Mjadala……. Haki Ya
Kuzaliwa Ya Watanzania Ughaibuni
John Mashaka |
Taifa letu likiwa katika mpito na wakati mgumu
wa kuandika rasimu ya katiba mpya ya watanzania, hatuna budi kuweka kando
itikadi zetu za kisiasa, tofauti za kiimani na hata maslahi binafsi ili
tuungane katika kutafuta katiba itakayokidhi mahitaji yetu ya sasa na ya vizazi
vijavyo.
Katika mchakato huu, inatubidi tuwe makini na
wakweli katika kujadili hatma na haki ya kuzaliwa ya ndugu zetu ambao wanaishi
ughaibuni. Lazima tuwajumuishe na kuwapa haki zao za msingi; haki ya kuzaliwa
katika ardhi ya Tanzania ambayo ni
zawadi kutoka kwa mwenyezi Mungu. Hii ni haki ambayo kamwe haiwezi kubatilishwa
na mamlaka ya aina yeyote wala haiwezi kutenguliwa na binadamu yoyote. Ni
kujidanganya kudai kwamba waliochukua uraia wa kigeni warudi Tanzania kama
wageni.
Kwa makusudi kabisa, nimeamua kuchokonoa huu
mjadala wa haki ya kuzaliwa nikiwa na sababu nyingi za manufaa kwa taifa letu;
ya msingi ikiwa ni sababu ya kiuchumi na hatma ya taifa letu. Jamii ya
watanzania wanaoishi ughaibuni ni hazina adimu ya rasilimali watu wanaohitajika
katika maendeleo ya kiuchumi, kisiasa na kijamii ya Tanzania.
Ni kundi lenye uwezo mkubwa wa kiuchumi ambao
lazima tuwakumbatie. Mheshimiwa Rais Jakaya kikwete, Waziri Mkuu Mizengo Pinda,
Waheshimiwa Dr. Wilibrod Slaa, Freeman Mbowe, Bernard Membe, wote, kwa kipindi
kirefu wameunga mkono haki ya kuzaliwa ya watanzania wanaoishi ughaibuni kupata
haki zao za msingi za kurudi katika ardhi yao ya kuzaliwa bila masharti wala
vikwazo vya aina yoyote.
Bila shaka wapo wanasiasa wenye ajenda zao
binafsi ambao wamekuwa kikwazo kikubwa katika kuwazuia wazawa wa Tanzania wanaoishi
ughaibuni kupata haki sawa katika katiba mpya. Siwezi kuwalaumu, kwani pengine
wengi hawana uelewa wa faida ambazo zitapatikana kwa kuwapa ndugu zetu
waliozaliwa Tanzania haki ya kushiriki katika ujenzi wa taifa.
Mjadala huu tuaouanzisha lazima uweke katika mizani
faida na athari za kuwapa watanzania haki yao ya kuzaliwa na hatimaye kupata
uwiano ambao utakidhi na kujibu maswali mazito ambayo ndio chanzo cha vikwazo
vilivyopo kwa sasa.
Wiki chache zilizopita, Blogger-mwanasiasa
mmoja nchini Tanzania alitoa shutuma dhidi ya watanzania wajulikanao kama wana
Diasapora wanaodai haki zao za kuzaliwa katika ardhi ya Tanzania, huku akisahau
kwamba yeye mwenyewe alikuwa mwana Diaspora kwa miaka takribani thelathini. Hata
kama alikuwa na uraia wa nchi thelathini, mwisho wa siku alirudi katika ardhi
aliyozaliwa yaani, Tanzania. Nina imani kwamba anao wanafamilia ughaibuni ambao
ndoto yao kubwa ni kutambulika kama watanzania wenye haki zote ambazo kila
mzawa anazo.
Katika tafsiri isiyo rasmi ni kwamba amewatosa
ndugu zake. Warudi Tanzania wasirudi siyo tatizo kwake. Tofauti na mategemeo ya
wengi, huyu blogger alitegemewa kuwa mstari wa mbele kuhamasisha na kutetea
haki za kuzaliwa za watanzania wanaoishi ughaibuni.
Huyu blogger ndio picha kamili ya wanasiasa
ambao mara nyingi hutafuta nafasi za kupiga picha na wanadiaspora pindi
wanapotembea nchi nyingine ambako kuna watanzania. Wanasiasa hawahawa watakuwa
mstari wa mbele kujipanga uwanja wa ndege kuonyesha huzuni na huruma na hata
kumwaga machozi ya kinafiki pale majeneza ya wana Diaspora yanaporudishwa
katika ardhi yao ya kuzaliwa huku wakiwanyima haki zao za kuzaliwa wanapokuwa hai.
Wengi wa watanzania waliomba uraia wa nchi nyingine
siyo kwamba hawalipendi taifa lao,la hasha! Wengi ni wazalendo waliolazimika
kuchukua uraia wa nchi nyingine ili kupata ahueni kutokana na ugumu wa maisha unaowakabili
mamilioni ya watanzania. Wengine walitafuta vibali vya kuishi ili wapate elimu
ambayo Tanzania isingeweza kuwalipia.
Badala ya kutafuta chimbuko la tatizo au wazo fulani,
ni desturi yetu kama jamii kwa mjumbe kusulubiwa na hata kuuwawa ili kuliua
wazo au jambo linalotishia maslahi ya wachache. Kumshambulia John Mashaka
mathalani, hakutaweza kamwe kuliua swala ambalo wakati wake umewadia. Binafsi
nimeamua kubaki na uraia wangu wa kitanzania licha ya kuwa na nafasi ya
kuchukua uraia wa nchi nyingine. Kubwa ya yote, ninajikita kuanzisha huu
mjadala ili kuitetea Tanzania na rasilimali zake hasa rasilimali watu.
Kama taifa, tunawahitaji ndugu zetu wenye taaluma
mbali mbali waliotapakaa kote duniani na hata kufikia hatua ya kuchukua uraia
wa nchi nyingine. Napigania watanzania milioni 45 nikizingatia faida za
kiuchumi, kisiasa, kijamii ambazo zinapatikana na rasilimali watu wenye asili
ya kitanzania. Wazawa wanaopigania haki zao za kuzaliwa pamoja na vizazi vyao.
Ni muhimu hawa wanasiasa wakakumbushwa kuhusiana
na maamuzi yao ya kuwatenga watanzania walio nje ya nchi, hususan kuwanyima
haki zao za kuzaliwa. Inabidi wakumbushwe kwamba, wazaliwa wa Tanzania
wanaoishi ughaibuni wana ndugu zao Tanzania, ambao ndio wapiga kura wao. Na
ikiwa wanaamua kwa makusudi kuwatenga, basi kundi hili maarufu kama Diaspora
watumie uwezo wao, ushawishi wao na mbinu zote walizo nazo kuwaadhibu wanasiasa
wanaozuia haki zao za kuzaliwa.
Pengine niwakumbushie viongozi wa jumuiya za
watanzania popote walipo duniani kwamba haki haiombwi. Haki inadaiwa, na
asiyeweza kudai haki yake na hata kuiona haki yake kama zawadi au upendeleo
fulani basi huyo amepoteza haki yake ya kuishi.
Viongozi wa jumuiya za watanzania ughaibuni
hawana budi kuonyesha uwezo wao wa kuongoza kwa kuwa mstari wa mbele
wakiwahamasisha watanzania waliotapakaa duniani kudai haki zao za kuzaliwa. Inabidi
wapaze sauti zaidi ili viongozi wetu walioweka pamba masikioni wasikie madai
yao. Mashabiki wa CCM ,CUF, CHADEMA na wengineo wote wataathirika sawa. Kwa maana
hiyo, vita hivi havina mipaka, ni vita vya watanzania wa matabaka yote. Wana diaspora
lazima wawe na mshikamano kama watanzania.
Mungu Ibariki
Tanzania
John Mashaka
1 comment:
Mashaka john ni jinias
Post a Comment