Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora

Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora
----------------------WE THANK AND APPRECIATE YOU FOR VISITING CHADEMA DIASPORA BLOG. AGAIN, THANK YOU!-----------------------

Monday, June 10, 2013

RASIMU YA KATIBA MPYA: Mbowe, Lipumba wafunguka



   RASIMU ya Katiba mpya iliyozinduliwa wiki iliyopita imeendelea kuzua mjadala mkali kuhusu muundo wa serikali tatu, safari hii ikiwaibua Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia (CHADEMA), Freeman Mbowe na mwenzake wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahimu Lipumba. Mwenyekiti wa Taifa wa CUF, Profesa Lipumba alisema rasimu hiyo inauweka Muungano shakani kwakuwa haina muongozo wowote wa michango kutoka washirika wa Muungano. Lipumba amebainisha kuwa ikiwa rasimu hiyo itapitishwa kama ilivyo, basi kutakuwa na mgogoro mkubwa wa fedha za kuendeshea Serikali ya Muungano, na kwamba hatma yake ni kuvunjika kwa Muungano.


      Kwa mujibu wa taarifa aliyoituma kwa vyombo vya habari jijini Dar es Salaam jana, Tume ya Warioba haikufanya uchambuzi wa kina wa kuweka mazingira thabiti ya kukuza uchumi na maendeleo kwa Watanzania wote. Taarifa hiyo ya Lipumba imebainisha kuwa mapendekezo katika rasimu ya katiba haiibani serikali kuilazimisha kuwa na utaratibu mzuri wa bajeti.Iliongeza upungufu mwingine ni kutozingatia kwa ukamilifu mambo ya uchumi, hususan kubainisha vyanzo vya mapato vya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kudhibiti bajeti yake. “Ukizingatia mambo ya Muungano yaliyoorodheshwa na rasimu, Serikali ya Muungano haina vyanzo vya mapato ya kodi. Ibara ya 215 imeeleza vyanzo vya mapato ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano vitakuwa:


        “(a) ushuru wa bidhaa; (b) maduhuli yatokanayo na taasisi za Muungano; (c) mchango kutoka kwa washirika wa Muungano; na (d) mikopo kutoka ndani na nje ya Jamhuri ya Muungano. Katiba haizungumzii taasisi yeyote ya kukusanya kodi. “Jambo la saba la Muungano ni ushuru wa bidhaa na mapato yasiyo ya kodi yatokanayo na mambo ya Muungano. Mambo sita ya Muungano hayalipi ushuru wa bidhaa. Biashara siyo jambo la Muungano kwa hiyo ushuru wa forodha, kodi za ongezeko la thamani (VAT), excise duty, kodi ya mauzo haziwezi kuwa suala la Muungano. “Mwaka wa fedha wa 2010/11 mapato ya serikali asilimia 34.3 ni ushuru wa forodha na VAT katika bidhaa zinazoagizwa kutoka nje, asilimia 18.6 kodi (VAT na Excise duty) za bidhaa zinazozalishwa ndani ya nchi, asilimia 29 kodi ya mapato, kodi na tozo nyingine asilimia 10.5, mapato ya halmashauri asilimia 2.8. Kodi ni chanzo cha mapato ya serikali lakini pia ni sera ya uchumi.

      “Viwango gani vya kodi havina athari kubwa kwa wananchi maskini na kupunguza motisha ya uzalishaji na uwekezaji? Serikali za washirika wa Muungano hawatakubali Serikali ya Muungano kutoza kodi katika maeneo ambayo siyo ya muungano,” amebainisha Profesa Lipumba. “Katika mambo ya usimamizi wa matumizi ya serikali na kazi za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali rasimu hii ime-‘copy’ na ku-‘paste’ katiba ya sasa bila kutathmini kama mfumo wa sasa unafanya kazi. Eneo hili linahitaji kufanyiwa uchambuzi zaidi,” amesisitiza katika taarifa hiyo. Upungufu mwingine alioubainisha Profesa Lipumba ni kuhusu Ibara za 213 na 214 zinazozipa uwezo serikali za Muungano, Tanganyika na Zanzibar kukopa fedha ndani na nje ya nchi, ambapo amesema kuwa utaratibu huo haufai kwani unaweza kuiingiza nchi kwenye mgogoro mkubwa wa madeni ikiwa serikali zote tatu zitashindana kukopa fedha ndani na nje ya nchi.

    “Lazima pawe na mwongozo wa kudhibiti mikopo na kuongezeka kwa deni la taifa. Nchi inaweza kuingizwa katika mgogoro wa madeni. Uhuru wa serikali zote tatu kukopo ndani na nje ya nchi unaweza kusababisha kukua kwa madeni kupita kiasi. “Serikali za washirika zina vyanzo vya mapato wakati Serikali ya Muungano haina. Kwa rasimu hii serikali za washirika ndizo zinazokopesheka na siyo serikali ya Muungano,” amebainisha. Pendekezo lingine alilolipinga ni suala la kuwepo Benki Kuu tatu. Profesa Lipumba amesema kuwa ingawa rasimu haisemi hivyo, lakini maelezo ya Ibara za 217 na 218 yanaonyesha bila chembe ya shaka kuwepo kwa Benki Kuu, kwani Ibara ya 217 inaanzisha Benki Kuu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Ibara ya 218 inaziruhusu serikali za washirika wa Muungano kuanzisha benki zao zitakazokuwa na majukumu kama ya Benki Kuu ya Muungano.

        “Kazi ya Benki Kuu ni kusimamia benki za biashara, sera za fedha na hasa riba, na mfumo wa malipo. Kazi hizi zitafanywa na benki za washirika wa Muungano. Moja ya chanzo cha mgogoro wa sarafu ya Euro ni kutokuwepo usimamizi wa pamoja wa benki za biashara katika ukanda unaotumia sarafu hiyo. Hivi sasa Ukanda wa Euro unajaribu kuandaa utaratibu wa pamoja wa kuifanya Benki Kuu ya Ulaya (ECB),” alisema.

Mbowe aifagilia

          Naye Mwenyekiti wa Taifa wa CHADEMA, Mbowe alisema sehemu kubwa ya Watanzania wanaoilalamikia rasimu hiyo ni makada na wafuasi wa CCM. Mbowe alitoa kauli hiyo jana mkoani Mbeya alipokuwa akiwahutubia wananchi wa Kata ya Iyela, kwenye mkutano wa kumnadi mgombea udiwani wa CHADEMA, Charles Mkela. Alisema wafuasi wa CCM wanalia sasa kwa kuwa wakati wa kuzitafuna fedha za wananchi kupitia mfumo wa Muungano unakaribia kumalizika. Alibainisha kuwa makada hao na chama chao ni vema wakajiandae kuwa chama cha upinzani baada ya uchaguzi mkuu 2015. “Wapo wanaotaka kusikika ndani ya Muungano wakisema hiki chao, chao ni chao na hawataki chao kiwe chetu ila wao wanataka chetu kiwe chao na chao kiwe chao, hapa lazima tuseme Tanganyika lazima,” alisema.
Mbowe alisema ukombozi wa Tanzania utafanikiwa iwapo wananchi watashiriki kwenye mchakato wa kuandaa katiba mpya ili kuondoa mwanya wa kimfumo unaowafanya watawala na marafiki zao wajineemeshe kwa fedha za wavuja jasho.

        Alisema mfumo uliopo ndiyo umezalisha matabaka makubwa ya walio nacho na wasionacho aliyoyapinga baba wa taifa hayati Julius Nyerere. Aliongeza kuwa katiba ijayo iliyopiganiwa na Watanzania kwa muda mrefu lazima izae Tanganyika mpya na inapaswa kuweka mbele maslahi ya wananchi masikini. Alisema miongoni mwa hoja za msingi zilizotolewa na CHADEMA ni kuwepo kwa katiba mpya ya Watanzania inayotambua uwepo wa Serikali ya Tanganyika. Mbowe alisema anaamini uwepo wa Tanganyika utachangia kuwaondoa watu kwenye lindi kubwa la umasikini kwa kulinda na kutumia vyema rasilimali za nchi kwa ajili ya wananchi wote.

           Tangu kutoka kwa rasimu hiyo idadi kubwa ya viongozi na wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wanaipinga kwa madai itachochea zaidi mfarakano kuliko kuunganisha Tanzania.Waziri wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta juzi alikaririwa akimlaumu Warioba na tume yake kwa kukubali mapendekezo ya serikali tatu, kupunguzwa kwa idadi ya mawaziri na kupunguza mambo ya Muungano kutoka 22 hadi saba.Wakati Sitta akielekeza makombora yake kwa Warioba, Kamati Kuu (CC) ya CCM inatarajia kukutana leo kujadili rasimu hiyo iliyozinduliwa na Makamu wa Rais, Gharib Mohamed Bilal mwanzoni mwa wiki hii.

Source: Tanzania Daima (June 2013).RASIMU YA KATIBA MPYA: Mbowe, Lipumba wafunguka. Retrieved from  Tanzania Daima

No comments: