Dk Slaa aguna wauzaji kupewa tena ulaji
BAADA
ya kuiuzia Tanzania rada kwa bei ya dhuluma miaka kumi iliyopita, kampuni ya
BAE Systems ya Uingereza sasa imepewa zabuni ya kusambaza vifaa vya rada hapa
nchini, imefahamika. Kampuni hiyo ndiyo
iliyoiuzia Tanzania rada hiyo mwaka 2002 kwa thamani ya pauni milioni 28
(takribani Sh bilioni 40 kwa wakati huo), jambo lililozua mjadala mkali nchini
na katika Jumuiya ya Kimataifa. Hata hivyo, wiki iliyopita, Mamlaka ya
Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) ilitangaza kwamba imeipa kampuni hiyo tenda ya
kusambaza vipuri kwa ajili ya rada hiyo iliyopo katika Uwanja wa Ndege wa
Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa tangazo hilo la TCAA, zabuni iliyoipa ushindi BAE
ilikuwa na namba TCAA/G/1/2012-2013) na kwamba mkataba huo mpya una thamani ya
pauni za Uingereza 8,948 (T.Sh. milioni 22). Rada hiyo ambayo imekuwa na
tatizo la kuharibika mara kwa mara, inaonekana imepata matatizo tena na gharama
za zabuni hiyo ni kwa ajili ya kipuri zinazohitajika kwa ajili ya ukarabati
wake. Mmoja wa waliokuwa wabunge wa Bunge la Tanzania mwaka 2002 na
waliopiga kelele kuupinga ununuzi huo, Dk. Wilbrod Slaa, alisema hawezi kuingia
undani wa biashara hiyo mpya baina ya Tanzania na Uingereza kwa vile hajajua
haswa ni kitu gani kimenunuliwa, kwa thamani gani na kwanini.
“Unajua hiyo kampuni (BAE) bado ipo na inafanya kazi zake chini ya
sheria. Nashindwa kutoa ya moyoni kwa sababu sijajua nini haswa kimefanyika.
Ile rada ni ya kijeshi na inawezekana ni kwa ajili ya vifaa ambavyo anayeweza
kuviuza kwetu ni mwenye rada pekee,” alisema Katibu Mkuu huyo wa
CHADEMA. Juhudi za Raia Mwema kupata taarifa zaidi kuhusiana na suala hilo
kutoka ndani ya TCAA ziligonga mwamba kwa maelezo kwamba msemaji mkuu wa
taasisi hiyo ni Mkurugenzi Mkuu wake. Hata hivyo, gazeti hili linafahamu
kwamba Mkurugenzi Mkuu wa TCAA, Fadhili Manongi, yuko safarini nchini Malaysia
na hadi tunakwenda mitamboni alikuwa hajajibu maswali aliyotumiwa kwa njia ya
barua pepe (email).
Kampuni ya BAE imekuwa ikishutumiwa duniani kote kwa kufanya biashara
zisizo za kistaarabu, zenye utata na zisizojali hali halisi ya nchi
husika. Shirika hilo limewahi kuuza ndege za maangamizi kwa serikali za
Indonesia ili kuzisaidia kwenye mapambano dhidi ya watu wa Timor Mashariki
waliokuwa wakitaka kujitenga. BAE Systems pia wameingia katika kashfa kubwa ya
kuuza mitumba ya silaha katika nchi ya Saudi Arabia na Zimbabwe katika wakati
ambao Uingereza ilikuwa imeweka vibano kwa misaada ya kiuchumi kwa taifa hilo
la Afrika. Ununuzi wa rada hiyo ulipokewa kwa mshangao hadi nchini
Uingereza ambako aliyekuwa Waziri wa Maendeleo ya Afrika, Claire Short,
alipinga kwa madai kwamba bei ilikuwa ya juu kuliko kawaida na kwamba
haikutakiwa kupewa kipaumbele ilichopewa.
Mashirika makubwa ya kutoa mikopo kama vile Benki ya Dunia (WB) na
Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) yalikataa kuisaidia Tanzania kununua rada
hiyo na ni juhudi za BoT kutafuta mkopo wa riba kubwa kutoka Benki ya Barclays
ya Uingereza kwa kutumia akiba ya dhahabu ya taifa kama dhamana ya mkopo, ndiyo
iliyosaidia kupatikana kwa mkopo huo. Uchunguzi uliofanywa na Taasisi ya
Uchunguzi wa Makosa Makubwa Nchini Uingereza (SFO) mara baada ya kuibuka kwa
kashfa hiyo ulibaini kwamba baadhi ya viongozi wa juu wa serikali inawezekana
walipewa mlungula ili kufanikisha ununuzi huo. Baadhi ya waliotajwa kwenye
kashfa hiyo ni aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Andrew Chenge na
aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Dk. Idrissa Rashid.
Dili hilo la uuzwaji wa rada lilifanikishwa na dalali wa
kimataifa, Sailesh Vithlani ambaye sasa anatafutwa na Polisi pamoja na mshirika
wake wa kibiashara, Tanil Somaiya. Chenge alikuwa muhimu kwenye
kufanikisha ununuzi huo wa rada kwa vile ndiye aliyekuwa mshauri mkuu wa
serikali kwenye masuala ya mikataba na Dk. Rashid ndiye aliyekuwa mshauri mkuu
wa masuala ya kifedha ya serikali. Bila ya ushauri wao, rada hiyo huenda
isingenunuliwa. Uchunguzi wa SFO ulibaini Chenge kuwekewa kiasi cha dola
za Marekani milioni 1.5 kupitia kampuni yake ya Franton Investment iliyopo
katika visiwa vya Jersey vinavyofahamika kwa jina la mbingu ya wakwepa kodi (tax
haven). Fedha hizo ndizo baadaye zilimpa Chenge jina la Mzee wa
Vijisenti baada ya kudai kuwa fedha hizo zilikuwa ni “Vijisenti tu.” Wachunguzi
hao pia waliona namna namna Chenge alivyohamisha kiasi cha dola 600,000 kwenda
kwenye akaunti ya Rashid kwenye kipindi hichohicho cha mauzo ya rada.
Source:
Raia Mwema (August 2013). Vituko rada ya Chenge. Retrieved from Raia
Mwema
No comments:
Post a Comment