MWENYEKITI wa Tume ya
Mabadiliko ya Katiba, Jaji mstaafu Joseph Warioba, ametaja mambo manne
yaliyoishawishi Tume yake kupendekeza Muungano wa serikali tatu. Mambo hayo ni
Tanganyika kuvaa koti la Muungano, kuongezeka kwa mambo ya Muungano, mgongano
wa Katiba, michango na gharama za Muungano na mgao wa mapato ambayo alisema
yanahatarisha Muungano wa sasa wa serikali mbili. Jaji Warioba alisema
Zanzibar inalalamika kwamba Tanganyika imejificha kwenye koti la Muungano na
ndiyo inayofaidi na Wazanzibari wanaiita ni Serikali ya Tanzania Bara na sio ya
Muungano. Alisema orodha ya mambo ya
Muungano ni suala ambalo limelalamikiwa kwa muda mrefu na hatua zilizochukuliwa
ni kupunguza mambo ya Muungano.
Katika eneo hilo, alisema
suala la uhusiano wa kifedha pia limekuwa na utata kwa muda wa takribani miaka
40 na kiini chake ni malalamiko ya kutoka kila upande kuhusu nani anafaidi
rasilimali za Taifa. “Kwa tathmini ya Tume,
muundo wa serikali mbili hauwezi kubaki kwa hali ya sasa, Muungano wa Serikali
mbili waliotuachia waasisi siyo uliopo sasa,” alisema Warioba na kueleza kuwa
umebadilishwa mara nyingi wakati mwingine bila kufanya mabadiliko ya Katiba.
Muungano wa waasisi Alisema waasisi walituachia Muungano wa nchi moja yenye
serikali mbili na siyo nchi mbili zenye serikali mbili;
“Muundo wa serikali mbili,
unaweza kubaki tu kama orodha ya mambo ya Muungano haitapunguzwa, bali
itaongezwa. “La sivyo (kama mambo ya Muungano yatapunguzwa), Serikali ya
Muungano itabaki na rasilimali na mambo ya Tanzania Bara tu, katika hali ya
namna hiyo pande zote mbili zitaendelea kulalamika. Zanzibar kwa upande wake,
imekuwa ikidai kwamba fedha na rasilimali za Muungano zinatumika na kuinufaisha
Tanzania Bara chini ya kivuli cha Muungano. Aidha, kwa upande wa
Serikali ya Muungano, inadaiwa kwamba Tanzania Bara ndiyo inayochangia fedha na
rasilimali nyingi katika Muungano hivyo inayo haki ya kutumia fedha na
rasilimali hizo kwani Zanzibar kwa muda mrefu, imekuwa haichangii katika fedha
na rasilimali hizo za Muungano.
Jaji Warioba alisema kwa
kipindi cha miaka 30 kumekuwepo na hoja za muundo wa serikali tatu kama
kuchafuka kwa hali ya kisiasa Zanzibar chanzo chake ilikuwa serikali tatu, Tume
ya Jaji Nyalali, Kundi la G 55 ilikuwa ni kuundwa kwa serikali Tanganyika,
Kamati ya Jaji Kisanga ilipendekeza serikali tatu na pia Tume yake imepata
maoni ya wananchi kuwa wanataka serikali tatu. Jaji Warioba alisema
matendo ya Serikali katika kipindi cha miaka 30 na hatua zinazochukuliwa,
zimefanya mamlaka na madaraka ya Muungano yapungue na madaraka ya SMZ
yameongezeka na Serikali ya Muungano imebaki ikishughulikia mambo ya Tanzania
Bara tu kwa upande wa maendeleo.
“Jambo kubwa zaidi katika
kuchukua hatua hizi, ni kuvunjwa kwa Katiba, hili sio jambo dogo, kama Katiba
haitaheshimiwa nchi haitakuwa salama, mapendekezo ya Tume yanalenga kuondoa
matatizo yanayohatarisha kuyumba kwa Muungano ili kuzuia pande zote mbili
kuendelea kuchukua hatua zinazovunja Katiba,” alisema Warioba. Kuongezeka Akichangua mambo
hayo, Jaji Warioba alisema kuongezeka kwa mambo ya Muungano Wazanzibari wanadai
kuwa kunapunguza mamlaka ya Zanzibar. Alisema Tume ilifanya uchambuzi wa mambo
ya Muungano ili kubaini kama yanaingilia hadhi na mamlaka ya Zanzibar.
Alisema kati ya mambo 22,
Tume imebaini kuwa siyo mambo yote yanayotekelezwa kikamilifu na kimuungano na
alisema mambo mengi yamebadilishwa bila ya kubadili Katiba ama kwa makubaliano
kati ya pande zote mbili za Muungano au kwa hatua zilizochukuliwa na upande
mmoja. Jaji Warioba alisema katika
kipindi chote cha miaka 20 iliyopita, kamati nyingi zimeundwa kushughulikia
matatizo ya Muungano na baadhi yake zilipendekeza kuondoa mambo mengi zaidi
kutoka kwenye orodha ya mambo ya Muungano na akatoa mfano wa Tume ya Amina
Salum Ali ya Zanzibar, iliyopendekeza kuondolewa mambo 12.
Alisema mwaka 2003 Serikali
ya Mapinduzi Zanzibar, iliunda kamati nyingine kuchambua matatizo na kero za
Muungano na taratibu za kuziondoa na kamati hiyo ilipendekeza mambo 14 ambayo
yanatakiwa kuondolewa kwenye Muungano ikiwemo Polisi na mambo ya usalama.
Warioba alisema kuwa mambo hayo yakiondolewa kwenye orodha ya mambo ya
Muungano, serikali ya Muungano itakuwa imebaki na mambo ya Tanzania bara tu kwa
upande wa maendeleo. Alisema Tume ilitafakari
kama kuna uwezekano wa kuyarudisha mambo yaliyoondolewa kwenye orodha kutokana
na muafaka wa 1994, lakini tathmini ya Tume ni kwamba kufanya hivyo ni kuzua
mgogoro upya kwani itaonekana mamlaka ya Zanzibar yanaingiliwa.
Alisema wakati Tume ilipokuwa
inakusanya maoni ya wananchi wengi wa Zanzibar, wote walipendekeza mambo mengi
yaondolewe kwenye Muungano. Alitoa mfano kuwa wale
waliotaka serikali ya mkataba, walitaka mambo yote yaondolewe kwenye orodha ya
Muungano, isipokuwa suala la ulinzi na wale waliotaka serikali mbili walitaka
mambo yote ya uchumi yaondolewe kwenye orodha ya Muungano. Jaji Warioba alisema
kuyarudisha mambo ambayo hivi sasa yako chini ya Serikali ya Mapinduzi
Zanzibar, hata kama sio ya kikatiba kunaweza kuleta mgogoro wa kisiasa. Mgongano wa Katiba Jaji
Warioba alisema ibara ya 132 ya Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 imeweka
masharti kwamba sheria zinazotungwa na Bunge la Muungano hazitatumika Zanzibar
hadi zipelekwe kwenye Baraza la Wawakilishi.
Alisema jambo hilo limeleta
mgongano mkubwa kwani katika muafaka wa 1994, serikali zote zilikubaliana
kwamba Zanzibar ifanye mabadiliko kwenye Katiba yake ili mgongano huo wa Katiba
uondolewe. “Lakini hadi sasa muafaka
haujatekelezwa,” alisema Warioba na kuongeza kuwa zaidi ya hapo mabadiliko ya
Katiba ya Zanzibar ya mwaka 2010, yametamka wazi kwamba Zanzibar ni nchi kati
ya nchi mbili zinazounda Muungano wakati Katiba ya Muungano inaelekeza kwamba
Tanzania ni nchi moja. Alisema mabadiliko katika
Katiba ya Zanzibar pia yamehamisha baadhi ya madaraka ya Serikali ya Muungano
kwenda Zanzibar na akatoa mfano Katiba ya Jamhuri ya Muungano, inampa Rais wa
Jamhuri ya Muungano mamlaka ya kuigawa nchi katika maeneo, lakini Katiba ya
Zanzibar imeyahamisha madaraka hayo na kwenda kwa Rais wa Zanzibar.
Jaji Warioba alisema Tume
ilibaini kwamba haitakuwa rahisi kubadili Katiba ya Zanzibar kuifanya Zanzibar
kuonekana kuwa sehemu ya Muungano badala ya kuwa sura ya nchi. Alisisitiza kuwa
mabadiliko ya aina hiyo yanahitaji kura ya maoni kama Katiba ya Zanzibar
inavyoelekeza. “Kwa tathmini ya Tume,
baada ya kuwasikiliza wananchi wa Zanzibar ni dhahiri kwamba uwezekano wa
kufanya mabadiliko kwenye Katiba ya Zanzibar ili Zanzibar iwe sehemu ya nchi
moja badala ya kuwa nchi ni mdogo. Michango, mapato Jaji
Warioba alisema matumizi ya fedha za Muungano, michango ya pande zote mbili kwa
shughuli za Muungano na mgawo wa mapato ya Muungano, yamekuwa ni masuala yenye
utata kwa muda mrefu.
Alisema mwaka 1977 NEC ya
CCM ilitoa uamuzi kwamba mapato ya kodi za Muungano yabaki upande wa Muungano
yanapokusanywa lakini tatizo hilo halikumaliza matatizo. Alisema Zanzibar imekuwa
ikidai kwamba fedha na rasilimali za Muungano zinatumika na kuinufaisha
Tanzania Bara chini ya kivuli cha Muungano. Pia alisema kwa upande wa Serikali ya
Muungano inadaiwa kwamba Tanzania Bara ndiyo inayochangia fedha na rasilimali
nyingi katika Muungano. Kwa sababu hiyo Wabara
wanadai kuwa wanayo haki ya kutumia fedha na rasilimali hizo kwani Zanzibar kwa
muda mrefu imekuwa haichangii katika fedha za rasilimali hizo za Muungano.
“Kutokana na matatizo haya,
chombo maalum cha kikatiba yaani Tume ya Fedha kilianzishwa ili kushughulikia
masuala ya uhusiano wa kifedha baina ya Serikali ya Muungano na SMZ. Baada ya wajumbe wa Tume
hiyo kuundwa mwaka 2003 ikiwa ni baada ya miaka saba tangu kutungwa sheria ya
kuanzishwa kwake, Tume hiyo ilipendekeza kiwango cha uchangiaji gharama za
Muungano na kiwango cha mgawo na utaratibu wa mgawanyo wa mapato ya Muungano
baina ya serikali hizo. Warioba alisema tume hiyo
ilipendekeza kwamba masharti ya Katiba yatekelezwe kuanzishwa kwa akaunti ya
fedha ya pamoja ambapo fedha yote inayohusu gharama za Muungano itawekwa. “Hadi
sasa huu ni mwaka wa nane tokea mapendekezo hayo hakuna hata kati ya
mapendekezo hayo lililotekelezwa au kuchukuliwa hatua,” alisema Jaji Warioba.
Jaji Warioba alisema
tathmini ya Tume ni kwamba siyo rahisi mambo hayo kutekelezwa chini ya muundo
wa serikali mbili hiyo ni kwa sababu wizara za Serikali ya Muungano ni
mchanganyiko. Alisema zipo wizara ambazo zinashughulikia
mambo ya Muungnao tu na zipo zinazoshughulikia mambo ya Bara peke yake na zipo
zingine zinashughulikia mambo mchanganyiko
HABARI LEO
No comments:
Post a Comment