanganyika.”
(ii) Kwamba “suala la kuunganisha Jamhuri ya Watu wa Zanzibar na
Jamhuri ya Tanganyika halikuwahi kujadiliwa na kikao chochote cha Baraza la
Mapinduzi na Baraza la Mawaziri la Serikali ya Zanzibar au kujadiliwa na
taasisi yoyote ya Serikali ya Zanzibar.”
(iii) Kwamba anakumbuka “... kupokea maagizo kutoka kwa Rais wa
Zanzibar kuwa anataka kuufanya Muungano na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar na
Jamhuri ya Tanganyika na baadae alinionyesha mapendekezo ya rasimu ya Muungano
kati ya Jamhuri ya (Watu wa) Zanzibar na Jamhuri ya Tanganyika.”
(iv) Kwamba “... rasimu hiyo ililetwa na Mawaziri kutoka Serikali
ya Jamhuri ya Tanganyika na kukabidhiwa Rais ikiwa tayari imeshaandikwa
kuunganishwa Jamhuri hizi mbili.”
(v) Kwamba baada ya kuonyeshwa mapendekezo hayo ya Muungano, “...
niliagizwa na Rais wa Zanzibar nisimwonyeshe mtu yoyote na wala asipewe
Mwanasheria wa Serikali ya Zanzibar.”
(vi) Kwamba “... sikupata maagizo yoyote kutoka kwa Rais ili
kuwajulisha viongozi wa Baraza la Mapinduzi juu ya kuitisha kikao au kuja
kushuhudia makubaliano ya kuunganisha nchi ya Zanzibar yakitiwa sahihi.”
(vii) Kwamba, kwa sababu hiyo, “... hakuna shughuli yoyote au kikao
kilichofanyika kwa ajili ya kutia saini mkataba wa Muungano kwa mujibu wa
decree Na. 5 ya mwaka 1964 ya Serikali ya Jamhuri ya Watu wa Zanzibar.”
(viii) Bw. Rashid anaelezea utaratibu wa kisheria uliotakiwa kufuatwa: “...
Kwa mujibu wa Presidential Decree ya 1964, kila jambo lilitakiwa kujadiliwa na
kikao cha Baraza la Mapinduzi na kuarifiwa Mwanasheria Mkuu atayarishe
presidential decree kwa mujibu wa utaratibu na baadae sisi tusaini nikiwa mimi
Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Baraza la Mawaziri Zanzibar na asaini Rais wa
Jamhuri ya Watu wa Zanzibar na baadae kutolewa katika official gazette (gazeti
rasmi la serikali) huo ndio ulikuwa utaratibu.”
(ix) Kwamba kwa sababu utaratibu huo ulikiukwa, “... kitendo cha
kuunganisha Jamhuri ya Watu wa Zanzibar na Jamhuri ya Tanganyika hakikupata
Baraka za Baraza la Mapinduzi na kuthibitishwa na kikao halali cha Baraza la
Mawaziri la Zanzibar.”
(c)Katika kitabu chake The Partner-ship, Alhaj Aboud Jumbe
amesema yafuatayo kuhusu kusainiwa kwa Makubaliano ya Muungano:
(i) “Ilikuwa ni asubuhi ya Aprili 22, 1964 pale Julius Kambarage
Nyerere alipowasili Zanzibar. Rais huyo wa Jamhuri ya Tanganyika alikuja na
nakala ya mapendekezo ya Mkataba uliotayarishwa Tanganyika na ulioandikwa kwa
lugha ya Kiingereza. Waraka huo uliwakilisha jumla ya makubaliano ambayo
yalifikiwa siku hiyo hiyo baina ya Rais wa Jamhuri ya Tanganyika, Julius
Nyerere na Rais wa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar, Abedi Amani Karume. Makubaliano
hayo kwanza kabisa yalitiwa sahihi katika Ikulu ya Zanzibar na hapo baadae kuwa
ndio Mkataba wa Muungano, 1964.”
(ii) Aidha, “mimi nilikuwa Mjumbe wa Baraza la Mapinduzi, kwa
wakati mmoja au mwengine, kwa cheo kimoja au chengine kutokea kuanzishwa kwa
Baraza hilo hapo Januari 1964 hadi mwaka 1984 na nimeshindwa katika kumbukumbu
zangu kupata ushahidi wa kufanyika kikao cha Baraza la Mapinduzi kama ni
Zanzibar au Dar es Salaam ili kuthibitisha Mkataba wa Muungano.”
Kwa hiyo, Makubaliano ya Muungano yalipata
ridhaa ya upande mmoja tu, yaani Watanganyika kwa kupitia Bunge lao, wakati
Wazanzibari kwa kupitia Bunge lao, yaani Baraza la Mapinduzi, hawakuwahi kutoa
ridhaa yao kwa Muungano huu. Ni wazi, kwa hiyo, kwamba - kwa sababu hiyo -
Jamhuri ya Muungano ilizaliwa bila uhalali wowote wa kisheria. Kwa maneno ya
Profesa Shivji, “Hakuna shaka kwamba Muungano ‘ulilazimishwa.’”
(d) Katika kitabu chake kiitwacho 50 Years of Independence: A
Concise Political History of Tanzania, kilichochapishwa Januari ya mwaka
huu 2014, Mzee Pius Msekwa, Makamu Mwenyekiti mstaafu wa CCM na Katibu Mtendaji
wake wa kwanza amesema yafuatayo kuhusu mambo yaliyofanyika baada ya
Makubaliano ya Muungano kusainiwa:
(i) Tarehe 26 Aprili, 1964, yaani Siku ya Muungano, Rais Nyerere
alitunga Presidential Decree (Amri ya Rais) iliyoitwa The Transitional
Provisions Decree, 1964, yaani, Amri ya Masharti ya Mpito ya mwaka 1964,
iliyochapishwa katika Gazeti la Serikali la siku hiyo.[41] “Amri hiyo
iliwabadilisha watu waliokuwa watumishi wa Serikali ya Jamhuri ya Tanganyika na
kuwafanya watumishi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano.[42] Mahakama Kuu ya
Tanganyika iligeuzwa kuwa Mahakama Kuu ya Jamhuri ya Muungano[43]; na nembo ya taifa ya
Jamhuri ya Tanganyika iligeuzwa kuwa nembo ya taifa ya Jamhuri ya Muungano.”[44]
(ii) Tarehe hiyo hiyo, Rais Nyerere alitunga Amri nyingine ya Rais
iliyoitwa The Interim Constitution Decree, 1964, yaani, Amri ya
Katiba ya Muda ya mwaka 1964.[45] “Amri hii iliitangaza Katiba ya Tanganyika kuwa ndiyo Katiba
ya Muda ya Jamhuri ya Muungano.[46] Kifungu cha 4 cha Amri hii ndicho kilichoipatia Serikali ya
Muungano majukumu kuhusu mambo yote ya Muungano katika Jamhuri ya Muungano yote
na vile vile kwa mambo yasiyokuwa ya Muungano kwa upande wa Tanganyika.”
(iii) Tarehe 15 Juni 1964 Mwalimu Nyerere alitunga Amri nyingine tena
iliyoitwa The Transitional Provisions (No. 2) Decree, 1964, yaani, Amri
ya Masharti ya Mpito (Na. 2) ya mwaka 1964. Amri hii ilielekeza kwamba
mahali popote ambapo sheria zilizopo zimetaja jina la ‘Tanganyika’ basi jina
hilo lifutwe na badala yake jina la ‘Jamhuri ya Muungano’ liwekwe. Vile vile,
Amri hiyo ilielekeza, mahali popote ambapo ‘Serikali ya Tanganyika’ imetajwa,
au kwenye jambo au kitu chochote ambacho kwa namna yoyote kinamilikiwa au
kinahusishwa na Serikali hiyo, basi itachukuliwa kuwa ni Serikali ya Jamhuri ya
Muungano ndiyo iliyotajwa.
(iv) Kwa maneno ya Mzee Msekwa mwenyewe: “Tanganyika was thus
decreed out of existence. The cumulative effect of these legislative measures
was that the political entity which was Tanganyika, was decreed totally out of
existence. That is the reason why even the name of the geographical unit
formerly known as Tanganyika, had to be changed to Tanzania Mainland.”
Tafsiri ya maneno haya ni kwamba “uhai wa Tanganyika ulitolewa kwa njia hiyo
ya amri. Athari za jumla za Amri hizi ni kwamba eneo la kisiasa ambalo ndio
ilikuwa Tanganyika lilitolewa uhai wake moja kwa moja kwa amri. Hii ndiyo
sababu hata jina la eneo la kijiografia lililojulikana zamani kama Tanganyika
ilibidi libadilishwe na kuwa Tanzania Bara.”
2. Vitendo vya kuivika
Jamhuri ya Tanganyika joho la Muungano na kuigeuza kuwa ndio Jamhuri ya
Muungano hakikuwa na uhalali wowote kwa mujibu wa Makubaliano ya Muungano:
(a) ya (v) ya Hati ya Makubaliano ya Muungano ilitamka wazi
kwamba “sheria zilizopo za Tanganyika na za Zanzibar zitaendelea kutiliwa
nguvu katika maeneo yao....” Kwa maana hiyo:
(i) Rais Nyerere hakuwa na mamlaka yoyote kwa mujibu wa Makubaliano
ya Muungano wala chini ya Katiba na Sheria za Tanganyika ya kugeuza sheria zote
za Jamhuri ya Tanganyika kuwa sheria za Jamhuri ya Muungano hata kwa mambo
yasiyokuwa ya Muungano;
(ii) Rais Nyerere hakuwa na mamlaka yoyote kwa mujibu wa Makubaliano
ya Muungano wala kwa mujibu wa Katiba na Sheria za Tanganyika ya kuwageuza
watumishi wote wa Jamhuri ya Tanganyika kuwa watumishi wa Jamhuri ya Muungano
hata kwa mambo yasiyokuwa ya Muungano;
(iii) Rais Nyerere hakuwa na mamlaka yoyote kwa mujibu wa Makubaliano
ya Muungano au kwa mujibu wa Katiba na Sheria za Tanganyika ya kugeuza Mahakama
Kuu ya Tanganyika kuwa Mahakama Kuu ya Jamhuri ya Muungano;
(iv) Rais Nyerere hakuwa na mamlaka yoyote kwa mujibu wa Makubaliano
ya Muungano au kwa mujibu wa Katiba na Sheria za Tanganyika ya kugeuza Nembo ya
Taifa ya Jamhuri ya Tanganyika kuwa Nembo ya Taifa ya Jamhuri ya Muungano.
Nembo za Taifa, yaani ‘Bibi na Bwana’ inayotumika hadi leo hii ni Nembo ya
Taifa ya Jamhuri ya Tanganyika!
(v) Rais Nyerere hakuwa na mamlaka yoyote kwa mujibu wa Makubaliano
ya Muungano au kwa mujibu wa Katiba na Sheria za Tanganyika ya kufuta matumizi
ya jina la Tanganyika katika sheria zote za Jamhuri ya Tanganyika au katika
mambo au vitu vyote vilivyokuwa vinamilikiwa ama kuhusishwa na Jamhuri ya
Tanganyika hata kwa mambo yasiyokuwa ya Muungano ya Tanganyika;
(vi) Rais Nyerere hakuwa na mamlaka yoyote kwa mujibu wa Makubaliano
ya Muungano au kwa mujibu wa Katiba na Sheria za Tanganyika ya ‘kutoa uhai wa
nchi ya Tanganyika kwa njia ya Amri ya Rais’ au kwa njia nyingine yoyote ya
kisheria na kuigeuza kuwa Jamhuri ya Muungano.
MAMBO YA MUUNGANO NA KUMEZWA KWA ZANZIBAR
Mheshimiwa Mwenyekiti,
Kama tulivyokwishaonesha, kwa mujibu wa aya ya
(iv) ya Makubaliano ya Muungano na kifungu cha 5(1) cha Sheria ya Kuthibitisha
Mapatano ya Muungano, Mambo ya Muungano yaliyokubaliwa kwenye Makubaliano ya
Muungano yalikuwa kumi na moja. Haya ni mambo yaliyoko katika vipengele vya 1
hadi 11 vya Nyongeza ya Kwanza ya Katiba ya sasa ya Jamhuri ya Muungano.
Hata hivyo, kati ya mwaka 1964 and 1973 mambo
mengine sita – yanayoonekana katika vipengele 12 hadi 16 vya Nyongeza ya Kwanza
– yaliongezwa katika orodha ya Mambo ya Muungano. Hivyo basi, mwaka 1965
masuala ya fedha, sarafu na benki yaliongezwa; mwaka 1967 leseni ya viwanda na
takwimu, elimu ya juu na mambo yaliyokuwa katika Nyongeza ya X ya Mkataba wa
Jumuiya ya Afrika Mashariki yaliongezwa; mwaka 1968 yaliongezwa mambo ya
maliasili ya mafuta, petroli na gesi asilia; na mwaka 1973 mambo yanayohusu
Baraza la Mitihani la Taifa yaliongezwa.
Aidha, Mabadiliko ya Tano ya Katiba ya mwaka
1984 yaligawa kipengele cha Nyongeza ya X ya Mkataba wa Jumuiya ya Afrika
Mashariki na kutengeneza vipengele vinne vinavyojitegemea katika orodha ya
Mambo ya Muungano, yaani usafiri na usafirishaji wa anga, utafiti, utabiri wa
hali ya hewa na takwimu. Vile vile, Mabadiliko hayo yaliongeza kitu kipya katika
orodha ya Mambo ya Muungano: Mahakama ya Rufani ya Tanzania. Aidha, kipengele
cha 3, yaani ulinzi, kilifanyiwa marekebisho na kuwa ‘ulinzi na usalama.’ Na
mwaka 1992 ‘uandikishwaji wa vyama vya siasa’ nao uliongezwa katika orodha ya
Mambo ya Muungano.
Mheshimiwa Mwenyekiti,
Mambo yote yaliyoongezwa katika orodha ya Mambo
ya Muungano baada ya mwaka 1964 yalikuwa nje ya Makubaliano ya Muungano na nje
ya Sheria ya Mapatano ya Muungano na kwa hiyo yalikuwa batili. Hii ni kwa
sababu Sheria ya Mapatano ya Muungano – na sio Katiba za Muda za 1964 au 1965
au ya sasa - ndio Sheria Mama iliyozaa Muungano na kuweka mgawanyo wa madaraka
kati ya mamlaka za Jamhuri ya Muungano na mamlaka za Zanzibar. Sheria ya
Mapatano ya Muungano ilitungwa na Bunge la Katiba tofauti na sheria za kawaida.
Aidha, Katiba ya Muda, 1965 iliyotawala
Tanzania hadi 1977 iliiweka Sheria ya Mapatano ya Muungano kama Nyongeza ya
Pili katika Katiba na kuweka masharti kwamba Sheria hiyo haiwezi kurekebishwa
bila marekebisho hayo kuungwa mkono na theluthi mbili ya Wabunge wote wa
Tanganyika na wale wa Zanzibar. Vile vile, Katiba ya sasa ya Muungano inataja
kwamba moja ya Sheria ambazo mabadiliko yake yahitaji kuungwa mkono na theluthi
mbili ya Wabunge wote ni “Sura ya 557 (Toleo la 1965), Sheria ya
Kuthibitisha Mapatano ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ya mwaka 1964.”[47]
Zaidi ya hayo, kwa mujibu wa Katiba hiyo,
Orodha ya Mambo ya Muungano haiwezi kufanyiwa ‘mabadiliko yoyote’ bila kuungwa
mkono na theluthi mbili ya wabunge wote kutoka Tanganyika na theluthi mbili ya
wabunge wote kutoka Zanzibar.[48] Utafiti wetu umethibitisha kwamba hakuna nyongeza ya Mambo ya
Muungano hata moja iliyopitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano kwa kutumia
utaratibu wa kupigiwa kura ya kuungwa mkono na theluthi mbili ya wabunge wote
wa Tanganyika na idadi hiyo hiyo ya wabunge wa kutoka Zanzibar.
Kifungu cha 5 cha Sheria ya Muungano, ambacho
ndicho chenye misingi mikuu ya Muungano hakijawahi kurekebishwa tangu Sheria
yenyewe ilipotungwa mwaka 1964. Badala yake, Bunge limekuwa na tabia ya kukwepa
kuigusa kabisa Sheria ya Muungano na badala yake limekuwa likifanya marekebisho
ya orodha ya Mambo ya Muungano iliyowekwa kwa mara ya kwanza katika Katiba za
Muda za mwaka 1964 na 1965 kwa kuongeza vipengele katika orodha hiyo.
Lengo la marekebisho haya limekuwa mara zote ni
kuinyang’anya Zanzibar mamlaka yake chini ya Makubaliano ya Muungano na Sheria
ya Kuthibitisha Mapatano ya Muungano. Ndio maana katika Mapendekezo ya
Halmashauri Kuu ya CCM Kuhusu Marekebisho ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano na
Katiba ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar yaliyotolewa tarehe 27 Januari,
1983, CCM ilitamka kwamba “... msingi wa kuwa na orodha ya mambo ya muungano
katika Katiba ni kuonyesha mamlaka ya Serikali ya Zanzibar ambayo yalikabidhiwa
kwa Serikali ya Muungano; na msingi wa kuongeza mambo zaidi katika orodha ya
mambo ya muungano, kama ambavyo imefanyika mara kwa mara, ni kuhamisha mamlaka
zaidi ya Serikali ya Zanzibar kwenda kwa Serikali ya Muungano.”
Profesa Shivji anasema - katika The Legal
Foundations of the Union - kwamba Bunge la Jamhuri ya Muungano halikupewa
mamlaka ya kuongeza Mambo ya Muungano bali lilipewa mamlaka ya kutunga sheria
zinazohusu Mambo ya Muungano kama yalivyofafanuliwa katika Sheria ya Muungano.
Kwa maana hiyo, nyongeza zote zilizofanyika katika orodha ya Mambo ya Muungano
tangu mwaka 1964 zilikiuka Makubaliano ya Muungano na Sheria ya Muungano na ni
batili. Ndio maana, kwa muda mrefu, Wazanzibari wamelalamikia masuala haya,
hasa hasa masuala ya fedha, sarafu na mafuta na gesi asilia.
Vitendo hivi vya kukiuka Makubaliano ya
Muungano vilipata Baraka za kikatiba mwaka 1984 wakati ibara mpya ya 64(4) ya
Katiba ya sasa ya Muungano ilipotungwa: “Katiba yoyote iliyotungwa na Bunge
kuhusu jambo lolote haitatumika Tanzania Zanzibar ila kwa mujibu wa masharti
yafuatayo:
(a) Sheria hiyo iwe imetamka wazi kwamba itatumika Tanzania Bara na
vile vile Tanzania Zanzibar au iwe inafuta inabadilisha, kurekebisha au kufuta
Sheria inayotumika Tanzania Zanzibar; au
(b) Sheria hiyo iwe inabadilisha au kurekebisha au kufuta sheria
iliyokuwa inatumika tangu zamani Tanzania Bara ambayo ilikuwa inatumika pia
Tanzania Zanzibar kwa mujibu wa Mapatano ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar
ya mwaka 1964, au kwa mujibu wa Sheria yoyote ambayo ilitamka wazi kwamba
itatumika Tanzania Bara na vile vile Tanzania Zanzibar....”
Ibara hii ya Katiba ililipa Bunge la Jamhuri ya
Muungano mamlaka ya kutunga ‘sheria yoyote’ kuhusu ‘jambo lolote’, hata kama
sio la Muungano na sheria hiyo itatumika Tanzania Zanzibar! Ibara hii inakiuka
moja kwa moja masharti ya aya ya iii(a) ya Makubaliano ya Muungano ambayo
ilisema wazi kwamba Bunge la Zanzibar “... litakuwa na mamlaka kamili ndani
ya Zanzibar kwa mambo yale ambayo hayajawekwa chini ya mamlaka ya Bunge na
Serikali ya Jamhuri ya Muungano....” Aidha, ibara hiyo inakinzana na ibara
ndogo ya (2) ya ibara ya 64 inayotamka kwamba “mamlaka yoyote ya kutunga
sheria katika Tanzania Zanzibar juu ya mambo yote yasiyo mambo ya Muungano
yatakuwa mikononi mwa Baraza la Wawakilishi.”
Mheshimiwa Mwenyekiti,
Vitendo vya kupuuza Makubaliano ya Muungano na
Sheria ya Muungano iliyoridhia Makubaliano vilifikia kilele chake tarehe 21
Novemba, 2000 pale Mahakama ya Rufani ya Tanzania ilipotamka – katika kesi ya Serikali
ya Mapinduzi Zanzibar dhidi ya Machano Khamis Ali na Wenzake 17 – kwamba
Zanzibar sio nchi na wala sio dola. Bali, kwa mujibu wa Mahakama ya Rufani, “hakuna
ubishi wa aina yoyote kwamba Jamhuri ya Muungano ni nchi moja na dola moja.”
Kama tulivyokwisha kuonyesha, suala la Mahakama ya Rufani ya Tanzania yenyewe
kuwa suala la Muungano liliingizwa kwenye orodha ya Mambo ya Muungano kinyemela
na kinyume na Makubaliano ya Muungano na Sheria ya Muungano. Jibu la
Wazanzibari juu ya ukiukwaji wa muda mrefu wa Makubaliano ya Muungano na Sheria
ya Muungano iliyoridhia Makubaliano hayo lilikuwa ni kupitisha Sheria ya
Mabadiliko ya Kumi ya Katiba ya Zanzibar mwaka 2010.
Mheshimiwa Mwenyekiti,
Tarehe 13 Agosti, 2010, wakati Bunge la Jamhuri
ya Muungano likiwa limevunjwa kwa ajili ya maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa 2010,
Baraza la Wawakilishi la Zanzibar lilipitisha Sheria ya Mabadiliko ya Kumi ya
Katiba ya Zanzibar, 1984. Mabadiliko haya yaliweka msingi wa kikatiba wa
Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Zanzibar inayoshirikisha CCM na Chama cha
Wananchi (CUF). Kwa sababu hiyo, Sheria ya Mabadiliko ya Katiba imepigiwa upatu
kama Katiba ya Muafaka na, kwa kiasi fulani, hii ni kweli.
Hata hivyo, Sheria ya Mabadiliko ya Katiba
imekwenda mbali zaidi. Sheria hii sio tu imehoji uhalali wa orodha ya Mambo ya
Muungano ya tangu mwaka 1964 na nyongeza zake zilizofuata, bali pia imehoji pia
misingi muhimu ya Sheria ya Muungano iliyoridhia Makubaliano ya Muungano. Kwa
mtazamo huu, Katiba ya sasa ya Zanzibar inaelekea kuwa ni tangazo la uhuru wa
Zanzibar zaidi kuliko waraka wa muafaka kati ya vyama viwili vilivyokuwa
mahasimu.
Aya ya (i) ya Makubaliano ya Muungano na
kifungu cha 4 cha Sheria ya Muungano vilitangaza muungano wa Jamhuri ya
Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar na kuundwa kwa “Jamhuri moja huru
itakayoitwa Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.” Makubaliano ya
Muungano hayakuua nchi washirika wa Muungano huu. Hii inathibitishwa sio tu na
masharti ya Makubaliano ya Muungano yanayoashiria kuendelea kutumika kwa sheria
za Tanganyika na Zanzibar ‘katika maeneo yao’ tu, bali vifungu vya Katiba
zilizofuatia Makubaliano ya Muungano.
Hivyo basi, hata baada ya mabadiliko ya jina
kwenda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Katiba na sheria mbali mbali
ziliendelea kutumia jina la Tanganyika na Zanzibar. Kwa mfano, Sheria ya
Kuongeza Muda wa Kuitisha Bunge la Katiba, 1965[49], iliyosainiwa na Rais Nyerere tarehe 24 Machi,
1965, inataja, katika vifungu vyote vitatu, ‘Sheria za Muungano wa Tanganyika
na Zanzibar.’
Aidha, Sheria ya Kutangaza Katiba ya Muda ya
Tanzania ya tarehe 11 Julai, 1965[50], ilitangaza kwamba ‘Tanzania ni Jamhuri Huru ya Muungano’[51]; kwamba eneo lake ni “... eneo lote la
Tanganyika na Zanzibar ...”[52] na kwamba chama kimoja cha siasa “... kwa Tanganyika kitakuwa
Tanganyika African National Union (TANU)....”[53] Kwa wakati wote wa uhai wake, Katiba ya Muda haikuwahi kutamka
kuwa Tanzania ni nchi moja. Kwa upande wake, licha ya kuanza kutumia jina la
Tanzania Bara na Tanzania Visiwani kwa mara ya kwanza[54], Toleo la Kwanza la Katiba ya sasa ya Muungano
lilitamka kwamba Tanzania ni ‘Jamhuri ya Muungano.’[55] Hapa pia hapakuwa na tamko la ‘nchi moja.’
Mheshimiwa Mwenyekiti,
Maneno ya ibara ya 1 ya Katiba ya sasa ya
Muungano kwamba “Tanzania ni nchi moja na ni Jamhuri ya Muungano”
yaliingia katika kamusi ya kikatiba na kisiasa ya nchi hii kufuatia ‘kuchafuka
kwa hali ya kisiasa ya Zanzibar’ na kung’olewa madarakani kwa Rais Aboud Jumbe.
Kufuatia hali hiyo, Katiba ya Jamhuri ya Muungano ilifanyiwa marekebisho makubwa[56] ambayo, pamoja na mengine, yalitangaza kuwa “Tanzania
ni nchi moja na ni Jamhuri ya Muungano.”[57] Kwa sababu ya upinzani mkubwa wa Wazanzibari, Marekebisho hayo
ya Katiba yaliondoa pia maneno ‘Tanzania Visiwani’ na kuweka ‘Tanzania
Zanzibar’ badala yake. Maneno ‘Tanzania Bara’ yalibaki kama yalivyowekwa mwaka
1977.
Kwa maana hiyo, dhana ya Tanzania kama nchi
moja haijatokana na Makubaliano ya Muungano bali ilitokana na siasa za
Muungano, yaani mvutano kati ya viongozi wa Tanganyika wakiwa wamevalia joho la
Jamhuri ya Muungano na viongozi wa Zanzibar waliotaka uhuru zaidi kwa nchi yao.
Pili, dhana hiyo haina umri mkubwa sana kuliko inavyodhaniwa, kwani iliingia
kwenye Katiba mwaka 1984, miaka thelathini iliyopita, na miaka ishirini baada
ya Muungano.
Tatu, Makubaliano ya Muungano hayakuua
Tanganyika, licha ya mabadiliko mengi ya kikatiba na ya kisheria ya tangu siku
za mwanzo kabisa za Muungano. Bali kilichoiondoa Tanganyika katika lugha ya
kikatiba na kisheria ni Katiba ya sasa ya Muungano pale ilipoacha kutumia neno
Tanganyika na badala yake ikaingiza neno ‘Tanzania Bara’ mwaka 1977.
Sasa mabadiliko haya ya Katiba ya Muungano
yamehojiwa na maneno ya ibara ya 2 ya Katiba mpya ya Zanzibar yanayotamka
kwamba “Zanzibar ni miongoni mwa nchi mbili zinazounda Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania.” Kwa maneno haya, Zanzibar imeturudisha rasmi kwenye
Makubaliano ya Muungano kwamba Jamhuri ya Muungano haikuzaliwa kutokana na kifo
cha nchi mbili zilizoungana, bali nchi hizo zimeendelea kuwepo. Kwa maana hiyo,
Katiba ya Zanzibar ni tangazo la uhuru wa Tanganyika vile vile, kwani kwa miaka
hamsini Tanganyika imejificha nyuma ya pazia la Tanzania.
Ibara ya 2(2) ya Katiba ya Muungano inampa Rais
wa Jamhuri ya Muungano – kwa kushauriana kwanza na Rais wa Zanzibar - mamlaka
ya kuigawa Tanzania Zanzibar katika mikoa, wilaya au maeneo mengineyo. Vile
vile, ibara ya 61(3) ya Katiba ya Muungano inampa Rais wa Zanzibar mamlaka ya
kuteua Wakuu wa Mikoa katika Tanzania Zanzibar ‘baada ya kushauriana na Rais.’
Masuala ya mgawanyo wa nchi katika mikoa na mamlaka za mikoa hiyo sio, na
hayajawahi kuwa, Mambo ya Muungano kwa mujibu wa Sheria ya Muungano. Vile vile
hayapo katika orodha ya Mambo ya Muungano.
Ni wazi kwa hiyo, kwamba ibara za 2(2) na 61(3)
za Katiba ya Muungano zilikuwa zinakiuka matakwa ya Sheria ya Muungano na kwa
hiyo ni batili. Sasa wazanzibari ‘wamejitangazia uhuru’ kwa kutangaza – katika
ibara ya 2A ya Katiba mpya ya Zanzibar – kwamba “... Rais (wa Zanzibar)
aweza kuigawa Zanzibar katika mikoa, wilaya na maeneo mengineyo kwa kufuata
utaratibu uliowekwa na sheria iliyotungwa na Baraza la Wawakilishi.” Aidha,
kwa ibara ya 61(1), Rais wa Zanzibar hawajibiki tena kushauriana na Rais wa
Muungano pale anapofanya uteuzi wa wakuu wa mikoa ya Zanzibar.
Wakati ambapo Sheria ya Muungano ilikuwa
imetambua na kuhifadhi mamlaka ya Rais wa Zanzibar kama mkuu wa dola ya
Zanzibar, Mahakama ya Rufani ya Tanzania – katika Kesi ya Machano Khamis Ali
na Wenzake – ilitishia moja kwa moja msingi huo kwa kutamka kwamba Zanzibar
sio nchi na wala sio dola na kwa hiyo haiwezi kutishiwa na kosa la uhaini. Sasa
ibara ya 26(1) ya Katiba mpya Zanzibar ‘imerudisha’ dola ya Zanzibar kwa
kutamka kwamba “kutakuwa na Rais wa Zanzibar ambaye atakuwa Mkuu wa Nchi ya
Zanzibar, Kiongozi Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi.”
Aidha, kwa kutambua kwamba ‘Mahakama ya Rufani
ya Jamhuri ya Muungano’ sio moja ya Mambo ya Muungano kwa mujibu wa Sheria ya
Muungano, Katiba ya sasa ya Zanzibar imetamka kwamba katika kesi zinazohusu
‘kinga za haki za lazima, wajibu na uhuru wa mtu binafsi’, uamuzi wa majaji
watatu wa Mahakama Kuu ya Zanzibar “... utakuwa ni wa mwisho na hautokatiwa
rufaa kwenye Mahakama ya Rufaa ya Tanzania.”
Kifungu cha 5(1)(a)(iii) na (iv) cha Sheria ya
Muungano kinataja ‘ulinzi’ na ‘polisi’ kama sehemu ya mambo kumi na moja ya
Muungano. Na hivyo ndivyo inavyosema aya ya (iv)(c) na (d) ya Makubaliano ya Muungano.
Ijapokuwa ‘ulinzi’ ulichakachuliwa baadae kwa kuongezwa maneno ‘na usalama’,
bado ni sahihi kusema kwamba masuala ya ulinzi na polisi ni masuala halali
ambayo Sheria ya Muungano iliyakasimu kwa Serikali ya Muungano. Na kwa sababu
hiyo, ni sahihi kwa Katiba ya Muungano kutamka – kama inavyofanya katika ibara
ya 33(2) - kwamba “Rais (wa Jamhuri ya Muungano) atakuwa Mkuu wa Nchi,
Kiongozi wa Serikali na Amiri Jeshi Mkuu.”
Hata hivyo, katika kile kinachoonekana kama
hojaji kubwa ya msingi huu wa Makubaliano ya Muungano na Sheria ya Muungano,
ibara ya 121 ya Katiba ya sasa ya Zanzibar imeunda majeshi ya Zanzibar
inayoyaita ‘Idara Maalum.’ Majeshi haya, kwa mujibu wa ibara ya 121(2) ni Jeshi
la Kujenga Uchumi (JKU); Kikosi Maalum cha Kuzuia Magendo (KMKM); Chuo cha
Mafunzo (cha wahalifu), na Idara Maalum nyingine yoyote ambayo Rais wa Zanzibar
anaweza kuianzisha ‘ikiwa ataona inafaa....’
Kuthibitisha kwamba Idara Maalum ni majeshi,
ibara ya 121(4) inakataza watumishi wa Idara Maalum ‘... kujishughulisha na
mambo ya siasa....’ Makatazo haya hayatofautiani na makatazo ya wanajeshi
kujiunga na vyama vya siasa yaliyoko katika ibara ya 147(3) ya Katiba ya
Muungano.
Sio tu kwamba Katiba mpya ya Zanzibar
inaanzisha majeshi bali pia inamfanya Rais wa Zanzibar kuwa Amiri Jeshi Mkuu wa
majeshi hayo. Kwa mujibu wa ibara ya 123(1) ya Katiba hiyo, “Rais atakuwa
Kamanda Mkuu wa Idara Maalum na atakuwa na uwezo wa kufanya chochote kile
anachohisi, kwa maslahi ya Taifa (la Zanzibar), kinafaa.” Kwa maoni yetu,
hakuna tofauti yoyote ya msingi kati ya maneno ‘Amiri Jeshi Mkuu’ na ‘Kamanda
Mkuu’ bali, kwa kiasi kikubwa, ni mpangilio wa maneno hayo tu.
Aidha, kwa mujibu wa ibara ya 123(2), mamlaka
ya Rais wa Zanzibar chini ya ibara ndogo ya (1) yanaingiza “... uwezo wa
kutoa amri ya kufanya shughuli yoyote inayohusiana na Idara hiyo kwa manufaa ya
Taifa.” Kwa maoni yetu, haya ni mamlaka ya kutangaza au kuendesha vita
ambayo, kwa mujibu wa ibara ya 44(1) ya Katiba ya Muungano, ni mamlaka pekee ya
Rais wa Jamhuri ya Muungano.
Kifungu cha 5(1)(b) cha Sheria ya Muungano
kilitamka kwamba muundo wa Serikali ya Zanzibar utakuwa kama utakavyoamuliwa na
sheria za Zanzibar pekee. Na hivyo ndivyo ilivyokubaliwa katika aya ya (iii)(a)
ya Makubaliano ya Muungano. Hata hivyo, licha ya muundo wa Serikali ya Zanzibar
kutokuwepo katika orodha ya Mambo ya Muungano, Katiba ya Muungano imetenga Sura
ya Nne nzima kuzungumzia ‘Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Baraza la
Mapinduzi la Zanzibar na Baraza la Wawakilishi la Zanzibar.’
Kwa mujibu wa Profesa Shivji katika The
Legal Foundations of the Union, Sura ya Nne ya Katiba ya Muungano “...
haina ulazima wowote na ni kuingilia, bila kualikwa, kwenye mambo ambayo yako
ndani ya mamlaka pekee ya Zanzibar.” Ndio maana Katiba mpya ya Zanzibar –
kwa usahihi kabisa - imefanya mabadiliko katika muundo wa Serikali ya Mapinduzi
Zanzibar bila ya kuzingatia matakwa ya Sura ya Nne ya Katiba ya Muungano.
Vifungu vinavyohitaji kura ya maoni ni vifungu
vyote vya Sehemu ya Kwanza ya Sura ya Kwanza inayohusu Zanzibar kama nchi na/au
dola; kifungu cha 9 kinachohusu Serikali na watu wa Zanzibar; vifungu vyote vya
Sura ya Tatu inayohusu kinga ya haki za lazima, wajibu na uhuru wa mtu binafsi;
na kifungu cha 26 kinachohusu Rais wa Zanzibar na mamlaka yake. Vifungu vingine
ni pamoja na kifungu cha 28 kinachohusu muda wa urais; Sehemu ya Pili na ya
Tatu ya Sura ya Nne zinazohusu Makamu wawili wa Rais, Baraza la Mawaziri na
Baraza la Mapinduzi; kifungu cha 80A kinachohifadhi haki ya kura ya maoni; na
vifungu vya 121 na 123 vinavyohusu Idara Maalum na mambo yanayohusiana nayo.
Kuweka masharti ya kura ya maoni kuhusu
mabadiliko ya vifungu tajwa vya Katiba mpya ya Zanzibar kuna athari ya moja kwa
moja kwa uhai wa Muungano wetu. Hii ni kwa sababu hata vifungu ambavyo
tumeonyesha kwamba vinakiuka misingi mikuu ya Makubaliano ya Muungano na Sheria
ya Muungano haviwezi kubadilishwa bila kura ya maoni ya Wazanzibari. Kwa maneno
mengine, kwa mujibu wa Katiba ya sasa ya Zanzibar, masuala ya kama Tanzania ni
nchi moja au la, majeshi ya ulinzi, polisi, n.k. ambayo yamekuwa Mambo ya
Muungano kwa mujibu wa Makubaliano ya Muungano na Sheria ya Muungano sio Mambo
ya Muungano tena hadi hapo wananchi wa Zanzibar watakapoamua – kwa kura ya
maoni – kuyarudisha kwa mamlaka ya Muungano. Huku ni kutangaza uhuru wa
Zanzibar bila kutaja neno uhuru!
Kwa mtazamo wa Katiba ya sasa ya Zanzibar,
hakuna tena ‘nchi moja’ inayozungumzwa katika Katiba ya sasa ya Muungano bali
tuna ‘nchi mbili’ zinazozungumzwa katika Makubaliano ya Muungano. Kwa mtazamo
huo huo, masuala ya ulinzi na usalama, polisi, n.k. sio tena Mambo ya Muungano
kwa sababu sasa kila nchi ina majeshi yake na kila moja ina Amiri Jeshi Mkuu
wake. Aidha, tuna marais wawili, wakuu wa nchi wawili na viongozi wa serikali
wawili.
Mabadiliko haya ya kikatiba yanadhihirishwa
wazi na taratibu za kiitifaki wakati wa Sherehe za Mapinduzi Zanzibar ambako
siku hizi Rais wa Zanzibar ndiye anayekagua gwaride rasmi la vikosi vya ulinzi
na usalama, kupigiwa mizinga ishirini na moja na anakuwa wa mwisho kuingia, na
wa mwisho kutoka, uwanjani huku Rais wa Jamhuri ya Muungano akiwa wa pili
kiitifaki.
Kwa upande mwingine, kwa mtazamo wa Katiba ya
sasa ya Zanzibar, Rais wa Muungano hana tena mamlaka ya kugawa mikoa na wilaya
kwa upande wa Zanzibar, na wala hawezi kumshauri tena Rais wa Zanzibar
anapoteua Wakuu wa Mikoa wa Tanzania Zanzibar. Aidha, Mahakama ya Rufani ya
Tanzania – licha ya kuwa moja ya Mambo ya Muungano kwa mujibu wa Katiba ya
Muungano - haina tena mamlaka ya kusikiliza na kuamua rufaa zinazohusu haki za
msingi na uhuru wa mtu binafsi zinazotoka Zanzibar. Yote haya hayapo na
hayajawahi kuwapo katika Makubaliano ya Muungano na Sheria ya Muungano.
Tangu mwanzo Muungano wa Tanganyika na Zanzibar
haukuwa Muungano wa usawa. Huu ni Muungano ulioipa Tanganyika – ikiwa imevalia
koti la Jamhuri ya Muungano - mamlaka ya kuingilia uhuru na mamlaka ya
Zanzibar. Hii inathibitishwa na Hati ya Makubaliano ya Muungano yenyewe.
Kwanza, kwa kutamka kwamba katika kipindi cha mpito “Katiba ya Jamhuri ya
Muungano itakuwa ni Katiba ya Tanganyika...”, ni wazi kwamba Mshirika wa
Muungano aliyekuwa na nguvu katika Muungano huu ni Tanganyika.
Pili, kwa kuweka orodha ya mambo 11 ya
Muungano, ni wazi kwamba Zanzibar ilinyang’anywa mamlaka juu ya masuala hayo na
mamlaka hayo yalihamishiwa kwa Tanganyika ikiwa imevaa koti la Jamhuri ya
Muungano. Kwa maana hiyo, Zanzibar ilinyang’anywa mamlaka yake juu ya masuala
ya nchi za nje, ulinzi, polisi, mamlaka ya hali ya hatari, uraia, uhamiaji,
biashara ya nje na mikopo na masuala mbali mbali ya kodi. Hati ya Makubaliano
ya Muungano yenyewe inasema wazi kwamba “Bunge na Serikali (ya Jamhuri ya
Muungano) litakuwa na mamlaka kamili kwenye mambo hayo kwa Jamhuri ya Muungano
na, kwa nyongeza, mamlaka kamili kwa ajili ya mambo mengine yote ya na kwa
ajili ya Tanganyika.”
Tatu, kwa kutangaza kwamba rais wa kwanza wa
Jamhuri ya Muungano atakuwa Mwalimu Nyerere na Makamu wa kwanza wa Rais atakuwa
Sheikh Abeid Karume; na kwa kutangaza kwamba Makamu wa Kwanza wa Rais atakuwa
ndiye msaidizi mkuu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano katika utekelezaji wa
majukumu yake ya kiutendaji kuhusu Zanzibar, ni wazi kwamba Hati ya Makubaliano
ya Muungano nafasi ya chini (subordinate position) ya Zanzibar katika
Muungano.
Nne, kwa kuzifanya alama za utaifa (national
emblems) za Tanganyika kuwa ndio alama za taifa za Jamhuri ya Muungano,
kuna-emphasize superior position ya Tanganyika ndani ya Muungano na
subaltern position ya Zanzibar katika Muungano huu. Ukweli huo huo unahusu
masuala ya kuzifanya taasisi na watumishi wa Serikali ya Tanganyika kuwa ndio
taasisi na watumishi wa Jamhuri ya Muungano. Kama Maalim Seif Shariff Hamad
anavyomalizia Maoni yake kwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba tarehe 13 Januari,
2013: “Mfumo (wa Muungano) uliopo sasa hauinufaishi Zanzibar na hivyo
haukubaliki kwa Wazanzibari. Koti la Muungano kama lilivyo sasa linabana sana.
Wakati umefika tushone koti jipya kwa mujibu wa mahitaji ya zama hizi.”[58]
Baada ya nusu karne ya ukiukaji wa Hati ya
Makubaliano ya Muungano, na kwa hali ya sasa ya kisiasa na kikatiba ya
Zanzibar, ni wazi Hati ya Makubaliano ya Muungano haiwezi kuwa msingi wa
Shirikisho la Jamhuri za Tanganyika na Zanzibar tunayoipendekeza. Aidha, Katiba
Mpya haiwezi kuwa ni mwendelezo wa Hati ya Makubaliano ya Muungano ambayo, kama
ambavyo tumeonyesha, haijawahi kuheshimiwa katika miaka hamsini tangu kusainiwa
kwake.
Kwa maoni ya wajumbe walio wachache wa Kamati
Namba Nne, wakati umefika wa kujenga mahusiano kati ya nchi hizi mbili katika
msingi ulio imara zaidi na wa usawa zaidi. Ndio maana tunapendekeza kwamba
Katiba Mpya ndiyo iwe msingi wa Shirikisho la Jamhuri za Tanganyika na
Zanzibar.
Ibara ya 2
Mheshimiwa Mwenyekiti,
Ibara ya 2 ya Rasimu inafafanua eneo la Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania. “Eneo la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni eneo lote
la Tanganyika likijumuisha sehemu yake ya bahari na eneo lote la Zanzibar
likijumuisha sehemu yake ya bahari.” Wajumbe walio wachache wa Kamati Namba Nne
wanapendekeza ibara hiyo ifutwe yote na kuandikwa upya kama ifuatavyo: “Eneo
la Shirikisho la Jamhuri za Tanganyika na Zanzibar ni eneo lote la Tanganyika
likijumuisha sehemu yake ya bahari, maziwa na mito, pamoja na eneo lake la
anga; na eneo lote la Zanzibar ikiwa ni pamoja na visiwa vidogo vinvyozunguka
Visiwa vya Unguja na Pemba na eneo lake la bahari pamoja na eneo lake la anga.”
Mapendekezo haya ya wajumbe walio wachache
katika Kamati Namba Nne yanashawishi kutambuliwa na kufafanuliwa kwa mipaka ya
nchi hizi mbili Washirika wa Muungano. Hii itasaidia kuepusha migogoro
inayoweza kujitokeza hasa hasa kuhusu rasilmali zinazopatikana baharini kama
vile mafuta, gesi asilia na rasilmali uvuvi. Aidha, kwa sababu ya kuwepo kwa
migogoro ya mipaka katika maeneo ya maji kama ule kati ya Jamhuri ya Muungano
na Malawi, wajumbe walio wachache wa Kamati Namba Nne wanafikiri kwamba ni
muhimu kwa Sheria kuu ya nchi kutamka na kufafanua mipaka yetu.
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
1977, imefafanua eneo la Jamhuri ya Muungano kama ifuatavyo: “Eneo la
Jamhuri ya Muungano ni eneo lote la Tanzania Bara na eneo lote la Tanzania
Zanzibar, na ni pamoja na sehemu yake ya bahari ambayo Tanzania inapakana
nayo.”[59] Aidha, ibara ya 1 ya
Katiba ya Zanzibar, 1984, inafafanua ‘Zanzibar na mipaka yake’ kama ifuatavyo: “Zanzibar
ni nchi ambayo eneo la mipaka yake ni eneo lote la Visiwa vya Unguja na Pemba
pamoja na Visiwa vidogo vilivyoizunguka na bahari yake ambayo kabla ya Muungano
wa Tanganyika na Zanzibar ikiitwa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar.”
Wajumbe walio wachache wa Kamati Namba Nne
wanatambua ukweli kwamba ufafanuzi wa mipaka ya Jamhuri ya Muungano uliopo
katika Katiba ya sasa ya Jamhuri ya Muungano ni mfinyu sana na hautoshelezi
mahitaji ya sasa ya kiuchumi na kisiasa. Kwanza, licha ya Jamhuri ya Muungano
kupakana na maziwa kama vile Victoria, Tanganyika na Nyasa ambayo tunayachangia
na nchi jirani za Kenya, Uganda, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo,
Zambia, Malawi na Msumbiji; na Mto Ruvuma tunaouchangia na Msumbiji, maelezo
haya ya Katiba ya sasa hayatambui uwepo wa maeneo hayo.
Pili, Katiba ya sasa ya Jamhuri ya Muungano
haitofautishi kati ya eneo la bahari la Tanganyika na eneo la bahari la
Zanzibar. Hii ni hatari kwani inaweza kuwa chanzo cha migogoro ya mipaka kati
ya nchi hizi mbili hasa kwa vile masuala ya rasilmali asilia zilizoko baharini
zimeondolewa kinyemela katika orodha ya mambo ya Muungano ama yanapendekezwa na
Rasimu kuondolewa katika orodha hiyo.
Tatu, Katiba ya sasa ya Jamhuri ya Muungano na
hata ya Zanzibar hazitambui milki ya Jamhuri ya Muungano au ya Zanzibar juu ya
anga la Jamhuri ya Muungano au la Zanzibar. Anga ni rasilmali muhimu hasa
katika masuala ya usafiri wa anga, na mawasiliano ya simu na redio. Mapendekezo
haya ya wajumbe walio wachache kuhusu eneo la nchi yetu yatatua matatizo
yaliyotajwa hapa.
IBARA YA 3
Ibara ya 3 ya Rasimu inahusu ‘Alama na Sikukuu
za Taifa.’ Ibara ya 3(1) inapendekeza Alama za Taifa kuwa ni Bendera ya Taifa,
Wimbo wa Taifa na Nembo ya Taifa kama zitakavyoainishwa katika sheria husika za
nchi. Kwa upande wake, ibara ya 3(2) inapendekeza Sikukuu za Kitaifa kuwa ni “Siku
ya Uhuru wa Tanganyika itakayoadhimishwa tarehe 9 Disemba; Siku ya Mapinduzi ya
Zanzibar itakayoadhimishwa tarehe 12 Januari; Siku ya Muungano wa Tanganyika na
Zanzibar itakayoadhimishwa tarehe 26 Aprili; na Sikukuu nyingine
zitakazoainishwa na sheria za nchi.” Kwa mujibu wa ibara 3(3), kila Sikukuu
ya Kitaifa itakuwa ni siku ya mapumziko.
Mheshimiwa Mwenyekiti,
Alama za Taifa ni suala muhimu sana kwa
utambulisho wa historia na utamaduni wa nchi yoyote. Kwa sababu mbali mbali za
kihistoria tulizozielezea kwa kirefu katika maoni yetu kuhusu ibara 1 ya
Rasimu, suala la alama za taifa za Jamhuri ya Muungano limejaa utata mtupu. Kwa
upande mmoja, alama za taifa ambazo zimeendelea kutumika katika kipindi chote
cha miaka hamsini ya Muungano ni Alama za Taifa la Tanganyika ambazo zilifanywa
kuwa za Jamhuri ya Muungano pale Tanganyika ilipovikwa joho la Jamhuri ya
Muungano kati ya tarehe 26 Aprili na 15 Juni, 1964.
Mfano mzuri ni wa Nembo ya Taifa, maarufu kama
‘Bibi na Bwana.’ Alama hiyo ya Taifa iliwekwa na Sheria ya Nembo ya Taifa,
Sura ya 504 ya Sheria za Tanganyika, yaani The Public Seal Act, Chapter
504 of the Laws, ya mwaka 1962 na ilianza kutumika Siku ya Jamhuri, yaani
tarehe 9 Disemba 1962. Hata hivyo, kufuatia kuzaliwa kwa Muungano, Alama hiyo
ya Taifa la Tanganyika iligeuzwa na kuwa Nembo ya Taifa ya Jamhuri ya Muungano
kwa kutumia Amri ya Masharti ya Mpito ya Mwalimu Nyerere ya tarehe 26 Aprili,
1964.
Kwa upande mwingine, matumizi ya Alama nyingine
za Taifa ni kielelezo kingine cha utamaduni wa ukiukaji sheria ambao umejengeka
katika nusu karne ya Muungano. Suala hili linahusu Bendera ya Taifa na Wimbo wa
Taifa. Kwanza, wakati Bendera ya sasa ya Taifa ilianza kutumika kufuatia
kushushwa kwa Bendera za Taifa za Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar
katika Umoja wa Mataifa, baada ya maelekezo ya Mwanasheria Mkuu wa Umoja wa
Mataifa Stavropoulos ya tarehe 13 Mei, 1964, Bunge la Jamhuri ya Muungano
halikutunga sheria yoyote ya kuwezesha uwepo wa Alama hii muhimu ya Taifa hadi
tarehe 7 Mei, 1971, zaidi ya miaka saba baada ya kuzaliwa Muungano!
Pili, baada ya kutungwa kwake na ikiwa na lengo
la kuficha ukweli kwamba Bendera ya Taifa ilikuwa imetumika kwa zaidi ya miaka
saba bila uhalali wowote wa kisheria, Sheria ya Bendera ya Taifa na Nembo ya
Taifa,[60] yaani The National
Flag and Coat of Arms Act, ilitamka kwamba Bendera ya Taifa imeanza
kutumika tangu tarehe 26 Aprili 1964,[61] yapata miaka saba kabla sheria yenyewe haijatungwa!
Tatu, licha ya ukweli kwamba ‘Bibi na Bwana’
ilianza kutumika tangu tarehe 9 Disemba, 1962, na licha ya Mwalimu Nyerere
kuigeuza Nembo hiyo ya Tanganyika kuwa ya Jamhuri ya Muungano kwa Amri yake ya tarehe
26 Aprili, 1964, kifungu cha 4 cha Sheria ya Bendera ya Taifa na Nembo ya
Taifa kilishurutisha kwamba ‘Bibi na Bwana’ nayo itakuwa Nembo ya Taifa ya
Jamhuri ya Muungano kuanzia tarehe 26 Aprili, 1964.
Nne, Wimbo wa Taifa unaotumiwa sasa, yaani ‘Mungu
Ibariki Afrika’, ni Wimbo wa Taifa wa Tanganyika ambao ulifanywa kuwa Wimbo wa
Taifa wa Jamhuri ya Muungano bila ya msingi wowote wa kisheria. Hii ni kwa
sababu, Sheria ya Alama za Taifa haitambui Wimbo wa Taifa kama mojawapo
ya Alama za Taifa. Aidha, Amri ya Masharti ya Mpito ya Mwalimu Nyerere
iliyohalalisha Nembo ya Taifa ya Tanganyika kutumika kama Nembo ya Taifa ya
Jamhuri ya Muungano haikuhusu Wimbo wa Taifa.
Kwa nchi na serikali ambayo imejidai kwa
‘upekee’ wake katika mambo mengi, kushindwa kutambua hata Wimbo wake Taifa ni
kitendo cha fedheha kubwa sana kwa nchi yetu na wale ambao wameitawala tangu
uhuru. Nchi nyingine za ki-Afrika zimetupita mbali katika kuenzi Alama zao za
Taifa kwa kuzitambua kikatiba. Hivyo, kwa mfano, ibara ya 9(1) na (2) na Nyongeza
ya Pili ya Katiba ya Kenya, 2010, imefafanua Alama za Taifa za Kenya pamoja
na kuweka maneno ya Wimbo wa Taifa wa nchi hiyo. Vivyo hivyo, ibara ya 4 na Nyongeza
ya Nne ya Katiba ya Zimbabwe, 2013, nayo imeweka Alama za Taifa za Zimbabwe
pamoja na maneno na muziki wa Wimbo wa Taifa wa nchi hiyo. Sisi, tunaojidai
kuwa mfano wa kuigwa na nchi nyingine duniani, hatujaitaja Bendera yetu ya
Taifa mahali popote katika Katiba na Sheria zetu!
Mheshimiwa Mwenyekiti,
Zaidi ya kupendekeza nyongeza ndogo kwenye
ibara ya 3(2), wajumbe walio wengi wa Kamati Namba Nne hawakuona tatizo lolote
la mapendekezo ya ibara ya 3 ya Rasimu. Hata hivyo, mkanganyiko ambao
tumeuonyesha kuhusu jambo hili muhimu unaonyesha haja kubwa ya kuwa na mwanzo
mpya kikatiba katika masuala ya Alama za Taifa. Kwa sababu hiyo, wajumbe walio
wachache wanapendekeza kwamba ibara ya 3(1) ya Rasimu ifanyiwe marekebisho ili
iweze kusomeka ifuatavyo:
(a) Bendera ya Taifa ya Shirikisho na Bendera za Taifa za Nchi
Washirika wa Shirikisho;
(b) Wimbo wa Taifa wa Shirikisho na Nyimbo za Taifa za Nchi
Washirika wa Shirikisho;
© Nembo ya Taifa ya Shirikisho na Nembo za Taifa za Nchi Washirika
wa Shirikisho,
kama zitakavyoainishwa katika sheria husika za
nchi.”
Mheshimiwa Mwenyekiti,
Wajumbe walio wachache wa Kamati Namba Nne
wanapendekeza pia marekebisho katika ibara ya 3(2) ya Rasimu. Kama ilivyo hivi
sasa, ibara hiyo inaendeleza upotoshaji wa historia ya Jamhuri ya Muungano na
ya nchi washirika wa Muungano. Kwanza, kupendekeza kuendelea kuadhimisha Siku
ya Uhuru wa Tanganyika wakati Tanganyika yenyewe haitambuliwi kikatiba ni
kuendeleza unafiki wa kikatiba na wa kisiasa ambao umeendelea kwa nusu karne.
Kama taifa, hatuwezi kuendelea kuishi katika uongo kwa namna hii.
Pili, Zanzibar haikupata uhuru wake Siku ya
Mapinduzi ya tarehe 12 Januari, 1964. Zanzibar ilipata uhuru wake siku ya
tarehe 10 Disemba, 1963, ikiwa na Serikali halali iliyochaguliwa na wananchi
kwenye uchaguzi huru na wa haki kwa mujibu wa sheria zilizokuwepo wakati huo.
Uhuru huo ulitambuliwa na jumuiya ya kimataifa pale Zanzibar ilipokubaliwa
kujiunga kama mwanachama wa 99 wa Umoja wa Mataifa tarehe 16 Disemba, 1963.[62] Hata Sheikh Abedi Karume, aliyekuja kushikilia
uongozi wa Zanzibar ya baada ya Mapinduzi na mwasisi wa Muungano, alitambua
uhuru huo wa Zanzibar. Katika hotuba yake ya kuukaribisha Uhuru wa Dola ya
Zanzibar wa tarehe 10 Disemba, 1963, Sheikh Karume alitamka maneno yafuatayo:
“Leo tarehe 10 Disemba,
1963, ZANZIBAR imekuwa Huru. Hii leo sisi watu wa visiwa hivi tumepata haki ya
kuchukuwa mahala petu kuwa ni Dola sawa na nyengine katika umoja wa Nchi za
Dola za Commonwealth. Kwa uchache, kuwa mwanachama katika umoja huo, kuna maana
kwamba nchi hii ni huru chini ya mpango wa Sirikali ambayo msingi wake
umejengwa juu ya kuendelea kwa ridhaa ya wananchi.
“Ili kufikilia matarajio
yetu hayo tunayo moja katika Katiba zenye msingi madhubuti iliyohusika na
shuruti za haki za binadamu, haki za mambo ya siasa na uhuru wa dola yoyote
nyengine. Ni wajibu wa watu wote wa dola yetu mpya, kila mmoja katika sisi bila
ya kujali fikra zetu za siasa au madaraka yetu kusaidia kweli kweli Katiba yetu
iweze kufanya kazi. Pamoja na manufaa, haki na uhuru ambayo yote hayo
yamepatikana baada ya nchi kuwa huru.”
Mwezi mmoja baada ya kutamka maneno hayo,
‘Sirikali ambayo msingi wake umejengwa juu ya ... ridhaa ya wananchi’
ilipinduliwa kwa nguvu za kijeshi, na Sheikh Karume akafanywa kuwa Rais wa
Jamhuri ya Watu wa Zanzibar iliyotokana na Mapinduzi hayo!
Ukweli huu wa kihistoria, hata kama utakuwa ni
mchungu kwa baadhi ya watu, unahitaji kutambuliwa ili kuiwezesha nchi yetu kuwa
na mapatano na mwafaka wa kitaifa. Na mahali pa kuanzia mchakato wa mapatano ya
kitaifa ni kufichua historia hii iliyofichwa kwa nusu karne kwa kuifanya Siku
ya Uhuru wa Zanzibar kuwa Sikukuu ya Kitaifa sawa na Siku ya Uhuru wa
Tanganyika na Siku ya Mapinduzi. Kwa sababu hiyo, wajumbe walio wachache wa
Kamati Namba Nne wanapendekeza marekebisho yafuatayo katika ibara ya 3(2) ya
Rasimu:
(a) Kwa kufuta aya yote ya (c) na kuibadilisha na aya mpya ya (c)
itakayosomeka ‘Siku ya Uhuru wa Zanzibar itakayoadhimishwa tarehe 10 Disemba.’
(b) Kwa kuingiza aya mpya ya (d) itakayosomeka ‘Siku ya Shirikisho
la Jamhuri za Tanganyika na Zanzibar itakayoadhimishwa katika tarehe ya
kupitishwa Katiba Mpya ya Shirikisho la Jamhuri za Tanganyika na Zanzibar.’
Mapendekezo haya yanaiondoa Siku ya Muungano
kama Sikukuu ya Kitaifa. Kwa sababu ambazo tumezielezea kwa kirefu kuhusiana na
ibara ya 1 ya Rasimu, ni wazi kwamba Muungano wa aina hii haustahili kuendelea
kupewa enzi ya kuwa na Sikukuu yake ya Kitaifa.
Wajumbe wa Kamati Namba Nne walikuwa na mjadala
mkali sana kuhusu mapendekezo ya ibara ya 4 ya Rasimu. Ibara hiyo inahusu
‘Lugha ya Taifa na lugha za alama.’ Ibara ya 4(1) inakifanya Kiswahili kuwa
Lugha ya Taifa ambayo “... itatumika katika mawasiliano rasmi ya kitaifa na
kiserikali.” Ibara ya 4(2) inaruhusu matumizi ya lugha ya Kiingereza au ‘lugha
nyingine yoyote’ kama “... lugha rasmi ya mawasiliano ya kiserikali pale
itakapohitajika.” Mwisho, ibara ya 4(3) inaitaka Serikali kuweka “... mazingira
yatakayowezesha kuwepo kwa mawasiliano mbadala zikiwemo lugha za alama, maandishi
yaliyokuzwa na nukta nundu kwenye sehemu muhimu za umma na katika vyombo vya
habari vinavyotangaza habari zake kitaifa kwa ajili ya watu wenye mahitaji
maalum.”
Wajumbe walio wachache wa Kamati Namba Nne
wanapendekeza marekebisho yafuatayo katika ibara ya 4 ya Rasimu.
“4(1) Lugha ya Taifa ya
Shirikisho itakuwa ni Kiswahili na itatumika katika shughuli zote za umma na
mawasiliano yote rasmi ya kitaifa na kiserikali.
“4(2) Kiswahili kitakuwa
ndio Lugha ya Mahakama za Shirikisho na pia Lugha ya Mabunge ya Shirikisho na
Sheria, Muswada, Maazimio na nyaraka nyingine za kibunge zitakuwa katika Lugha
ya Kiswahili.
“4(3) Bila ya kuathiri
masharti ya ibara ndogo ya (1) na (2), lugha ya Kiingereza au lugha nyingine
yoyote inaweza kutumika kuwa lugha rasmi ya mawasiliano ya kiserikali pale
itakapohitajika.
“4(4) Mamlaka ya nchi-
(a) zitakuza na kulinda utajiri wa lugha za watu wa Shirikisho la
Jamhuri; na
(b) zitakuza uendelezaji na matumizi ya lugha za makabila na
jumuiya za Shirikisho la Jamhuri pamoja na kuweka mazingira yatakayowezesha
kuwepo kwa mawasiliano mbadala zikiwemo lugha za alama, maandishi yaliyokuzwa
na nukta nundu kwenye sehemu muhimu za umma na katika vyombo vya habari
vinavyotangaza habari zake kitaifa kwa ajili ya watu wenye mahitaji maalum.”
Mheshimiwa Mwenyekiti,
Sababu za mapendekezo haya ya wajumbe walio
wachache zinajionyesha wazi. Tanzania ni nchi ya asili ya Kiswahili. Hata hivyo,
na licha ya matamko ya wanasiasa na watawala katika kipindi chote cha uhuru wa
Tanganyika na Zanzibar na tangu Muungano wa mwaka 1964, Kiswahili hakijawahi
kutambuliwa rasmi kikatiba kama Lugha ya Taifa au hata lugha rasmi ya shughuli
za kiserikali. Tofauti pekee ni Zanzibar ambayo Katiba yake imetambua Kiswahili
kuwa lugha rasmi ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar na lugha ya sheria za
Zanzibar.[63] Hata Kenya, ambayo
Kiswahili chake ni cha kuungaunga, imetambua Kiswahili kuwa Lugha ya Taifa ya
Jamhuri ya Kenya na moja ya lugha mbili rasmi za nchi hiyo.[64]
Sababu ya pili ni haja ya kuondokana na
utamaduni tuliourithi kutoka kwa wakoloni ambao ulifanya Kiswahili iwe na hadhi
ya chini kulinganisha na Kiingereza katika shughuli za kiserikali, kimahakama na
kibunge. Hadi sasa lugha rasmi ya Muswada na Sheria zinazotungwa na Bunge la
Jamhuri ya Muungano ni Kiingereza.
Hata pale ambapo Sheria imetafsiriwa kwenda
kwenye Kiswahili, kama ambavyo imetokea mara kwa mara, sheria za tafsiri za
sheria zimeelekeza kwamba panapotokea mgongano wa kisheria kati ya lugha hizo
mbili, basi lugha iliyotungiwa sheria hiyo, yaani Kiingereza, ndiyo inayotiliwa
nguvu na tafsiri ya Kiswahili inatanguka.
Aidha, licha ya sheria za nchi kuweka bayana
kwamba lugha ya Mahakama ni Kiswahili au Kiingereza, sheria hizo zimesisitiza
kwamba lugha ya kumbukumbu za Mahakama itakuwa ni Kiingereza. Katiba Mpya ni
fursa muhimu ya kupandisha hadhi lugha yetu ya taifa kwa kuifanya kuwa lugha ya
shughuli zote za kiserikali, kimahakama na kibunge.
Tatu, Katiba Mpya inatupa fursa muhimu ya
kutambua, kulinda na kukuza lugha zetu za asili na lugha za alama. Lugha ni
sehemu muhimu ya utambulisho na utajiri wetu wa kiutamaduni. Hata hivyo, tangu
uhuru, lugha za makabila yetu zimepigwa vita kuwa kuzitambua, kuzikuza na
kuziendeleza kutajenga ukabila na utengano wa kitaifa. Aidha, dhana potofu
imejengwa kwamba kukuza na kuendeleza Kiswahili ndio njia pekee ya kujenga
umoja na utengamano wa kitaifa.
Mwelekeo wa sasa wa kikatiba katika nchi za
Afrika ni kutambua na kuendeleza lugha za watu wa Afrika kama sehemu ya utu
wetu, utambulisho wetu na utajiri wetu wa kiutamaduni. Kwa mfano, Katiba za
nchi za Ghana,[65] Kenya[66] na Zimbabwe[67] zimetambua lugha za asili za nchi zao kama sehemu ya
utambulisho na utajiri wao wa kiutamaduni.
Ibara za 5, 6 na 9 za Rasimu zilipitishwa na
Kamati Namba Nne kwa kuungwa mkono na theluthi mbili za wajumbe wote wa Kamati
kutoka Tanzania Bara na theluthi mbili ya wajumbe wote wa kutoka Zanzibar kama
inavyotakiwa na kifungu cha 26(2) cha Sheria na kanuni ya 64(1) ya Kanuni.
Hivyo, kwa mujibu wa kanuni ya 32(3) ya Kanuni, maoni haya hayahusu ibara hizo za
Rasimu.
IBARA YA 8
Mheshimiwa Mwenyekiti,
Ibara ya 8 ya Rasimu inahusu ‘Ukuu na utii wa
Katiba’ na ilizua mjadala mkali sana katika Kamati Namba Nne. Wajumbe walio
wengi kwenye Kamati hawakupendekeza marekebisho yoyote katika ibara hiyo. Hata
hivyo, wajumbe hao walipiga kura kupinga marekebisho yaliyopendekezwa na
wajumbe walio wachache.
Mapendekezo hayo ni kwamba ibara ya 8(1)
iongezewe maneno ‘kwa kadri yatakavyohusika na utekelezaji wa mambo ya
Muungano.’ Lengo la marekebisho haya ni kuhakikisha kwamba Katiba ya Shirikisho
la Jamhuri inakuwa na ukuu katika mambo yote yanayohusu Shirikisho, na Katiba
za Nchi Washirika zinakuwa na ukuu katika masuala yote yanayohusu Nchi
Washirika ambayo sio mambo ya Shirikisho. Mapendekezo haya yatalinda
u-shirikisho wa nchi yetu na mamlaka ya Nchi Washirika katika masuala yasiyo ya
Shirikisho.
Mheshimiwa Mwenyekiti,
Mapendekezo haya hayaongezi kitu chochote kipya
katika kamusi ya kikatiba ya nchi yetu. Hii ni kwa sababu, hata ibara ya 64(5)
ya Katiba ya sasa ya Muungano inayohusu ukuu wa Katiba ya Muungano imeweka wazi
kwamba ukuu huo unahusu mambo ya Muungano tu: “Bila ya kuathiri kutumika kwa
Katiba ya Zanzibar ... kuhusu mambo yote ya Tanzania Zanzibar yasiyo mambo ya
Muungano, Katiba hii itakuwa na nguvu ya sheria katika Jamhuri nzima ya
Muungano na endapo sheria nyingine yoyote itakiuka masharti yaliyomo katika
Katiba hii, Katiba ndiyo itakuwa na nguvu, na sheria hiyo nyingine, kwa kiasi
inachokiuka Katiba, itakuwa batili.”
Ukuu huu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano
katika mambo ya Muungano pekee unathibitishwa pia na ibara ya 4 ya Katiba ya
Zanzibar inayohusu ukuu wa Katiba ya Zanzibar: “Katiba hii ni Katiba ya
Zanzibar na itakuwa na nguvu za kisheria nchini kote na isipokuwa kutokana na
kifungu cha 80 ikiwa sheria yoyote inatofautiana na Katiba hii, basi Katiba hii
ndiyo itayokuwa na nguvu na sheria hiyo itakuwa batili kwa kiwango kile ambacho
kinahitilafiana.”
Kama ambavyo tumeeleza kwa kirefu kuhusu ibara
ya 1 ya Rasimu, kwa miaka hamsini ya Muungano wetu, Serikali ya Jamhuri ya
Muungano imenyakua mamlaka ya Zanzibar kwa mambo ambayo hayakuwa mambo ya
Muungano kwa mujibu wa Hati ya Makubaliano ya Muungano. Hilo limefanyika kwa
njia mbali mbali lakini kwa kiasi kikubwa kwa kuongeza orodha ya mambo ya
Muungano kwenye Katiba au kwa kutunga sheria za kawaida na kuzifanya kuwa
sheria za Muungano.
Endapo mapendekezo ya ibara ya 8 ya Rasimu
yataachwa yalivyo bila kurekebishwa, athari yake kubwa itakuwa ni kufuta kabisa
haiba ya u-shirikisho (federalism) ambayo imekuwa sehemu ya mfumo wetu wa
kikatiba kwa nusu karne. Hakutakuwa tena na tofauti kati ya mambo ya shirikisho
na mambo yasiyo ya shirikisho yaliyoko chini ya mamlaka ya Nchi Washirika.
SURA YA SITA
IBARA YA 60
Rasimu ya Katiba Mpya inapendekeza mabadiliko
makubwa katika muundo wa Jamhuri ya Muungano katika maeneo mawili. Kwanza,
ibara ya 60(1) ya Rasimu inapendekeza “... muundo wa shirikisho lenye
serikali tatu ambazo ni Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Serikali
ya Mapinduzi ya Zanzibar; na Serikali ya Tanzania Bara.”
Pili, Rasimu inapendekeza mabadiliko makubwa
katika orodha ya Mambo ya Muungano. Kwa mujibu wa aya za 62(1) na 63 za Rasimu,
Serikali ya Jamhuri ya Muungano itakuwa na mamlaka ya utekelezaji kwa mambo
yote yaliyoorodheshwa katika Nyongeza ya Katiba kuwa Mambo ya Muungano. Mambo
ya Muungano yaliyoorodheshwa katika Nyongeza hiyo ni Katiba na mamlaka ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ulinzi na usalama, uraia na uhamiaji na sarafu
na Benki Kuu. Mambo mengine ya Muungano ni mambo ya nje, usajili wa vyama vya
siasa na ushuru wa bidhaa na mapato yasiyo ya kodi yatokanayo na mambo ya
Muungano. Kwa ujumla, Rasimu inapendekeza kuwa na Mambo ya Muungano saba.
Kama ambavyo tumeonyesha katika Sura ya Kwanza,
suala la Mambo ya Muungano limekuwa na utata mkubwa katika miaka hamsini ya
Muungano. Sasa Rasimu inapendekeza Mambo ya Muungano kuwa saba, na kati ya hayo
ni Mambo matano tu – Katiba na mamlaka ya Jamhuri ya Muungano, ulinzi na
usalama, uraia, uhamiaji na mambo ya nje - ambayo yalikuwepo kwenye orodha ya
mwanzo ya Mambo ya Muungano. Na katika Mambo 11 yaliyoongezwa baada ya
Muungano, ni mambo mawili tu – sarafu na Benki Kuu na usajili wa vyama vya
siasa – ambayo yamebaki katika Rasimu. Kwa ujumla, Rasimu inapendekeza kuondoa
Mambo 16 yaliyopo katika orodha ya sasa ya Mambo ya Muungano na kuongeza jambo
moja jipya – ushuru wa bidhaa na mapato yasiyo ya kodi yatokanayo na mambo ya
Muungano – katika orodha hiyo.
Mapendekezo ya Rasimu kuhusu Mambo ya Muungano
yanaashiria mabadiliko makubwa katika muundo wa sasa wa Muungano, na katika
Hati za Makubaliano ya Muungano zilizosainiwa mwaka 1964. Kama tulivyoonesha
kuhusu ibara ya 1 ya Rasimu, mapendekezo haya ya ibara ya 60 Rasimu hayawezi
kuitwa ‘Mwendelezo wa Hati ya Makubaliano ya Muungano.’
Mapendekezo ya muundo wa shirikisho lenye
serikali tatu na Mambo ya Muungano yamezua mjadala mkubwa wa kisiasa na
kitaaluma. Katika mhadhara wake juu ya Rasimu ya Kwanza, Profesa Shivji alihoji
madai ya aya ya 1(3) ya Rasimu. Kwa mujibu wa Profesa Shivji, “... Hati (ya
Makubaliano ya Muungano) iliweka serikali mbili; sasa iweje rasimu
inayozungumzia serikali tatu iwe na msingi ambao ulijengeka kwenye serikali
mbili?... Katiba iliyojikita kwenye serikali tatu haiwezi, kwa vyovyote vile,
ikawa mwendelezo wa Hati (za Makubaliano ya Muungano).”[68]
Kama lilivyo jina la mhadhara wake, hoja hii ya
Profesa Shivji ina ‘utatanishi’ mkubwa, kwani kumekuwa na mabishano makubwa na
ya kihistoria kuhusu tafsiri halisi ya Makubaliano ya Muungano juu ya muundo wa
Muungano. Katika kitabu chake Pan Africanism or Pragmatism?, Profesa
Shivji mwenyewe amedai kwamba Rais wa pili wa Zanzibar Aboud Jumbe Mwinyi na
wasaidizi wake wa karibu waling’olewa madarakani mwaka 1984 kwa sababu ya
kuhoji, pamoja na mambo mengine, muundo wa Muungano wa Serikali Mbili kwa madai
kwamba Hati za Makubaliano ya Muungano zilikuwa zimeweka utaratibu wa muundo wa
shirikisho lenye Serikali Tatu.
Miaka kumi na saba kabla ya kuchapishwa kitabu
hicho, Tume ya Nyalali iliyoteuliwa na Rais Ali Hassan Mwinyi kuchunguza kama
Tanzania iendelee kuwa na chama kimoja cha siasa au vyama vingi ilipendekeza
muundo wa Shirikisho lenye Serikali tatu.[69] Mwaka mmoja baadaye, mwasisi wa Muungano na Rais wake wa
kwanza, Mwalimu Nyerere aliandika yafuatayo kuhusu madai ya Rais Jumbe
yaliyopelekea ‘kuchafuka kwa hali ya hewa ya kisiasa’ Zanzibar: “Huko nyuma
baadhi ya viongozi wa Zanzibar wapinzani wa Muungano wamewahi kudai tufanye
referendum kwa Zanzibar kuhusu Muungano. Tukakataa kwa sababu safi kabisa.”[70]
Katika kitabu hicho hicho, Mwalimu Nyerere
alisema yafuatayo juu ya kilichotokea kwenye Bunge la Jamhuri ya Muungano mwaka
1993:
“Tarehe 30 Julai, 1993 wakati mkutano wa
bunge la bajeti ukiendelea, zaidi ya wabunge 50 kwa pamoja walitoa taarifa ya
kusudio la kuwasilisha hoja Bungeni ambayo inadai (kwamba) kuendelea na mfumo
huu wa Muungano usiowaridhisha wananchi wengi wa upande mmoja ni kuhatarisha
kuendelea kudumu kwa Muungano.... Hivyo basi wabunge hawa wanaliomba Bunge ...
liazimie kwamba Serikali ... ilete Muswada Bungeni kabla ya Februari 1994,
kurekebisha katiba ya Jamhuri ya Muungano ili kuwezesha uundaji wa ‘Serikali ya
Tanganyika’ ndani ya Muungano....
Tarehe 20 Agosti, 1993
wabunge wahusika waliwasilisha taarifa nyingine ... iliyokuwa inalitaka Bunge
... liazimie kwamba Serikali ... iandae kura ya maoni ambayo itafanyika kabla
ya 31 Desemba, 1994 ili kupata maoni ya wananchi wa Tanzania juu ya kuundwa kwa
“Serikali ya Tanganyika” ndani ya Muundo wa Muungano....”
Aidha, miaka kumi na moja kabla ya kuchapishwa
kwa kitabu cha Profesa Shivji, Tume ya Kissanga iliyoteuliwa na Rais Benjamin
Mkapa kuchunguza masuala mbali mbali ya kikatiba, nayo ilipendekeza muundo wa
Shirikisho lenye Serikali tatu.
MUUNDO WA SERIKALI MBILI UMESHINDWA!!!
Mapendekezo ya kubadili muundo wa Muungano
yaliyotolewa na Tume mbali mbali za kikatiba pamoja na Rasimu yanathibitisha
mambo mawili. Kwanza, Muungano umekuwa na migogoro isiyoisha na ambayo
haijapatiwa ufumbuzi hadi sasa. Jambo la pili ni kwamba, baada ya karibu nusu
karne ya maisha yake, muundo wa Muungano wenye Serikali mbili umeshindwa na
hauwezi tena kutatua migogoro ya Muungano.
Sehemu kubwa ya migogoro hiyo inatokana na
historia ya kuanzishwa kwake. Kama ambavyo wasomi wa historia ya Muungano
wameonyesha, Muungano huu ulianzishwa kwa sababu ya shinikizo la mataifa
makubwa ya Magharibi yaliyokuwa na hofu kwamba Mapinduzi ya Zanzibar yangeleta
siasa za kijamaa katika pwani ya Afrika Mashariki kwa sababu, mara tu baada ya
Mapinduzi hayo, Jamhuri ya Watu wa Zanzibar ilitambuliwa na nchi za kijamaa za
wakati huo. Aidha, watawala wa nchi za Afrika Mashariki, na hasa waasisi wa
Muungano Mwalimu Nyerere na Sheikh Abeid Amani Karume, walikuwa na hofu ya
tawala zao kupinduliwa kutokana na mfano wa Mapinduzi ya Zanzibar.
Sababu zote hizi zilipelekea Muungano kufanywa
kwa siri kubwa, na kwa vyovyote vile, bila kupata ridhaa ya wananchi wa
Tanganyika au Zanzibar au ya vyombo vyao vya uwakilishi. Kama ambavyo
tumekwishaonesha katika maoni haya, sio tu kwamba Baraza la Mapinduzi
lililokuwa linatawala Zanzibar wakati huo lilikataa pendekezo la Muungano, bali
pia halikutunga sheria ya kuridhia Hati za Makubaliano ya Muungano baada ya
Sheikh Karume kuamua kuunganisha Zanzibar na Tanganyika bila ridhaa ya Baraza
la Mapinduzi!
Kwa upande wake, Bunge la Tanganyika
liliitishwa kwa dharura siku tatu baada ya kusainiwa kwa Hati za Makubaliano ya
Muungano na kutakiwa kupitisha Sheria ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar
siku hiyo hiyo kwa kutumia hati ya dharura! Sheria hiyo ilipitishwa bila
mjadala wowote wa maana na kesho yake, tarehe 26 Aprili, 1964, Muungano wa
Tanganyika na Zanzibar ukazaliwa rasmi! Kwa hiyo, kama ambavyo Profesa Shivji
na wasomi wengine wa Muungano wameonyesha, Muungano ulizaliwa bila uhalali wa
kisheria wala baraka za kisiasa za wananchi wa nchi hizi mbili.
Sehemu nyingine kubwa ya migogoro ya Muungano
imetokana sio kwa sababu ya namna ulivyozaliwa, bali na utekelezaji wa masharti
ya Hati za Makubaliano ya Muungano. Hii ni kwa sababu, wakati Muungano umetukuzwa
katika majukwaa ya kisiasa, umekuwa ukikiukwa kwa vitendo - hasa hasa na
Serikali ya Jamhuri ya Muungano - wakati wote wa historia yake ya karibu miaka
hamsini. Kama tulivyoonesha, mbinu kubwa iliyotumiwa kukiuka masharti ya Hati
ya Makubaliano ya Muungano ilikuwa kuongeza Mambo ya Muungano kwenye orodha ya
Mambo ya Muungano yaliyokuwa kwenye Hati za Makubaliano ya Muungano
zilizosainiwa mwaka 1964.
‘KERO ZA MUUNGANO’ AU ‘MUUNGANO WA KERO’?
Mheshimiwa Mwenyekiti,
Mfano mwingine unaoonyesha kwamba muundo wa
Muungano wa Serikali Mbili umeshindwa kutatua matatizo ya Muungano ni kile
kinachojulikana katika kamusi ya kisiasa ya nchi yetu kama ‘Kero za Muungano.’
Tangu kung’olewa madarakani kwa Rais Jumbe mwaka 1984, mjadala wowote juu ya
‘Hati ya Kuzaliwa’ ya Muungano – kama Jumbe alivyoziita Hati za Makubaliano ya
Muungano wakati akijitetea mbele ya Kikao Maalum cha Halmashauri Kuu ya CCM –
imekuwa, kwa maneno ya Jumbe, ‘dhambi.’ Na tangu wakati huo, migogoro inayohusu
Mambo ya Muungano imeacha kutaja ‘Hati za Makubaliano ya Muungano’, badala yake
migogoro hiyo imefichwa ndani ya lugha ya ‘Kero za Muungano.’
Kinachoitwa ‘kero za Muungano’ kiuhalisia ni
migogoro juu ya Mambo mbali mbali ya Muungano kati ya Serikali ya Jamhuri ya
Muungano na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar. Hii inadhihirishwa na ‘Hoja za
Muungano’ zilizojadiliwa katika vikao mbali mbali vilivyofanywa kati ya
Serikali zote mbili kati ya Oktoba 2012 na Machi 2013: hisa za Serikali ya
Mapinduzi Zanzibar zilizokuwa katika Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki;
usajili wa vyombo vya moto; malalamiko ya wafanya biashara wa Zanzibar kutozwa
kodi mara mbili; mapendekezo ya Tume ya Pamoja ya Fedha; mgawanyo wa mapato;
ushiriki wa Zanzibar katika taasisi za nje; utafutaji na uchimbaji mafuta na
gesi asili; ajira kwa watumishi wa Zanzibar katika taasisi za Muungano; uvuvi
kwenye ukanda wa uchumi wa bahari kuu; ongezeko la gharama za umeme kutoka
TANESCO kwenda ZECO; na ushiriki wa Zanzibar katika Jumuiya ya Afrika
Mashariki.
Katika ‘hoja’ hizi ni ongezeko la gharama za
umeme kati ya TANESCO na ZECO pekee ambayo haina uhusiano wowote na masuala ya
Muungano. Kwa upande mwingine, hisa za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika
Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki, wafanya biashara wa Zanzibar kutozwa kodi
mara mbili; mapendekezo ya Tume ya Pamoja ya Fedha na mgawanyo wa mapato yana
uhusiano wa moja kwa moja na ‘mikopo na biashara za nchi za nje’, ‘kodi ya
mapato na ushuru wa forodha’, mambo yanayohusiana na ‘sarafu na fedha’ yaliyoko
katika orodha ya Mambo ya Muungano ambayo ni Nyongeza ya Kwanza ya Katiba ya
Muungano.
Aidha, ushiriki wa Zanzibar katika taasisi za
nje na katika Jumuiya ya Afrika Mashariki ni masuala yenye uhusiano wa moja kwa
moja na ‘mambo ya nchi za nje’ kwenye orodha ya Mambo ya Muungano. Vile vile,
utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi asili yanahusiana na ‘maliasili ya
mafuta ... na gesi asilia’ katika orodha ya Mambo ya Muungano; wakati uvuvi
katika Ukanda wa Uchumi wa Bahari Kuu yanahusiana moja kwa moja na ‘Katiba ya
Tanzania’ inayotangaza sehemu ya bahari inayopakana na Tanzania kuwa ni sehemu
ya eneo la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mwisho, ‘hoja’ ya ajira kwa
watumishi wa Zanzibar katika taasisi za Muungano iko katika ‘utumishi katika
Serikali ya Jamhuri ya Muungano’ kwenye orodha ya Mambo ya Muungano.
Tumeonyesha jinsi ambavyo ‘Kero za Muungano’
zimekuwa sehemu ya historia yote ya Muungano. Kwa mujibu wa Katiba ya Muungano,
kero hizi zinazohusu tafsiri ya masuala ya Muungano zilitakiwa kuamuliwa na
Mahakama Maalum ya Katiba iliyoundwa chini ya ibara ya 125 ya Katiba. Idadi ya
wajumbe wa Mahakama hiyo haijatajwa lakini ibara ya 127(1) inatamka kwamba
wajumbe wake ni “... nusu ya jumla ya wajumbe wote watakaoteuliwa na
Serikali ya Jamhuri ya Muungano na nusu nyingine ... watateuliwa na Serikali ya
Mapinduzi Zanzibar.” Kwa mujibu wa ibara ya 128(2) ya Katiba, akidi ya
kikao cha Mahakama hiyo ni wajumbe wote; na “kila suala linalohitaji uamuzi
... litaamuliwa kwa kufuata kauli ya theluthi mbili ya wajumbe kutoka Tanzania
Bara na theluthi mbili ya wajumbe kutoka Tanzania Zanzibar.” (ibara
ya 128(3) Na kwa mujibu wa ibara ya 126(3), uamuzi wa Mahakama Maalum ya Katiba
“... utakuwa ndio wa mwisho (na) hakutakuwa na haki ya kukata rufaa popote.”
Licha ya Katiba ya Muungano kuweka utaratibu
huu wa kutatua migogoro ya tafsiri ya Katiba kuhusu masuala ya Muungano,
Mahakama Maalum ya Katiba haijawahi kuitishwa kusikiliza migogoro mingi kuhusu
tafsiri ya Katiba kuhusu masuala ya Muungano. Jaribio pekee la kukiitisha
chombo hiki cha kikatiba kutatua migogoro hiyo lilizimwa mwaka 1984 wakati
aliyekuwa Rais wa Zanzibar Aboud Jumbe, Waziri Kiongozi Ramadhani Haji Faki na
Mwanasheria Mkuu Bashir Kwaw Swanzy walipong’olewa madarakani kwa kile
kilichoitwa ‘kuchafuka kwa hali ya hewa ya kisiasa’ Zanzibar. Profesa Shivji
yupo sahihi anaposema - katika Pan Africanism or Pragmatism? – kwamba
‘pengine Mahakama hiyo haikupaswa kufanya kazi’!
Badala ya kutatua matatizo ya Muungano kwa njia
zilizowekwa kikatiba, Serikali ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar
zimeanzisha taratibu za kirasimu zilizoko nje kabisa ya mfumo wa kikatiba wa
Muungano. Ndio maana Taarifa ya Utekelezaji Bajeti Mwaka wa Fedha 2012/13:
Kipindi cha 01 Julai hadi 31 Desemba, 2012, iliyowasilishwa Bungeni tarehe
23 Januari mwaka huu inaelezea uratibu wa vikao vitatu vya Sekretarieti ya
Kamati ya Pamoja ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya
Mapinduzi Zanzibar, iliyoundwa mwaka 2006 ili “... kushughulikia changamoto
zinazojitokeza katika utekelezaji wa Mambo ya Muungano....”
Vile vile, kwa mujibu wa Taarifa hiyo,
vikao vya Kamati ya Makatibu Wakuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano na wa
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na mawaziri wa Serikali hizo vilivyokaa kati ya
tareje 20 Desemba 2012 na 13 Januari 2013 vilikutana kujadili ‘Hoja za
Muungano.’ Haihitaji msisitizo kusema kwamba vikao hivyo vyote havitambuliwi
kikatiba. Katika mazingira haya, ni halali kuuliza swali kama pande zote mbili
za Muungano zinataka kuendelea na Muungano kabla hata ya kujadili muundo wake.
Mheshimiwa Mwenyekiti,
Katika mhadhara wake wa kuaga Kigoda cha
Mwalimu, Profesa Shivji amehitimisha uchambuzi wake wa Rasimu kwa kusema kwamba
muundo wa Muungano unaopendekezwa “... ni tegemezi na ... ni dhaifu kwa
sababu umejengwa juu ya mchanga wa dhamira na nia nzuri badala ya msingi wa
mawe ya nguvu za kikatiba zilizowekwa na wananchi wenyewe. Ni kama kwamba suala
la Muungano ni (la) ujirani mwema badala ya umoja wa nchi.”[71] Kwingineko katika mhadhara huo, mwanazuoni
huyu maarufu ‘amediriki kusema’ kwamba “muundo wenyewe wa serikali tatu
uliopendekezwa (na Rasimu) ni compromise kati ya wale waliosimamia
serikali mbili na wale waliopigania muungano wa mkataba, kwa maneno sahihi,
kuuvunja muungano.”[72]
Ijapokuwa hajasema wazi wazi, Profesa Shivji
anaonyesha kupendelea kwamba muundo wa sasa wa Muungano wa serikali mbili ni
bora zaidi na hauna budi kuendelea. Kwa maneno yake, “... compromise inazaa
uamuzi legelege. Compromise juu ya muundo ... imezaa muundo wa muungano
legelege. Kuna maeneo mengi ... yatazaa migogoro ambayo hatimaye inaweza
kuuvunja Muungano. Kero za Muungano zitaendelea, safari hii kutoka pande zote
mbili.”[73]
Si sahihi kupuuza hoja na kauli za mwanazuoni
huyu maarufu. Hata hivyo, ni muhimu kuhoji uhalali wake kwa kuangalia historia
halisi ya Muungano wetu. Kwanza kabisa, kama ambavyo Profesa Shivji mwenyewe
amedhihirisha katika maandishi yake ya zaidi ya miaka ishirini, Muungano huu
haujawahi kuwa Muungano wa watu wa Tanganyika na Zanzibar, bali ulikuwa na
umeendelea kuwa Muungano wa watawala kwa maslahi ya watawala wa ndani ya nchi
yetu na wa nchi za kibeberu!
Tatu, kwa kuangalia mwelekeo wa siasa za sasa
za kikatiba za Zanzibar, ni wazi kwamba wananchi wa Zanzibar wanapendelea uhuru
kuliko kuendelea na Muungano huu. Profesa Shivji anathibitisha hili kwa kauli
yake kwamba “Wazanzibari kwa muda mrefu tu wamedai haki yao ya kujiamulia
mambo yao wenyewe.”[74] Nne, kwa sababu ya kuwa Muungano wa watawala badala ya kuwa
Muungano wa wananchi; kwa sababu ya kutoheshimiwa na watawala hao; na kwa
sababu ya mwelekeo wa siasa za Zanzibar za sasa, ‘Kero za Muungano’ haziwezi
kutatuliwa kwa kutumia muundo wa sasa wa Serikali mbili. Compromise ya
serikali tatu, katika mazingira haya, ni njia pekee iliyobaki ya kuwa na
Muungano, hata kama ni muundo dhaifu na legelege kama anavyolalamika Profesa
Shivji! Nje ya serikali tatu ni uhuru kamili wa ‘Washirika wa Muungano’ na
kuzaliwa upya kwa Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar.
BILA MUUNGANO KUWEPO NI VITA???
Katika hitimisho la mhadhara wake, Profesa
Shivji ametoa ‘picha ya kiama’ (doomsday scenario) endapo Muungano
utavunjika kwa sababu ya kukubaliwa muundo wa shirikisho lenye serikali tatu: “Muungano
ukivunjika hakuna mwananchi atakayenusurika, awe wa Tanganyika au wa Zanzibar.”[75]
Pili, kuna nchi nyingi ambazo zimepigana vita
ya wenyewe kwa wenyewe kwa muda mrefu kwa sababu ya kulazimisha muungano
usiokubaliwa na upande mmoja au mwingine katika umoja huo. Ethiopia na Eritrea
ni mfano mmojawapo. Mwaka 1952 Ethiopia ilisaini makubaliano kati yake na
Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa yaliyoifanya Eritrea sehemu ya Shirikisho la
Ethiopia na hivyo kumaliza utawala wa Uingereza katika koloni hilo la zamani la
Italia.
Hata hivyo, tarehe 14 Novemba, 1962, Mfalme
Haile Selassie I wa Ethiopia alivunja makubaliano hayo kwa nguvu na kuifanya
Eritrea kuwa sehemu ya Himaya yake. Vita vya ukombozi vilivyosababishwa na
kitendo hicho vilichukua karibu miaka thelathini hadi Ethiopia iliposhindwa
mwaka 1991 na Eritrea kujipatia uhuru kamili.[77] Vile vile Profesa Shivji anaufahamu mfano huu vizuri sana, kwa
sababu alikuwa mmoja wa wanazuoni wengi waliounga mkono wa Chama cha Ukombozi
wa Watu wa Eritrea (Eritrean People’s Liberation Front - EPLF),
kilichoongoza mapambano ya uhuru wa nchi hiyo.
Sudan ya zamani ni mfano mwingine wa vita
vilivyosababishwa na kulazimisha muungano usiotakiwa na upande mmoja.[78] Mnamo Februari, 1953, Uingereza na Misri
zilizokuwa zinatawala Sudan ya Kusini na ya Kaskazini kama maeneo tofauti kwa
utaratibu wa Condominium zilikubaliana kukabidhi uhuru kwa shirikisho la
Sudan ifikapo tarehe 1 Januari, 1956. Hata hivyo, kabla ya tarehe hiyo kufika,
viongozi wa Sudan Kaskazini walikiuka makubaliano ya kuunda serikali ya
shirikisho. Matokeo yake ni kwamba wananchi wa Sudan Kusini waliasi na
kuanzisha kile kinachojulikana katika historia kama Vita ya Kwanza ya Wenyewe
kwa Wenyewe ya Sudan (First Sudanese Civil War au Anyanya I Rebellion).
Vita hiyo ilianza Agosti, 1955 na ilimalizika kwa kusainiwa kwa Makubaliano ya
Amani ya Addis Ababa ya mwaka 1972. Makubaliano hayo yalirudisha mfumo wa Shirikisho
ulioipa Sudan Kusini mamlaka makubwa ya utawala wa ndani. Makubaliano ya Addis
Ababa hayakudumu muda mrefu kwa sababu Serikali Kuu ya Sudan iliyahujumu.
Matokeo yake, mwaka 1978 Maasi ya Anyanya II yalianza tena. Makubaliano ya
Addis Ababa yalivunjika kabisa mwaka 1983 na Vita ya Pili ya Wenyewe kwa
Wenyewe ya Sudan (Second Sudanese Civil War) ilianza mwaka 1983 hadi
ilipoisha baada ya kusainiwa kwa Mkataba wa Amani wa Nairobi wa tarehe 9
Januari, 2005.
Chini ya Mkataba wa Amani wa Nairobi, Sudan Kusini
ilijitawala kwa masuala ya ndani kwa miaka sita hadi 2011 wananchi wa Sudan
Kusini walipopiga kura ya maoni na kuamua kujitenga na Sudan ya Kaskazini.
Tarehe 9 Julai, 2011, Jamhuri ya Sudan Kusini ilizaliwa kama nchi huru. Ni
kweli kwamba bado kuna mgogoro wa mpaka kati ya Jamhuri hiyo mpya na Sudan
Kaskazini. Hata hivyo, mgogoro huo hauwezi kulinganishwa na vita vya wenyewe
kwa wenyewe iliyochukua miaka hamsini kuanzia 1955 hadi 2005! Hapana shaka
kwamba Profesa Shivji anaifahamu historia hii vema, kwani zama za ujana wake
alisoma katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam pamoja na Dk. John Garang, mwasisi
wa Chama/Jeshi la Ukombozi wa Watu wa Sudan (Sudanese People’s Liberation
Movement/Army – SPLM/A).
Tatu, zipo nchi ambazo zinaendelea kuwa na vita
kwa sababu ya kulazimisha umoja ambao upande mmoja unaukataa. India (mgogoro wa
Jimbo la Kashmir), Hispania (Jimbo la Basque) na Angola (Jimbo la Cabinda) ni
mifano mizuri. Ni vigumu kuamini kwamba Profesa Shivji hafahamu mifano ya nchi
hizi pia. Ni wazi, kwa hiyo, kwamba hoja serikali tatu = kuvunja Muungano =
vita na maangamizi ni hoja yenye lengo la kutisha wananchi ili wasiweze
kujadili masuala yote yanayohusu Muungano ikiwamo kuachana nao.
Na nne, hoja ya Profesa Shivji kwamba wanaodai
kuwe na Muungano wa shirikisho lenye serikali tatu ni ‘viongozi wachache’ wenye
‘uchu wa madaraka’ ni ya kusikitisha sana. Hii ni sawa sawa na kuwaita Rais
Aboud Jumbe na wasaidizi wake, au wajumbe wa Tume ya Nyalali, au ya Kissanga au
hata ya sasa ya Warioba, au Wabunge wa G55, waroho wa madaraka kwa sababu tu
hawakukubaliana na mfumo wa serikali mbili ambao Shivji mwenyewe amekiri mara
nyingi umeshindwa kutatua matatizo na ‘Kero za Muungano’!
Tangu kuchapishwa kwa Rasimu, kumejitokeza
kauli kwamba kuwa na muundo wa Muungano wenye serikali tatu itakuwa ni gharama
kubwa kwa nchi maskini kama ya kwetu. Viongozi na makada wa CCM wameidaka hoja
hii ya gharama za Muungano kama ndio turufu yao ya kuendelea na muundo wa sasa
wa Muungano wa Serikali mbili. Katika Ufafanuzi wake, CCM imedai kwamba
“gharama za uendeshaji wa Serikali zilizopo hivi sasa ni kubwa. Kuwepo kwa
Serikali ya tatu kutakuwa ni gharama ya ziada na hivyo kuwa mzigo mkubwa kwa
wananchi.”
Kwa upande wake, Profesa Shivji amezungumzia
suala hili kama ifuatavyo: “Kwa upande wa gharama, ni wazi kwamba kuendesha
serikali ya muungano kutakuwa na gharama kubwa. Kazi inayofanywa na taasisi
moja au idara moja katika muundo uliopo sasa itahitaji taasisi mbili. Kwa
mfano, badala ya kuwa na Tume moja ya uchaguzi, sasa kutakuwa na tume mbili,
moja ya Muungano na nyingine ya Bara. (Ukiongeza ya Zanzibar kutakuwa na Tume
tatu za uchaguzi. Na hivyo hivyo kuhusu tume nyingine. Ukiangalia juu juu tu,
licha ya taasisi na idara za kawaida katika serikali, kuna tume karibu nane na
mabaraza mawili yenye wajumbe wazito ambao bila shaka watakuwa na mishahara
minono na marupurupu poa. Wananchi wamekwishaanza kuonyesha wasiwasi wao kwa
kuwaongezea mzigo wa kubeba serikali kamili nyingine, zaidi ya hizi mbili
tulizonazo.”
Hoja hii ya gharama za kuendesha serikali tatu
ni red herring, yaani ina lengo la kuwatoa wananchi kwenye mjadala wa
msingi juu ya kushindwa kwa muundo wa sasa wa Muungano kutatua ‘Kero za
Muungano’, kwa kuwaaminisha kwamba muundo wa sasa una gharama nafuu zaidi
kuliko muundo wa serikali tatu. Kwanza, kwa kadri ya ufahamu wetu, hadi sasa
hakuna mtu yeyote aliyefanya uchambuzi wa ulinganifu wa gharama za kuendesha
serikali – iwe moja, mbili au tatu – katika nchi yetu. Hata Ufafanuzi wa
CCM uko kimya juu ya jambo hili. Kwa sababu hiyo, hakuna ushahidi wowote wa
kuthibitisha kwamba kuendesha serikali tatu ni ghali zaidi kuliko kuendesha
serikali mbili. Kwa vyovyote vile, kama suala la gharama za kuendeshea serikali
ndio jambo muhimu zaidi katika kuamua muundo wa Muungano, kwa nini tusiwe na
serikali moja tu, kuliko mbili za sasa au tatu zinazopendekezwa na Rasimu?
Pili, na muhimu zaidi, kama tukichukua
mapendekezo ya Mambo ya Muungano kama kigezo cha kupima ukubwa wa serikali – na
kwa hiyo gharama za kuiendeshea – basi gharama za serikali ya Muungano zinaweza
kuwa ndogo sana. Hii ni kwa sababu, haiwezekani – kwa mambo saba ya Muungano
yanayopendekezwa na Rasimu – kuwa na serikali kubwa ya Muungano. Kwa Mambo hayo
ya Muungano, hakutakuwa na zaidi ya wizara nne za Serikali ya Muungano. Hivyo,
kwa mfano, kutakuwa na wizara ya katiba na sheria itakayoshughulikia masuala ya
Katiba na mamlaka ya Jamhuri ya Muungano; wizara ya ulinzi itakayokuwa na
majukumu ya ulinzi na usalama wa Jamhuri ya Muungano; wizara ya fedha
itakayoshughulikia masuala ya sarafu na benki kuu, na ushuru wa bidhaa na
mapato yasiyo ya kodi yatokanayo na Mambo ya Muungano; na wizara ya mambo ya
nje. Masuala yaliyobaki, yaani uraia na uhamiaji na usajili wa vyama vya siasa
hayastahili kuwa na wizara zinazojitegemea kwa hiyo yanaweza kuwekwa chini ya
mojawapo ya wizara zilizotajwa hapo juu.
Ibara ya 98(2) ya Rasimu inapendekeza ukomo wa
ukubwa wa Baraza la Mawaziri la Jamhuri ya Muungano kuwa mawaziri wasiozidi
kumi na tano. Kwa upande mwingine, ibara ya 98(3) inaelekeza kwamba “Serikali
ya Jamhuri ya Muungano itakuwa na Wizara kwa kuzingatia mamlaka ya Serikali kwa
mujibu wa Katiba hii.” Sasa kama mamlaka ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano
yako kwenye mambo saba ya Muungano kwa mujibu wa Rasimu hii, je, hao mawaziri
wasiozidi kumi na tano watatoka wapi na watatimiza majukumu gani? Ni wazi
kabisa kwamba mapendekezo ya ibara ya 98(2) yanakinzana na matakwa ya ibara za
62(1) na 63 zinazohusu mamlaka ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano juu ya Mambo
ya Muungano.
Kwa mtazamo huo huo wa ibara ya 98(3) na orodha
ya Mambo ya Muungano kama kipimo cha ukubwa wa Serikali ya Muungano, taasisi
nyingine zinazopendekezwa na Rasimu haziwezi kuwa kubwa sana na nyingine
hazitakuwepo kabisa. Kwa mfano, Katibu Mkuu Kiongozi na Makatibu Wakuu
wanaopendekezwa katika ibara za 105 na 106 za Rasimu hawawezi kuzidi idadi ya
Wizara nne zilizotajwa hapo juu zitakazoshughulikia Mambo ya Muungano. Kwa
maana hiyo, kwa kuzingatia idadi ya Makatibu Wakuu wenyewe, Kamati Maalumu ya
Makatibu Wakuu inayoelezwa katika ibara ya 107; na Sekretarieti ya Baraza la
Mawaziri inayotajwa katika ibara ya 108, hazina maana wala umuhimu wowote
kikatiba.
Au tuchukue mapendekezo yanayohusu Bunge la
Jamhuri ya Muungano. Kwa mujibu wa ibara ya 105(4) ya Rasimu, kila Jimbo la
Uchaguzi litawakilishwa na wabunge wawili kwa kuzingatia jinsia zao. Ibara ya
113(2)(a) inabainisha ‘Jimbo la Uchaguzi’ kuwa ni kila mkoa kwa upande wa
Tanzania Bara na wilaya kwa upande wa Zanzibar. Aidha, kwa mujibu wa ibara ya
113(2)(b), kutakuwa na wabunge watano wa kuteuliwa na Rais kuwakilisha watu
wenye ulemavu. Tukichukua idadi ya mikoa ishirini na tano ya Tanzania Bara na
wilaya 10 za Zanzibar kwa sasa, Bunge la Jamhuri ya Muungano litakuwa na
wabunge 75.
Kwa mapendekezo ya muundo wa serikali tatu,
Bunge la Zanzibar litakuwa na Wabunge hamsini wa majimbo ya sasa ya uchaguzi;
wakati bunge la Tanganyika litakuwa na wabunge 189 wa majimbo ya uchaguzi ya
sasa. Kwa maana hiyo, muundo wa Muungano wa serikali tatu utakuwa na mabunge
matatu yenye jumla ya wabunge 314.
Kwa kulinganisha, Bunge la Jamhuri ya Muungano
la sasa lina idadi ya wabunge 239 wa majimbo ya uchaguzi – 189 wa majimbo ya
uchaguzi ya Tanzania Bara na hamsini ya Zanzibar. Vile vile, kuna wabunge 102
wa Viti Maalumu, 10 wa kuteuliwa na Rais na watano wanaowakilisha Baraza la wawakilishi
Zanzibar na Mwanasheria Mkuu, kwa idadi ya jumla ya wabunge 357.
Kwa upande wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar,
kuna wawakilishi hamsini wanaowakilisha majimbo ya uchaguzi, kumi wa kuteuliwa
na Rais wa Zanzibar, ishirini wa Viti Maalum na Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar,
kufanya jumla ya wawakilishi themanini na moja. Kwa maana hiyo, kwa muundo wa
sasa wa Muungano, mabunge mawili tuliyonayo yana idadi ya wabunge 438. Idadi
hiyo ni kubwa kuliko idadi ya wabunge wa mabunge matatu yatakayokuwepo chini ya
muundo wa serikali tatu kwa wabunge 124!
Na sio Bunge ambalo linaweza kuwa na gharama
ndogo kuliko gharama za sasa. Taasisi za Muungano zinazopendekezwa kama vile
Tume ya Uhusiano na Uratibu wa Serikali (ibara ya 109); Tume ya Utumishi wa
Mahakama (ibara ya 180); na Tume ya Utumishi wa Umma (ibara ya 186) haziwezi
kuwa kubwa sana kwa kuzingatia ukubwa wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano kwa
mujibu wa Rasimu.
Aidha, uwepo wa taasisi nyingine kama vile Tume
ya Maadili ya Uongozi na Uwajibikaji (ibara ya 200) na Tume ya Haki za Binadamu
(ibara ya 208) unakinzana na matakwa ya aya za 62(1) na 63 za Rasimu na kwa
hiyo haziwezi kugharimiwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano!
Vile vile, majukumu ya utekelezaji wa Mambo
mengine ya Muungano kama uchaguzi na usajili wa vyama vya siasa yanaweza
kutekelezwa na taasisi husika za Washirika wa Muungano kwa makubaliano na
masharti maalumu chini ya aya ya 59(3) ya Rasimu. Hii nayo itapunguza gharama
za kuendesha Serikali ya Jamhuri ya Muungano.
Ni wazi – kwa mtazamo huu – kwamba gharama za
kuendeshea muundo wa shirikisho lenye serikali tatu zinaweza kuwa hata ndogo
kuliko gharama za kuendeshea muundo wa Muungano wa serikali mbili za sasa.
Pendekezo la Rasimu kuhusu muundo wa Serikali
tatu limeleta hoja juu ya faida za Muungano kwa kila upande wa Washirika wa
Muungano. Hivyo, kwa mfano, katika Ufafanuzi wake CCM imedai kwamba
pendekezo hili litaleta “... urasimu na utata wa kisheria katika umiliki na
uendeshaji wa shughuli za kiuchumi na kijamii.” CCM inafafanua zaidi juu ya
jambo hili: “Urasimu wa kibiashara na umilikaji ardhi utaongezeka kwa sababu
biashara, ardhi na umilikaji wa mali wa aina nyingine si mambo ya Muungano.”
Kwingineko katika Ufafanuzi wake, CCM
inadhihirisha kwamba msimamo wake juu ya muundo wa Serikali tatu unatokana na
hofu ya athari za muundo huo kwa maslahi ya kiuchumi ya Wazanzibari walioko, au
wenye vitega uchumi, Tanzania Bara. Hivyo basi, “muundo wa Serikali mbili una
urasimu mdogo wa kisheria na hivyo kutoa fursa nyingi za kiuchumi na kijamii
hususan kwa Wazanzibari ambao eneo lao la ardhi ni dogo wakati idadi ya wakaazi
inaongezeka mwaka hadi mwaka.” Aidha, kwa mujibu wa CCM, “muundo uliopo
unawawezesha Wazanzibari kumiliki ardhi na rasilmali nyingine zilizoko Tanzania
Bara kama raia wa Tanzania, ingawaje ardhi na rasilmali nyingine za kiuchumi si
masuala ya Muungano.”
Mheshimiwa Mwenyekiti,
Inajulikana kwamba, kwa mujibu wa sheria za
Zanzibar, Watanzania Bara hawana haki ya kumiliki ardhi Zanzibar, licha ya kuwa
raia wa Tanzania. Aidha, licha ya kuwa raia wa Tanzania, Watanzania Bara
wanaoajiriwa katika sekta binafsi Zanzibar wanatakiwa kutimiza masharti
ya vibali vya ajira sawa na raia yeyote wa nchi za kigeni. Yote haya ni nje ya
ukweli kwamba Watanzania Bara hawawezi kuajiriwa katika taasisi yoyote ya
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, tofauti na Wazanzibari ambao wanaajiriwa na
taasisi za Serikali ya Jamhuri ya Muungano hata kwa mambo yasiyokuwa ya
Muungano.
Vile vile, yote haya ni nje ya ukweli kwamba
wakati Wazanzibari wanaweza kikatiba kushiriki shughuli za kisiasa na kiutawala
Tanzania Bara hata kwa mambo yasiyokuwa ya Muungano, Watanzania Bara hawana
uwezo huo. Hivyo basi, kwa utaratibu huu, Wabunge wa Zanzibar katika Bunge la
Jamhuri ya Muungano wanashiriki katika mijadala ya mambo yasiyo ya Muungano ya
Tanzania Bara, Wazanzibari wanashikilia nafasi za juu za kisiasa kama vile
uwaziri katika wizara zisizokuwa za Muungano na Baraza la Wawakilishi Zanzibar
lina uwakilishi maalum katika Bunge la Jamhuri ya Muungano. Wananchi wa
Tanzania Bara hawana haki ya kushiriki katika mambo haya kwa upande wa
Zanzibar.
Mheshimiwa Mwenyekiti,
Upinzani wa CCM dhidi ya pendekezo la Rasimu
juu ya muundo wa Serikali tatu unadhihirisha ushawishi mkubwa wa Zanzibar
katika siasa za ndani ya CCM, hasa hasa katika zama hizi za vyama vingi na vita
za makundi mbali mbali ndani ya chama hicho. Katika mazingira haya, mtu yeyote
anayetaka kupitishwa kuwa mgombea urais kwa kupitia CCM anakuwa anahitaji kura
za CCM Zanzibar ili kushinda katika kinyang’anyiro hicho.
Kwa kauli ya Mwalimu Nyerere katika kitabu
chake Uongozi Wetu na Hatima ya Tanzania: “Sababu moja kubwa
iliyofanya viongozi wetu wasitake kuwaudhi ‘Wazanzibari’ ... ni umuhimu wa kura
za Zanzibar katika kumteua mwanachama wa CCM kuwa Mgombea wa Urais wa Jamhuri
ya Muungano. Kwa kiongozi yeyote anayeliona jambo hilo kuwa ni muhimu kupita
mengine yote, kuwaudhi ‘Wazanzibari’ ni dhambi ambayo haina budi iepukwe kwa kila
njia.” Hofu hii ya ‘kuwaudhi’ Wazanzibari ndio imepelekea CCM kutaka
kulinda maslahi ya kiuchumi ya Wazanzibari kwa kukataa muundo wa Serikali tatu.
[1]Hotuba ya Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya
Katiba, Mhe. Joseph S. Warioba, Wakati wa Kukabidhi Ripoti ya Tume kwa Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete na Rais wa
Zanzibar, Mhe. Dkt. Ali Mohamed Shein, 30 Desemba, 2013, Dar es Salaam.
Imenukuliwa kutoka Baraza la Katiba Zanzibar, Katiba Tuitakayo: Muhtasari wa
Rasimu ya Pili na Mapendekezo, Januari, 2014.
[2] Imenukuliwa kutoka Bango Kitita la Randama ya Rasimu ya Katiba ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Februari, 2014, uk. 4
[3] Imenukuliwa kutoka kwenye Bango Kitita la Randama...,
uk. 135.
[4] Tafsiri
ya Kiswahili ya kitabu hiki ilichapishwa na Amana Publishers, Dar es Salaam,
mwaka 1995.
[5] Ibid.,
uk. 24.
[6] Kamati Maalum ya Baraza la Mapinduzi Zanzibar, Muhtasari
Mkuu wa Taarifa ya Kamati ya BLM ya Kujenga Hoja Juu ya Masuala ya Muungano wa
Tanzania, aya ya 36, uk. 12.
[7] Tume pia imezitaja sifa hizi kuwa ndio sifa za msingi
za nchi inayofuata mfumo wa shirikisho. Angalia Bango Kitita la Randama...,
uk. 6-7.
[8] Tanzania: The Legal Foundations of the Union,
Second Expanded Edition, uk. 35.
[9] Ibid.,
uk. 37
[10] Ibid.,
uk. 34
[11] ‘The Consolidation of the Union: A Basic Re-Appraisal.’
Makala hii iliwasilishwa katika Semina iliyoandaliwa na Chama cha Mawakili
Tanganyika tarehe 27-29 Julai, 1983, na baadae kuchapishwa katika kitabu
kilichohaririwa na Maprofesa Chris M. Peter na Haroub Othman, Zanzibar and
the Union Question, kilichochapishwa na Kituo cha Huduma za Kisheria cha
Zanzibar mwaka 2006.
[12] Eastern
African Law Review (1981-1983), 73-137
[13] The
Legal Foundations ... ibid., uk. xi-xii.
[14] uk. 1
[15] Ibid.,
uk. 2-3
[16] Ibid.,
uk. 1
[17] Ibid.,
uk. 2
[18] Ibid.,
uk. 2
[19] Ibid.,
uk. 1
[20] Bango
Kitita la Randama ... uk. 5
[21] Ibid.,
uk. 5-7
[22] Mapendekezo ya Wajumbe wa Kamati Na. 4 ya Bunge Maalum
Kuhusu Marekebisho ya Sura ya Kwanza ya Rasimu ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania.
[23] Sheria Na. 22 ya mwaka 1964, Sura ya 557.
[24] Ibid.,
kifungu cha 4.
[25] Ibara
ya 98(1)(a) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977.
[26] Sheria
Na. 61 ya 1964. Sheria hii ilipata ridhaa ya Rais Nyerere tarehe 10
Disemba, 1964.
[27] Angalia
pia kifungu cha 3(2) cha Sheria hiyo.
[28] Imenukuliwa kutoka Juma Duni Haji, Nyerere na Siasa za Muungano Zanzibar:
Mapinduzi Kayapindua 1964, uk. 36.
[29] Mawasiliano haya yanapatikana katika kitabu cha Harith
Ghassany, Kwaheri Ukoloni, Kwaheri Uhuru: Zanzibar na Mapinduzi ya
Afrabia, kilichochapishwa nchini Marekani mwaka 2010, kurasa 414-420.
[30] Ref. L.D/760/Vol. XXXIV/66 ya tarehe 22 Juni, 2005,
Kuh. ‘KUPATIWA NAKALA YA HATI YA MKATABA WA MUUNGANO WA TANGANYIKA NA
ZANZIBAR.’
[31] Aya ya (iii)(a)
[32] Aya ya (iii)(b)
[33] Aya ya (iii)(c)
[34] Aya ya
(iii)(d)
[35] Aya ya
(iv)
[36] Aya ya
(vi)(a)
[37] Aya ya
(vi)(b)
[38] Aya ya
(vii)(a)
[39] Aya ya
(vii)(b)
[40] Aya ya
(vii)(b)
[41] Tangazo
la Serikali Na. 245 la tarehe 1 Mei, 1964.
[42] Kifungu
cha 3(1)
[43] Kifungu
cha 6(1)
[44] Kifungu
cha 10
[45] Tangazo
la Serikali Na. 246 la tarehe 1 Mei, 1964.
[46] Kifungu
cha 2
[47] Ibara
ya 98(1)(a) ikisomwa pamoja na Nyongeza ya Pili, Orodha ya Kwanza.
[48] Ibara
ya 98(1)(b) ikisomwa pamoja na Nyongeza ya Pili, Orodha ya Pili.
[49] Sheria
Na. 18 ya mwaka 1965.
[50] Sheria
Na. 43 ya mwaka 1965
[51] Ibara
ya 1
[52] Ibara
ya 2(1)
[53] Ibara
ya 3(2)
[54] Ibara ya 2(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, 1977, Toleo la 1977.
[55] Ibara
ya 1
[56] Sheria ya Marekebisho ya Tano ya Katiba ya Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania, 1977, Na. 15 ya 1984.
[57] Ibara ya 1. Mabadiliko hayo pia yalilazimisha
mabadiliko katika Katiba Mpya ya Zanzibar iliyotungwa mwaka huo ambapo ibara
yake ya 1 ilitamka kwamba ‘Zanzibar ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano.’
[58]
[59] Ibara
ya 2(1)
[60] Sheria
Na. 15 ya 1971. Sheria hiyo ilianza kutumika tarehe 7 Mei, 1971.
[61] Ibid.,
kifungu cha 3
[62] Angalia picha za ujumbe wa Zanzibar siku ya Zanzibar
kukubaliwa rasmi kuwa mwanachama wa Umoja wa Mataifa ulioongozwa na Waziri Mkuu
Mohamed Shamte Hamadi na Waziri wa Mambo ya Nje Sheikh Ali Muhsin Barwani na
Balozi wa kwanza wa Zanzibar Umoja wa Mataifa Maalim Hilal Mohamed, Kwaheri
Ukoloni, Kwaheri Uhuru..., ibid., uk. 463-465
[63] Ibara
ya 87 ya Katiba ya Zanzibar, 1984.
[64] Ibara
ya 7(1) na (2) ya Katiba Mpya ya Kenya, 2010.
[65] Ibara
ya 39(3) ya Katiba ya Jamhuri ya Ghana, 1992.
[66] Ibid.,
ibara ya 7(3)
[67] Ibara ya 6 ya Katiba ya Zimbabwe, 2013. Ibara ya
6(1) inatambua lugha 16 za Zimbabwe kuwa ni ‘lugha zinazotambuliwa rasmi’; na
ibara ya 6(3)(a) inaelekeza dola na taasisi na mashirika ya serikali
kuhakikisha kwamba lugha zote zinazotambuliwa rasmi zinatumiwa kwa usawa.
Aidha, ibara ya 7(a) inaielekeza mamlaka ya nchi hiyo kuhakikisha kwamba Katiba
ya Zimbabwe inatafsiriwa kwenye lugha zote zilizotambuliwa rasmi.
[68] Issa G.
Shivji, Utatanishi na Ukimya Katika Rasimu ya Katiba Mpya: Mhadhara wa Kuaga
Kigoda cha Mwalimu, Dar es Salaam, Juni, 2013.
[69] Tanzania,
Tume ya Rais ya Mfumo wa Chama Kimoja au Vyama Vingi vya Siasa Tanzania, Vitabu
Vitatu, 1991.
[70] Mwalimu
Julius K. Nyerere, Uongozi Wetu na Hatima ya Tanzania, Harare, 1993.
[71] Ibid.,
uk.
[72] Ibid.,
uk. 35
[73] Op.
cit.
[74] Ibid.,
uk.
[75] Ibid.,
uk. 36
[76] Ibid.,
uk. 37
[77]
Historia ya vita ya ukombozi wa Eritrea imeelezwa na Michela Wrong katika
kitabu chake I Didn’t it For You: How the World Used and Abused a Small
African Nation, Harper Perennial, London, 2005.
[78] Scopas S. Poggo, War
and Conflict in Southern Sudan, 1955-1972, University of California, Santa
Barbara, 1999; Hizkias Assefa, Mediation of Civil Wars, Approaches and
Strategies – The Sudan Conflict, Westview Press, Colorado, 1987; Edgar
O’Ballance, The Secret War in the Sudan: 1955-1972, Faber & Faber,
Hamden, 1977; and Cecil Eprile, War and Peace in the Sudan, 1955-1972,
David & Charles, London, 1974.
No comments:
Post a Comment