Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora

Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora
----------------------WE THANK AND APPRECIATE YOU FOR VISITING CHADEMA DIASPORA BLOG. AGAIN, THANK YOU!-----------------------

Wednesday, June 5, 2013

Kawambwa abanwa bungeni



          MOTO wa matokeo mabaya ya kidato cha nne mwaka 2012, umeendelea kumwakia Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, ambapo wabunge wamepinga hatua ya serikali kufuta matokeo hayo na kuyapanga upya badala ya wanafunzi waliofeli kurudia mitihani. Wabunge hao walitoa malalamiko hayo wakati wakichangia hotuba ya bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka 2013/14 iliyowasilishwa bungeni jana na Waziri Shukuru Kawambwa, wakisema utaratibu wa ‘standardization’ uliotumika ni siasa na hauna maana. Mbunge wa Karagwe, Deogratius Ntukamazina (CCM), alisema kama mwalimu mzoefu hakubaliani na utaratibu huo kwa vile unaangamiza mfumo wa elimu na kuwapa wanafunzi jeuri ya kufeli. “Standardization ni siasa, sikubaliani na hili hata kidogo. Mwalimu Nyerere aliwahi kuelezwa hili na aliyekuwa mtawala wa Kiingereza nchini kuwa unaweza ukafanya siasa kwenye kila kitu lakini si kwenye elimu,” alisema.

         Aliongeza kuwa baada ya serikali kubaini kasoro hiyo ilipaswa kuishughulikia kwa kuwatahini wanafunzi upya. Ntukamazina alifafanua kuwa matokeo hayo yalichangiwa na uzembe wa pande zote tatu yaani wanafunzi ambao wameacha kusoma na kutazama filamu za Kimarekani, serikali ambayo haitimizi matakwa ya walimu na wazazi. Naye mbunge wa Mchinga, Saidi Mtanda (CCM), alisema kuwa kabla ya Kawambwa na naibu wake, Philipo Mulugo, kujiuzulu, Bodi ya Baraza la Mitihani na Kamati ya Kutunuku Madaraka zinatakiwa kuvunjwa kwa kutowajibika. Alisema watendaji wake ndio walimchakachua Waziri Kawambwa kwa kutumia mifumo tofauti ya usahihishaji mitihani na kupanga madaraja.


              Msemaji mkuu wa kambi ya upinzani bungeni kwa wizara hiyo, Susan Lyimo, alisema hatua ya serikali kulitupia mzigo Baraza la Mitihani ili kuhalalisha makosa iliyoyafanya ni usaliti.“Kwa uchambuzi huu ni wazi sasa kuwa ukweli ni lazima usemwe hata kama utauma namna gani ili taifa lisonge mbele kwa kuwa ni dhahiri kuwa watoto wetu walifeli kwa sababu ya mfumo wetu wa elimu. “Tunapenda kuionya serikali kuwa mchezo huu wa kisiasa uliochezwa ili kupunguza hasira za wananchi ni mchafu ambao haulipeleki taifa letu mbele kwa kuwa hauelezei vyanzo vya matatizo yanayosababisha anguko la elimu nchini na mfumo wetu wa elimu,” alisema. Lyimo alisema kuna ushahidi wa kutosha kwamba serikali inahusika sana kusababisha anguko kuu la matokeo ya kidato cha nne 2012.

     “Novemba 14, 2012 Kamishna wa Elimu Profesa E. P. Bhalalusesa alimwandikia Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Taifa yenye kichwa cha habari “Yah: Utaratibu wa matumizi ya alama za maendeleo ya mtahiniwa na viwango vya ufaulu katika mitihani ya Taifa,” alisema. Alisema ni dhahiri kwamba kuporomoka kwa elimu nchini, pamoja na sababu nyingi zilizotajwa na tume mbalimbali za uchunguzi, kuna tatizo pia la kiuongozi katika Wizara ya Elimu. “Kambi Rasmi ya Upinzani inamtaka Waziri Kawambwa na naibu wake, Mulugo, watumie busara zao na kujipima kama kweli pamoja na majanga makubwa yaliyotokea katika elimu ambayo madhara yake yatadumu kwa vizazi vingi, wanastahili kuendelea kuongoza wizara,” alisema.

       Mbunge wa Viti Maalum, Margaret Sitta, alipendekeza uwekwe mfumo mzuri wa kuhudumia walimu katika masuala ya mishahara na kupanda madaraja na vile vile idara ya ukaguzi wa shule na vyuo ipewe meno na fedha za kutosha kuweza kufanya kazi yake ipasavyo. Sitta pia aliungana na kambi ya upinzani kupendekeza kuwa wahadhiri wastaafu wapewa mikataba ya miaka miwili miwili ili waendelee kulisaidia Taifa kwa wakati ambao wana uwezo wa kufanya kazi.

Source: Kamkara E. (June 2013). Kawambwa abanwa bungeni. Dodoma. Retrieved from Tanzania daima

No comments: