MWENYEKITI wa Taasisi ya
Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Reginald Mengi, amesema wamesikitishwa na kauli
ya Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo kuwa Watanzania
hawawezi kufanya uwekezaji katika uchumi wa gesi na mafuta na badala yake wanaweza
kuwekeza katika biashara ya machungwa na juisi.
Kauli ya Mengi ambaye pia ni
Mwenyekiti wa Kampuni za IPP inatokana na madai yaliyotolewa hivi karibuni na
Serikali kuwa uwekezaji wa vitalu vya gesi unahitaji mtaji wa kuanzia Dola
milioni 100 za Marekani.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Mengi alisema siyo
sahihi kwa Profesa Muhongo kusemea uwezo wa Watanzania kushiriki katika uchumi
wa gesi na mafuta ni mdogo.
“Tumesikitishwa na inasikitisha kuona kwamba
waziri wa nishati na madini anaona Watanzania waendelee kuwekeza katika uchumi
wa machungwa na juisi.
“Kauli aliyoitoa Profesa Muhongo kwa vyombo vya habari
inaonyesha wazi kwamba Serikali haina juhudi za makusudi kuhakikisha Watanzania
washiriki katika uchumi wa gesi,”alisema.
Alisema ushiriki wa uchumi wa gesi
na mafuta hauhitaji rasilimali fedha bali unahitaji ujuzi wa kwenda katika
masoko ya mitaji.
“Kwanza naomba ieleweke kuwa sisi hatupingi wawekezaji
kutoka nje ya nchi bali tunataka mgeni akija na sisi tunufaike kwa sababu hii
ni nchi yetu, hakuna mahali kwingine tutaenda kisha tutasema ni nyumbani kwetu
zaidi ya Tanzania.
“Hapa ni suala la ujuzi wa biashara na uwekezaji, zaidi ya
hapo Watanzania wanaweza kwenda katika masoko ya mitaji na kuwa na utaratibu
maalumu utakao wawezsha kushiriki kwa ukamilifu,” alisema Mengi.
Alisema
ingawa Profesa Muhongo kukataa kukutana nao kujadili suala hilo kwa madai hana
muda, wao hawatakwenda kwa Rais Jakaya Kikwete kutoa malalamiko yao bali
watafuata mfumo rasmi wa kuwasiliana naye.
Source: Mtanzania (Sept. 2013).Mengi asikitishwa na kauli ya Waziri Muhongo. Retrieved from Mtanzania
No comments:
Post a Comment