Siku moja baada ya Rais Jakaya Kikwete kuzindua Bunge na kuponda ripoti ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Mwenyekiti wa Tume hiyo Jaji Joseph Warioba amesema jukumu walilopewa kwa mujibu wa sheria wamelikamilisha na wanawaachia wananchi waamue. Akizungumza na Mwananchi jana asubuhi, Jaji Warioba alisema alichokizungumza Rais Kikwete ni maoni yake na kwamba hawezi kuyajadili. “Rais Kikwete alichozungumza ni maoni yake, kwa sasa sipendi kuyazungumzia hayo, ” Jaji Warioba alieleza. Alisema wamemaliza jukumu walilopewa na kwamba sasa jukumu lote lipo mikononi mwa Bunge. Jaji Warioba alisema Tume yake ilikusanya maoni kutoka kwa wananchi, mabaraza ya wilaya ya Katiba na Taasisi mbalimbali, wakatengeneza rasimu ambayo sasa wameikabidhi kwa Bunge Maalumu la Katiba.
Jaji Warioba pia alikataa kuzungumzia zogo lililoibuka bungeni na kusababisha rasimu kuwasilishwa Jumatano, baada ya kikao cha Jumanne kuvunjika. Hali hiyo ilitokana na UKAWA kudai muda wa saa 1:30 uliokuwa umepangwa Jaji Warioba ahutubie bungeni uongezwe na kanuni inayoelekeza Rais Jakaya Kikwete ahutubie kabla Jaji Warioba hajawasilisha rasimu izingatiwe, baada ya kutangazwa kuwa Rais angehutubia baada ya rasimu kuwasilishwa.
Profesa Baregu
Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Profesa Mwesiga Baregu alisema alitarajia Rais Kikwete angezindua Bunge Maalumu na siyo kutoa maagizo na vitisho kwa wajumbe. Alisema hajui lengo la Rais kufanya alichofanya lakini ana hakika kwa kutoa ufafanuzi wa hoja zilizotokana na maoni ya wananchi ndani ya rasimu, ameingilia kazi za Tume na hivyo amevunja Sheria ya Mabadiliko ya Katiba (Sura ya 83 toleo la mwaka 2012), inayosema:
“21.-(b) atakayejifanya kuwa mjumbe wa Tume au Sekretarieti; au (c) atakayeendesha programu ya elimu juu ya mabadiliko ya katiba kinyume na masharti ya sheria hii, atakuwa ametenda kosa.
(3) atakayetiwa hatiani kwa kutenda kosa kinyume na Sheria hii, atawajibika kulipa faini isiyopungua Sh2,000,000 (milioni mbili) na isiyozidi Sh5,000,000 (milioni tano) au kifungo kwa muda usiopungua mwaka mmoja na usiozidi miaka mitatu au adhabu zote mbili.
Sheria hiyo inaendelea kuelekeza, (4) Hatua zozote zilizochukuliwa chini ya kifungu hiki hazitachukuliwa kuwa zimefikia ukomo na zitaendelea kuwa na nguvu ya kisheria hata baada ya Sheria hii kukoma kutumika.” Profesa Baregu alisema sheria imezungumzia mtu yeyote, hajui kwa Rais inakuwaje.
“Sijui ameona Bunge halitoshi, haliwezi kung’amua mambo au limepungukiwa kiasi cha kushindwa kumudu majukumu yake? Sielewi ila amevunja sheria na amelivunjia Bunge hadhi yake kiasi kwamba hata kazi yake inaweza isiaminike,” alieleza.
Profesa Baregu alisema Rais Kikwete amejipa jukumu la kujibu na kujadili hoja za rasimu na hivyo kuwa sehemu ya Bunge Maalumu. Alisema wakati wabunge wanahimizwa kutumia mfumo wa maafikiano katika kuamua mambo, Rais amewajengea msingi wa mgawanyiko na chuki, hali itakayoathiri mpango wa kulipatia taifa Katiba inayotokana na wananchi. Profesa Baregu alitaja baadhi ya kauli za Rais Kikwete ambazo zinaweza kuathiri mchakato kuwa ni kujirudia kwa kauli; “Nyie ndiyo mnaotunga Katiba (Wabunge wa Bunge Maalumu) kazi imebaki kwenu.” na maelekezo kwamba serikali tatu zitapatikana, lakini labda baada ya yeye (Rais Kikwete) kuondoka madarakani.
Jaji Ramadhan
Jaji Ramadhani alisema wao Tume wamemaliza kazi yao na kwamba sasa wanawaachia wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba na wananchi waamue. “Tumemaliza kazi yetu na sasa tunawaachia wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba na wananchi,” alisema. Hata hivyo, alisema ikitokea wajumbe wa Bunge hilo wakihitaji ufafanuzi wa jambo lolote, yeye binafsi anaahidi kutoa ushirikiano. Kuhusu hotuba ya Rais Kikwete bungeni juzi, alisema yeye alikuwa Arusha akishughulika na vikao vya Mahakama ya Kimataifa ya Haki za Binadamu na kwamba hakuwa amepata muda wa kuipitia na kuitafakari kwa kiwango cha kuizungumzia. “Ninasoma na kuitazama kupitia vyombo vya habari na ninafahamu nyie wanahabari huwa mnalenga pale palipowakuna. Hivyo nikitulia na kupata hotuba halisi aliyotoa nikaitafakari; nitaizungumzia,” alieleza.
Rais Kikwete akizindua Bunge juzi mjini Dodoma, alisema rasimu ya pili iliyowasilishwa bungeni na Jaji Warioba ina makosa mengi ya kiuandishi. Alisema ina mambo mengi, baadhi yalitakiwa kuwekwa kwenye Sheria. “Mbolea, mbegu, pembejeo vyote vimewekwa humo, hata umri na haki ya mtoto kupewa jina vinawekwa humo, yakiwekwa yote kama yalivyo, serikali haitaweza kuyatekeleza itashtakiwa mahakamani kila wakati,” alieleza. Rais Kikwete aliwataka wajumbe wa Bunge Maalumu kusoma neno kwa neno, mstari kwa mstari na kujiridhisha na mambo watakayoidhinisha yaingie kwenye Katiba itakayopendekezwa. Alisema watakachoona kinafaa kurekebishwa, kuboreshwa au kufutwa wasisite kufanya hivyo kwa sababu inatakiwa Katiba bora, inayotekelezeka na ambayo haitalalamikiwa kiasi cha kulazimika kuibadilisha muda mfupi baada ya kupitishwa.
Huku akishangiliwa na baadhi ya wajumbe, alisema wakichagua Serikali tatu watatakiwa kuondoa mambo yote yanayoweza kukanganya utendaji wa Serikali za washirika na ile ya Muungano. Lakini wakichagua Serikali mbili, mengi yatatekelezeka. Rais Kikwete alisema serikali zote mbili zimeamua kwa dhati kutumia fursa ya mchakato wa mabadiliko ya Katiba kutatua mambo matatu kati ya sita ambayo bado hayajatatuliwa kutoka kwenye orodha ya kero 31 za Muungano zilizoainishwa na Zanzibar.
Majura E., / Mwananchi
No comments:
Post a Comment