Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira imesema vigogo wakubwa wa serikali wanaongoza kwa kujihusisha na biashara ya pembe za ndovu ndiyo maana zoezi la kuzuia majangili halifanikiwi kwa miaka mingi. Mwenyekiti wa Kamati hiyo, James Lembeli, alitoa kauli hiyo jana jijini Dar es Salaam, muda mfupi baada ya Kamati yake kumaliza kikao katika ofisi ndogo za Bunge na kusema kuwa wabunge wamepiga kelele kwa muda mrefu kuhusu tatizo la ujangili wa kuua tembo, lakini serikali inawapuuza kwa kuwa vigogo wake ndiyo wanaohusika. Lembeli alisema kamati yake imeshindwa na inasubiri nguvu za Mwenyezi Mungu kuwaadhibu watendaji wa serikali wanaoshindwa kudhibiti mauaji ya wanyama hao katika mbuga na mapori ya akiba ingawa wanajulikana.
Aidha, alisema vyombo vya dola navyo watumishi wake wanahusika kwa kuwa wanaona wakubwa wao ambao ni vigogo wa serikali wanafanya biashara hiyo haramu ambayo inazidi kuangamiza tembo kila mwaka. Lembeli alisema anaamini kuwa serikali haina takwimu sahihi za idadi ya tembo waliopo kutokana na idadi kubwa kuuawa kila mwaka. Kwamba wao kama wabunge wameshatoa ushauri mara kadhaa, lakini hakuna kinachofanyika kumaliza tatizo hilo. Alisema Kamati yake mara kadhaa imekuwa ikishauri namna ya kukabiliana na vitendo vya ujangili wa kuua tembo, lakini serikali imekuwa haichukui hatua na kwamba baadhi ya bandari ikiwamo ya Dar es Salaam zinatumika kusafirisha meno ya tembo. “Kila siku serikali ipo kwenye vikao, mara utasikia tupo kwenye mchakato, lakini hakuna chochote kinachofanyika ili kumaliza tatizo hilo mpaka sasa,” alisema.
Aliongeza kuwa mwaka 2011, Rais Jakaya Kikwete alitembelea Wizara ya Maliasili na Utalii na kuwauliza kama wanahitaji awaongezee nguvu ili kupambana na ujangili, lakini wao mpaka sasa wamekaa kimya hawajasema kama wameshindwa ili wapatiwe msaada. Lembeli alisema kamati yake inasikitika kuona tembo wanamalizika mbugani, huku watendaji wakiendelea kukalia ofisi na kupokea mishahara na kuomba Mungu atawahukumu siku ya mwisho. Majangili wanatumia silaha nzito na maboga kwa kuyaweka sumu na tembo anapokula humchukua dakika 20 kupoteza uhai na hapo majangili hao huchukua meno yao.Tembo wanaouawa na majangili wanapatikana katika pori la akiba la Selous ambalo linadaiwa kuwa na udhaifu katika ulinzi na kwa mujibu wa takwimu katika hifadhi hiyo kulikuwa na tembo 110,000, lakini kwa sasa wapo 20,000 tu.
Meno ya tembo hutengenezea vitu vya urembo kama pete, bangili, mikufu na vitu hivyo huvaliwa na watu wakubwa kama wafalme na malkia. Meno hayo pia hutengenezea vijiti vya kulia chakula ambavyo Wachina huvitumia sana. Vile vile hutengenezea vinyago (sanamu kama ya Yesu Kristo) au picha mbalimbali za watu maarufu na huuzwa kwa gharama kubwa sana. Kwa mujibu wa utafiti wa Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori, kwa siku wanauawa tembo 30, kwa mwezi 850 na kwa mwaka tembo 10,000 na kwamba idadi hiyo ni ya wanyama hao walioko kwenye hifadhi tu. Taarifa zilizopo zinaonyesha kuwa mwaka 2009 kulikuwa na tembo 109,000 katika hifadhi zote, lakini mwaka huu idadi hiyo imepungua chini ya 70,000. Hivi karibuni, baadhi ya watumishi katika vyombo vya dola wakiwamo askari polisi na wanajeshi wamekuwa wakikamatwa na meno ya tembo matukio ambayo yanaelezwa kuwa ni hatari kwa kuwa wao ndiyo walinzi wa usalama na maliasili za taifa.
Source: Makore R. (August 2013).Mbunge:Vigogo serikalini majangili. Retrieved from Ippmedia/Nipashe
No comments:
Post a Comment