Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora

Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora
----------------------WE THANK AND APPRECIATE YOU FOR VISITING CHADEMA DIASPORA BLOG. AGAIN, THANK YOU!-----------------------

Wednesday, June 12, 2013

Maajabu ya Lwakatare



        TUKIO la kukamatwa kwa Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Wilfred Lwakatare na kuachiwa kwake kwa dhamana, limeweka historia ya ajabu katika maisha yake. 
Lwakatare alikamatwa Machi 11 mwaka huu kwa tuhuma za makosa ya ugaidi kabla ya kufutwa na kubaki na shitaka moja la kupanga njama za kutaka kumdhuru Mhariri Mtendaji wa gazeti la Mwananchi, Denis Msacky. Jana,  Juni 11, Lwakatare aliachiwa kwa dhamana ikiwa ni tarehe ile ile inayofanana na siku aliyokamatwa, yaani Machi 11.

           Jambo jingine la kushangaza, Lwakatare alikamatwa ikiwa ni siku sita zimepita tangu kutokea kwa tukio la kuvamiwa na kushambuliwa kwa Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri nchini (TEF) na Mhariri Mtendaji wa magazeti ya New Habari 2006, Absalom Kibanda na jana alipata dhamana ikiwa ni siku ya sita tangu Kibanda aliporejea nchini akitokea nchini Afrika Kusini kwa matibabu. Akizungumza na waandishi wa habari nje ya mahakama mara baada ya kupata dhamana, huku akiwa ameshika kitabu kilichoandikwa ‘Tough Time Never Last, But Tough People Do’, Lwakatare alisema katika yote yaliyotokea anamuachia Mwenyezi Mungu.


     Alisema ingawa kwa sasa hawezi kuzungumza aliyonayo moyoni mpaka atakapokutana na kujadiliana na viongozi wa chama chake, aliahidi kufichua siri iliyo nyuma ya tukio lake kesho. “Kama alivyosema Kibanda kuwa ana mengi ya kuzungumza, nami pia nina mengi lakini kwanza lazima nishauriane na wanasheria wangu pamoja na viongozi wa chama, naahidi kufanya hivyo siku ya Alhamisi,” alisema Lwakatare. Baada ya kutoka kuzungumza na waandishi wa habari, Lwakatare aliongozana na baadhi ya wakurugenzi wa CHADEMA kuelekea makao makuu ya chama hicho huku wafuasi wao wakishinikiza msafara wa magari utembee taratibu kwa ajili ya watu kuweza kumsindikiza.

Wakili wake ataka uhuru zaidi wa mahakama

        Mmoja wa mawakili wanaomtetea Lwakatare, Peter Kibatala, alisema msingi wa dhamana ya Lwakatare ni matokeo ya ujasiri wa Mahakama Kuu chini ya Jaji Lawrence Kaduri kuamua kumfutia mteja wao kesi ya ugaidi aliyofunguliwa awali. Kibatala alitahadharisha kuwa wakati huu wa kujadili rasimu ya Katiba mpya, wananchi wasijikite kujadili mambo ya Muungano na uwepo wa serikali tatu, badala yake wapiganie uhuru wa mahakama uwe mkubwa zaidi. Lwakatare alipata dhamana baada ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Kisutu, Aloyce Katemana, kusema dhamana yake iko wazi ikiwa atatimiza masharti.

       Masharti waliyowekewa pamoja na Ludovic Joseph ni kuwa na wadhamini wawili watakaosaini dhamana ya sh mil. 10 kila mmoja, pamoja na washtakiwa kukabidhi mahakamani hapo hati zao za kusafiria. Sharti jingine ni marufuku kutoka nje ya Jiji la Dar es Salaam bila ruhusa ya mahakama. Kutokana na masharti hayo, wadhamini wa Lwakatare waliweza kuyatimiza huku mshitakiwa mwenzake katika kesi hiyo, Ludovick, akishindwa kutimiza masharti, hivyo kurejeshwa rumande hadi Juni 24, mwaka huu. Wakati Ludovick akirejeshwa rumande, baadhi ya wafuasi wa CHADEMA waliofurika katika viwanja vya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, walisikika wakimtaka Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mwingulu Nchemba, kumuwekea dhamana mtuhumiwa huyo.

          Kelele za wanachama hao wa CHADEMA, zimetokana na video inayoonekana siku hizi kwenye U tube, ikimwonesha Mwingulu akitamba kwamba ndiye aliyenunua vifaa vinavyodaiwa kutumiwa na Ludovick kumrekodi Lwakatare. Akitangaza uamuzi wa kutoa dhamana kwa washitakiwa, Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Kisutu, Alocye Katemana, alisema amefikia uamuzi wa kukubaliana na mawakili wa washitakiwa walioomba mahakama iwapatie dhamana kwa sababu ina mamlaka ya kufanya hivyo na kwamba anatupilia mbali ombi la mawakili wa upande wa serikali uliotaka mahakama isiwape dhamana.

          “Ili mshitakiwa apate dhamana ni lazima awe na wadhamini wawili wanaotoka taasisi zinazotambulika kisheria,  ambapo  kila mdhamini atatakiwa asaini dhamana ya sh milioni 10 pamoja na washitakiwa wenyewe kusamilisha hati  za kusafiria mahakamani na kutotoka  nje ya Jiji la Dar  es Salaam bila kibali cha mahakama,” alisema Katemana. Uamuzi huo ulitolewa saa mbili asubuhi, lakini Lwakatare na mwenzake walilazimika kusubiri hadi saa nane mchana ili upande wa mashitaka  upate nafasi ya kuhakiki barua na nyaraka za wadhamini. Mei 8, mwaka huu, Jaji Lawrence Kaduri wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam alitoa uamuzi wa kuwafutia makosa matatu ya ugaidi washitakiwa baada ya kuona hati ya mashitaka haijitoshelezi kuwafungulia mashitaka hayo.

Source: Hamis A. (June 2013). Maajabu ya Lwakatare. Retrieved from Tanzania Dama

No comments: