Kwa hesabu zangu za haraka haraka,
Rais Kikwete amenitaja mara nne katika hotuba yake:
"... Mheshimiwa Tundu Lissu
alitoa maoni yake."
"Siyo tu kauli ya Mheshimiwa
Tundu Lissu ni uzushi na uongo mtupu, bali pia ni ya unafiki, fitina na
uzandiki wa hali ya juu."
"... (K)wa Mheshimiwa Tundu
Lissu kudai kuwa mapendekezo ya TEC na CCT hayakuheshimiwa ni uongo wa mchana
usiokuwa na kichwa wala miguu."
"Kama ni kwa sababu za
Mheshimiwa Tundu Lissu nimeshasema hazina ukweli wowote."
Na kwa hesabu zangu hizo hizo, Rais
amesema 'ameambiwa', 'amefahamishwa' au 'ameelezwa' juu ya yaliyojiri kwenye
Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala na baadaye Bungeni mara tisa!!! Katika
hotuba yake, Rais hajaliambia Taifa ni nani hasa '(w)aliyemwambia' au
'kumfahamisha' au 'kumweleza' mambo hayo.
Katika hali nadhani sitakosea
kusema kwamba yote aliyoyasema Mheshimiwa Rais Dokta Jakaya Mrisho Kikwete ni
mambo ya 'sikiasema' (au hearsay) kama wanavyosema wanasheria. Kisheria
ushahidi wa sikiasema hauna thamani yoyote. Kwa maneno mengine, maneno ya JK
hayana thamani yoyote kiushahidi, hata kwa ushahidi wa kipropaganda za kisiasa
alizozifanya juzi.
Lakini ni kauli zangu zipi ambazo
zimezua mashambulizi haya makubwa from the First Citizen? Kwa wasiokumbuka,
nilisema yafuatayo katika hotuba yangu ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni:
"Katika kutekeleza majukumu yake ya kuuchambua Muswada huu, Kamati ...
Ilikutana na wadau wengi mbali mbali. Hivyo, kwa mfano, Kamati ilipata maoni ya
taasisi za kidini na za kiraia; taasisi za elimu ya juu na za kitaaluma; vyama
vya siasa na asasi nyingine. Kwa sababu ambazo Kamati haikuelezwa vizuri na
uongozi wa Bunge hili tukufu, mapendekezo ya Kamati kwenda Zanzibar kwa lengo
la Kukusanya maoni ya wadau wa Zanzibar juu ya Muswada huu muhimu kwa
mustakbala wa Jamhuri ya Muungano yalikataliwa."
Nikaendelea kusema: "(Ni)
muhimu Bunge lako tukufu lifahamu ukweli huu kwamba wadau pekee
walioshirikishwa kutoa maoni yao juu ya Muswada ni Watanzania Bara tu.
Wazanzibari hawakupatiwa fursa hiyo na hawakushirikishwa kabisa, licha ya
Sheria yenyewe kuwa na mambo mengi yanayoihusu Zanzibar."
Kuhusu uteuzi wa Wajumbe wa Tume ya
Mabadiliko ya Katiba nilisema yafuatayo: "... Uteuzi wa Wajumbe wa Tume
uliofanywa na Rais na ambao unatumiwa Kama mfano (wa kuteua Wajumbe 166 wa
Bunge Maalum) wenyewe ulikuwa na walakini kubwa. Katika hili, kuna ushahidi wa
Wawakilishi wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Baraza la Kikristo
Tanzania (CCT) na asasi mbali mbali za kiraia zikiwemo za walemavu
waliowasilisha maoni ya taasisi zao kwa Kamati juu ya Muswada huu. Wawakilishi
hao waliiambia Kamati kwamba ijapokuwa waliandikiwa na Rais kuwasilisha majina
ya Wajumbe wao kwa ajili ya kuteuliwa kwenye Tume, na walifanya hivyo, hakuna
hata moja ya majina waliyopendekeza aliyeteuliwa na Rais kuwa Mjumbe wa Tume.
Badala yake, Rais aliteua watu aliowaona yeye na washauri wake wanafaa. Kama
taarifa za wadau hawa ni za kweli maana yake ni kwamba Rais na Mwenyekiti huyu
wa CCM Taifa hawezi kuaminika tena kuteua Wajumbe halisi wa taasisi hizi katika
Bunge Maalum...."
To wind up, Kamati ilitengeneza
orodha ya taasisi na watu binafsi wa Zanzibar ambao ilitaka kupata maoni yao.
Hatukuonana na hata mmoja wa taasisi na watu binafsi hao kwa sababu Kamati
haikuruhusiwa kwenda Zanzibar. Aidha, Kamati haikukutana na mwakilishi hata
mmoja wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar. Pili, Wawakilishi wa TEC (Father Dr.
Charles Kitima), CCT (Mchungaji Rohho) na wa SHIVYAWATA (nimemsahau jina) ndio
walioiambia Kamati kwamba mapendekezo yao hayakuheshimiwa katika uteuzi wa Wajumbe
wa Tume. Mimi sikuyatoa uchochoroni, yalisemwa hadharani mbele ya Kamati!
Sasa kama ni uongo, fitina,
uzandiki na mapambo ya aina hiyo aliyonipamba nayo Rais, basi ninakiri kuwa I'm
guilty as charged!!!
Tundu Lissu
No comments:
Post a Comment