UVCCM sasa yataka atimuliwe
HOFU ya
harakati za Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa, kuwania urais katika uchaguzi
mkuu utakaofanyika mwakani imezidi kukitesa Chama Cha Mapinduzi (CCM), safari
hii Umoja wa Vijana wa chama hicho (UVCCM), ukitaka atimuliwe. Jana UVCCM
imemtaka Makamu Mwenyekiti wa CCM (Bara), Philip Mangula, kuwang’oa watu
wanaotangaza kuwania uongozi kabla ya wakati, na wanaomwaga fedha kwa wajumbe
wa mkutano mkuu ili kuwashawishi wawaunge mkono katika nia zao. Tamko hilo
la UVCCM linakazia kauli iliyotolewa wiki iliyopita na Mangula, kuwa CCM
itawaadhibu makada wake wanaotangaza au kufanya kampeni za urais kabla ya
wakati uliowekwa na chama hicho. Wakati
chama hicho kikionekana kutikiswa na ushawishi wa Lowassa, mbunge huyo anadaiwa
kuendelea kujiimarisha katika kile alichokiita safari ya kuwapatia Watanzania
elimu bure kwa kukutana na wafanyabiashara wa mkoani Arusha.
Tanzania
Daima Jumapili, limedokezwa kuwa Januari 2, mwaka huu, Lowassa aliendelea na
harakati zake za kujipanga kugombea urais 2015 kwa kuwaandalia chakula cha
mchana marafiki zake zaidi ya 100. Hafla hiyo
ilifanyika majira ya saa saba mchana kwenye eneo la Papa King lililopo karibu
na hoteli ya Lush Garden ambalo hutumika kwa michezo ya watoto. Kwenye
hafla hiyo, Lowassa hakutoa hotuba, badala yake alikuwa anapita kwenye meza za
wageni wake na kuwashukuru kwa kuhudhuria ibada yake ya shukurani aliyoifanya
siku ya mwaka mpya. Kwa mujibu
wa mmoja wa watu walioshiriki kwenye hafla hiyo, mbunge huyo alikuwa akiwaomba
wasisite kuitikia wito wake wa kukutana nao Juni 1, mwaka huu. Alibainisha
kuwa mkutano huo wa Juni 1 utawakutanisha marafiki, wanasiasa na
wafanyabiashara mbalimbali, na watachangisha fedha za kutekeleza mikakati yake
ya kuifikia safari aliyoianza mwaka huu. Katika kikao
kilichofanyika Januari 2, mwaka huu, kada wa CCM aliyekuwa mbunge katika Mkoa
wa Mwanza mwaka 2005-2010, alikabidhiwa jukumu la kuratibu posho na fedha za
kujikimu kwa baadhi ya watu waliohudhuria.
UVCCM
wataka atimuliwe
Akizungumza
na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Katibu Idara ya Uhamasishaji
na Chipukizi Taifa, Paul Makonda, alisema Kamati ya Maadili inayoongozwa na
Mangula, inapaswa itafasiri hasira ya wanaCCM kwa vitendo. Makonda
alisema UVCCM wameamua kuwa wakali kwa watu wasiofuata kanuni na ilani ya chama
chao, ambacho kinaweza kuanguka kama kisipowadhibiti. Ingawa
katika mkutano wa jana Makonda hakutaja majina ya makada wa CCM wanaodaiwa
kukiuka kanuni kwa kutangaza nia mapema, lakini anaonekana kumlenga Lowassa. Licha ya
kuonekana kumlenga Lowassa, si Mangula wala Makonda waliokuwa na ubavu wa
kutaja hadharani jina la mbunge huyo aliyetangaza safari ya kuwaletea
Watanzania elimu bure na huduma bora za kijamii.
Lowassa
katika hotuba yake ya kufunga mwaka 2013 na kuukaribisha mwaka mpya 2014
nyumbani kwake Monduli, alikaririwa akisema ameanza rasmi safari aliyoiita ya
matumani ya ndoto zake, ambayo pia itatimiza ndoto za Watanzania za kupata
elimu bure, maji safi na maendeleo ya uhakika. Mbunge huyo
ambaye amekuwa akitajwa kuwa mmoja wa wagombea wa nafasi ya urais kupitia CCM
katika uchaguzi mkuu wa 2015, aliyasema hayo katika ibada ya shukrani ya
kuupokea mwaka mpya, katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT),
Usharika wa Monduli. Katika hafla
hiyo, Lowassa anadaiwa kuwasafirisha baadhi ya wajumbe wa vikao muhimu vya
uamuzi vya chama na kuwapa fedha, malazi na kadi za Krismasi ambazo zinadaiwa
kuambatanishwa na fedha.
Kauli ya
UVCCM, kumuonya Lowassa na wengine wanaodaiwa kuvunja kanuni, inafanana na ile
ya Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye na ya Mangula, ambaye alikaririwa
hivi karibuni kuelezea kuundwa kwa timu ya kuwachunguza makada wake wanaodaiwa
kutangaza nia ya kuwania uongozi kabla ya wakati. Kwa upande
wa Nape, yeye alikaririwa akidai kuwa Lowassa amevunja kanuni, hivyo kupoteza
sifa ya kugombea nafasi za uongozi ndani na nje ya CCM. Makonda
alisema kuwa vijana wa CCM hawatakubali kuona mshikamano unavunjika kwa sababu
ya watu wanaogawa fedha na kuahidi kutoa elimu bora. “Watu wanatangaza
kutoa elimu bora kwanini wasifanye hayo kupitia chama, kinachofanywa sasa ni
mwelekeo wa kubomoa mshikamano ndani ya CCM, kudhoofisha na hatimaye kutuengua
katika uongozi wa nchi,” alisema.
Makonda
alisema watu hao ni wasaliti wasio na woga wala aibu kwa kujiaminisha kuwa
wanagombea urais, ubunge, udiwani na nafasi nyingine za kupigiwa kura baada ya
kuanza kampeni za kishindo za rushwa na vishawishi mbalimbali nje ya utaratibu,
kanuni na maadili ya CCM. “Hali hii
inatishia kabisa kutoweka kwa mshikamano ndani ya chama, na inasababisha
makundi yanayoundwa na wagombea hawa wasio rasmi yanayopita nchi nzima
kushawishi kwa fedha na rushwa nyingine kwa makundi ya kijamii, ya
kijasiriamali ili kuungwa mkono. “Watu hawa
wameweka pembeni ilani ya CCM ya 2010 na kutumia ilani zao binafsi za kumwaga
pesa nchi nzima, kusambaza elimu kama njugu bila kuelezea vyanzo vya mapato vya
serikali zao za kusadikika,” alisema.
Alisema
kuwa CCM ina taratibu za kupata uongozi, hivyo kufanya kinyume ni uasi,
upungufu wa busara na ukosefu wa sifa ya uongozi hali inayozidi kukitia doa
chama. “Dhamira ya
CCM ni kutuunganisha wote kuwa kitu kimoja, dalili zozote nje ya tunu hizo ni
usaliti, hauna budi kupigwa vita kwa nguvu zote, hasa sisi vijana, na
tusiangalie nyani usoni kwani hakuna mtu yeyote aliye juu au mkubwa kuliko
chama, hivyo bandu bandu hii iliyoanza tusiivumilie itatuweka pabaya,” alisema
Makonda. Alisema kuwa asiyetaka
kufuata maadili, miiko na kanuni za CCM ni ruksa kuondoka.
Source: Mnale H. (Jan. 2014). Lowassa aiumiza CCM. Retrieved from Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment