Bunge la Tanzania kwa mara nyingine limeingia katika mzozo wakati wa mjadala
unaoendelea wa muswaada wa marekebisho ya sheria ya mabadiliko ya katiba
ambao umesusiwa na wabunge ya kambi ya upinzani kwa madai ya kutoshirikisha
maoni ya upande mmoja wa muungano yaani Zanzibar. Mzozo huo ulizusha
vurugu kubwa ambapo pia inadaiwa baadhi ya wabunge wa upinzani baada ya kutoka
nje walivutana askari wa bunge na kudiriki kutaka kurushiana ngumi
baada ya Naibu Spika wa Bunge Job Ndugai, kuamuru kutolewa nje kwa
kiongozi wa upinzani bungeni Bw. Freeman Mbowe, na wabunge wa upinzani kuzuia
kiongozi huyo kutolewa ukumbini ambapo mbunge wa Mbeya Mjini CHADEMA Joseph
Mbilinyi alianza kutolewa nje, kutokana na kuzuia kiongozi wao kutolewa nje ya
ukumbi wa bunge.
Amri hiyo ya naibu spika, ya kumtoa nje bwana Mbowe ilikuja mara
baada ya Kiongozi huyo wa Upinzani bungeni kukataa kutii mamlaka ya kiti ya
kukaa chini ili kupisha mjadala wa muswaada wa sheria ya marekebisho ya sheria
ya mabadiliko ya katiba wa mwaka 2013, uendelee . Kutokea kwa tafrani hiyo
kulitokana na mbunge wa Mkoani, Bw. Ali Khamis Seif kuomba muongozo wa spika,
akitaka hoja iliyokuwa mbele ya bunge ya kujadili muswada wa marekebisho ya
sheria ya mabadiliko ya katiba iahirishwe, na Naibu Spika kuamua kuitisha kura
ambapo wabunge wasiounga mkono mjadala huo uahirishwe wakiwa wengi kutoka chama
tawala CCM, walishinda.
Mbunge wa Iringa Mjini, CHADEMA Mchungaji Peter Msigwa
alifafanua nini hasa kiongozi huyo wa upinzani bungeni alikuwa anataka kusema
wakati Naibu Spika wa bunge alipoamuru akae chini, ambapo alisema alitaka
kufafanua alichodai upotoshwaji uliofanywa na mwanasheria mkuu wa serikali juu
ya muswada huo. Pamoja na tafrani hiyo, Mjadala wa muswada wa marekebisho
ya sheria ya mabadiliko ya katiba uliendelea ambapo muswada huo unapendekeza
mambo mbalimbali ikiwemo idadi ya wajumbe wa bunge la katiba na namna ya
kuwapata, idadi ya siku za mjadala wa rasimu na mengineyo.
Source: VOA (Sept. 2013).Vurugu zagubika bunge la
Tanzania. Retrieved from VOA Sauti ya Amerika
No comments:
Post a Comment