MBUNGE wa Iramba
Magharibi, Mwigulu Nchemba (CCM), amechafua hali ya hewa bungeni kwa kuitaka
Serikali kuwachukuliwa hatua viongozi wa juu wa Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (CHADEMA). Mbunge huyo alisema mwenyekiti wa chama hicho, Freeman
Mbowe pamoja na Katibu Mkuu wake, Dk. Wilbroad Slaa, wanapaswa kuchukuliwa
hatua kwa madai ya kusababisha mauaji ya raia.
Mwigulu, ambaye pia ni Naibu
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Bara, alisema katika kipindi cha
miaka miwili tangu nchi ilipotoka kwenye uchaguzi, viongozi hao wamekuwa
wakihamasisha maandamano na kusababisha umwagaji wa damu za Watanzania.
“Mheshimiwa
Naibu Spika, katika kipindi cha miaka miwili tangu nchi yetu ilipomaliza
Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010, Mbowe na Dk. Slaa wamekuwa wakitoa kauli za wazi
na hata kusababisha mauaji ya watu bila hatia.
“Kutokana na hali hii, sijui
Serikali inafanya nini katika kuwachukulia hatua, kwani viongozi hawa wamekuwa
wakitafuta umaarufu wa kisiasa kwa kuchochea chuki na mauaji dhidi ya raia.
“Kwa
hali hiyo, tangu kipindi hicho hadi leo hii wanasubiri nini badala ya kwenda
kuwaweka jela, kwani huko ndiko wanatakiwa kuwa,” alisema.
Mwigulu, alisema
kukosekana kwa maadili kwa baadhi ya viongozi wa siasa, ambao wamekuwa
wakitumia majukwaa na kuhubiri umwagaji damu ni hatari kwa taifa.
Alisema
viongozi hao wamekuwa wakitumia majukwaa hayo na kusababisha vifo vya wananchi,
huku akitaja vurugu zilizotokea katika mikoa ya Morogoro, Iringa, Arusha na
Singida.
Akijibu swali hilo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Utawala Bora),
George Mkuchika, alisema Serikali inafanya kazi kwa mujibu wa sheria, ikiwa ni
pamoja na kukusanya ushahidi na kwamba mahakama ndicho chombo chenye uamuzi wa
mwisho dhidi ya adhabu kwa raia au kiongozi yeyote wa kisiasa.
Kauli hiyo ya Mwigulu
ilionekana kuchafua hali ya hewa ndani ya Bunge, ambapo Mbunge wa Nyamagana,
Ezekiel Wenje (Chadema), alisimama na kuomba mwongozo wa Spika, huku akimtaka
Mwigulu kuthibitisha kauli yake, vinginevyo aombe radhi.
Wenje alisema hoja ya
Mwigulu imekosa mashiko na ina lengo la kuwadhalilisha viongozi wa Chadema,
huku akisahau kuwa baada ya uchaguzi wa Arumeru Mashariki, aliyekuwa Mwenyetiki
wa Chadema tawi la Usa River, Omari Mbwambo, aliuawa na watu anaodaiwa kuwa ni
wafuasi wa CCM.
Awali katika swali la msingi, Mbunge wa Same Mashariki, Anne
Kilango (CCM), alitaka kujua Serikali inachukua hatua gani kwa wanasiasa wanaokiuka
maadili na kusababisha uvunjifu wa amani.
“Wanataaluma kama vile madaktari,
wahandisi, wahasibu na hata wakandarasi pindi wanapokiuka maadili ya kazi zao
huchukuliwa hatua kwa kufutiwa leseni zao.
“Vile vile viongozi wa kisiasa
wanayo maadili yanayowaongoza, kwanini pale wanapokiuka maadili ya kazi zao
hawachukuliwi hatua kama ilivyo katika makundi hayo? (taaluma),” alisema
Kilango.
1 comment:
KWA MTU YEYOTE ANAYEMFAHAMU MWIGULI NA TABIA YAKE HAWEZI KUSHANGAZWA NA MATAMSHI YAKE HAYO!anachofanya Mwigulu ni kutafuta si tu kuwafurahisha mabosi wake, bali kudhihirisha jinsi alivyo mropokaji na msema ovyo!
Post a Comment