JESHI la Polisi wilayani Igunga, mkoani Tabora,
linashikilia malori nane mali ya Kampuni ya Kichina ya Sun Shine Mining Ltd,
kwa kosa la kusafirisha shehena ya mchanga wenye madini bila kibali cha
Serikali. Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana, Mkuu wa Wilaya
ya Igunga, Elibariki Kingu, alisema magari hayo yalikamatwa juzi saa 3 asubuhi,
mjini Igunga. Alisema magari hayo kila moja lina shehena ya
mchanga na yalikamatwa yakiwa njiani kuelekea wilayani Chunya, mkoani Mbeya.
“Tunawashukru mno wananchi ambao walitoa taarifa
polisi, ambao walifanikiwa kuyakamata magari haya, tumekamata malori nane
ambayo yamebandikwa namba bandia za usajili,” alisema DC Kingu. Alisema magari hayo, yalikuwa yakiendeshwa na
madereva wa Kitanzania, ambao walikuwa wakisindikizwa na raia wawili wa
Kichina. Aliwataja Wachina hao kuwa ni Zhu Chun Lei na Xang
Lei, ambao hata hivyo, walishindwa kujieleza kutokana na kuzungumza lugha ya
kwao tu.
Alisema kwa mujibu wa kibali walichokuwa nacho,
kinaonyesha muda wa matumizi umekwisha tangu Mei 16, mwaka huu. Alisema kibali hicho, chenye namba BL/SHY/0027,
kiliruhusiwa kusafirisha tani 300 za mchanga kutoka Igunga kwenda Chunya. “Jambo la kusikitisha ni kwamba, kibali hiki
matumizi yake yamemalizika tangu Mei 16, mwaka huu, lakini hawa jamaa
wameendelea kukitumia, huu ni wizi wa wazi,” alisema DC Kingu.
Alisema kibali hicho, kinaonyesha kilitolewa na mtu
aliyetajwa kwa jina la Maganga Z.Maganga, ambaye anadaiwa kuwa mmiliki. “Mpaka sasa hatujafanikiwa kumkamata Maganga,
polisi wanaendelea na kazi ya kumsaka ili aje atoe taarifa za kina za tukio
hili, tumebaini inawezekana Wachina hawa wanamtumia Maganga kama kivuli tu,”
alisema DC Kingu.
Alisema malori hayo, yamekamatwa yakiwa na namba
bandia za usajili ambazo ni T 420 CJL, T314 CJL, T320 CJL, T415 CJL, T407 CJL,
T591 CJL na T423 CJL. Alisema namba halali za magari hayo ni T584 CJL,
T597 CJL, T597 CJL, T 598 CJL, T586 CJL, T633 CJL na T595 CJL
Source; Karedia
K. (May 2013). Igunga. Retrieved from Mtanzania
No comments:
Post a Comment