Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora

Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora
----------------------WE THANK AND APPRECIATE YOU FOR VISITING CHADEMA DIASPORA BLOG. AGAIN, THANK YOU!-----------------------

Saturday, August 17, 2013

CCM wazidi kuvurugana


      MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mkoa wa Kagera, Constansia Buhiye amesema kamwe madiwani nane waliowafukuza hawawezi kurudi ofisini kama alivyoagiza Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Nape Nnauye. Wakati Buhiye akitoa msimamo huo, Nape aliliambia Tanzania Daima kuwa madiwani hao ni halali na suala lao linasubiri vikao vya Kamati Kuu (CC) ya chama vitakavyofanyika mkoani Dodoma wiki ijayo. Akizungumza na Tanzania Daima, Buhiye alisema vikao vya juu vya chama hicho hubariki kile kilichoamriwa na vikao vya chini, hivyo hadi sasa wanatambua madiwani hao si wanachama wao.

       “Umeniuliza namna chama chetu kilivyofanya Moshi au Songea kuwa waliomba kibali kutoka Kamati Kuu ya Taifa ili waweze kuwafukuza madiwani wao, hapa ni Bukoba. Songea wanajua walivyofanya na Moshi…, sisi Bukoba tunasisitiza madiwani hawa nane tayari tumewafukuza. “Mimi yale ya kikao niliyasema na ninayasimamia, madiwani hao hawawezi kurudi ofisini kama Nape alivyoagiza, sio wanachama wetu. Msimamo wa Nape upo tofauti na jinsi nilivyozoea kuendesha vikao vya chama,” alisema. Tanzania Daima imedokezwa kuwa Buhiye amekuwa na visasi dhidi ya uongozi wa chama makao makuu baada ya kuondolewa kwenye nafasi ya ujumbe wa Kamati Kuu ya Taifa ambayo sasa inashikiliwa na Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka.


       Hata hivyo, Buhiye alipoulizwa kuhusu suala la tofauti zake na viongozi wa CCM makao makuu, alisema jambo hilo halikujadiliwa kwenye kikao kilichowafukuza madiwani. Tanzania Daima liliwasiliana na Nape ambapo alisema madiwani hao wanasubiri uamuzi wa CC, lakini kwa sasa wanaendelea na nyadhifa zao kama kawaida. “Baada ya kikao kile cha Kagera, Katibu wa CCM alipaswa kutuandikia barua, sisi makao makuu ndio tungeridhia, ndio tungemwandikia Mkurungenzi wa Tume ya Uchaguzi, ndiye anayesema kuwa kata hizo zipo wazi, na atamwandikia Mkurugenzi wa Manispaa ya Bukoba. “Ukiangalia hawa viongozi wetu waliandika barua kwa mkurugenzi kitu ambacho ni kinyume cha sheria. Katibu wa Chama Cha Mapinduzi mkoani anawajibika kwa chama taifa sio kwa Mkurugenzi wa Manispaa,” alisema.

        Jana asubuhi katika andiko lake kupitia mtandao wa kijamii wa Jamii Forum, Buhiye aliandika kuwa “kumekuwa na mijadala kadhaa juu ya namna mambo yanavyokwenda ndani ya CCM, hasa kufuatia sakata la madiwani na meya wa Manispaa ya Bukoba. “Kimsingi hali si tete kama inavyojaribu kuelezwa. Taratibu, kanuni, sheria na katiba ya chama kupitia vikao vitatumika kulimaliza swala hili kwa amani kabisa. Mwisho wa siku lazima wananchi wa Bukoba na Manispaa yao wapate haki yao ya msingi!” Nape alifafanua: “Tafsiri rahisi hapa ni kuwa masilahi ya wananchi na nchi yao kwanza, masilahi ya chama na itikadi zetu baadae! Hivyo kwa kifupi kwa swala la Bukoba lazima masilahi ya wananchi wa Bukoba yatangulizwe mbele na yavuke ushabiki wa kiitikadi.

       “Hatuwezi kupofushwa na mapenzi kwa vyama vyetu tukafumbia macho masilahi mapana ya wanachi wa Bukoba. Hii haimaanishi sikipendi chama changu bali ukweli ni kuwa naipenda sana CCM yangu, lakini naipenda zaidi nchi yangu.” Hata hivyo, kwa mujibu wa Ibara ya 94 (14) ya Katiba ya CCM inatamka kuwa moja ya kazi za Halmashauri Kuu ya CCM ya Mkoa ni kumwachisha au kumfukuza uanachama mwanachama yeyote endapo itaridhika kwamba tabia na mwenendo wake vinamwondolea sifa za uanachama. Mwanachama anayeachishwa au kufukuzwa uanachama anaweza kukata rufaa kwa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM ya Taifa. Pia Ibara 94(15) inasema kuwa Halmashauri Kuu ya CCM ya Mkoa inao uwezo wa kumwachisha au kumfukuza uongozi kiongozi yeyote ambaye uteuzi wake wa mwisho unafanywa na Halmashauri Kuu ya CCM ya Mkoa.

Source: Isango J. (August 2013). CCM wazidi kuvurugana. Retrieved from Tanzania Daima

No comments: