Bilal Soud
KUTOKANA na maendeleo ya sayansi na teknolojia, matumizi ya simu yamekua kwa kasi hapa nchini. Ingawa si wote wanaotumia simu kwa ajili ya kufanya shughuli zao za kuwaingizia kipato, lakini kuna wengine huendesha ofisi zao kwa kutumia mawasiliano ya simu. Pamoja na kukua kimawasiliano kwa sababu ya simu, lakini pia zimekuwa ni miongoni mwa vyanzo vya ajali za barabarani. Godwin Ntongeji ni Katibu Chama cha Kutetea Abiria (CHAKUA), pia ni mtendaji katika usimamizi wa barabara. Anasema: “Ajali nyingi zinatokea kwa uzembe wa madereva na utumiaji wa simu uliokithiri pindi wanapoendesha vyombo hivyo vya moto.”Utumiaji wa dereva mmoja kwa basi ambalo linasafiri masafa marefu ni tatizo jingine, kwani husababisha dereva kuchoka na hatimaye kujikuta akisinzia wakati ameshikilia usukani na kusababisha ajali.
Hali hiyo si nzuri kwa gari kuwa na dereva mmoja, lakini abiria wamepewa nafasi ya kuwasiliana na mamlaka inayodhibiti masuala ya barabara kwa kupiga simu au ujumbe, pindi inapotokea tatizo au wahusika kwenda kinyume cha taratibu za barabarani, kufanya hivyo kutapunguza ajali kwa kiasi kikubwa. Kwa mtazamo wangu haikatazwi kufanya mawasiliano ya simu au kwa njia nyingine yoyote ilimradi ni mawasiliano, kwa sababu ni haki ya kila mmoja, lakini katika kutekeleza haki kuna taratibu na sehemu zake za kutekeleza haki hizo. Mfano mmoja ni kwamba, kusali ni haki ya kila mmoja lakini sala hiyo ukisalia kwenye ukumbi wa disko itakuwa ni vurugu na kujitafutia matatizo kati yako na watu wanaopenda burudani, kwani utakuwa umetenda haki mahala pasipo sitahili.
Moja ya masharti ya upasuaji ni kwamba daktari hukata mawasiliano yote baina yake na watu wengine, hujifungia katika chumba yeye na mgonjwa wake, hufanya hivyo ili kuepusha usumbufu unaoweza kujitokeza wakati akifanya kazi yake na kusababisha madhara, kikiwamo kifo kwa mgonjwa anayefanyiwa upasuaji. Daktari hufunga simu zake zote au kuziweka katika mtetemo na kuwa mbali nazo ili akipigiwa au kutumiwa ujumbe wa maandishi asisikie hadi amalize kazi yake au anamwachia jukumu la mawasiliano yake mtu mwingine pindi atakapokuwa katika majukumu yake. Suala hilo ni tofauti kwa madereva wa magari ya abiria na binafsi, kwani wengi wao hupokea simu zao na kushika usukani kwa mkono mmoja huku wakidai wao ni wazoefu na wanaweza kuendesha gari hata kama atatumia mkono mmoja na kudai miguu ndiyo inayohusika katika kuongeza na kupunguza kasi.
Hizo ni fikra potofu kwa madereva, ikumbukwe akili ndiyo kitu muhimu na kila kitu ambacho mwanadamu anafanya hutumia akili na kusaidiwa na viungo vingine kama miguu, mikono na macho ambayo hupokea taarifa kutoka kwenye ubongo na kuitekeleza kwa vitendo. Hivyo akili inapojishughulisha na kitu kingine na wakati huo huo mikono ikilazimishwa kuongoza gari bila mawasiliano na ubongo lolote linaweza kutokea. Hiyo ni sawa na kumpa mtoto mdogo aliye mgongoni akushikie noti ya sh 10,000 ukitarajia uitumie baadaye, lakini ukifanikiwa kuipata itakuwa msaada wa nguo uliombebea ambayo itakuwa imekwamisha pesa hiyo isianguke.
Unapopigiwa simu hujui mpigaji anataka kueleza ujumbe gani aliokusudia, jiulize unaendesha gari lenye abiria wasiopunguwa 60, unapokea simu na kupewa taarifa mkeo kafumaniwa, unasoma ujumbe umeandikwa mgonjwa ambaye ni mzazi wako amefariki dunia, unadhani mikono itaongoza gari wakati akili imesimama ghafla? Kwa nini usifikirie kuwa kazi yako ni zaidi ya daktari ambaye anafunga mawasiliano kwa ajili ya kuokoa nafsi ya mtu mmoja wakati wewe unatakiwa kuokoa nafsi zaidi ya 60 hadi 80 achilia mbali wanaosimamisha abiria wa njiani bila utaratibu maalumu.
Unadhani usipoithamini kazi yako nani ungependa achukue jukumu la kuithamini kazi hiyo? Hivi umesahau kuwa kimfaacho mtu chake! Itakuwaje ukifukuzwa kwa ajili ya kupokea simu mara moja tu na leseni ikachukuliwa na kufungiwa isitumike popote nchini? Utakuwa mgeni wa nani? Kwanini Watanzania tumekuwa kama punda asiyeenda bila fimbo? Unataka uwekewe askari kila kona unayopita hata kwenye pori kubwa unataka serikali ikujengee kituo cha askari wa barabarani? Ni fikra ambazo haziwezi kukubaliwa na ni suala lisilowezekana.
Ningeshauri kama unadhani simu yako ni muhimu sana kuliko thamani ya binadamu uliowabeba, ni bora ukatulia kwako na simu yako au ukamuajiri mtu atakaepokea simu zako zote wakati utakapokuwa safarini. Si sifa kufanya jambo ambalo unatambua lina madhara na maangamizi kwa roho za watu. Hakuna atakayekuona shujaa kwa kuongea kwa simu huku ukiendesha, bali watu watajua hujaiva katika taaluma yako na kudhani labda umepewa leseni kwakuwa mjomba ndiye anazigawa au umetumia pesa ili upate kazi kwa kuwa baba amekutafutia ajira ya udereza kwa magari ya bosi wake, hivyo sheria na kanuni za fani hiyo huzijui.
Upande mwingine unaoweza kusababisha ajali ni uchovu wa madereva pale wanapoendesha kwa muda mrefu bila kupumzika, kutokana na magari mengi ya mikoani yanaendeshwa na dereva mmoja. Mwili wa binadamu unahitaji kupumzika kila unapofanya kazi kwa muda fulani, inashangaza dereva analala saa tano usiku baada ya kupaki gari na kuamka saa tisa alfajiri ili kuingiza gari kituoni, hapo atapakia na kuondoka saa 12 asubuhi. Dereva huyu anaanza safari yake inayotumia saa zaidi ya tisa bila kupumzika.
Hivi mtu kama huyu akisinzia unawezaje kumlaumu, kila aliyesafiri hatua ndefu anatambua kwamba kuna wakati watu wote wanakuwa kimya ndani ya gari, ukiangalia wakati huo wengi wa abiria wanakuwa tayari wamelala, wewe uliyelala mapema ukisingizia safari na kuamka saa 11 asubuhi ifikapo saa nne asubuhi unakuwa umeshalala ndani ya safari. Unadhani mwili wako ni tofauti na wa dereva anayekuendesha, la hasha! Bila shaka kuna umuhimu wa kuwa na dereva zaidi ya mmoja ambapo watapokezana pale mmoja atakapoona kichwa kimekuwa kizito na hawezi kuendelea kuendesha ili apumzike.
Wamiliki wa magari wasihofie gharama za kuajiri watu wawili kwa kigezo cha posho bali wajali kutoa huduma bora na salama kwa abiria. Tumechoka kusikia ajali za mara kwa mara ambazo inapofuatiliwa inagundulika ni uzembe wa madereva, tusiendelee kuwatupia mzigo wa lawama wakati tunawatumikisha kama punda au mashine ya kusaga. Naishauri serikali kupitia Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Nchi Kavu na Majini (SUMATRA) isajili gari lenye madereva wawili kwa idadi fulani ya kilometa watakazoona kwao ndiyo kikomo kwa mmoja kuzimudu.
Gari lenye dereva mmoja linyang’nywe lesini, aidha elimu itolewe kabla ya kuchukua hatua hii. Taifa ni letu sote na wanaopoteza maisha ni ndugu wa karibu, tuhitaji kudhibiti suala hili ili hata kama likitokea iwe ni dharura pale inapofanyiwa uchunguzi, tukiamuwa tunaweza, mabadiliko hayahitaji nabii atumwe kwa ajili ya kudhibiti ajali. Kwa mujibu wa Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Mohammed Mpinga, mwaka 2010 ajali ziliongezeka na nyingi zilisababishwa na pikipiki.
Ajali za barabarani zilikuwa 24,471; ajali 3,109 zilisababisha vifo na ajali 2,011 zilisababisha majeruhi. Ajali zilizokuwa hazina vifo wala majeruhi ni 9,887, hizo zilihusisha vyombo vya usafiri na watembea kwa miguu. Katika ajali hizo 24,471, watu 3,469 walifariki dunia na wengine 17,699 kujeruhiwa. Anasema usafiri wa pikipiki ukishamiri kwa kiasi cha kushtusha kwenye ajali za barabarani. Katika ajali zilizotokea Januari hadi Oktoba mwaka jana, ajali za pikipiki zilikuwa 4,167 ambazo zilisababisha vifo vya watu 370 na kujeruhi watu 3,798.
Takwimu za mwaka 2012 zilizopo kwenye ripoti ya haki za binadamu iliyozinduliwa mwaka huu zinaonesha kuwa kulikuwa na ajali 11,438 ambazo zilisababisha vifo vya watu 4919. Katika takwimu hizo Mbeya kulikuwa na ajali 617 waliokufa ni 309; Pwani ajali 1,330 waliopoteza maisha ni 238; Kilimanjaro ajali 1,502 na kuua watu 208; Morogoro ajali 1,599 na kusababaisha vifo vya watu 285. Arusha kulikuwa na ajali 2,136 zilizosababisha vifo vya watu 192 na Iringa kulitokea ajali 791 zilizopoteza maisha ya watu 195; Mwanza ajali 533 na kuua watu 235.
Dar es Salaam ndiyo inaonekana kuongoza kwa kuwa na ajali 2,930 zilizosababisha vifo vya watu 431. Ajali hizi zilithibitika ni uzembe na kutojali sheria za barabarani wakati wa uendeshaji wa vyombo hivyo.
No comments:
Post a Comment