MUUNGANO wa Vyama vya Waandishi wa Habari nchini (UTPC), inakusudia kuishtaki serikali kutokana na mauaji ya kinyama ya mwandishi wa habari, Daud Mwangosi. Mkurugenzi Mtendaji wa UTPC Tanzania, Abubakar Karsan, alitoa msimamo huo jana jijini Mwanza wakati akijibu maswali ya waandishi wa habari, katika kikao cha maadhimisho ya mwaka mmoja tangu Mwangosi alipouawa Septemba 2 mwaka jana. Mwangosi ambaye wakati wa uhai wake alikuwa mwakilishi wa kituo cha televisheni ya Channel Ten mkoani Iringa, aliuawa na polisi wa Septemba 2 mwaka jana baada ya kulipuliwa na kitu kinachodhaniwa kuwa ni bomu. Mwangosi aliuawa kinyama wakati akitekeleza majukumu yake ya kazi, katika ufunguzi wa tawi la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), katika kijiji cha Nyololo ambapo baadaye ziliibuka ghasia baada ya polisi kuamuru wafuasi wa CHADEMA kutawanyika katika ufunguzi wa tawi hilo.
“Msimamo wa UTPC mpaka sasa ni kuishtaki serikali katika mauaji ya Daud Mwangosi. Hatutaishtaki kwa kosa la jinai, tutafungua mashtaka ya fidia. “Kwa kweli Mwangosi aliuawa kinyama sana. Na kwa mauaji haya serikali haiwezi kukwepa mkono wa sheria! “Inauma sana mwandishi kuuawa tena na polisi walinzi wa amani na usalama wa raia na mali zao,” alisema mkurugenzi huyo wa UTPC, Karsan. “Wakati Mwangosi anashambuliwa na askari polisi, alikimbia askari mmoja akawaambia wenzake huyu wanayemshambulia ni mwandishi wa habari, wamuache. Lakini muda huo huo akalipuliwa na bomu na mwili wake kusambaratika,” alisisitiza Karsan. Alisema hata mauaji ya mwandishi mwingine wa habari wa jijini Mwanza, George Masatu, Chama cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Mwanza (MPC), kilipaswa kwenda mahakamni kuishtaki serikali, na kuiomba mahakama iamuru kutolewa kwa ripoti ya uchunguzi wa madaktari wa Bugando kuhusu kifo cha Masatu.
Awali akifungua kikao hicho cha wanahabari mkoa wa Mwanza, Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti na Uchambuzi wa Sera na Utawala bora (Governance Links), Donard Kasongi, aliwasihi waandishi wa habari kushirikiana kutetea haki zao. “Waandishi wa habari ni mhimili mkubwa sana katika maendeleo ya taifa lolote lile duniani. Matukio ya kunyanyaswa na kuuawa kwa waandishi hayapaswi kufanyika kwa nchi inayoongozwa na utawala wa sheria na demokrasia,” alisema Kasongi. Kutoka Moshi, mwandishi Dixon Busagaga, anaripoti kuwa klabu ya waandishi wa habari mkoani Kilimanjaro (MECKI), imetoa wito kwa wamiliki wa vyombo vya habari, kujali maslahi yao na wanapata vitendea kazi ili kutekeleza wajibu wao vizuri. Mwenyekiti wa klabu hiyo, Rodrick Makundi alisema kuwa utafiti wa umoja wa vilabu vya wanahabari nchini (UTPC), unaonyesha kuwa zaidi ya asilimia 80 ya wanahabari nchini hawajaajiriwa na wanafanyakazi katika mazingira yasiyoridhisha.
Alisema kwa kutambua changamoto zinazowakumba wanachama wake, MECKI ipo katika hatua za mwisho za mchakato wa kuboresha utendaji kazi wa wanachama wake katika mpango ambao utatangazwa hivi karibuni. Ili kuendeleza mahusiano mazuri baina ya wanahabari na wadau na kuepuka kupelekana mahakamani, klabu hiyo imeunda kamati ya maadili na usuluhishi yenye wajumbe watano chini ya uenyekiti wake, Japhary Ali ambaye ni wakili wa kujitegemea na ofisa mtendaji utawala wa kiwanda cha sukari TPC. Akizungumzia tukio la kuuawa kwa Mwangosi, Makundi alisema (MECKI), inaungana na wanahabari wote nchini, kuendelea kutoa pole kwa familia ya Mwangosi na IPC iliyopoteza kiongozi shujaa. “Tunaendelea kulaani matukio yote yanayofanywa na baadhi ya vyombo vya dola na taasisi katika kunyima uhuru wa kupata habari na kudhoofisha kwa namna moja au nyingine juhudi za wanahabari katika kutekeleza majukumu yao,” alisema Makundi.
Kutoka Iringa, Francis Godwin anaripoti kuwa maandamano ya kumbukumbu ya kifo cha Mwangosi, jana yalitikisa mji wa Iringa. Maandamano hayo ambayo yameanza majira ya saa 4 asubuhi katika viwanja vya bustani ya manispaa ya Iringa yalipita kuzunguka maeneo mbalimbali ya mji wa Iringa kabla ya kupokelewa na mwenyekiti wa IPC, Frank Leonard, katika ukumbi wa maktaba ya mkoa kwa mkutano wa wadau wa habari. Katika maeneo ambayo maandamano hayo yamepita ikiwemo eneo la Uhindini, Mashine Tatu, Soko Kuu na stendi kuu ya mabasi ya mikoani, wananchi walilazimika kusitisha shughuli zao kushuhudia maandamano hayo ambayo yaliongozwa na Askari wa Usalama Barabarani. Akizungumza baada ya kupokea maandamano hayo, Leonard alisema kuwa lengo la maandamano hayo ni kumkumbuka Mwangosi pamoja na kutazama changamoto zinazowakabili wanahabari.
Alisema kuwa hakuna mtanzania asiyetambua mchango wa Mwangosi katika uhai wake na kuwa kutokana na mchango wake umoja wa vilabu vya waandishi wa habari Tanzania (UTPC) umeanzisha tuzo maalumu kwa wanahabari itakayopewa jina la Daudi Mwangosi na mshindi atapewa sh milioni 10. Kutoka jijini Dar es Salaam, Lucy Ngowi, anaripoti kuwa Meneja Utafiti Machapisho Utunzaji Haki wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), John Mireny, amesema kuwa haoni jitihada za dhati zinachukuliwa baada ya kifo cha aliyekuwa mwandishi wa habari wa Channel Ten, David Mwangosi. Mireny ambaye pia alikuwa kiongozi katika timu ya uchunguzi wa kifo cha Mwangosi alisema pamoja na kesi hiyo kuwepo mahakamani bado kuna chengachenga hali inayodhihirisha kuwa uhuru wa vyombo vya habari bado uko shakani. Alitoa ushauri kuwa uhuru wa vyombo vya habari ulindwe kwenye Katiba mpya ikiwa ni pamoja na uhuru wa habari, uhuru wa uhariri na ule wa kupata habari.
Source: Tanzania Daima ( Sep 2013).UTPC kuishtaki serikali mauaji ya Mwangosi. Retrieved from Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment