Madiwani wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na Chama cha NCCR Mageuzi ambao ni wajumbe wa Baraza la Katiba la Wilaya ya Buhigwe Mkoa wa Kigoma wametofautiana kuhusu mapendekezo ya Rasimu ya kwanza ya Katiba juu ya muundo wa Muungano kuwa wa Serikali tatu. Tofauti hizo zilitokea jana wakati Diwani wa CCM Kata ya Mnamila, Eveline Muhungu aliposimama kuchangia kuhusu mapendekezo yake juu ya Muungano ambapo alitaka Muundo wa Serikali kwenye Rasimu ya kwanza ya Katiba ubadilishwe na uwe wa Serikali mbili. Hatua hiyo ilisababisha Diwani wa Chadema, Kata ya Janda Emmanuel Petro kusimama na kusema kuwa hakuna haja ya kuwa na Serikali mbili na muundo sahili wa Muungano ni kuwa na Serikali tatu.
Mapendekezo hayo yalipingwa vikali na Diwani wa Kata ya Mzenze, NCCR Mageuzi, Abesta Mkeya ambaye alisema suluhisho la migogoro ya Muungano na kuwaenzi waasisi wa taifa hili ni kuwa na muundo wa Serikali moja, lakini sio tatu wala mbili. Hata hivyo madiwani hao walionyesha wazi kuwa wanachokijadili kwenye baraza hilo ni misimamo ya vyama vyao na siyo maoni waliyotumwa na wananchi. Maoni ya madiwani hao yanakuja huku ikiwa tayari Chama Cha Mapinduzi kimeshatangaza msimamo wake kuwa mapendekezo yao ni kuwa na muundo wa Serikali mbili, jambo ambalo linapingana na vyama vingine vya siasa ikiwa ni pamoja na Chama cha Wananchi, (CUF) ambao msimamo wao ni muundo wa Serikali tatu.
Kwa mujibu wa mapendekezo ya Rasimu ya Kwanza ya Katiba Ibara ya 57 (1) inasema Jamhuri ya Muungano itakuwa na muundo wa shirikisho lenye Serikali tatu ambazo ni (a) Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania , (b)Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na (c)Serikali ya Tanzania Bara. Muhungu alisema, “Ifahamike kwamba muundo wa Serikali tatu ni kuwapa mzigo wananchi, kwani wao ndiyo watatozwa kodi kubwa kuendesha Serikali hizo.
Source; Mhando A. (July 2013).Chadema, CCM, NCCR sasa wavutana kwa Muungano.Retrieved from Mwananchi
No comments:
Post a Comment