Tunawaona
wamesambaza watu wao, wanafanya mikutano ya ndani na hadhara, juu ya rasimu ya
Katiba Mpya, badala ya kujenga hoja, wanapiga kelele. Kelele ziko zaidi kwenye
muundo wa muungano, hususan serikali tatu. Wanataka serikali mbili. Hoja
hazionekani. Wamekomaa tu 'gharama...gharama...gharama..." Huo ukubwa wa
gharama (kulinganisha na ufisadi wanaofanya wa matrilioni, ikiwemo misamaha ya
kodi inayofika asilimia 2 ya pato la taifa) hawauoneshi kwa hoja.
Badala ya
kudanganya wananchi kwa hoja mfu kama za akina Nape, Mwigulu, Mwenyekiti wao wa
wazee, ambaye haoni haya kutosema ukweli mbele ya kadamnasi, waje wajenge hoja.
Waache kupiga kelele.
E. SABABU ZA
KUUNGA MKONO MUUNDO WA SERIKALI TATU
1. MUUNDO WA
SERIKALI MBILI UMESHINDWA KUTEKELEZEKA
(A) TANGU
KUSAINIWA KWA HATI ZA MAKUBALIANO YA MUUNGANO, HATI HIZO HAZIJAHESHIMIWA NA
MAMLAKA ZA SERIKALI YA MUUNGANO NA YA ZANZIBAR KAMA IFUATAVYO:
(i) Mamlaka ya
kutunga sheria ya iliyokuwa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar haikutunga sheria ya
kuridhia Hati za Makubaliano ya Muungano na kwa hiyo Muungano haukupata uhalali
wa kisheria kwa upande wa Zanzibar;
(ii) Orodha ya
Mambo ya Muungano imeongezwa kinyume na Hati za Makubaliano ya Muungano kutoka
mambo 11 yaliyoko kwenye Hati za Makubaliano ya Muungano hadi mambo 22 yaliyoko
katika Nyongeza ya Kwanza ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya sasa. Lengo na
athari ya kuongeza orodha ya Mambo ya Muungano imekuwa ni kuipokonya Zanzibar
mamlaka yake katika mambo ambayo hayakuwa ya Muungano;
(iii) Utaratibu
wa kikatiba wa kutatua migogoro ya Muungano haujawahi kuheshimiwa wala kufuatwa
badala yake migogoro ya kikatiba ya Muungano inajadiliwa kwa taratibu za
kirasimu ambazo zimeshindwa kuitatua;
(B) ZANZIBAR
HAIRIDHIKI TENA NA MUUNGANO NA INATAKA UHURU
Mabadiliko ya
kikatiba ya hivi karibuni, pamoja na madai ya Zanzibar juu ya ‘Kero za
Muungano’ yanaonyesha dhahiri kwamba Zanzibar hairidhiki tena na misingi mikuu
ya Muungano iliyoko kwenye Hati za Makubaliano ya Muungano na Katiba ya Jamhuri
ya Muungano ya sasa:
(i) Katiba ya
sasa ya Zanzibar inaitangaza Zanzibar kuwa ‘nchi’ na kutangaza mipaka yake na
eneo lake la bahari;
(ii) Katiba
mpya ya Zanzibar inatamka kwamba ‘Zanzibar ni miongoni mwa nchi mbili
zinazounda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.’ Kama Zanzibar ni moja ya ‘nchi
mbili’, nchi ya pili ni Tanganyika ambayo ndiyo ilikuwa Mshirika wa Zanzibar
katika Hati za Makubaliano ya Muungano;
(iii) Zanzibar
ni dola, hata kama haina mamlaka kamili, kwa sababu ina vyombo vyote vya dola
kama Serikali, Bunge na Mahakama. Aidha, Zanzibar ina viashiria (trappings) za
dola kama Bendera ya Taifa, Wimbo wa Taifa na Rais wake hukagua gwaride la
heshima wakati wa Sherehe za Mapinduzi;
(iv) Katiba ya
sasa ya Zanzibar inatamka kwamba Rais wa Zanzibar ni Mkuu wa Nchi ya Zanzibar
na Kamanda Mkuu wa Vikosi vya Idara Maalumu, yaani vikosi vya kijeshi vya
Zanzibar;
(v) Katiba ya
sasa ya Zanzibar inaunda vikosi vya kijeshi vya Zanzibar vinavyoitwa vikosi vya
Idara Maalumu na kumfanya Rais wa Zanzibar Amiri Jeshi Mkuu wa vikosi hivyo
mwenye mamlaka ya kutangaza hali ya hatari au kutangaza na kuendesha vita;
(vi) Katiba ya
sasa ya Zanzibar inakataa mamlaka ya Mahakama ya Rufani ya Jamhuri ya Muungano
kwa kukataza rufaa kwenye Mahakama hiyo kwa kesi zinazohusu haki za binadamu,
tafsiri ya Katiba ya Zanzibar, mambo ya Kiislamu yanaoanzia katika Mahakama za
Kadhi na mambo mengine yanayoweza kuainishwa kwenye Katiba ya Zanzibar au
kwenye sheria iliyotungwa na Baraza la Wawakilishi;
(vii) Katiba ya
sasa ya Zanzibar imemnyang’anya Rais wa Jamhuri ya Muungano mamlaka ya kuigawa
Zanzibar katika mikoa, wilaya na maeneo mengine, na Rais wa Zanzibar hahitaji
tena kushauriana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wakati anapofanya uteuzi wa
Wakuu wa Mikoa na Wilaya wa Zanzibar;
(viii) Katiba
ya sasa ya Zanzibar imekataza kutumika kwa sheria zinazohusu mambo ya Muungano
zitakazotungwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano mpaka kwanza zipelekwe mbele ya
Baraza la Wawakilishi Zanzibar;
(ix) Katiba ya
sasa ya Zanzibar imekataa mamlaka ya Bunge la Jamhuri ya Muungano ya kutoza
kodi zinazohusiana na Mambo ya Muungano mpaka kwanza kuwepo mashauriano na
makubaliano baina ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Jamhuri
ya Muungano;
(x) Katiba ya
sasa ya Zanzibar inaweka msimamo kwamba mambo yote yaliyoorodheshwa katika
kipengele (i) – (ix) hayawezi kubadilishwa bila kura ya maoni ya wananchi wa
Zanzibar kuhusu mabadiliko hayo;
(x) Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar inayaita ‘Kero za Muungano’ Mambo mbali mbali ya Muungano
yaliyomo katika Hati za Makubaliano ya Muungano na yalioongezwa baada ya Hati
hizo. Mambo ya Muungano ambayo sasa ni ‘kero’ ni hisa za Serikali ya Mapinduzi
Zanzibar zilizokuwa katika Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki, masuala ya kodi
kwa bidhaa zinazoingizwa Zanzibar na mgawanyo wa mapato kati ya Zanzibar na
Tanzania Bara; ushiriki wa Zanzibar katika taasisi za nje na katika Jumuiya ya
Afrika Mashariki; utafutaji na uchimbaji mafuta na gesi asili na uvuvi kwenye
ukanda wa uchumi wa bahari kuu; na ajira kwa watumishi wa Zanzibar katika
taasisi za Muungano.
MADAI YA MUUNDO
WA SHIRIKISHO LA SERIKALI TATU NI YA MUDA MREFU
Mapendekezo ya
Rasimu juu ya muundo wa shirikisho lenye serikali tatu sio mapya, bali ni madai
ya miaka mingi ya wananchi wa Tanzania:
(i). Mwaka 1984
Rais wa pili wa Zanzibar Aboud Jumbe Mwinyi, Waziri Kiongozi Ramadhani Haji
Faki na Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar Bashir Kwaw Swanzy waling’olewa madarakani
na Wazanzibari wengine wengi kuwekwa kizuizini kwa sababu ya kuhoji muundo wa
Muungano wa Serikali Mbili kwa madai kwamba Hati za Makubaliano ya Muungano
zilikuwa zimeweka muundo wa shirikisho la Serikali Tatu;
(ii). Mwaka 1991
Tume ya Rais ya Mfumo wa Chama Kimoja au Vyama Vingi vya Siasa iliyoundwa na
Rais Ali Hassan Mwinyi ilipendekeza muundo wa Shirikisho lenye Serikali tatu;
(iii). Vyama vya
siasa vikuu vya upinzani, yaani CHADEMA, CUF na NCCR Mageuzi, vimekuwa na
msimamo wa kuundwa kwa shirikisho la serikali tatu tangu vilipoanzishwa mwaka
1992;
(iv). Mwaka 1993
Wabunge 55 kwa pamoja walitoa taarifa ya kuwasilisha hoja Bungeni iliyodai
kwamba kuendelea na mfumo wa Muungano wa serikali mbili usiowaridhisha wananchi
wengi wa upande mmoja ni kuhatarisha kuendelea kudumu kwa Muungano. Hivyo
Wabunge hawa waliliomba Bunge liazimie kwamba Serikali ilete Muswada Bungeni
kurekebisha Katiba ya Jamhuri ya Muungano ili kuwezesha uundaji wa ‘Serikali ya
Tanganyika’ ndani ya Muungano;
(v). Mwaka 1998
Tume ya Kukusanya Maoni Juu ya Katiba, White Paper Na. 1 ya 1998 iliyoteuliwa
na Rais Benjamin Mkapa kuchunguza masuala mbali mbali ya kikatiba, nayo
ilipendekeza muundo wa Shirikisho lenye Serikali tatu;
SHIRIKISHO LA
SERIKALI TATU HALIWEZI KUWA NA GHARAMA KUBWA KULIKO MUUNGANO WA SERIKALI MBILI
WA SASA
Tangu
kuchapishwa kwa Rasimu, viongozi wa CCM na baadhi ya wananchi na wanazuoni
wamedai kwamba muundo wa Muungano wenye serikali tatu utakuwa na gharama kubwa
kwa nchi maskini kama ya kwetu. Hata hivyo, uchambuzi wa Rasimu yenyewe
unaonyesha kwamba gharama za kuendeshea muundo wa shirikisho lenye serikali
tatu zinaweza kuwa hata ndogo kuliko gharama za kuendeshea muundo wa Muungano
wa serikali mbili za sasa:
(i) Hadi sasa
hakuna mtu yeyote au taasisi iliyofanya uchambuzi wa ulinganifu wa gharama za
kuendesha serikali – iwe moja, mbili au tatu – katika nchi yetu. Kwa sababu
hiyo, hakuna ushahidi wowote wa kuthibitisha kwamba kuendesha serikali tatu ni
ghali zaidi kuliko kuendesha serikali mbili;
(ii) Kama suala
la gharama za kuendeshea serikali ndio jambo muhimu zaidi katika kuamua muundo
wa Muungano, wanaopinga shirikisho la serikali tatu wangeeleweka kama
wangependekeza muundo wa serikali moja tu, badala ya serikali mbili za sasa
wanazoziunga mkono, au tatu zilizopendekezwa na Rasimu;
(iii) Kama
mapendekezo ya Rasimu juu ya Mambo ya Muungano yakichukuliwa kuwa kigezo cha
kupima ukubwa wa serikali – na kwa hiyo gharama za kuiendeshea – basi gharama
za serikali ya Muungano zinaweza kuwa ndogo sana:
(a). Kwa mambo
saba ya Muungano yanayopendekezwa na Rasimu, hakutakuwa na zaidi ya wizara nne
za Serikali ya Muungano. Hivyo, kwa mfano, kutakuwa na wizara ya katiba na
sheria itakayoshughulikia masuala ya Katiba na mamlaka ya Jamhuri ya Muungano;
wizara ya ulinzi itakayokuwa na majukumu ya ulinzi na usalama wa Jamhuri ya
Muungano; wizara ya fedha itakayoshughulikia masuala ya sarafu na benki kuu, na
ushuru wa bidhaa na mapato yasiyo ya kodi yatokanayo na Mambo ya Muungano; na
wizara ya mambo ya nje. Masuala yaliyobaki, yaani uraia na uhamiaji na usajili
wa vyama vya siasa hayastahili kuwa na wizara zinazojitegemea kwa hiyo yanaweza
kuwekwa chini ya mojawapo ya wizara zilizotajwa hapo juu;
(b). Aya ya 93(2)
ya Rasimu inapendekeza ukubwa wa Baraza la Mawaziri la Jamhuri ya Muungano kuwa
mawaziri wasiozidi kumi na tano. Hata hivyo, aya ya 93(3) inaelekeza kwamba
“Serikali ya Jamhuri ya Muungano itakuwa na Wizara kwa kuzingatia mamlaka ya
Serikali kwa mujibu wa Katiba hii.” Kwa maana nyingine ukubwa wa Serikali
lazima uzingatie Mambo saba ya Muungano. Kwa sababu hiyo, Serikali ya Jamhuri
ya Muungano haiwezi kuwa na mawaziri wengi kuliko Mambo saba ya Muungano;
(c). Kwa mtazamo
huo huo wa aya ya 93(3) na orodha ya Mambo ya Muungano kama kipimo cha ukubwa
wa Serikali ya Muungano, haiwezekani Katibu Mkuu Kiongozi na Makatibu Wakuu
wanaopendekezwa katika aya za 98 na 99 za Rasimu kuwa zaidi ya wanne;
(d). Kwa
kuzingatia idadi ya Makatibu Wakuu wenyewe, Kamati Maalumu ya Makatibu Wakuu
inayoelezwa katika aya ya 100 na Sekretarieti ya Baraza la Mawaziri inayotajwa
katika aya ya 101, hazina maana wala umuhimu wowote kikatiba;
(e). Kwa
kuzingatia mapendekezo ya Rasimu kuhusu Bunge la Jamhuri ya Muungano katika aya
ya 105, kwa idadi ya sasa ya mikoa ya Tanzania Bara na wilaya za Zanzibar,
Bunge la Jamhuri ya Muungano litakuwa na wabunge 75. Kwa mapendekezo ya muundo
wa serikali tatu, endapo Bunge la Zanzibar litakuwa na Wabunge hamsini wa
majimbo ya sasa ya uchaguzi, wakati bunge la Tanganyika litakuwa na wabunge 189
wa majimbo ya uchaguzi ya sasa. Kwa maana hiyo, muundo wa Muungano wa serikali
tatu utakuwa na mabunge matatu yenye jumla ya wabunge 314;
(f). Kwa
kulinganisha, Bunge la Jamhuri ya Muungano la sasa lina idadi ya wabunge 357 – 189
wa majimbo ya uchaguzi ya Tanzania Bara na hamsini ya Zanzibar; 102 wa Viti
Maalumu; 10 wa kuteuliwa na Rais; watano wanaowakilisha Baraza la wawakilishi
Zanzibar na Mwanasheria Mkuu. Kwa upande wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar,
kuna jumla ya Wawakilishi 81 - 50 wanaowakilisha majimbo ya uchaguzi, 10 wa
kuteuliwa na Rais wa Zanzibar, 20 wa Viti Maalum na Mwanasheria Mkuu wa
Zanzibar. Kwa maana hiyo, kwa muundo wa sasa wa Muungano, mabunge mawili
tuliyonayo yana idadi ya wabunge 438. Idadi hiyo ni kubwa kuliko idadi ya
wabunge wa mabunge matatu yatakayokuwepo chini ya muundo wa serikali tatu kwa
wabunge 124!
(g). Taasisi
nyingine za Muungano zinazopendekezwa kama vile Tume ya Mahusiano na Uratibu wa
Serikali (aya ya 102); Tume ya Utumishi wa Mahakama (aya ya 172); na Tume ya
Utumishi wa Umma (aya ya 178) haziwezi kuwa kubwa sana kwa kuzingatia ukubwa wa
Serikali ya Jamhuri ya Muungano kwa mujibu wa Rasimu;
(h). Taasisi
nyingine kama vile Tume ya Maadili ya Uongozi na Uwajibikaji (aya ya 188) na
Tume ya Haki za Binadamu (aya ya 194) hazipo kwenye orodha ya Mambo ya Muungano
na uwepo wao kwenye Rasimu unakinzana na matakwa ya aya za 59(1) na 60 za
Rasimu. Kama majukumu ya taasisi hizo hayahusu Mambo ya Muungano, Tume hizo
haziwezi kugharimiwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano;
(i). Majukumu ya
utekelezaji wa Mambo mengine ya Muungano kama uchaguzi na usajili wa vyama vya
siasa yanaweza kutekelezwa na taasisi husika za Washirika wa Muungano kwa
makubaliano na masharti maalumu chini ya aya ya 59(3) ya Rasimu. Hii nayo
itapunguza gharama za kuendesha Serikali ya Jamhuri ya Muungano;
MUUNDO WA
SHIRIKISHO LA SERIKALI TATU UTALETA VITA???
Kumejitokeza
hoja kwamba muundo wa shirikisho la serikali utapelekea Muungano kuvunjika, na
“Muungano ukivunjika hakuna mwananchi atakayenusurika, awe wa Tanganyika au wa
Zanzibar.” Dhana hii ya ‘serikali tatu ni kiama’ na mifano inayotolewa kuiunga
mkono ina malengo ya kiitikadi ya kuwatisha wananchi wasijadili Muungano na
masuala muhimu yanayouhusu:
(i) Kuna mifano
ya nchi zilizovunja muungano wao bila kuwepo vita au migogoro ya mipaka.
Jamhuri za Czech na Slovakia zilizotokana na kuvunjika kwa Jamhuri ya zamani ya
Czechoslovakia ni mojawapo ya nchi hizo;
(ii) Kuna nchi
nyingi ambazo zimepigana vita ya wenyewe kwa wenyewe kwa muda mrefu kwa sababu
ya kulazimisha muungano usiokubaliwa na upande mmoja au mwingine katika umoja
huo. Ethiopia na Eritrea; Sudan na Sudan Kusini, na hata Yugoslavia ya zamani
ni mifano ya nchi hizo;
(iii) Zipo nchi
ambazo zinaendelea kuwa na vita kwa sababu ya kulazimisha umoja ambao upande
mmoja unaukataa. India (mgogoro wa Jimbo la Kashmir), Hispania (Jimbo la
Basque) na Angola (Jimbo la Cabinda) ni mifano mizuri.
Tumaini
Makene
CHADEMA
Senior Information(Press) Officer
0752
691569/ 0688 595831
No comments:
Post a Comment