HOTUBA YA MHESHIMIWA DKT. JAKAYA MRISHO KIKWETE, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA KWA WANANCHI, TAREHE 31 JULAI, 2013
Utangulizi
Ndugu wananchi;
Kama ilivyo ada naomba
nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehma, kwa kutujalia uzima na
kutuwezesha kwa mara nyingine tena kutekeleza utaratibu wetu huu mzuri
tuliojiwekea wa Rais kuzungumza na taifa kila mwisho wa mwezi.
Ndugu Wananchi;
Mwezi Julai, 2013 ulikuwa
wa neema kubwa ya wageni kwa nchi yetu wakiwemo watu na viongozi mashuhuri
duniani. Natoa shukrani nyingi kwa Watanzania wenzangu kwa jinsi tulivyowapokea
wageni wetu zaidi ya 1,700. Wamefurahi kuwepo kwao nchini na wameondoka wakiwa na
kumbukumbu nzuri ya nchi yetu. Wageni wetu wamekuwa wa manufaa makubwa kwa nchi
yetu. Wamesaidia kuitangaza Tanzania duniani na kuendeleza fursa za kukuza
utalii, biashara na uwekezaji nchini na kwingineko katika Afrika.
Mkutano wa Smart Partnership
Ndugu wananchi;
Wageni wetu wa kwanza ni
wale waliokuja kuhudhuria Mkutano wa Global 2013 Smart Partnership
Dialogue uliofanyika Dar es Salaam tarehe 28 Juni hadi 1 Julai, 2013.
Mkutano huo ulihudhuriwa na watu zaidi ya 800 kutoka mabara yote duniani
wakiwemo Watanzania. Miongoni mwa waliohudhuria ni pamoja na wakuu wa nchi na
Serikali, viongozi wastaafu, wanadiplomasia, wawakilishi wa mashirika na
taasisi za kimataifa, makampuni ya ndani na nje, wafanyabiashara, wasomi, asasi
za kijamii na watu wa makundi mbalimbali katika jamii. Makampuni yetu 21 nayo
yaliungana na makampuni mengine 28 kutoka nje ya nchi kushiriki kwenye
maonesho ya matumizi ya sayansi na teknolojia yaliyofanyika sambamba na mkutano
huo.
Ndugu Wananchi;
Agenda kuu ya majadiliano
ya mwaka huu ilikuwa ni “Matumizi ya teknolojia kama nyenzo ya kuleta
maendeleo ya kijamii na kiuchumi Barani Afrika (Leveraging Technology
for Africa’s Social-Economic Transformation: The Smart Partnership Way).
Tuliichagua mada hii kwa kuwa ni ukweli ulio wazi kuwa matumizi ya sayansi na
teknolojia ndiyo chachu kubwa iliyoleta mageuzi na maendeleo ya kiuchumi na
kijamii katika nchi. Ndiyo siri ya mafanikio katika nchi zilizoendelea na
zinazopiga kasi kubwa ya maendeleo duniani.
Bahati mbaya sana kumekuwa
na maendeleo na matumizi madogo ya sayansi na teknolojia katika Afrika. Ndiyo
maana nchi za Afrika ziko nyuma kimaendeleo ukilinganisha na zile
zilizoendelea. Katika mkutano huo umuhimu wa kuendeleza na kuongeza matumizi ya
sayansi na teknolojia kwa ajili ya maendeleo Barani Afrika ulitambuliwa na
kusisitizwa.
Mkutano ulihimiza na
kusisitiza kuwa sera, mikakati na mipango ya maendeleo ya nchi za Afrika zitoe
kipaumbele kwa kuendeleza matumizi ya sayansi na teknolojia. Nchi zetu
zimehimizwa kuwekeza katika elimu ya sayansi na teknolojia pamoja na kujenga
uwezo wetu wa ndani wa uvumbuzi, ubunifu, umiliki na uendelezaji wa sayansi na
teknolojia. Aidha, imesisitizwa kwa nchi zetu ziongeze kasi ya kutumia sayansi
na teknolojia katika shughuli mbalimbali za kiuchumi na kijamii ili kuongeza
ufanisi na kasi ya maendeleo.
Ndugu Wananchi;
Jambo la kutia faraja kwetu
nchini ni kwamba mambo yote hayo tunayafanya. Tunachotakiwa sasa ni kufanya
vizuri zaidi na kuongeza uwekezaji na kasi ya kuendeleza matumizi ya sayansi na
teknolojia katika shughuli za maendeleo ya kiuchumi na kijamii nchini.
Tutaendelea kuboresha sera, kuboresha mazingira ya uwekezaji na kwa ajili ya
maendeleo ya sayansi na teknolojia nchini.
Ziara ya Rais wa Marekani Nchini Tanzania
Ndugu wananchi;
Mgeni wetu wa pili alikuwa
Rais wa Marekani, Mheshimiwa Barack Obama, aliyefanya ziara nchini kwetu kati
ya tarehe 1 - 2 Julai, 2013. Lengo la ziara yake ilikuwa kuimarisha uhusiano wa
kihistoria uliopo kati ya Marekani na Tanzania. Kama mjuavyo, nchi zetu mbili
zina uhusiano wa kibalozi tangu Uhuru wa Tanganyika mwaka 1961 na Mapinduzi
Matukufu ya Zanzibar mwaka 1964.
Uhusiano wetu umepita
katika vipindi mbalimbali na kwamba hivi sasa umekuwa mzuri zaidi kuliko wakati
mwingine wowote katika historia ya nchi zetu mbili. Kumekuwepo na ongezeko
kubwa la misaada ya maendeleo kutoka Marekani na uwekezaji wa vitega uchumi na
biashara navyo vinakua. Pia ziara za kiserikali za viongozi wa nchi zetu
kutembeleana zimeongezeka. Kama mtakavyokumbuka, mwaka 2008 aliyekuwa Rais wa
Marekani Mheshimiwa George W. Bush alifanya ziara ya siku nne nchini. Pia
Mawaziri mbalimbali wa Serikali ya Marekani wametembelea Tanzania akiwemo
Mheshimiwa Hilary Clinton akiwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani aliyekuja
mwaka 2011.
Ndugu Wananchi;
Nchi ya Marekani imekuwa
mshirika wetu muhimu wa maendeleo katika nyanja mbalimbali. Kwa upande wa afya
kwa mfano, tunapata msaada mkubwa katika mapambano dhidi ya malaria na UKIMWI.
Katika maendeleo ya elimu, nako wanatusaidia katika mafunzo ya wataalamu
mbalimbali pamoja na upatikanaji wa vitabu vya sayansi na hisabati kwa ajili ya
shule za sekondari. Kupitia Mfuko wa Changamoto za Milenia, Marekani
inatusaidia katika kuimarisha miundomuinu ya barabara, umeme na maji. Ujenzi wa
barabara za Tanga – Horohoro, Namtumbo – Songea – Mbinga; Tunduma – Sumbawanga
na baadhi ya barabara za Pemba, ujenzi wa njia ya pili ya kupeleka umeme Unguja
kutoka Dar es Salaam, ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Mafia na usambazaji wa umeme
katika Mikoa 10 ya Tanzania bara ni miongoni mwa matunda ya msaada wa Mfuko
huo. Pamoja na hayo, ipo miradi ya kuongeza maji katika jiji la Dar es Salaam
na Manispaa ya Morogoro ambayo inaendelea kutekelezwa.
Ndugu Wananchi;
Wakati wa ziara yake, Rais
Obama alielezea na kusisitiza dhamira yake na ya Serikali yake ya kuimarisha
zaidi uhusiano na ushirikiano mzuri uliopo kati ya nchi zetu. Alielezea
kuridhika na hatua tuliyofikia ya kukuza demokrasia nchini, utawala bora na
kuwekeza katika maendeleo ya watu wetu. Aliahidi kuendelea kuunga mkono juhudi
zetu. Katika hili ameahidi kuongeza misaada ya maendeleo na kiufundi katika
sekta za afya, elimu, kilimo, barabara, nishati na maendeleo ya vijana. Pia,
alithibitisha kwamba nchi yetu itaendelea kunufaika na ufadhili wa Awamu ya
Pili ya Mfuko wa Changamoto za Millenia. Katika awamu hii, maeneo yatakayopewa
kipaumbele hapa kwetu ni umeme na barabara za vijijini. Mazungumzo ya miradi
itakayotekelezwa katika awamu hiyo yanaendelea vizuri.
Power Africa
Ndugu Wananchi;
Rais Obama alitumia fursa
ya ziara yake nchini kuzindua mpango wa Serikali yake wa kusaidia maendeleo ya
sekta ya umeme katika Bara la Afrika. Mpango huu unaoitwa “Power Africa
Initiative” umetengewa kiasi cha dola za Marekani bilioni 7 na Serikali
ya Marekani na makampuni binafsi ya nchi hiyo yameahidi kuwekeza dola
bilioni 9 katika mpango huo. Kwa kuanzia, nchi sita za Afrika
(Ethiopia, Ghana, Nigeria, Tanzania, Liberia na Kenya) ikiwemo Tanzania
zitahusishwa.
Bila ya shaka Mpango huo
ukikamilika utasaidia sana kuimarisha upatikanaji wa umeme barani Afrika ambayo
ni nyenzo muhimu katika kuleta maendeleo ya kiuchumi na kijamii. Ni ukweli ulio
wazi kuwa ukosefu wa umeme wa kutosha na wa uhakika ni sababu kubwa
inayokwamisha maendeleo ya haraka katika nchi za Afrika. Hivyo basi, msaada huu
ni muhimu sana kwetu. Kwa ajili hiyo nimeagiza Wizara ya Nishati na Madini iandae
mkakati madhubuti wa namna Tanzania itakavyoshiriki na kufaidika na mpango huo.
Nataka mpango huo utakapoanza kutekelezwa utukute sisi tupo tayari kutumia
fursa zake.
Vile vile, ndugu wananchi,
katika ziara hiyo Rais Obama alielezea nia ya Serikali yake kutaka kuwepo
mpango wa kukuza ushirikiano wa biashara na uwekezaji baina ya nchi yake na
nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki. Nimeelekeza Wizara husika yaani Wizara ya
Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Wizara ya Viwanda, Biashara na Masoko nao watengeneze
mkakati utakaoonesha jinsi tulivyojipanga kufaidika na mpango huo. Lazima
tujiandae vyema na mapema tunufaike saiwa na mpango huo.
Ziara ya Rais Mstaafu wa Marekani Nchini
Ndugu Wananchi;
Sambamba na ziara ya Rais
Obama, nchi yetu ilipata bahati ya kutembelewa tena na Rais Mstaafu wa
Marekani, Mheshimiwa George W. Bush na mkewe Laura Bush, tarehe 1 hadi 3 Julai,
2013. Kwa udhamini wa asasi ya George W. Bush Foundation waliandaa Mkutano wa
Wake wa Marais wa Afrika uliofanyika hapa Dar es Salaam, tarehe 2 na 3 Julai,
2013. Mama Michelle Obama naye alishiriki mkutano huo uliozungumzia kuimarisha
maendeleo na afya ya wanawake Barani Afrika.
Katika mkutano huo, pia,
Mheshimiwa George W. Bush alizindua mpango wa kuimarisha mapambano dhidi ya
kansa ya shingo ya kizazi na matiti barani Afrika. Kufuatia Mpango huo,
Serikali ya Marekani imetoa dola milioni 3 na mashine 16 za Cryo Therapy
zinazotumia baridi kali kuua chembechembe za kansa. Msaada huo ni muhimu hasa
ukizingatia kuwa kila mwaka hapa nchini zaidi ya Watanzania 21,000 wanapata
maradhi ya kansa. Kati ya hao asilimia 29.4 ni wanawake wanaopata
magonjwa ya kansa ya shingo ya uzazi na asilimia 6.2 wanapata kansa ya
matiti. Naamini Mpango huu utatusaidia sana katika kuimarisha mapambano dhidi
ya maradhi haya yanayowasumbua na kuua kina mama wengi nchini. Nimeitaka Wizara
ya Afya na Ustawi wa Jamii kuweka utaratibu mzuri ili msaada huo utumike
ipasavyo na kuwanufaisha walengwa.
Ziara ya Waziri Mkuu Mstaafu wa Uingereza Nchini
Ndugu Wananchi;
Tarehe 23 mwezi Julai, 2013
pia tulitembelewa na Waziri Mkuu Mstaafu wa Uingereza, Mheshimiwa Tony Blair.
Katika mazungumzo yetu Mheshimiwa Blair aliahidi kuisaidia nchi yetu kupitia
taasisi yake ya Africa Governance Initiative kusaidia kusambaza umeme wa jua
katika shule zetu za sekondari vijijini, maboresho ya shirika letu la umeme
(TANESCO) na kusaidia uanzishaji na uimarishaji wa Kitengo cha Rais cha
Ufuatiliaji Utekelezaji wa Programu za Maendeleo (Presidential Delivery Bureau
- PDB). Tunamshukuru kwa ahadi yake hiyo itakayochangia katika jitihada za
kujiletea maendeleo.
Ziara ya Waziri Mkuu wa Thailand Nchini
Ndugu Wananchi;
Tarehe 30 Julai, 2013
tulimpokea Mheshimiwa Yingluck Shinawatra, Waziri Mkuu wa Thailand aliyefanya
ziara ya siku tatu nchini. Lengo la ziara yake ni kuimarisha uhusiano mzuri
uliopo kati ya Thailand na Tanzania. Katika ziara hiyo, tumezindua Jukwaa la
Wafanyabiashara wa Thailand na Tanzania (Thai-Tanzania Business Forum) ili
kukuza biashara na uwekezaji baina ya nchi zetu. Waziri Mkuu Yingluck
Shinawatra alitumia fursa hiyo kufafanua sera ya Thailand kwa Afrika
inayosisitiza kukuza ushirikiano wa karibu wa kiuchumi na kibiashara. Pia
amepata nafasi ya kutembelea Hifadhi ya Taifa ya Serengeti kujionea mwenyewe
jinsi nchi yetu ilivyobarikiwa kwa kuwa na kivutio hicho cha aina yake.
Alipokuwa kule nchi zetu zilitiliana saini maelewano ya ushirikiano katika
kulinda na kuhifadhi wanyama pori.
Katika mazungumzo yangu na
yeye, tumekubaliana kuchukua hatua thabiti kukuza ushirikiano katika nyanja
mbalimbali. Tumetiliana saini mikataba mitano ya ushirikiano kwa mambo
yafuatayo: Kukuza na kulinda vitega uchumi; kubadilishana wafungwa; ushirikiano
wa kiufundi; na ushirikiano kwa masuala ya madini. Aidha, Waziri Mkuu huyo
ameahidi kuwahimiza wawekezaji wa nchini mwake kuja Tanzania kuwekeza katika
sekta mbalimbali za uchumi ikiwemo kilimo, utalii, viwanda nakadhalika. Pia,
Waziri Mkuu wa Thailand ameahidi kuwa Serikali yake itatoa ufadhili kwa vijana 10
kusoma Shahada ya Uzamili nchini humo. Vile vile, nchi hiyo itaanza kuleta
wataalamu wa afya wa kujitolea kuja kushirikiana na wataalam wetu kuimarisha
huduma ya afya nchini.
Ziara hizi zinaonesha
utayari wa dunia kuunga mkono jitihada zetu za kujiletea maendeleo. Naomba
Watanzania wenzangu tutumie vizuri utayari huo wa dunia kuongeza kasi ya
maendeleo yetu. Tusijikwaze wenyewe.
Ziara ya Kagera
Ndugu wananchi;
Kuanzia tarehe 24 hadi 29
Julai, 2013, nilifanya ziara Mkoani Kagera. Nilishiriki kwenye Maadhimisho ya
Siku ya Mashujaa na kuzindua jengo jipya la Mahakama Kuu. Pia niliweka jiwe la
msingi la upanuzi wa kiwanja cha ndege cha Bukoba na kuweka mawe ya msingi ya
ujenzi wa kiwango cha lami kwa barabara za Kigoma – Lusahunga na Kyaka –
Kayanga – Bugene. Vile vile nilizindua Wilaya mpya ya Kyerwa na kukagua
shughuli za maendeleo pamoja na kuona na kusikiliza changamoto mbalimbali
zinazowakabili wananchi ili kuzitafutia majawabu.
Sherehe za Kumbukumbu ya
Mashujaa zilifana sana. Niliwapongeza viongozi wa Jeshi na wa Mkoa kwa
maandalizi mazuri ya sherehe hizo. Pia nilirudia kumpongeza Mkuu wa Majeshi,
Jenerali Davis Mwamunyange, kwa uamuzi wake wa busara wa kufanya sherehe za
kumbukumbu za mashujaa wetu pale Kaboya badala ya kufanyikia Dar es Salaam tu
kama ilivyokuwa miaka ya nyuma. Ni uamuzi muafaka na wa busara kwani pale
Kaboya ndipo walipolala mashujaa wetu waliopoteza maisha yao kutetea mipaka na
uhuru wa nchi yetu dhidi ya Nduli Iddi Amin. Hali kadhalika, kule Naliendele,
Mtwara ambapo sherehe za mashujaa zilifanyika mwaka wa juzi, ndipo walipozikwa
mashujaa wetu waliopoteza maisha kuisaidia nchi jirani na rafiki ya Msumbuji
kutetea Uhuru wake dhidi ya wakoloni, makaburu na vibaraka wao wa ndani ya
Msumbiji.
Ndugu Wananchi;
Katika hotuba yangu pale
Kaboya niliwakumbusha Watanzania wenzangu kwamba katika kuwakumbuka mashujaa
wetu wale na sisi tulio hai, hatuna budi kutambua wajibu wetu wa kuwa tayari
kujitolea muhanga kwa ajili ya kulinda uhuru wa mipaka ya nchi yetu.
Nilisisitiza utayari wa nchi yetu kulinda mipaka yake na kwamba mfano wa mashujaa
waliolala pale ni fundisho kwa mtu ye yote anayetamani kumega kipande cho chote
cha ardhi ya nchi yetu. Atakiona cha mtema kuni kilichomkuta Nduli Iddi Amini
au hata zaidi.
Nimesikia kuwa kauli yangu
ile imetafsiriwa visivyo na kupotoshwa na baadhi vyombo vya habari na hata
majirani zetu. Tafsiri hizo ni potofu. Sikumtaja mtu ye yote au nchi yo yote.
Nilikuwa nazungumzia wajibu wa majeshi yetu na raia wa nchi yetu wa kulinda
uhuru na mipaka yetu na kwamba hatutamruhusu mtu au nchi yo yote kutupokonya
wala kuichezea haki yetu hiyo ya msingi. Tuko tayari kuitetea hata kama gharama
yake ni maisha yetu kama walivyofanya mashujaa waliolala Kaboya.
Mahakama Kuu
Ndugu Wananchi;
Katika ufunguzi wa Mahakama
Kuu ya Bukoba nilisisitiza dhamira na utayari wa Serikali yetu kuiwezesha
Mahakama ya Tanzania kuwa na Mahakama Kuu katika kila Mkoa. Baada ya kukamilika
kwa Mahakama Kuu ya Bukoba bado kuna Mikoa 14 hainazo. Katika bajeti ya mwaka
wa fedha 2013/14 tumetenga fedha za kujenga Mahakama Kuu katika Mikoa 7 na
nilirudia ahadi yangu kuwa katika mwaka ujao wa fedha tutatoa fedha za
kumalizia Mikoa 7 iliyosalia. Niliamua tuongeze kasi ya kujenga Mahakama Kuu
hizo ili kuiwezesha Mahakama ya Tanzania kutimiza ipasavyo wajibu wake wa kutoa
haki nchini.
Maendeleo ya Mkoa wa Kagera
Ndugu Wananchi;
Nilipokuwa Kagera
nilifurahishwa na utekelezaji wa shughuli mbalimbali za maendeleo ya kiuchumi
na kijamii. Taarifa za Mkoa na Wilaya zimefafanua kwa kina mambo mazuri
yaliyofanyika na yanayoendelea kufanyika Mkoani. Wameelezea furaha yao kwa
mafanikio yaliyopatikana ambayo baadhi nimeyashuhudia au hata kushiriki
kuyazindua na kuweka mawe ya msingi. Taarifa hizo pia zimelezea mambo mengi
zaidi wanayotaka yafanyike na matatizo mapya na hata ya zamani ambayo wanataka
yapatiwe ufumbuzi.
Katika mazungumzo yangu na
viongozi na wananchi, yapo mambo ambayo yako kwenye uwezo wao kijijini,
Wilayani na Mkoani kuyapatia ufumbuzi. Tulikubaliana na kuelekezana nini
kifanyike. Yapo mengine mengine ambayo yanahitaji nguvu ya taifa tumeyachukua
kuja kuyafanyia kazi. Kuna baadhi yaliwahusu Mawaziri ambao nilikuwa nao
ziarani waliyasemea na kuyafanyia kazi palepale yalipojitokeza.
Ulinzi na Usalama
Ndugu Wananchi;
Kuna mambo matatu yahusuyo
usalama ambayo yalizungumzwa na wananchi kwa uchungu mkubwa ambayo niliamua
tuyashughulikie kitaifa. Mambo hayo ni ujambazi wa kutumia silaha kuteka
magari, kupora mali na watu kuuawa. Jambo la pili ni wahamiaji kutoka nchi
jirani wanaoingia, kuishi na kufanya shughuli nchini kinyume cha sheria. Na
tatu, mifugo kuingizwa kwa wingi nchini bila kufuata taratibu husika na mingine
kuingizwa katika hifadhi za wanyama.
Ndugu wananchi;
Nilitoa maagizo kwa wakuu
wa vyombo vya ulinzi na usalama yaani JWTZ, Polisi, Usalama wa Taifa na
Uhamiaji watengeneze mpango kabambe wa kuyashughulikia matatizo hayo.
Watayarishe na kutekeleza operesheni maalum itakayo au zitakazokomesha
ujambazi, kuondoa wahamiaji wasiokuwa halali na kuondoa mifugo iliyoingizwa
nchini kinyume na utaratibu na ile iliyoko kwenye maeneo yasiyo stahili.
Aidha, niliwataka majambazi
wajisalimishe na wasalimishe silaha zao ndani ya wiki mbili na siku hizo
zinaanzia tarehe 29 Julai, 2013 nilipomaliza ziara yangu Mkoani humo. Kwa
wahamiaji wanaoishi nchini kinyume cha sheria nimewataka watumie muda huo
kuondoka nchini au kuhalalisha ukaazi wao. Hivyo hivyo kwa mifugo iliyoingizwa
nchini kinyume na sheria au ile iliyoko kwenye maeneo yasiyostahili. Ndani ya
muda huo watu wote waondoe mifugo yao au wajitokeze kufuata taratibu zilizopo.
Ndugu Wananchi;
Nilisema nilipokuwa Mkoani
Kagera na narudia tena leo kuwa baada ya siku 14 kupita, vyombo vya ulinzi na
usalama vitaendesha operesheni maalum ya kushughulikia matatizo hayo. Nilisema
kuwa operesheni hiyo itafanyika katika Mikoa ya Kigoma, Kagera na Geita kwa
wakati mmoja. Napenda kuwahakikishia kuwa hapatakuwa na mahali pa kukimbilia
wala kujificha. Nawashauri wale wote wanaohusika na ujambazi, uhamiaji haramu
na uingizaji haramu wa mifugo waamue kuchukua hatua muafaka sasa. Wasisubiri
operesheni iwakute, wala wasifikirie kuwa hili ni jambo la kupita. Safari hii
itakuwa endelevu.
Ndugu Zangu;
Hatuwezi kukubali hali hii
niliyoikuta Mkoani Kagera ikaachwa kuendelea. Italeta madhara makubwa zaidi
siku za usoni. Haiwezekani raia katika nchi yake, akose uhuru na usalama wa
kutembea peke yake mpaka asindikizwe na Polisi. Na, baya zaidi hata Polisi nao
wanashambuliwa na kuuawa watakavyo majambazi. Uhalifu huu lazima ukomeshwe,
uishe na usijirudie tena.
Pia, haiwezekani hali ya
watu kutoka nchi jirani kuingia nchini, kuishi na kufanya shughuli na kutoka
watakavyo. Hatuzuii watu kuingia na kuishi Tanzania lakini wafuate sheria na
taratibu za kuhamia na kuishi katika nchi yetu. Nchi yetu ina sifa na ukarimu
huo. Hakuna uthibitisho mkubwa zaidi ya ule wa mwaka 1982, Rais Julius Nyerere
wakati ule alipowaruhusu wakimbizi wanaopenda kuwa raia wa Tanzania wafanye
hivyo. Wakimbizi 30,000 tu waliitumia fursa hiyo. Mwaka 2010 tuliwapa
uraia wakimbizi 160,000 wa kutoka Burundi. Kwa sababu hiyo
hatuoni sababu ya watu kufanya wanayoyafanya sasa kule Mkoani Kagera. Hatuwezi
kuacha hali hiyo iendelee ilivyo.
Ndugu Wananchi;
Nilipokuwa Mkoani Kagera
nilielezea kusikitishwa kwangu na vitendo vya baadhi ya watendaji na viongozi
wa vijiji na wananchi kuwaruhusu watu kuingia na kuishi nchini kinyume cha
sheria. Nimewataka waache mtindo huo. Nimeagiza na wao wajumuishwe katika
operesheni ijayo. Watakaobainika kujihusisha na vitendo hivyo haramu
wachukuliwe hatua zipasazo kisheria. Aidha, niliwataka Maafisa wa Uhamiaji
watimize ipasavyo wajibu wao. Ukweli ni kwamba, mambo haya kuendelea kwa muda
mrefu kiasi hiki ni kwa sababu ya udhaifu wa mamlaka husika. Vile vile, nimewataka
TAKUKURU nao watimize wajibu wao. Hapa kuna uthibitisho tosha wa kuwepo kwa
vitendo vya rushwa vinavyohusisha wahamiaji hao na maofisa wa vijiji na idara
husika za Serikali. Mimi naamini kama TAKUKURU ikiwabana na Uhamiaji wakichemka
vya kutosha tatizo hili lingepungua sana au hata kutokuwepo kabisa.
Uhusiano na Nchi ya Rwanda
Ndugu wananchi;
Katika kipindi cha miezi
miwili sasa hususan tangu mwishoni mwa mwezi Mei, 2013, uhusiano baina ya nchi
yetu na Rwanda unapitia katika wakati mgumu. Kauli za viongozi wa Rwanda dhidi
yangu na nchi yetu ni ushahidi wa kuwepo hali hiyo. Napenda kuwahakikishia
Watanzania wenzangu na ndugu zetu wa Rwanda kuwa mimi, Serikali ninayoiongoza
na wananchi wa Tanzania tunapenda kuwa na uhusiano mzuri na ushirikiano wa
karibu na Rwanda kama ilivyo kwa nchi zote jirani. Kama majirani kila mmoja
anamuhitaji mwenzake, hivyo lazima tuwe na uhusiano mwema na ushirikiano mzuri.
Napenda kusisitiza kuwa
mimi na Serikali ninayoiongoza tutakuwa wa mwisho kufanya kitendo au vitendo
vibaya dhidi ya Rwanda au nchi yo yote jirani au yo yote duniani. Hatuna sababu
ya kufanya hivyo kwani ni mambo ambayo hayana tija wala maslahi kwetu.
Ndugu Wananchi;
Ukweli ni kwamba wakati
wote tumekuwa tunajihusisha na mambo ya kukuza na kujenga ujirani mwema na
kufanya mambo ambayo yatasaidia kuimarisha uhusiano wetu kwa maslahi ya nchi
zetu. Hiyo ni moja ya nguzo kuu ya Sera ya Mambo ya Nje ya Tanzania. Huo ndiyo
ukweli kuhusu uhusiano wetu na nchi ya Rwanda kabla na hata baada ya
sintofahamu iliyojitokeza sasa. Napenda kuwahakikishia ndugu zetu wa Rwanda
kuwa kwa upande wetu hakuna kilichobadilika wala kupungua katika uhusiano na
ushirikiano wetu. Mambo yapo vile vile. Kwa upande wangu, binafsi, sijasema lo
lote kuhusu Rwanda pamoja na maneno mengi ya matusi na kejeli yanayotoka kwenye
vinywa vya viongozi wa Rwanda dhidi yangu. Siyo kwamba siambiwi yanayosemwa au
sijui kusema au sina la kusema, la hasha. Sijafanya hivyo kwa sababu sioni
faida yake. Kwangu mimi sioni kama kuna mgogoro wa aina yo yote. Busara
inatuelekeza kuwa tusikuze mgogoro usiokuwepo. Waingereza wanasema “two
wrongs do not make a right”.
Ndugu Wananchi;
Kama mjuavyo uhusiano wetu
na Rwanda umekuwa mzuri kwa miaka mingi. Tunashirikiana na kusaidiana kwa mambo
mengi baina ya nchi zetu kitaifa na katika kanda yetu ya Afrika Mashariki na
Nchi za Maziwa Makuu, katika Umoja wa Afrika na hata kimataifa. Uhusiano
unaelekea kupata mtikisiko baada ya mimi kutoa ushauri kwa Serikali ya Rwanda
kuzungumza na mahasimu wao. Ushauri ule niliutoa kwa nia njema kabisa kwani
bado naamini kuwa kama jambo linaweza kumalizwa kwa njia ya mazungumzo njia
hiyo ni vyema itumike. Isitoshe, ushauri ule niliutoa pia kwa Serikali ya Kongo
na kwa Serikali ya Uganda. Katika mkutano ule Rais Yoweri Museveni wa Uganda
aliunga mkono kauli yangu. Rais wa Rwanda hakusema cho chote pale mkutanoni.
Baada ya kurudi nyumbani ndipo tukaanza kuyasikia maneno tuliyoyasikia na
tunayoendelea kuyasikia.
Kwa kweli nimestaajabu sana
na jinsi walivyouchukulia ushauri wangu na wanayoyafanya. Havifanani kabisa, completely
out of proportion and out of context. Mimi nilifanya vile kwa kuzingatia
mila na desturi zetu za miaka mingi katika ukanda wetu. Tumekuwa tunakutana
katika mikutano na vikao mbalimbali tunazungumza na kushauriana kwa uwazi juu
ya njia za kushughulikia matatizo na masuala mbalimbali kila yanapotokea.
Wakati wote tumeyachukulia kuwa ni mambo yanayotuhusu sote hivyo kupeana
ushauri ni wajibu wetu wote. Na mara nyingi ushauri kwa wanaogombana kuzungumza
tunautumia sana. Iweje leo mtu kutoa ushauri ule lionekane jambo baya na la
ajabu. Jambo la kushutumiwa na kutukanwa! Siyo sawa hata kidogo!! Ushauri si
shuruti, ushauri si amri. Una hiyari ya kuukubali au kuukataa. Muungwana
hujibu: “Siuafiki ushauri wako”. Hakuna haja ya kutukana wala kusema maneno
yasiyostahili wala kusema yasiyokuwepo na ya uongo.
Ndugu Wananchi;
Napenda kurudia kusema kuwa
mimi binafsi na Serikali yetu ya Tanzania hatuna ugomvi wala nia yo yote mbaya
na Rwanda. Tunapenda tuendelee kuwa na uhusiano mzuri na Rwanda. Labda wenzetu
wanalo lao jambo dhidi yetu ambalo sisi hatulijui. Maana na sisi tunasikia
mengi yanayozungumzwa na kudaiwa kupangwa kufanywa na Rwanda dhidi yangu na
nchi yetu. Hatupendi kuyaamini moja kwa moja tunayoyasikia lakini hatuyapuuzi.
Ndugu Wananchi;
Kabla ya kumaliza, naomba
kutumia nafasi hii pia kuwatakia Waislamu wote nchini heri na baraka tele
katika kukamilisha ibada muhimu ya kufunga mwezi Mtukufu wa Ramadhan. Naomba
tuendelee kuwatakia heri ili wamalize salama na tuweze kusherehekea kwa furaha
na bashasha tele siku kuu ya Idd el Fitr pindi itakapowadia.
Mwisho kabisa, nawaomba
Watanzania wenzangu wote tuendelee kushirikiana na kuishi kwa upendo, umoja na
mshikamano kama ilivyo kawaida yetu.
Mungu Ibariki Tanzania!
Mungu Ibariki Afrika!
Asanteni Sana Kwa
Kunisikiliza.
No comments:
Post a Comment