MGAWANYO mbovu wa rasilimali za nchi pamoja na kupuuzwa kwa wananchi wa maeneo zinapopatikana rasilimali hizo, umetajwa kuwa chimbuko la vurugu zinazoshamiri katika sehemu nyingi nchini. Katika mjadala wa bajeti ya Wizara ya Mifugo na Maendeleo ya Uvuvi mwishoni mwa wiki, wabunge wengi walionesha kuchukizwa na kitendo cha serikali kutenga fedha kidogo kwa wizara hiyo ambayo ingeweza kuchangia uchumi wa taifa kwa asilimia 60. Wizara hiyo iliomba sh bilioni 163 lakini ikaidhinishiwa sh bilioni 47, jambo ambalo wabunge wengi hususan wanaotoka katika maeneo ya ufugaji na uvuvi walidai kuwa huo ni udhalilishaji.
Walisema kuwa wafugaji wa Tanzania wamekuwa kama yatima kutokana na kutokuwa na anayewajali kiasi cha kufikia hatua ya kuwalazimisha wafugaji kupunguza mifugo yao pasipo kujali kuwa ndiyo rasilimali yao wanayoitegemea. Katika hilo waliishushia lawama serikali ya CCM kuwa imekuwa chanzo cha vurugu hizo za kugombania rasilimali za nchi kutokana na hatua yake ya kutoweka utaratibu mzuri wa kuwanufaisha wananchi wanaotoka maeneo yenye rasilimali hizo. Mbunge wa Maswa Magharibu, John Shibuda (CCM), aliishambulia CCM akisema isivilaumu vyama vya upinzani kuhusu vurugu za kugombania rasilimali nchini kwa vile ndio chanzo cha ajenda ya vurugu hizo.
“Wafugaji na mifugo yao wanauawa, hakuna anayejali, serikali iko kimya lakini Mtwara wametikisa kwa kuonesha cheche wakapelekewa viwanda, je, sisi Wasukuma mnasubiri tufanye kama Mtwara ndipo viwanda vyetu vya pamba, nguo, ngozi vitakuja?” alihoji. Alisema kuwa maisha ya wafugaji yamekuwa kambi ya rushwa, kwani hakuna kikosi kazi cha kuwashughulikia, hivyo akawataka wawe makini na kura zao kwa vile ndiyo silaha yao 2015. “Vurugu za Mtwara ni cheche, lakini vurugu za wafugaji ni za kimya kimya, ila zitakuwa na madhara makubwa kwa vile hawaoni uwepo wa rasilimali hizo kwao,” alisema.
Mbunge wa Dole, Sylvester Mabumba (CCM) alimtaka Waziri wa Mifugo, Dk. David Mathayo, ajiuzulu akidai kuwa amekosa mikakati na ubunifu katika kuikwamua wizara hiyo ikiwa ni pamoja na kuwasaidia wafugaji. “Wafugaji hawa wakati mwingine ndizo kura za CCM, hivyo kama serikali haitazungumza nao na kuwatatulia matatizo yao, 2015 haiko mbali wataiangusha CCM na kuwapa wapinzani ambao watakuwa wanajibu hoja zao na kuwapa matumaini,” alisema. Wabunge wengine wakiwamo Ibrahim Sanya (Mji Mkongwe), Richard Ndassa (Sumve), Sylvester Mabumba (Dole), Rose Kamili (Viti Maalumu), Danstan Kitandula (Mkinga) na Rukia Kimwaga, waliitaka serikali itafute fedha mahali popote na kuiongezea wizara hiyo sh bilioni 40. Hata wakati Bunge limekaa kama kamati kupitia mafungu, wabunge hao waliendelea kuonesha msimamo wa kutaka wizara hiyo iongezewe fedha kiasi cha sh bilioni 40 vinginevyo wangeshika mshahara wa waziri.
Sitta amnusuru Mathayo
Serikali baada ya kuona hali hiyo, Waziri wa Ushirikiano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Samuel Sitta, ambaye alikuwa akikaimu nafasi ya Waziri Mkuu alilazimika kusimama kutuliza upepo wa wabunge. Alisema kuwa serikali inatambua hoja nzito za wabunge kuhusu sekta ya wafugaji, jambo alilodai kuwa liliwasaidia kupata darasa. “Niwachukue kidogo nyuma ya pazia kuhusu hoja hii ili muone nini tumefanya baada ya kusikiliza hoja zenu. Rais Kikwete yuko Tokyo, Japan, Waziri Mkuu yuko Dar es Salaam na Waziri wa Fedha yuko Morocco,” alisema.
Alifafanua kuwa pamoja na kutokuwepo kwa viongozi hao, baada ya kuwasiliana nao alizungumza na Naibu Waziri wa Fedha ambaye alisema kuwa alifanya kazi kubwa usiku kucha kujaribu kutafuta fedha hiyo na kisha alifanikiwa kupata sh bilioni 20. Sitta alisema kuwa japo kiwango hicho hakijakidhi hitaji bado wanazungumza na viongozi hao wakuu ambao watajadiliano kwa siku tatu kuanzia Juni 7 mwaka huu. “Hoja imekubalika, kiwango tulichoweza kupata ni sh bilioni 20 na hizi tumejaribu kufanya kama tulivyofanya kwenye kutafuta fedha za kuongeza kwenye bajeti ya Wizara ya Maji kwa kupunguza matumizi mengineyo kwenye baadhi ya wizara,” alisema.
Source; Kamkara E. (May 2013). Rasilimali zawagawa wabunge. Retrieved from Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment