Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora

Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora
----------------------WE THANK AND APPRECIATE YOU FOR VISITING CHADEMA DIASPORA BLOG. AGAIN, THANK YOU!-----------------------

Tuesday, April 15, 2014

Tundu Lissu atikisa Bunge

Mbowe na Jussa wapigilia msumali wa mwisho      

Mjumbe wa Bunge la Katiba, Tundu Lissu amesema Tanganyika ilikufa kwa amri iliyotolewa na Mwalimu Julius Nyerere na siyo kwa makubaliano katika hati ya Muungano. Lissu alitoa kauli hiyo jana alipopata fursa ya kukamilisha dakika 16 za hotuba yake ya ufafanuzi wa maoni ya walio wachache iliyokuwa imekatishwa baada ya matangazo ya moja kwa moja ya Televisheni ya Taifa (TBC1) kukatika Jumamosi iliyopita. Huku akinukuu maneno yaliyopo katika vitabu vilivyoandikwa na Profesa Issa Shivji na Makamu Mwenyekiti mstaafu wa CCM, Pius Msekwa, Lissu alisema Jamhuri ya Muungano ilizaliwa bila uhalali wa kisheria kwa kuwa hayakuwapo makubaliano ya kila upande wa Muungano. Alisema Aprili 26, 1964 (Siku ya Muungano), Mwalimu Nyerere alitoa amri ya masharti ya mpito ya mwaka 1964 ambayo pamoja na mambo mengine iliifuta Tanganyika. Akichambua kitabu cha ‘50 Years of Independence: A Concise Political History of Tanzania’ (Miaka 50 ya Uhuru: Historia fupi ya Tanzania), kilichoandikwa na Msekwa na kuchapishwa Januari mwaka huu, Lissu alisema:
      “Msekwa anasema katika kitabu hicho kuwa amri hiyo ilichapishwa katika Gazeti la Serikali la siku hiyo. Kwanza, iliwabadilisha waliokuwa watumishi wa Serikali ya Jamhuri ya Tanganyika kuwa watumishi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano.” Alisema hata Mahakama Kuu ya Tanganyika iligeuzwa kuwa Mahakama Kuu ya Jamhuri ya Muungano na nembo ya Taifa ya Jamhuri ya Tanganyika iligeuzwa kuwa nembo ya Taifa ya Jamhuri ya Muungano. Alisema tarehe hiyohiyo, Mwalimu Nyerere alitoa amri ya Katiba ya muda ya mwaka 1964 na ilitangaza kuwa Katiba ya Tanganyika ndiyo iwe Katiba ya muda ya Jamhuri ya Muungano. “Kifungu cha nne cha amri hii ndicho kilichoipatia Serikali ya Muungano majukumu kuhusu mambo yote ya Muungano katika Jamhuri ya Muungano yote na vilevile kwa mambo yasiyokuwa ya Muungano kwa upande wa Tanganyika,” alisema Lissu huku akishangiliwa na baadhi ya wajumbe wa Bunge hilo.
         Alisema Juni 15, 1964, Mwalimu Nyerere alitoa amri nyingine iliyoitwa ‘Amri ya Masharti ya Mpito’ ambayo ilieleza kwamba mahali popote ambako sheria zilizokuwapo zimetaja jina la ‘Tanganyika’ basi jina hilo lifutwe na badala yake jina la ‘Jamhuri ya Muungano’ liwekwe. Huku akimnukuu Msekwa, Lissu alisema kigogo huyo wa CCM katika kitabu chake amesema, “Uhai wa Tanganyika ulitolewa kwa njia hiyo ya amri. Athari za jumla za amri hizi ni kwamba eneo la kisiasa ambalo ndiyo ilikuwa Tanganyika lilitolewa uhai wake moja kwa moja kwa amri. Hii ndiyo sababu hata jina la eneo la kijiografia lililojulikana zamani kama Tanganyika ilibidi libadilishwe na kuwa Tanzania Bara.” Hata hivyo, alipoulizwa kuhusu kauli hiyo ya Lissu aliyoitoa jana, Msekwa alisema: “Kitabu kipo na ukikisoma kwa umakini utagundua kuwa alichokisema Lissu siyo ambacho kimeandikwa. Sasa umhoji kuhusu hayo aliyoyasema, muulize ameyapata wapi?”
Kuhusu Shivji
      Akimnukuu Profesa Shivji katika kitabu chake ‘Pan Africanism or Pragmatism? Lessons of Tanganyika – Zanzibar Union’, Lissu alisema Profesa huyo ameeleza kuwa Muungano huo ulilazimishwa. “Profesa Shivji amethibitisha kwamba kile kinachoitwa Sheria ya Kuthibitisha Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ya mwaka 1964 iliandaliwa na kuandikwa na maofisa wa sheria wa Tanganyika wakiwa Tanganyika,” alisema. Alisema kuwa Profesa huyo ameeleza sababu ya ukweli wa kisiasa uliokuwapo wakati huo ambao Baraza la Mapinduzi kwa jumla wake halikukaa kuukubali Muungano. “Profesa Shivji alisema hakuna shaka kwamba Muungano ‘ulilazimishwa.’ Hivyo, maofisa wa kisheria wa kigeni wa Serikali ya Tanganyika (waliokuwa pia marafiki wa Nyerere) walitumia mbinu ya kisheria ya kuchapisha Sheria ya kuthibitisha Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, mwaka 1964,” alisema huku akikatishwa mara kwa mara na wajumbe waliokuwa wakiomba miongozo ya mwenyekiti.
        “Profesa ameeleza kuwa, kwa sababu utaratibu huo ulikiukwa, kitendo cha kuunganisha Jamhuri ya Watu wa Zanzibar na Jamhuri ya Tanganyika hakikupata baraka za Baraza la Mapinduzi na kuthibitishwa na kikao halali cha Baraza la Mawaziri la Zanzibar,” alisema Lissu na kuongeza: “Jamhuri ya Muungano ilizaliwa bila uhalali wowote wa kisheria kwa maneno ya Profesa Shivji.” Alisema hata aliyekuwa Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu wa Baraza la Mawaziri wa Serikali ya Jamhuri ya Watu wa Zanzibar, Salim Said Rashid kati ya Januari 18 na Juni 1964, alitamka kuwa: “Hakuwahi kupokea maagizo kutoka kwa Rais wa Zanzibar kwa ajili ya kuitisha kikao cha kujadili na kupitisha mkataba wa kuunganisha Jamhuri ya Watu wa Zanzibar na Jamhuri ya Tanganyika,” alisema Lissu. Alisema katika kitabu hicho, Profesa Shivji alieleza jinsi Rashid alivyoeleza utaratibu wa kisheria uliotakiwa kufuatwa: “... Kwa mujibu wa amri ya mwaka 1964; kila jambo lilitakiwa kujadiliwa na kikao cha Baraza la Mapinduzi na Mwanasheria Mkuu kuarifiwa atayarishe ‘presidential decree’ kwa mujibu wa utaratibu.”
     Alisema baadaye yeye (Rashid), akiwa Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Baraza la Mawaziri Zanzibar alitakiwa asaini na kisha Rais wa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar na baadaye kutolewa katika gazeti la Serikali. Alipotakiwa kutoa ufafanuzi wa kauli hiyo ya Lissu kuhusu kitabu chake, Profesa Shivji alijibu kwa ujumbe mfupi wa maneno akisema: “Itakuwa vizuri ukisoma wewe mwenyewe.”
Mbowe: Takwimu za Tume zimetengenezwa na vigogo wa Serikali
           Akichangia maoni ya walio wachache kutoka Kamati Namba Nane, Freeman Mbowe alisema kitendo cha wajumbe wanaotokana na CCM kubeza takwimu za Tume ya Jaji Joseph Warioba ni kuwakana Watumishi wa Serikali akisema ilikuwa na watumishi wa Serikali 190 wakiwamo wanasheria waandamizi. “Tunapohukumu Tume imefanya kazi chafu ya kuchakachua takwimu hizi, mjue zimetengenezwa na watumishi waandamizi kutoka Jamhuri ya Muungano na Serikali ya Zanzibar. Kwa hiyo wanaobeza taarifa ya Tume, wajue wanaikana Serikali, wanawakana watu ambao wana dhamana ya kusimamia nchi hii,” alisema na kuongeza: “Tunapata wapi ujasiri wa kuwadhalilisha wajumbe wa Tume ya Rais iliyoongozwa na Warioba?... Tume iliyojaa viongozi walioitumikia nchi hii kwa uaminifu mkubwa, tunafanyaje jambo hili?”
     Mbowe alisema Jaji Warioba aliwahi kushika nyadhifa mbalimbali za juu ikiwamo Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais na kuhoji wajumbe wanapataje ujasiri wa kuwadhalilisha. Aliwataja wajumbe wengine wa tume hiyo wanaoheshimika kuwa ni pamoja na Jaji Mkuu mstaafu, Agustino Ramadhan na Waziri Mkuu mstaafu, Dk Salim Ahmed Salim. Mbowe pia alishangaa kiwango cha fedha kilichotumiwa na tume hiyo Sh68.88 bilioni kufanya utafiti ambao leo wajumbe walio wengi kutoka CCM wanaukana. Alisema endapo wajumbe wanapuuza msingi wa Rasimu iliyotokana na Tume ya Jaji Warioba, ni vyema Bunge hilo lisiwepo ili CCM wakae upya na kutengeneza rasimu wanayoitaka ya serikali mbili. Alisema Tanzania haiwezi kupata Katiba Mpya kwa uongo na rushwa na kuzuia watu kujadili kasoro za muungano kwa uhalisia wake.
Jussa awabana mawaziri SMZ
          Akitoa ufafanuzi kuhusu maoni ya wajumbe walio wachache wa Kamati Namba Sita, Ismail Jussa aliwabana mawaziri watatu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), kwa kushindwa kueleza udhaifu wa muundo wa serikali mbili bungeni wakati kwenye semina ya Baraza la Wawakilishi kuhusu mchakato wa katiba walisema hivyo wazi. Alisema mawaziri hao walilalamikia jinsi wanavyodhalilishwa na muundo wa serikali mbili wanapokwenda nje ya nchi. “Kuna rekodi hata ya CD, siyo ya Hansard tu (kumbukumbu rasmi za Bunge), hata ukiitaka mheshimiwa mwenyekiti nitakupatia. Haya yalikuwa katika semina ya Baraza la Wawakilishi iliyoitishwa na Spika wetu, Mzee Pandu Ameir Kificho,” alisema. Aliwataja mawaziri hao kuwa ni Dk Mwinyi Haji Makame, Haroun Ally Seleman na Omary Yusuf Mzee. “Walichofanywa Dodoma sijui mheshimiwa mwenyekiti, lakini wote pamoja na wengine walionyesha jinsi mfumo huu (serikali mbili) hautusaidii Zanzibar na umetukwamisha,” alisema.
      Alitoa mfano mwingine kuwa kuna siku Zanzibar walikuwa wakijadili muswada wa utalii ambapo yeye alipendekeza waweke kipaumbele cha ajira kwa Wazanzibari kwa kuwa wizara hiyo si ya Muungano na kilikataliwa. “Mimi na Asha Bakari tu wa CCM tulitoka nje na akalalamika kuwa wenzake wamemgeuka. Kwa tabia hii mheshimiwa mwenyekiti tunapokuwa Zanzibar, tunasema wengine tunapokuja Dodoma tunaufyata, Wazanzibari watatuhukumu,” alisema. Awali akisoma maoni ya walio wengi, Mwenyekiti wa Kamati Namba Sita, Stephen Wassira alisema walio wengi walipendekeza muundo wa serikali mbili kwa sababu unatoa fursa kubwa ya kisiasa, kiuchumi na kijamii kwa pande zote mbili na kuondoa tabaka la ukabila na udini ndani ya Jamhuri. “Mfumo wa serikali mbili ukifanyiwa marekebisho ya kikatiba utaondoa kero na manung’uniko ambayo yameelezwa kuwa msingi wa mapendekezo ya Tume ya kutaka mfumo wa serikali tatu,” alisema.
Butahe F., & Mjema D. / Mwananchi

No comments: