Taarifa ambazo zimetufikia kupitia kituo cha WAPO Radio
FM zinaeleza kwamba kuna bomu limelipuliwa kwenye kanisa katoliki la Mtakatifu
Karoli, Ruanga huko USA River jijini Arusha, ambapo wanakwaya takriban 6 wamejeruhiwa.
Kwa mujibu wa taarifa hizo ambazo zimetufikia, zinaeleza
kwamba watuhumiwa ni jeshi la Polisi, na kwamba walirusha kitu kinachosadikiwa
kuwa bomu - lililojeruhi 6, ambapo 4 kati yao wameruhusiwa baada ya matibabu
kwenye hospitali ya Mission na ya Wilaya ya Arumeru.
Majira ya saa sita na nusu, waumini walidai kuona gari
la polisi likipita kwa kasi, na lilipowakaribia walistuka mlipuko ukiwarusha
pembeni, ambapo walijikuta na majeraha na usoni, mapajani na maeneo mbalimbali
ya mwili. Kisha baada ya hapo gari ilisogea mbele na kuanza kurusha mabomu kwa
watu wowote iliokutana nao.
Hadi sasa inaelezwa kuwa uchunguzi umeshaanza kufanyika,
huku Kamanda Liberatus Sabas akikataa kuzungumzia zaidi suala hilo.
Alipotafutwa na WAPO Radio FM, hakueleza kwa kina, lakini akasema kuwa sio
suala la kwaya kama ambavyo imeelezwa, bali ni wakinadada wawili na kwamba
hawezi kuzungumza zaidi, bali kesho (Ijumaa) atatoa taarifa rasmi na iliyo
kamili kwa vyombo vya habari.
Alipoulizwa kuwa kama ni kweli jeshi la Polisi
linatuhumiwa kuhusika, alisema kuwa atazungumza kesho kuhusiana na tukio hilo.
Tukio hili limetokea ikiwa ni siku mbili zimepita tokea kuapishwa kwa Inspekta
Jenerali wa Polisi mpya, Ernest Mangu ambaye amechukua nafasi ya IJP Said Mwema
aliyestaafu.
Source:
Gospel Kitaa.
No comments:
Post a Comment