Uchaguzi
wa mdogo wa Jimbo la Chalinze umefanyika huku ukigubikwa na kasoro kadhaa,
ikiwa ni pamoja na watu wachache kujitokeza vituoni kupiga kura, wapiga kura
kulalamika ‘kupokwa’ vitambulisho vyao, vituo kuwa majumbani kwa watu, huku pia
kukiwa na hofu ya vurugu.
Kasoro
hizo zilijidhihirisha jana wakati wapiga kura shughuli ya upigaji kura
ilipokuwa ikiendelea katika maeneo mbalimbali ya jimbo hilo ambapo wananchi wa
Chalinze walikuwa wakipiga kura mbunge wao, kuziba nafasi iliyoachwa wazi na
aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Said Bwanamdogo aliyefariki mapema mwaka
huu.
Gazeti hili liliweza kuzunguka katika vituo mbalimbali vya kupigia kura
ambapo lilishuhudia idadi ya watu wachache wakiwa wamejitokeza kutimiza haki na
wajibu wao wa kikatiba wa kuchagua kiongozi wanayemtaka.
Katika kituo cha
kupigia kura, Ofisi ya Maji Changa namba 2, hadi muda wa kufunga vituo ukiwa
umebakia nusu saa, walikuwa wamejitokeza wapiga kura 75 kati ya 328
walioandikishwa katika daftari la kudumu la wapiga kura.
Kituo hicho, kilikuwa
miongoni mwa vituo kadhaa vilivyokuwa majumbani mwa watu, kikiwa katika nyumba
ya Mzee Issa Mbogo, kinyume cha sheria ya uchaguzi.
Katika kituo cha
Tukamisasa hadi muda wa kufunga vituo ukiwa unakaribia mwisho, yalikuwa
yametukika madaftari mawili pekee, kati ya madaftari sita ambayo yalipaswa kuwa
kituoni hapo, ambapo kila daftari linajumuisha wapiga kura 50.
Mbali ya vituo
kama hivyo ambavyo viko maeneo ya vijijini, hata vituo vilivyokuwa kata za
mjini kama Builingu, pia hazikuwa na wapiga kura wengi.
Mathalani Kituo cha
Ofisi ya Mtendaji Namba 2; waliopiga kura walikuwa 64 kati ya wapiga kura 383,
Namba 3; waliopiga kura ni 62 kati ya 383.
Kata nyingine ya Pera ambayo pia
iko maeneo ya mjini, Kituo cha Shule ya Msingi Namba 1; waliopiga kura ni 88, kati
ya walioandikishwa 443, Kituo cha Pera Shule ya Msingi Namba 2; waliopiga kura
ni 100 kati ya wapiga kura 443.
Kituo cha Chamulungu Namba 1; waliopiga kura
100 kati ya 336, huku Chamulungu II wakipiga kura 88 kati ya 325.
Wapiga kura
kupokwa vitambulisho
Baadhi ya wapiga kura katika kata ya Ubena, walitoa
malalamiko yao wakimtuhumu Katibu wa CCM Tawi la Lulenge kwamba alifika
majumbani mwao wakati wanaume hawapo na kuchukua vitambulisho vya kupigia kura
akisema kuwa anakwenda kuandikisha namba zao.
Akizungumza kwa uchungu mmoja wa
wananchi hao aliyejitambulisha kwa jina la alisema kuwa kitendo hicho hicho si
sahihi na akazitaka mamlaka husika kuchukua hatua stahiki.
“Hapa unavyoniona
nimeshindwa kupiga kura hadi sasa…jina langu na namba yangu vipo kwenye daftari
kwenye kituo kile pale, lakini sina kitambulisho. Juzi natafuta kitambulisho
change, mke wangu ananiambia alikuja Rajab Said ambaye ni Katibu wa Tawi la CCM
Lulenge, eti alikwenda kuandikisha namba zetu.
“Hadi muda huu ninaokuambia,
hajarudisha vitambulisho kwa sababu siko peke yangu, kuna wengine kama 9 hivi
ninawafahamu nao pia vimechukuliwa,” alisema Simon Pojoro.
Kwa upande wake
Said akijibu tuhuma hizo, Said alisema kuwa madai hayo si kweli nay eye hajui
suala hilo wala hakuhusika kwa namna yoyote kwa wapiga kura kukosa haki yao ya
kuchagua mbunge wao, akisema huo ni uzushi.
Tuhuma za gari ya CCM ‘kumwinda’
mgombea wa CHADEMA
Wakati huo huo, akizungumzia mwenendo wa uchaguzi huo,
mgombea ubunge wa CHADEMA, Mathayo Torongey alisema kuwa gari aina ya Land
Cruiser ‘hard top’, T 630 BFJ, inayomilikiwa na CCM, ilikuwa ikimfuatilia kila
mahali alikokwenda wakati akipita maeneo mbalimbali kukagua vituo, kama sheria
inavyomruhusu.
“Tena bahati nzuri nimefika hapa kupita kwenye hiki kituo nimeikuta
hii gari, hii ndiyo imekuwa ikinifuatilia tangu asubuhi. Wamekuja pale Mdaula
akashuka kijana mmoja...yule pale…akiwa na sime na nondo, tulipomshtukia
akarudi ndani ya gari akabadili nguo akavua tisheti ya bluu aliyokuwa nayo
akavaa koti hilo la kijeshi kama mnavyomuona hapo,” alisema Torongey huku
akionesha gari na huyo mtu.
“Tunashukuru kuwa kulikuwa na polisi pale,
tuliwapatia taarifa naona wamechukua hatua, tumelikuta gari hili likiwa liko
hapa na hawa askari, lakini nashangaa hawajapelekwa kituoni na unawasikia
wanavyozungumza kwa jeuri mbele ya polisi,” aliongeza.
Mbele ya waandishi wa
habari, gari ile iliyokuwa na watu wengi ndani, huku kuionekana silaha
mbalimbali na bendera ya CCM, iliruhusiwa kuondoka maeneo hayo, ikiamriwa
ielekee kituoni (bila kusindikizwa na polisi), ambapo kiongozi mmoja, ambaye ni
katibu wa chama hicho wilaya moja ya Iringa, akijigamba kwa kusema ‘tutakwenda
kituoni baada ya kumaliza kazi zetu.
”
Matokeo ya awali
Kata ya Pera;
Malivundo Ofisi ya Mtendaji; CCM 77, CHADEMA 2, CUF , AFP 1, NRA 1.
Kimbugi;
CCM 11, CHADEMA 1, CUF 0, AFP 0, NRA 0
Magange Ofisi ya Kitongoji; CCM 101,
CHADEMA 1, NRA 0, AFP 0
Pingo Shule ya Msingi Namba 1; CCM 31, CHADEMA 1, CUF
1, NRA 0, AFP 0
Pingo Ofisi ya Kitongoji Namba 2; CCM 61, CHADEMA 4, CUF
2, AFP 1, NRA 0
Pingo Namba 1; CCM 66, CHADEMA 0, NRA 0, AFP 0
Kurugenzi ya
Habari CHADEMA
No comments:
Post a Comment