MKURUGENZI wa fedha na utawala wa kampuni ya mikopo ya Faidika, Joseph Kidaha, amedaiwa kuanza kampeni za kuwania ubunge Jimbo la Tabora Kaskazini. Kidaha amedaiwa kuzunguka jimbo zima na kutoa fedha, ahadi za kujenga soko la kina mama Kata ya Ufuluma, ‘diary’ zilizoandikwa Faidika na kugongwa muhuri na anuani yake ya ‘Joseph Kidaha Bukumbi Uyui, Tabora. Vitu vingine ambavyo amedaiwa kutoa ni kanga za Faidika, skafu, mipira mitatu, jezi seti mbili, kofia na kulipia ada baadhi ya wanafunzi 15 wasiokuwa na uwezo wa kulipa ada. Pia imedaiwa kuwa matukio hayo amekuwa akiyafanya bila kupitia ofisi za CCM wilaya ambapo baadhi ya viongozi wamekuwa na taarifa zake lakini wameshindwa kuchukua hatua za kumdhibiti.
Baadhi ya wanachama wa CCM Wilaya ya Uyui wamedai kada huyo licha ya kutoa fedha, vitu na ahadi mbalimbali pia amezunguka jimbo zima akijipanga kuwania ubunge, na kwamba viongozi wa CCM wilaya chini ya Mwenyekiti wake, Musa Ntimizi, wamekuwa wakimbeba. “Mwanachama mwenzetu ameaanza mbio za kuwania ubunge mapema anazunguka kwa kificho jimbo zima, anamwaga fedha vitu mbalimbali na ahadi, haya anayafanya lakini uongozi umekaa kimya bila kutoa onyo wakati ni kosa,” alisema. Kidaha ambaye kwenye kura za maoni alishika nafasi ya pili baada kushindwa na Mbunge wa sasa, Shafin Sumar, ni mzaliwa wa Kata ya Bukumbi, Wilaya ya Uyui.
Gazeti hili lilimtafuta Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Uyui, Musa Ntimizi kufafanua hatua ya kada huyo kuanza kampeni za kuwania ubunge, alisema ni kweli taarifa hizo anazo lakini wanashindwa kuchukua hatua kutokana na stahili ya kada huyo. “Taarifa zake zipo hapa ofisini, aliwahi kuja na kuripoti tu kuwa yupo katika shughuli za kijamii Jimbo la Tabora Kaskazini lakini tunashindwa kumdhibiti kwani hakuna sehemu anafanya kampeni za wazi,” alisema Ntimizi. Jitihada mbalimbali zilifanyika za kumtafuta Kidaha bila mafanikio, hata kumpigia simu ya kiganjani zaidi ya mara nne lakini hakupokea.
Source: Tanzania Daima (August 2013).Kada wa CCM aanza kampeni za ubunge. Retrieved from Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment