OFISI ya Msajili wa Vyama vya Siasa imeendelea kujikanganya kuhusu uundwaji wa makambi ya vijana za Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA). Akizungumza na gazeti hili jana, Naibu Msajili, Rajab Baraka Juma, alisema kuwa haamini kama CHADEMA wanaweza kuanzisha makambi hayo ya kuwaandaa vijana kiukakamavu kwa ajili ya ulinzi wa mikutano yao na viongozi. Alisema kauli za wanasiasa wakati mwingine hutolewa kwa bahati mbaya kutokana na kushangiliwa na wafuasi wao, hivyo amaamini kwamba CHADEMA watafuata utaratibu katika kuanzisha makundi hayo. Juma aliongeza kuwa shughuli za ulinzi na usalama ni jukumu la polisi, hivyo ni kinyume cha sheria za nchi kwa chama cha siasa kuwa na jeshi.
Alisema kauli iliyotolewa na CHADEMA iliwatisha kwa kuweka bayana kwamba hawana imani na Jeshi la Polisi kwa sababu haliwatendei haki. “Ofisi yangu inaruhusu chama chochote cha siasa kilichopo kihalali kuanzisha makundi ya vijana kwa ajili ya ulinzi lakini si kufanya kazi za polisi kwa kujichukulia hatua mikononi. “CHADEMA wamesema hawana imani na polisi halafu wanaanzisha kundi la vijana waende kwenye makambi wakafundishwe ulinzi, wakirudi wakiwa kwenye mikutano yao wakimwona mtu anahatarisha amani watamnyuka,” alisema. Alisema kuwa kwa vile hawana imani na polisi watasema kuwa wakimpeleka mtuhumiwa atatoka tu. “Lakini pia wasiseme fulani anafanya na sisi tufanye, si sawa,” alisema kiongozi huyo alipotakiwa kueleza kuhusu makundi ya vijana wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) maarufu kama ‘Green Guards’.
Awali ofisa huyo alisema iwapo CHADEMA itaendelea na msimamo wake wa kuanzisha makundi hayo watachukuliwa hatua ambayo hakuieleza bayana. Lakini jana msaidizi huyo alisema watafanya uchunguzi kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama. “Tumejiridhisha na kazi zinazofanywa na ‘Green Gurds’ ya CCM lakini pia tunaridhishwa na kazi zinazofanywa na vyama vyote, ndiyo maana huwa tunafanya nao mikutano kila baada ya muda na tunazungumza, wa kupongeza tunampongeza, tunasemana na wa kumwonya,” alisema. Hivi karibuni uongozi wa CHADEMA ulisema utaanzisha makundi ya vijana wakakamavu kwa ajili ya ulinzi wakati wa mikutano yao ya kisiasa, kauli iliyotafsiriwa na polisi kama hatua ya kuzusha vurugu.
Source: Irene M. ( July 2013). Tendwa bado utata mtupu . Retrieved from Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment