Ikulu imetajwa kuwa ni moja kati ya taasisi zinazonuka rushwa Tanzania kutokana na utendaji wake. Hayo yamo katika mada iliyowasilishwa na Mbunge wa Magu, Dk Festus Limbu kwenye semina ya siku moja ya kuwajengea uwezo, wajumbe wa Kamati za Bunge za Kudumu za Bajeti, Hesabu za Serikali (PAC) na Hesabu za Serikali za Mitaa, (LAAC) kuhusu rushwa, iliyofanyika mjini Dodoma juzi. Katika semina hiyo iliyoandaliwa na Ofisi ya Bunge kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), Dk Limbu alisema: “Rushwa imeenea kila mahali, katika sekta na nyanja zote (horizontal) na kwa ngazi zote, kuanzia Ikulu hadi ofisi ya kitongoji, balozi, kaya na mtu binafsi.”
Alisema kuwa rushwa hiyo inajidhihirisha kwa namna mbalimbali ikiwamo mipango mibovu ya Serikali, mashirika ya umma, mikataba mibovu, taratibu mbovu za ununuzi, ujangili, uhalifu, upendeleo na hongo. Huku akisikilizwa kwa makini na wabunge, Dk Limbu alisema kwa mujibu wa Taasisi ya 2012 Corruption Perception Index iliyopima nchi 176 kwa rushwa, Tanzania inashika nafasi ya 102 ikiwa na alama asilimia 35, huku Rwanda ikitajwa kuwa na rushwa ndogo ya asilimia 53 duniani. Naye Naibu Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Dodoma, Sosthenes Kibwengo akiwasilisha mada yake, aliitupia lawama Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), kuwa ndiyo inayochelewesha kesi za rushwa wahusika wanaponaswa.
“Nimezunguka nchi mbalimbali duniani, hadi China huko kote taasisi zao ziko huru, zinamkamata mtu, zinamfungulia mashtaka na kumfikisha mahakamani bila kupitia kwa DPP, lakini mfumo wetu hauipi uhuru Takukuru,” alisema akiongeza: “Takukuru inamkamata mtu kwa rushwa, inamfungulia mashtaka na baada ya hapo yanapelekwa kwa DPP, naye anaamua mtuhumiwa hana makosa, Takukuru ijitegemee, ipeleke watu moja kwa moja mahakamani.” Alisema pia kwamba rushwa imekuwa kitu cha kawaida Tanzania na kwamba watu wanaomba rushwa bila woga.
“Utakuta mtu anashughulikiwa jambo lake na watu wakimaliza wanamuuliza, sasa unatuacha-achaje?...,” alisema na kuamsha kicheko kwa wabunge. Baadhi ya waliochangia ni pamoja na Mbunge wa Ukonga, Eugene Mwaiposa aliyesema adhabu kwa wapokea na watoa rushwa ni ndogo wakati Maria Hewa alisema maofisa wa Takukuru hutoa siri za watu wanaokwenda kutoa taarifa za wanaodai rushwa kwani hata yeye yalimkuta.
Source: Mwananchi (June 2013). Dk Limbu: Ikulu inanuka rushwa. Retrieved from Mwananchi
No comments:
Post a Comment