Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora

Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora
----------------------WE THANK AND APPRECIATE YOU FOR VISITING CHADEMA DIASPORA BLOG. AGAIN, THANK YOU!-----------------------

Monday, August 26, 2013

Utandazaji bomba la gesi Mtwara-Dar kuanza leo




       Utandazaji wa  mradi wa bomba la kusafirishia gesi kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam unatarajia kuanza leo huku zoezi hilo likitarajiwa kukamilika kabla ya Disemba mwakani. 
Hayo yalisemwa na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, wakati akikagua maendeleo ya utekelezaji wa mradi huo eneo la Somanga Fungu Wilaya ya Kilwa mkoani Lindi. Alisema awali zoezi hilo lilitakiwa kukamilika Januari,2015, lakini huenda likawahi kumalizika kutokana na kuwapo kwa vifaa vya kisasa kutoka Kampuni ya China ya CPP watakaofanya kazi ya kulitandaza. Kipande kimoja cha bomba chenye inchi 36 kina uzito wa tani tano na kipande cha bomba chenye inchi 24 kina uzito wa tani tatu.

      “Kazi inayoanza siku ya Jumatatu (leo) ni kuunganisha vipande hivyo vya bomba na vitaunganishwa kwa teknolojia ya kisasa kwa kuhakikisha mabomba hayo hayapati kutu,” alisema Profesa Muhongo. Kuhusu uwezekano wa kulihujumu bomba hilo, alisema mtu yoyote atakayejaribu kufanya kitendo hicho atakiona cha moto. “Hakuna atakayelichezea bomba hili, yeyote atakayelichezea bomba hili atapambana na mkono wa serikali,” alisema na kufafanua kuwa  mabomba hayo yatachimbiwa chini kwenye urefu usiopongua mita 4 kwenye ardhi, huku mabomba yatakayowekwa chini ya bahari yenye inchi 24 yakiwekewa zege na kufikia uzito wa tani 10. Aliongeza kuwa zoezi ya kuanza kufunga mitambo itayotumika kutandaza mabomba hayo chini ya bahari itaanza Septembe 16, mwaka huu kwa kuwa kazi hiyo inahitaji umakini mkubwa.

     Alisema bomba hilo pindi litakapokamilika uzalishaji wa umeme nchini utaongezeka kutoka Megawati 1,500 hadi kufikia Megawati 3,000 mwaka 2015 na kuuza umeme kwa nchi jirani. Naye Mhandisi kutoka Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Baltazari Thomas, alisema zaidi ya Watanzania 180 wanatarajia kuajiriwa katika mradi huo na kueleza kuwa hadi sasa kuna wafanyakazi zaidi ya 1,600 wa kitanzania ambao ni vibarua. Balozi wa China nchini, Lu Yong Ring, alisema kupitia gesi hiyo wananchi wa Tanzania watapiga hatua kimaendeleo kutokana na kuwapo kwa umeme wa uhakika utakaowasaidia kufanya biashara zao.


Source: Ippmedia (August 2013).Utandazaji bomba la gesi Mtwara-Dar kuanza leo. Retrieved from Ippmedia/Nipashe

No comments: