TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI:
09/06/2013
MAONI YA AWALI YA MWENYEKITI WA CUF KUHUSU
RASIMU YA KATIBA MPYA
UTANGULIZI;
Kwanza naipongeza Tume ya Jaji Warioba kwa kazi
kubwa waliofanya ya kuratibu maoni na kuja na mapendekezo ya katiba mpya ambayo
hayakushinikizwa na matakwa ya Chama tawala cha CCM. Tume imeonyesha ujasiri
mkubwa na hakika wahafidhina wa chama hicho watachukia sana.
Mambo mengi yaliyopendekezwa na Chama Cha
Wananchi CUF yameingizwa katika Rasimu ya Katiba. Mambo hayo ni pamoja na mfumo
wa Muungano wa serikali tatu, kuruhusiwa mgombea binafsi, Rais kutangazwa
kushinda akipata zaidi ya asilimia 50 ya kura zote zilizopigwa la sivyo
uchaguzi urudiwe kwa wale wawili walio ongoza kwa kura, Tume huru ya uchaguzi,
Mawaziri kutokuwa wabunge, Spika kutokuwa mbunge, haki za watu wenye ulemavu,
haki za binadamu na mengine mengi.
Hata hivyo mambo mengi muhimu kama vile
umilikaji wa ardhi, maliasili na rasilimali za nchi kutumiwa kwa manufaa ya
wananchi wote, elimu, afya, mazingira ya kukuza uchumi unaoleta neema kwa
wananchi wote, wajibu, uwezo na uhuru wa serikali za mitaa hayajaingizwa ndani
ya katiba kikamilifu kwani rasimu ya katiba imeshughulikia mambo ya muungano.
Mambo ya Muungano ni saba: Katiba na mamlaka ya
Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania, Ulinzi na Usalama wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Uraia na
Uhamiaji, Sarafu na Benki Kuu, Mambo ya Nje, Usajili wa Vyama vya Siasa
na Ushuru wa bidhaa na mapato yasiyo ya kodi yatokanayo mambo ya Muungano.
Mwongozo wa Tume kuhusu utoaji wa maoni
ulijikita katika maeneo yafuatayo; Misingi na Maadili ya
Kitaifa, Madaraka ya Wananchi, Muundo wa Nchi na Taifa ndani ya Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania, Haki za Binadamu na Wajibu wa Wananchi, Ardhi,
Maliasili na Mazingira, Mihimili ya Nchi (Ardhi, Watu na Utawala), Mihimili ya
Utawala (Serikali, Bunge na Mahakama), Serikali za Mitaa, Muundo na Mamlaka yake,
Vyombo vya Ulinzi na Usalama. Mambo mengi muhimu kwa mwananchi wa
kawaida ikiwa ni pamoja na serikali za mitaa, umilikaji wa ardhi, haki za
huduma za afya na elimu, na matumizi ya maliasili hayajaingizwa katika katiba
hii na yanatarajiwa kuingizwa kwenye katiba ya Tanzania Bara. Rasimu ya katiba
kwa wananchi wa Tanzania Bara haijakamilika mpaka Rasimu ya katiba ya Tanzania
Bara itakapokuwa tayari. Hotuba ya uzinduzi wa katiba ya Jaji Warioba
haikulifafanua suala hili. Hakuna mantiki ya kupigia kura ya maoni katiba ya
jamhuri ya muungano bila kuwa na katiba ya Tanzania Bara kwa upande wa bara na
marekebisho ya katiba ya Zanzibar isikinzane na katiba ya jamhuri ya muungano
kwa upande wa zanzibar. Katiba ya Tanzania Bara na katiba ya Zanzibar iwe ni
sehemu ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano.
Kuwepo kwa rasimu ya katiba ya Tanzania Bara
kutasaidi kuondoa kuweka asasi mbili au tatu zinazofanya kazi moja. Kwa mfano
Tume ya Uchaguzi, Jeshi la Polisi, Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali,
Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa ya serikali ya Muungano ikafanya kazi
pia kwa serikali ya Tanzania Bara ikiwa wananchi wa Tanzania Bara hawana tatizo
na utaratibu huo.
MAPENDEKEZO YA JUMLA;
1. Pendekezo langu la msingi ni kwamba, kura ya
maoni isubiri kukamilishwa kwa rasimu ya katiba ya Tanzania Bara na zote
zikajadiliwa na wananchi kwa pamoja. Sina pingamizi kuwa Wajumbe wa Tume wa
Tanzania Bara waandae rasimu ya Katiba ya Tanzania Bara, na wajumbe wa Zanzibar
waandae mapendekezo ya marekebisho ya katiba ya Zanzibari ili isikinzane na
katiba ya Jamhuri ya Muungano. Muda wa kuyatekeleza haya na kubadilisha sheria
zifuate matakwa ya katiba mpya kabla ya uchaguzi mkuu wa 2015 haupo. Serikali
imeeleza kuwa haina nia na Rais Kikwete hataki kabisa kujiongezea muda kwa
kisingizio cha kukamilisha utaratibu wa katiba mpya. Wananchi pia wamechoka
wanataka mabadiliko.
2. Katika masuala ya haki za binadamu ningependa
Katiba itamke wazi kuwa mwanamke mjamzito ana haki ya kupata lishe bora na
huduma za afya wakati wa ujauzito na kujifungua. Vile vile watoto bila kujali
uwezo wa wazazi wao wana haki ya lishe bora, huduma za msingi za afya na elimu
inayomuandaa mtoto kukabiliana na changamoto za maisha.
3.
Pendekezo la Rasimu ya Katiba ya kuwepo Tume
Huru ya Uchaguzi ni la msingi. Pendekezo hili lianze kufanyiwa kazi mara moja
ili kufanya mabadiliko ya sheria ya uchaguzi na Tume ya uchaguzi ili uchaguzi
wa 2015 uendeshwe na Tume iliyo Huru kweli. Mchakato wa mabadiliko ya katiba
utaendelea baada ya uchaguzi mpaka ukamilike na sheria husika kufanyiwa
mabadiliko.
4.
Siyo lazima Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti wa
Tume ya Uchaguzi wawe watu waliyewahi kushika wadhifa wa Jaji wa Makakama ya
Juu, Mahakama ya Rufani au Mahakama Kuu na ameshika wadhifa huo kwa kipindi
kisichopungua miaka mitano kama Rasimu ya Katiba inavyoelekeza katika
kifungu 181(4). Masuala ya kusimamia uchaguzi ni ya utawala na uendeshaji
kuliko ya kutafsiri sheria. Majaji siyo wasimamizi na mameneja wazuri wa
utawala na logistics. Nchini Ghana mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ambaye
kafanya vizuri siyo Jaji bali ni Profesa wa sayansi ya siasa – Jaji Lewis
Makame kwa miaka zaidi ya 15 na hakufanikiwa kujenga Tume ya Uchaguzi yenye
uwezo na kuaminika. Ni vyema wigo wanaoweza kuomba kuwa wenyeviti wa Tume
ukapanuliwa na kuingiza wenye uzoefu wa utawala na logistics. Tume ina
mwanasheria wake ambaye ataelekeza na kushauri masuala yahusiyo sheria.
5.
Kasoro kubwa ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano ni
kwamba haina nyenzo za kutimiza malengo muhimu ya katiba yenyewe. Ibara ya 6(b)
imeeleza kuwa “lengo kuu la Serikali litakuwa ni maendeleo na ustawi wa
wananchi.” Mambo ya uchumi yote isipokuwa Benki Kuu na sarafu hayamo katika
orodha ya mambo ya Muungano. Hata suala la uratibu wa sera za uchumi halimo.
Ibara ya 7(2) inaeleza “mamlaka ya nchi na vyombo vyake
vinawajibika kuelekeza sera na shughuli zake zote kwa lengo la kuhakikisha
kwamba: (c)Serikali itahakikisha kuwa shughuli zinazofanywa zinatekelezwa kwa
njia ambazo zitahakikisha kwamba utajiri wa Taifa unaendelezwa, unahifadhiwa na
unatumiwa kwa manufaa ya wananchi wote kwa jumla na pia kuzuia mtu kumnyonya
mtu mwingine; (d)ardhi ikiwa rasilimali kuu na msingi wa Taifa, inalindwa, inatunzwa
na kutumiwa na wananchi wa Tanzania kwa manufaa, maslahi na ustawi wa kizazi
cha sasa na vizazi vijavyo; (e)maendeleo ya uchumi wa Taifa yanapangwa na
kukuzwa kwa ulinganifu na kwa pamoja na kwa namna ambayo inawanufaisha wananchi
wote; (f)kila mtu mwenye uwezo wa kufanya kazi anafanya kazi, na kazi maana
yake ni shughuli yoyote ya halali inayompatia mtu kipato chake; (j)utajiri wa
rasilimali na maliasili za Taifa unaelekezwa katika kuleta maendeleo, kuondoa
umaskini, ujinga na maradhi”. Serikali ya Muungano haina nyenzo ya
kusimamia mambo hayo.
6.
Ibara ya 11 inazungumzia utekelezaji wa malengo
ya taifa. Kifungu (2) kinaeleza “Serikali itatoa taarifa Bungeni si
chini ya mara moja katika kila mwaka, kuhusu hatua zilizochukuliwa na mamlaka
ya nchi ili kuhakikisha utekelezaji wa malengo ya Taifa yaliyoainishwa katika
Katiba hii. (c) kiuchumi, Serikali inachukua hatua zinazofaa ili: (i) kuwaletea
wananchi maisha bora kwa kuondoa umaskini; (ii) kuhakikisha kwamba shughuli za
Serikali zinatekelezwa kwa njia ambazo zitahakikisha kuwa utajiri wa Taifa
unaendelezwa, unahifadhiwa na unatumiwa kwa manufaa ya wananchi wote kwa jumla
na pia kuzuia mtu kumnyonya mtu mwingine; (iii) kuweka mazingira bora kwa ajili
ya kuanzisha na kuendeleza vyombo vya uwakilishi wa wakulima, wafugaji na
wavuvi; (iv) kuweka mazingira bora ya kufanya biashara na kukuza fursa za
uwekezaji; (v) kuweka mazingira bora kwa ajili ya kukuza kilimo, ufugaji na
uvuvi kwa kuhakikisha kuwa wakulima, wafugaji na wavuvi wanakuwa na ardhi na
nyenzo kwa ajili ya kuendeleza shughuli zao; (vi) kuweka mazingira bora ya
uzalishaji wa mazao kwa wakulima, wafugaji na wavuvi, utafutaji na uendelezaji
wa masoko ya mazao yao; (vii) kuweka utaratibu mzuri wa upangaji na usimamiaji
wa mizania ya bei za mazao na pembejeo; (viii) kuimarisha na kuendeleza
uwekezaji wa ndani, upatikanaji wa pembejeo za kilimo, maeneo ya ufugaji na
vifaa vya uvuvi; (ix) kuhakikisha kunakuwa na upatikanaji wa fursa na nafasi za
wazi kwa watu wote na kuanzisha shughuli za kiuchumi na kukuza mazingira yaliyo
bora kwa ajili ya kuhamasisha sekta binafsi katika uchumi; (x) kuhakikisha kuwa
kila mtu mwenye uwezo wa kufanya kazi anapata fursa ya kufanya kazi, kwa maana
ya kufanya shughuli yoyote halali inayompatia kipato; (xi) kuweka utaratibu unaofaa
kwa ajili ya kufanikisha utekelezaji wa haki ya mtu kujipatia elimu na kuwa
huru kupata fursa sawa ya kutafuta elimu katika fani anayoipenda hadi kufikia
upeo wowote kulingana na stahili na uwezo wake. Mambo yote haya siyo ya
muungano”. Serikali ya Muungano itawezaje kutoa taarifa Bungeni kwa
mambo ambayo haiyasimamii.
7.
Ukizingatia mambo ya Muungano yaliyoorodheshwa
na Rasimu, Serikali ya Muungano haina vyanzo vya mapato ya kodi. Ibara
ya 215 imeeleza Vyanzo vya mapato ya Serikali ya Jamhuri ya
Muungano vitakuwa:“(a) ushuru wa bidhaa; (b) maduhuli yatokanayo na taasisi
za Muungano; (c) mchango kutoka kwa Washirika wa Muungano; na (d) mikopo kutoka
ndani na nje ya Jamhuri ya Muungano”. Katiba haizungumzii taasisi
yeyote ya kukusanya kodi. Jambo la saba la muungano ni Ushuru wa
bidhaa na mapato yasiyo ya kodi yatokanayo na mambo ya Muungano. Mambo sita ya
Muungano hayalipi ushuru wa bidhaa. Biashara siyo jambo la Muungano kwa
hiyo ushuru wa forodha, kodi za ongezeko la thamani (VAT), excise duty, kodi ya
mauzo haziwezi kuwa suala la Muungano. Mwaka wa fedha wa 2010/11 Mapato ya
serikali Asilimia 34.3 ushuru wa forodha na VAT katika bidhaa zinazoagizwa toka
nje, Asilimia 18.6 kodi (VAT na Excise duty) za bidhaa zinazozalishwa ndani ya
nchi. Asilimia 29 kodi ya mapato. Kodi na tozo nyingine asilimia 10.5, Mapato
ya halmashauri asilimia 2.8. Kodi ni chanzo cha mapato ya serikali lakini pia
ni sera ya uchumi. Viwango gani vya kodi havina athari kubwa kwa wananchi
maskini na kupunguza motisha ya uzalishaji na uwekezaji? Serikali za washirika
wa Muungano hawatakubali Serikali ya Muungano kutoza kodi katika maeneo ambayo
siyo ya muungano. Katiba haina muongozo wowote wa michango toka
washirika wa Muungano. Rasimu hii ilivyo ikipitishwa kutakuwa na mgogoro mkubwa
wa fedha za kuendeshea serikali ya Muungano na hatma yake itakuwa Muungano
kuvunjika.
8.
Katika mambo ya uchumi Tume haikufanya uchambuzi
wa kina wa kuwa na katiba inayojenga mazingira mazuri ya kukuza uchumi unaoleta
maendeleo kwa wote. Katiba haiibani serikali iwe na utaratibu mzuri wa bajeti.
Katika mambo ya usimamizi wa matumizi ya serikali na kazi za Mdhibiti na
Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali rasimu hii ime –“copy” na
ku-“paste” katiba ya sasa bila kutathmini kama mfumo wa hivi sasa
unafanya kazi. Eneo hili linahitaji kufanyiwa uchambuzi zaidi.
9.
Ibara za 213 na 214 zinawapa uwezo Serikali ya
Jamhuri ya Muungano na Serikali ya Mshirika wa Muungano “zitakuwa na
mamlaka ya kukopa fedha ndani na nje ya Jamhuri ya Muungano kwa ajili ya
kugharamia shughuli zilizo chini ya mamlaka yake.” Katika utaratibu
huu nchi inaweza kughubikwa na madeni ikiwa serikali tatu zitashindana kukopa
ndani na nje ya nchi. Lazima pawe na mwongozo wa kudhibiti mikopo na
kuongezeka kwa deni la taifa. Nchi inaweza kuingizwa katika mgogoro wa
madeni. Uhuru wa serikali zote tatu kukopa ndani na nje ya nchi inaweza
kusababisha kukua kwa madeni kupita kiasi. Serikali za washirika zina
vyanzo vya mapato serikali ya muungano haina. Kwa Rasimu ya Katiba hii serikali
za washirika ndizo zinazokopesheka na siyo serikali ya muungano.
10.
Rasimu ya Katiba bila kusema hivyo inapendekeza
kuwepo na Benki Kuu tatu. Ibara ya 217 inaeleza“Kutakuwa na Benki Kuu ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itakayojulikana kuwa “Benki Kuu” ambayo itakuwa
na majukumu yafuatayo: (a) kutoa sarafu, kudhibiti na kusimamia mzunguko wa
sarafu; (b) kuandaa na kusimamia Sera na Mipango inayohusiana na sarafu; (c)
kudhibiti na kusimamia masuala ya fedha za kigeni; na (d) kusimamia Benki za
Washirika wa Muungano.” Ibara ya 218 inaeleza “Serikali za
Washirika zitakuwa na Benki zitakazokuwa najukumu la kutunza akaunti ya fedha
za Serikali husika, kusimamia Sera za Kifedha na benki za biashara katika
mamlaka zao.” Kazi ya Benki Kuu ni kusimamia Benki za Biashara, sera
za fedha na hasa riba, na mfumo wa malipo. Kazi hizi zitafanywa na Benki za
Washirika wa Muungano.Moja ya chanzo cha mgogoro wa Euro ni
kutokuwepo usimamizi wa pamoja wa Benki za biashara. Hivi sasa Ukanda wa Euro
unajaribu kuandaa utaratibu wa pamoja wa kuifanya Benki Kuu ya Ulaya (ECB)
kusimamia Benki za Biashara. Kama tuna sarafu moja tuwe na Benki Kuu
moja. Benki Kuu isiposimamia benki za biashara haitaweza kudhibiti na kusimamia
ujazi wa fedha (money supply)
11.
Ibara ya 105 inaeleza “(2) Wajumbe wa
Bunge watakuwa wa aina zifuatazo: (a) Wabunge waliochaguliwa kuwakilisha
majimbo ya uchaguzi; (3) Kwa madhumuni ya Ibara ya ndogo (2)(a), kila mkoa kwa
upande wa Tanzania Bara na wilaya kwa upande wa Zanzibar, itakuwa ni jimbo la
uchaguzi”. Nini vigezo vya kufanya mikoa na wilaya kuwa majimbo ya
uchaguzi? Utaratibu wa kuanzisha mikoa na wilaya ni wa serikali washirika au wa
Serikali ya Muungano? Hata hivyo ibara ya 180 (a) inaeleza “mamlaka
zinazosimamia uchaguzi kutangaza majimbo kwa madhumuni ya uchaguzi wa wabunge.” Majimbo
ya uchaguzi yataundwa na Tume au tayari yameishatajwa na katiba?
12.
Mamlaka ya Bunge katika kuisimamia serikali
katika masuala ya bajeti ni madogo. Ibara ya 107 (2) inaeleza, “katika
kutekeleza majukumu yake, Bunge litakuwa na madaraka yafuatayo: (c) kujadili
mgawanyo na kuidhinisha matumizi ya fedha kwa Wizara, taasisi na mashirika ya
Serikali; (d) kujadili utekelezaji wa kila Wizara wakati wa Mkutano wa Bunge wa
kila mwaka wa bajeti; (e) kujadili na kuidhinisha mpango wowote wa muda mrefu
au wa muda mfupi unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali katika Jamhuri ya
Muungano; (f) kutunga sheria ya kusimamia utekelezaji wa mpango wowote wa muda
mrefu au muda mfupi”. Hata hivyo Mambo ya Muungano hayahusishi
Mpango wa Maendeleo wa taifa.
13.
Ibara ya 177 inaeleza “Bila ya kuathiri
masharti ya Katiba hii, utumishi wa umma na uongozi katika Jamhuri ya Muungano
utazingatia misingi kwamba utoaji wa ajira na uteuzi wa viongozi utakuwa kwa
uwiano baina ya Washirika wa Muungano, kwa kuzingatia weledi na taaluma katika
eneo au nyanja husika.” Nini maana ya uwiano? Je maana yake nusu ya
wafanyakazi watoke Zanzibar na nusu watoke Tanzania Bara?
14.
Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa ni
muhimu iwemo ndani ya Katiba. Rasimu haina asasi hii muhimu ya usimamizi na
uwajibikaji. Tunarudia pendekezo letu kuwa Katiba ieleze kuwepo kwa Tume ya
Kupambana na Kuzuia Rushwa na kueleza kazi zake. Tume hii iwe na uhuru wa kupeleka
kesi mahakamani bila idhini ya Mkurungezi wa Mashtaka ya Umma (DPP).
15.
Katiba imejaa imani kuwa vyeti vya shule na vyuo
ndiyo elimu na hekima na kwa kutumia sifa za vyeti vya elimu inawanyima haki
wananchi wengi kushiriki na kuwania uongozi katika ngazi mbalimbali. Ibara ya
75(f) inaeleza sifa moja ya Rais kuwa “anayo angalau shahada ya kwanza
ya chuo kikuu kinachotambuliwa kwa mujibu wa sheria za nchi.” Cheti
cha shahada siyo kipimo kizuri cha elimu, hekima na uwezo wa kuongoza. Bill
Gates hakumaliza masomo yake ya shahada ya kwanza Chuo Kikuu cha Harvard.
Aliona anapoteza muda akaanzisha kampuni ya Microsoft. Kama Bill Gates angekuwa
Mtanzania, Rasimu ya Katiba ingemzuia kugombea Urais kwa kuwa hana cheti cha
shahada. Steve Jobs pia hakumaliza na kupata shahada badala yake alifanya
masomo aliyoyaona muhimu na kuanzisha kampuni ya Apple. Hapa Tanzania sidhani
kama Said Salim Bakhresa ana shahada yeyote. Taarifa iliyoko Wikipedia na
gazeti la Forbes inaeleza aliacha shule akiwa na miaka 14 na akaanza biashara
ya kuuza potato mix. Kama taarifa hii ni kweli basi huenda hata darasa la 8
hakumaliza. Lakini uwezo, uzoefu na elimu itokanayo na uzoefu wa kazi ni kubwa
kuliko hata mtu mwenye PhD ya biashara. Mzee Bakhresa hana sifa ya kugombea
Urais kwa kuwa hana shahada ya kwanza. Sina uhakika kama Freeman Mbowe ana
shahada. Ikiwa hana siyo haki kumzuia kugombea Urais kwa sababu hiyo. Mwache
agombee na wengine wajenge hoja hana maadili na uwezo wa kuongoza nchi. John
Major alikuwa Waziri Mkuu wa Uingereza mwaka 1991 – 97 hana shahada ya Chuo
Kikuu. Kuna watu wengi wenye shahada nyingi lakini hawana hekima wala busara.
Vyeti vingi vys siku hizi ni vya kughushi na inawezakana kabisa usiweze
kugundua kuwa vimeghushiwa. Sifa ibakie kusoma na kuandika kiswahili. Wache
wapiga kura waamue kuwa elimu ya mgombea haitoshi kumfanya kuwa Rais. Sifa ya
elimu ya mgombea ubunge ni kidato cha nne. Rasimu itamzuia Mzee Bakhresa hata
kugombea ubunge kwa sababu hana cheti cha kidato cha nne. Kuna Watanzania wengi
waliomaliza darasa la nane au la saba la zamani wenye elimu bora kuliko
aliyemaliza kidato cha nne hivi karibuni. Kuna watu wengi wamemaliza darasa la
7 wana uzoefu mzuri na wana uwezo wa kuwawakilisha wananchi katika Bunge.
Vigezo vya vyeti vya elimu visitumiwe kuwanyima wananch haki zao za kisiasa.
Kigezo cha shahada pia kimeingizwa katika uteuzi wa Mawaziri. Watu wenye uzoefu
na uwezo wa uongozi lakini hawana vyeti vya shahada hawawezi kuteuliwa kuwa
mawaziri. Nastaajabu hii obsession na vyeti imetoka wapi?
16.
Ibara ya 31 inazungumzia Dini. “(1)
Kila mtu anao uhuru wa mawazo, imani na uchaguzi katika mambo ya imani ya dini
na anao uhuru pia wa kubadilisha dini, imani yake au kutokuwa na imani na dini.
Kifungu cha (5) Ni marufuku kwa mtu, kikundi au taasisi ya dini kutumia uhuru
wa kutangaza dini kwa kukashifu imani na dini nyingine, kujenga chuki au
kuchochea vurugu na ghasia kwa madai ya kutetea imani au dini”. Tatizo
ya ibara hii ni tafsiri ya kukashifu. Imani za dini zina tofauti. Imani ya
msingi ya dhehebu moja inaweza kuwa kufuru kwa dhehebu lingine na ikatafsiriwa
kuwa ni kukashifu. Kuna masuala ambayo jamii inapaswa kujenga maelewano ya
kuvumiliana na kuheshimiana na kukubali tofauti za imani bila kugombana.
Kuliweka katika katiba inaweza kujenga chuki na ikatafsiriwa kuwa inalenga
kundi fulani. Ibara na 5 imelenga kikundi au taasisi ya dini. Je
vikundi ambavyo siyo vya dini vinaruhusiwa kukashifu imani na dini?
17.
Serikali ya Muungano itakuwa na Jeshi la ulinzi,
Polisi na Usalama wa Taifa. Serikali za washirika zinaruhusiwa kuwa na polisi
na usalama wa taifa. Inawezekana serikali ya Muungano ikaongozwa na Chama A,
Serikali ya Zanzibar ikaongozwa na chama B na serikali ya Tanzania Bara
ikaongozwa na chama C. Serikali zote zina polisi na usalama wa taifa wake,
haitakuwa kasheshe ndani ya nchi? Sina uhakika katiba imeweka bayana utaratibu
wa kuzuia migongano kati ya vyombo vya Muungano na vyombo vya Washirika.
Haya ni mapendekezo ya awali tu, mapendekezo
mengine yataendelea kutolewa kwa kadri ambavyo tutazidi kuichambua rasimu hii
ya katiba. Natoa wito kwa Watanzania wote kuhakikisha kuwa wanaitafuta rasimu
hii bila kuchoka, kuisoma na kuielewa na kuendelea kutoa mapendekezo yao kwa
tume ya mabadiliko ya katiba iwe ndiyo lengo kuu.
Kwa sababu tume imetangaza kuwa itachapisha
rasimu katika magazeti ya serikali kwa maana ya HABARI LEO na ZANZIBAR LEO,
tunaona kama huku ni kuififisha rasimu isiwafikie watanzania wengi zaidi.
Kuna haja ya dhati, tume ikaitangaza rasimu
katika magazeti mbalimbali ya kila wiki na ya kila siku ili kuhakikisha kuwa
rasimu imefikiwa na imesomwa na watanzania wengi. Na nakala zitakazobakia
“returns” baada ya mauzo ya magazeti husika tume izinunue nakala hizo na
izisambaze kwa utaratibu maalum mikoani na vijijini.
Ni ushauri wetu kwa Tume pia kwamba baada ya
kazi kubwa waliyoifanya, wasikubali kuyumbishwa na wahafidhina wasiopenda
mabadiliko wanaotokana na CCM. Tume iwe na msimamo na iangalie wananchi
wanataka nini na itetee masuala ya msingi na ya maslahi ya wananchi ambayo
inaona ni muhimu yakatetewa kwa maslahi ya taifa na hasa kwa kuzingatia matakwa
ya wananchi.
Na mwisho, Tume ihakikishe kuwa masuala haya
tunayoyashauri kwa awamu yanapewa uzito na tafakuri pana ili kuipata katiba
itakayokuza uchumi imara, kuongeza ajira kwa vijana na kuinua maisha ya
wananchi wa kipato cha chini.
“Mungu Ibariki Tanzania”
Prof. Ibrahim Haruna Lipumba.
Mwenyekiti,
09 Juni 2013, Dar Es Salaam.
No comments:
Post a Comment